Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limefanikiwa kumtia mbaroni mtu mmoja anayedaiwa kuchoma moto jengo la mahakama ya mwanzo mjini Moshi .
Kwa Mujibu wa Taarifa ya jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro mtuhumiwa huyo ametajwa kwa jina la John Daud, (42), mkazi wa mtaa wa Lengua,Manispaa ya Moshi ambaye baada ya tukio hilo alikimbia .
Moto huo uliathili pia jengo la ofisi za ustawi wa jamii ingawa jengo hilo kwa sasa halitumiki kwa shughuli za kimahakama
Tukio hilo limetokea jana Agosti 24, 2026 majira ya saa mbili asubuhi mtaa wa Lengua, kata ya Mawenzi, Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kuchoma jengo la Mahakama ya Mwanzo ambalo halitumiki kwa shughuli za Mahakama na moto huo kuunguza vyumba vinne pamoja na nyaraka mbalimbali zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya ofisi hizo na kukimbia.
Jitihada za kuzima moto huo zilifanyika na Jeshi la zimamoto na Uokoaji na Wananchi bila kusababisha madhara yoyote kwa binadamu.
Aidha, thamani ya mali zilizoungua bado haijafahamika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kupata taarifa ya tukio hilo msako mkali ulifanyika na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo akiwa katika hafla za Maulidi leo Agosti 25, 2026.
Uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na mamlaka na vyombo vingine na utakapokamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zake.
Taarifa hii ni kutoka ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro chini ya kamanda wake SACP Simon Maigwa