Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
THE OPEN UNIVERSITY OF TANZANIA
OFFICE OF THE VICE CHANCELLOR
OFFICE OF THE VICE CHANCELLOR
P.O. Box 23409 Tel: 255-22-2668992/2668445 Dar es Salaam, Tanzania Fax: 255-22-2668759
http://www.out.ac.tz E-mail: vc@out.ac.tz
WARAKA WA TAHADHARI YA MAAMBUKIZI YA COVID 19 NA 21
WARAKA WA TAHADHARI YA MAAMBUKIZI YA COVID 19 NA 21
8 Februari 2021, Dar es Salaam,
Ndugu Wafanyakazi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,
Nianze kwa kuwatakieni heri ya mwaka mpya, kwani tangu mwaka huu uanze hatujaweza kukutana. Tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha salama. Wapo wenzetu wengi ambao hawakuweza kuvuka, siyo kwamba walitenda maovu zaidi yetu sisi. Ni kwa neema na rehema za Mungu tu, kwamba sisi bado tupo hai hata leo.
Nachukua fursa hii kuwatahadharisha wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kuwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu, au Covid 19/21, inazidi kushamiri mahali pote nchini mwetu. Ni budi kila mmoja wetu achukue tahadhari, kama inavyoelekezwa na viongozi wetu wa kitaifa. Ugonjwa huu inaeleweka, hauna tiba katika mahospitali yetu. Hata nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza zimeshindwa kuutibu. Chanjo inayopigiwa upatu, haijathibishwa kama inaweza kuuzuia. Wapo waliochanjwa na bado wameugua.
Hata hivyo, imethibitishwa kuwa taratibu za kijadi kama kujifukiza (Nyungu) zinaleta ahueni kwa walioathirika, ingawa haimaanishi kwamba virusi vile vitakufa. Pia dawa zilizobuniwa na wataalamu wa kitanzania kama vile Covidol na Nimricaf zinaonekana kutoa unafuu zikitumiwa pamoja na Nyungu. Inakuwa ni vigumu sana kuepuka maambukizi ikiwa hatuzingatii masharti ya kujikinga, ikiwepo kuepuka mikusanyiko ya watu kama vile harusi, misiba, viwanja wa michezo, masoko, na kadhalika. Watanzania wengi wanadhani ugonjwa huu utawapata wengine, wasitambue kuwa hata pale wanapopata maambukizi, huwa wamekuwa wazembe kujilinda.
Ni muda mfupi upo kuanzia mtu anapopata maambukizi hadi kuugua na kushindwa kupumua, hali inayolazimu mgonjwa kupelekwa hospitali ili awekewe hewa ya oksijeni kwa gharama kubwa akisubiri kufa! Tumepoteza watu wengi, na tungojee maafa makubwa zaidi kama hatutabadilika.
Naandika hapa kwa uchungu sana, ninapohesabu watu ambao wamefariki katika siku chache zilizopita. Wasomi na wasio wasomi. Wazee na hata vijana. Tutaendelea kupuuzia maelekezo ya viongozi wetu hadi lini? Wiki hii ilitangazwa kuwa ni wiki ya kupiga nyungu kitaifa. Je? Wewe umechukua hatua gani, kupiga nyungu, wewe na familia yako? Je? Unavaa barakoa unapokuwa kwenye mikusanyiko ya watu? Unapoenda sehemu za ibada? Unapoenda sokoni? Unapokuwa darasani? Unapopanda daladala? Na kadhalika. Je, unanawa kwa sabuni au kwa kutumia vitakasa mikono mara kwa mara? Kwa wale tunaoshika nyaraka maofisini tujitahidi kuvaa gloves, ama tutumie vitakasa mikono mara kwa mara. Kama hufanyi haya, basi ujihesabu kama mhanga mtarajiwa wa homa ya mapafu. Madereva pia wasituweke katika hatari, kwa maana wasizurure ovyo wanapokuwa hawatuendeshi. Ni vema madereva wakakaaa katika maeneo ya ofisi zao badala ya kuzurura ovyo, la sivyo itabidi viongozi waanze kujiendesha wenyewe.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoingia chuoni, tunasisitiza kuwa wakae majumbani na kusoma kwa mtandao (Online). Hatutaruhusu wanafunzi na wageni kuingia kwenye kampasi zetu bila sababu maalum, kama kuja kuchukua vyeti au kufanya “clearance”. Na pale inapobidi waingie, watakiwe kuvaa barakoa wakati wote. Waende kule wanakotakiwa kwenda, na si kuzurura kila mahali. Utaratibu ufanyike kuwasaidia wanaotaka kutumia maktaba kama ni lazima, Wengi wanaitumia maktaba yetu kama mahali pa kujisomea tu. Maelekezo haya ni kwa ajili ya makao makuu, vituo vyote vya mikoa na vituo vya uratibu vilivyoko nchini.
Kuhusu vikao, ratiba ya vikao itaendelea kama ilivyopangwa, lakini vikao vyote vitafanywa kwa njia ya mtandao wa Zoom, isipokuwa Baraza la Chuo ambalo sina mamlaka nalo. Tutafanya Mkutano Wa Baraza la Wafanayakazi uliokuwa umepangwa kuwa tarehe 15 Februari huko Morogoro, kwa njia ya Zoom. Kamati Tendaji ya Baraza pia itafanya mkutano wake kwa Zoom siku ya Ijumaa, tarehe 12 Februari. Tayari kuna baadhi ya wajumbe wanaumwa, na hatuwezi kuhatarisha maisha ya watu wengine. Pia Baraza la Serikali ya Wanafunzi (USRC) lililopangwa kufanyika mkoani Mara, tarehe 17-19 Februari, litaendeshwa kwa Zoom. Waandaaji wa mikutano hii watapata link ya vikao kutoka kwa Eng, Petro Sanga na kuisambaza kwa wakati kwa washiriki wote.
Tunatoa tahadhari kwa wote wanaokusudia kusafiri nchi za nje, kuwa kipindi hiki siyo salama sana kusafiri. Nchi nyingi zina maambukizi ya Covid, hata ukipimwa ukakutwa huna maambukizi, unaweza ukawa “carrier”. Tutahitaji wanaotoka nje kujitakasa kwa kupiga nyungu na kujitenga angalau kwa wiki moja.
Nimetoa maoni yangu, kama ushauri, nikiwa nawajibika pia kama kiongozi, kuwalinda wale wote ninaowaongoza. Asanteni sana, Mungu awalinde, tumalize huu mwaka salama.
Prof. Elifas Tozo Bisanda