COVID-19 & DEEP STATE: Nini maana ya Uhandisi Jamii unaotokea Duniani!?

COVID-19 & DEEP STATE: Nini maana ya Uhandisi Jamii unaotokea Duniani!?

SEHEMU YA TATU


DEEP STATE, COVID-19: Nini Maana ya Uhandisi Jaamii Unaotokea Duniani?




#3


Kuna watu wana wasiwasi kwa nini nagusia matukio kadhaa ambayo yanaonekana hayahusiani. Kama ni msomaji wangu wa siku nyingi utaelewa namna gani naandika Makala zangu... kama mtori... endelea kupakua, fuatana nami.



Kwenye kichwa cha habari ya makala hii nimeandika kuhusi Deep State na COVID-19.
Kabla sijaweka ushahisi wangu kwamba namna gani twapaswa kujiuliza maswali kuhusu hii Covid19 kwanza nataka nikupe ushahidi kuhusu Deep State na namna gani inafanya kazi na kwa nini nina wasiwasi hii Covid-19 inaweza kuwa karata iliyotupwa kwa umahiri kabisa na kwa makusudi.
Imetupwa na nani?


Here we go..


Jana niliwaeleza kwamba katika kitambulisho ambacho Raymond alikutwa nacho kilionyesha kwamba alikuwa ni muajiriwa wa kampuni inayoitwa Hyperion Protective Consultants ambayo nilieleza kuwa hii ilikuwa ni shell Company ya kampuni mama ya Blackwaters Worldwide ambao nikasema hawa ni moja ya 'contractors' wakuu wa CIA.
Kuna jambo la msingi sana kulielewa kuhusu hawa Blackwaters Worldwide kabla sijaendelea mbele sana.


Kama umekuwa mfuatiliaji wa vita ya Iraq basi sina shaka utakuwa umewahi kusikia kisanga cha Nisour Square Massacre.
Kisanga hiki cha Nisour Square Massacre pengine ndio moja ya skandali kubwa ya kwanza kufanya Marekani wakosolewe vikali na hatimaye wafanye mabadiliko makubwa katika oparesheni zao za pale Iraq.
Kisanga hiki kinahusu vifo vya Wairaq 17 huku wengine 20 wakijeruhiswa vibaya kwa kupigwa risasi mchana na hadharani kabisa na Wanajeshi wa Marekani ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa Balozi wa Marekani pale Iraq. Tukio hili lilitokea mwaka 2007 mwezi Septemba tarehe 16…


Sasa,

Nimegusia kisanga hiki sababu natamani nieleze kidogo kile ninachoelewa kuhusu "Deep State" na namna gani tunapaswa kuwa na hadhari na kutafakari kwa kina kuhusu mlipuko huu wa COVID-19.

Kwenye kisanga hiki cha Nisour Square Massacre baadae baada ya uchunguzi wa tukio hili ambalo lilishitua ulimwengu wakati huo, ikaja kubainika kwamba wanajeshi wale ambao walikuwa wanasindikiza ule msafara wa Balozi wa Marekani pale Iraq hawakuwa hasa "Wanajeshi wa Marekani". Kwamba ndio walikuwa ni raia wa Marekani, na ndio walikuwa ni wanajeshi lakini hawakuwa "Wanajeshi wa Marekani". Ilikuja kubainika kwamba wanajeshi wale walikuwa ni wanajeshi binafsi wa kampuni ya Blackwater Worldwide.
Ilikuwa ni mshituko mkubwa sana, sababu ni ilikiwa inaeleweka wazi juu ya uwepo wa PMCs (Private Millitary Companies) lakini hakuna ambaye alikuwa amewahi hata kuona kwamba ati hizi PMCs zimekuwa na ushawishi na nguvu kiasi kwamba mpaka wao ndio wanalinda 'diplomatic convoys' adhimu kama ya balozi wa Marekani tena kwenye eneo hatari kama Iraq. Na pia wanakuwa na mamlaka bila woga kupiga raia risasi.

Ulikuwa mshituko mkubwa sana kwenye ulimwengu wa Ulinzi na Usalama na kufanya watu waanze kuuliza maswali ambayo awali hayakuwahi kuulizwa.


Kwa utaratibu, umakini mkubwa na ushahidi naomba nieleze kwa undani kuhusu Deep State na kwa namna gani si tu kwamba ni 'conspiracy theory' kama unavyoweza kudhani na vipi tunaunga dot na tukio la mwaka 2011 pale Lahore Pakistan na inatupa tafasiri ipi na hii hamaki ya COVID-19.



Mwaka fulani hivi… miaka kadhaa iliyopita, yuko bwana mmoja hivi (najua kuwa wapwa watauliza ni mimi au si mimi… doesn't matter) alifika kwenye ubalozi wetu wa Tanzania Marekani, jijini Washington D.C ambapo jengo letu la ubalozi lipo mtaa wa North West, 22nd.
Ni miaka kadhaa tu nyuma kama miaka mitano hivi au sita… enzi hizo pale ubalozini wako akina mama Immaculata, akina Abbas Misana kama balozi mdogo, bwamdogo Mugendi Zoka mtoto wa shushushu nguli Jack Zoka akiwa mwambata wa Political Affairs, akina Kanali Mutta mwambata wa masuala ya Ulinzi… watoto wa mjini akina Emmanuel Swere… enzi hizo, miaka kadhaa iliyopita, bwana huyu alifika pale balozini.
Moja ya tongotongo ambayo bwana huyu aliitoa pale ni Washington ni suala dogo sana ambalo awali hakuwa analijua. Suala dogo sana lakini mpaka leo liko kwenye kumbukumbu kichwani… kwamba kwenye maongezi ya kawaida wakazi wa Washington wenyewe huwa lile eneo hawalitamki kama Washington kama sisi wengine.

Yani ni kama miaka ya zamani mtu akitoka mkoani kuja Dar es Salaam anasema anaenda "Bongo", lakini husingeweza kumsikia mkazi wa Dar anasema anaishi "Bongo" akimaanisha Dar es Salaam.
Pale Washington wakazi wa pale wenyewe wanapaita "The District". Yani mfano ukutane naye New York, kwenye maongezi anaweza kukwamba "..tommorow i'm flying back to the district.."
Au mara nyingine wanatumia D.C. Huu ni moja ya ushamba ambao bwana huyu ulimtoka miaka hii kadhaa nyuma.


Lengo sio kuongelea huu ushamba ambao bwana huyu aliutoa bali baadhi ya mambo kadhaa madogo madogo aliyayaona ambayo yalichochea hari ya ndani kufanya tafiti na kuuliza maswali kuhusu ushawishi na mlinganyo wa nguvu kwenye jukwaa la siasa za dunia.

Zaidi ya ushamba huo wa kwanza, kitu cha msingi zaidi ambacho bwana huyu alikiona kwa mara ya kwanza na kuchochea hari nafsini ilikuwa ni barabara inaitwa Beltway iko pale Washington.
Hii Beltway ni sehemu ya "interstate highway system"… yaani twaweza sema kama mfumo wa barabara kuu ambazo zinaunganisha majimbo yote ya Marekani. Sasa kwa pale Washington hii highway inaitwa Beltway.
Barabara hii iko tofauti kidogo sababu yenyewe inazunguka jimbo lote la Washington. Yaani kwamba kwa mfano ukiangalia kwenye ramani alafu tuseme kwa mfano uki-highlight hii barabara (Beltway) mfano kwa kui-bold kwenye ramani utaona inatokea umbo la duara na pale katikati ndio D.C penyewe.
Yaani chukua mfano barabara ya Bagamoyo, nenda mpaka pale Mbezi Beach Masana inapokutana na barabara ya Goba, kisha ukitokea Mbezi nenda na Morogoro Road mpaka Magomeni inapokutana na Barabara ya Kawawa alafu kutoka Magomeni mpakq Morocco. Unaona huo mzingo, hapo katikati sasa ndio iwe Washington na huo mzingo wote ni ndio hiyo highway ya Beltway. Kwamba barabara hii imezungunga kwa mzingo jimbo lote la Washington.

Bwana huyu alikaa muda kadhaa pale ubalozini.. na kama ujuavyo watu wa ubalozi huwa wana alikwa kwenye dhifa na hafla mbali mbali za kiserikali.
Katika maongezi na watu kadhaa kwenye dhifa hizi kapata kusikia jambo jipya ambalo nalo lilimtoa ushamba.. kuna neno alilisikia linatumika sana, "Beltway Politicians".
Binafsi kwenye maisha yangu pengine nafanya vitu viwili tu kwa ufanisi mkubwa… kusoma na kuandika. Nasoma vitu vingi sana kiasi kwamba kuna muda nahisi ni nadra kusikia kitu ambacho sijawahi kukisikia kabisa au sina idea nach hata kidogo… ni nadra mno.
Na kuhisi kwangu kote kwamba nasoma vitu vingi lakimi sikuwahi kulisikia neno hili "Beltway Politician" wala sijawahi hata kuliona limeandikwa mahala na wala sikuwa najua maana yake.

Wajua hata ukienda pale Bungeni Dodoma wana vimisemo vyao, wana vimaneno vyao ambavyo hata huwezi kuvikuta huku mtaani. Ndivyo ambavyo bwana huyu kwa mara ya kwanza naye alilisikia neno hili "Beltway Politician".

Binafsi kwa haraka nilihisi kwamba pengine maana ya neno hilo lina maana ya wanasiasa ambao labda wanafanya kazi zao ndani ya Beltway (Washington) kwa maana ya Maseneta na Congressmen na Congresswomen.
Lakini kadiri ambavyo bwana huyu alikuwa analisikia neno hili baadae ndio akaja kuelewa maana halisi ya "Beltway Politician".
Wanasiasa ndani ya Washington wanalitumia neno hili kuwaelezea wanasiasa wenzao ambao wanawahisi kuwa ni 'insiders' kwenye muhimili ambao sio serikali na wala sio bunge. Kwamba kuna muhimili wenye nguvu sana ndani ya Washington lakini sio serikali, sio mahakama na wala sio bunge na kuna baadhi ya wanasiasa wenzao ambao wanawashuku kuwa sehemu ya 'muhimili' huu.

Sasa, miaka ya hivi karibuni baada ya kuibuka matumizi ya neno "Deep State" akili yangu moja kwa moja zikakumbuka kumbukumbu ile ya miaka ile Washington ambapo kwa mara ya kwanza bwana yule alilisikia neno "Beltway Politicians".
Sasa je, Beltway Politicians ndio Deep State?? Jawabu ni hapana… Beltway Politician ni kasemu kadogo tu ndani ya Deep State. Deep State ni kitu kikubwa zaidi na hakuna muda ambao tunapaswa kuelewa kuhusu Deep State kama sasa..


Tuanze… kwa mara ya kwanza kabisa niiweke hii taarifa.
Nakala iende Kisarawe…


Twafahamu kuwa document yeyote kwenye serikali zetu zote duniani ambazo hazina ruhusa ya kuonwa na watu wengine zaidi ya walengwa huwa zina muhuri wa siri. Mara nyingi documents hizi zinakuwa zimebeba taarifa ambazo ni 'sensitive' na kama ikitokea kuonwa na watu wasiopaswa basi inaweza kuwa na madhara kwenye utunzaji wa usiri wa baadhi ya masuala yenye maslahi ya usalama wa nchi.

Serikali zote na Idara zote za ujasusi duniani wana mamia kama sio maelfu ya documents za namna hii zinazohitaji usiri.

Sasa,
Pale Marekani kama ilivyo kwa nchi nyingine nao wana maelfu ya document za namna hii.
Lakini katika documents hizo ziko documenst mbili ambazo kwa maoni yangu document hizi ni 'sensitive' zaidi kuliko document nyingine zozote zile… lakini ajabu document hizo mbili zote hazina muhuri wa SIRI na jambo la ajabu ni kwamba mpaka leo hii ninapoandika document hizi hazijawahi kuvuja mtandaoni.

Ziko mbili nyaraka hizi.. extremly sensitive lakini hazina muhiri wa siri na hazijawahi kuvuja na ndio maana hujawahi kuzisikia, na kamwe hutokuja kuwahi kuziona popote pale.

Nyaraka ya kwanza kati ya hizi mbili haina jina maalumu/mahususi hasa lakini ingekuwa hapa nchini kwetu kwenye kitengo cha kumlinda Mzee, basi watoto wa kijiweni 'Kisarawe' wageweza kuifahamu kwa jina la “Site Post Assignment Log."
Vijana wetu hapa nchini ya kwao wanaiita jina hilo lakini ile ya pale Marekani inayotumiwa na vijana wa Secret Service haina jina mahususi sana japo dhumuni ni la kufanana kabisa na hata la hawa wa hapa kwetu nyumbani.
Kwa hiyo mniruhusu hata hiyo ya Secret Service niite jina hilo hilo kwa minajiri ya kwenda sambamba kwenye kufanya rejea.

Sasa hii “Site Post Assignment Log" ya pale Marekani inayotumiwa na Secret Service yenyewe ndani yake inakuwa na jina la tukio, tarehe, saa alafu kisha unafuata mfululizo wa namba na herufi ambazo ziko kwenye codes.
Hii “Site Post Assignment Log" yenyewe inatumika kuonyesha maafisa wote wa Secret Service siku ya tukio fulani husika watakuwa wapi, watajipangaje, yupi atakuwa wapi, mbinu zitakazotumika kuimarisha ulinzi, procedures za emergency za kumuokoa Rais kama ikitokea kuna shambulio pamoja na code zote za ulinzi ambazo zitatumila kwenye hiyo siku husika.
Taarifa zote hizi zinakuwa kwenye hiyo nyaraka nyeti ya "Site Post Assignment Log".


Sasa,
Ikulu ya Marekani wana utamaduni kila mwaka wanafanya tukio linaitwa White House Correspondents’ Dinner. Hiki huwa ni chakula cha jioni ambacho kinaandaliwa na Ikulu kwa ajili ya wanahabari ambao wanaripoti habari za Ikulu kutoka kwenye vyombo vyote vya habari.
Mgeni rasmi anakuwa no Rais na anajumuika na wanahabari hao kupata chakula cha jioni lakini pia mara zote huwa anaalika pia na watu mbalimbali mashuhuri.
Tukio hilo japo linaandaliwa na Ikulu lakini huwa halifanyiki Ikulu. Huwa linafanyika kwenye moja ya Hoteli mashuhuri ambayo itachaguliwa kwa mwaka huo.

Kama umewahi kuona video mtandaoni ya Obama 'anampiga madongo' Trump kwa utani na mizaha mpaka Trump anafura na uso kuwa mwekundu kwa hasira, sasa video ile ni ya moja ya matukio kama hilo la Chakula cha jioni enzi za Urais wa Obama.

Sasa, niwapeleke kwenye White House Correspondents’ Dinner ya mwaka 2011. Hii yenyewe ilifanyika tarehe 30 April.
Wahudhuriaji walikuwa hao wanahabari wenyewe, Rais Obama, mkewe Michelle, Mwanasheria Mkuu, Mwenyekiti wa Joint Chief of Staffs, Mkurugenzi wa CIA, Magavana wa majimbo sita walikuwepo, wabunge ishirini na sita wa Congress, Meya wa New York, Waziri mwenye dhamana ya Hazina pamoja na watu wengine kadhaa muhimu.

Wote hawa walikuwa sehemu hii moja kwa wakati mmoja… kwenye hii dhifa.

Sisi tulioko nyumbani ambao tunatazama kwa runinga matukio haya huwa tunaburudika kwa hotuba mwanana pamoja na utani wa comedians ambao mara zote huwa ndio ma-MC wa shughuli hizi. Lakini kiusalama tukio kama hili huwa ni moja la kupasua kichwa kwa wanausalama wanaomlinda rais Secret Service.
Sababu tarehe ya tukio hili na mahala ambapo litafanyika huwa inatangazwa miezi kadhaa kabla. Fikiria kama wewe ni mtu mwenye nia mbaya dhidi ya Rais, yaani miezi kadhaa kabla, unakuwa unafahamu Rais pamoja na karibia nusu ya serikali yote watakuwa wapi, tarehe ngapi na saa ngapi… fursa adhimu iliyoje.


Tukio hili la mwaka 2011 lilikuwa linafanyika Hoteli inayoitwa Washington Hilton (siku hizi inaitwa Hinckley Hilton). Ni hoteli hii hii ambayo mwaka 1981 Rais Ronald Regan alishambuliwa kwa risasi.

Wageni wote waalikwa walikuwa wamewasili, na zilikuwa zimebakia kama dakika ishirini tu kabla msafara wa Rais Obama kuwasili. Wakati wanausalama wanafanya 'sweep' za mwisho mwisho ka la ta msafara wa Rais kuwasili, moja ya Maafisa Usalama walioko Ikulu akawasiliana na wenzake walioko eneo la tukio kwamba moja ya mabinti ambao ni Staff wa Ikulu alikuwa amepoteza PIN za kumpa accesss ya maeneo ambayo Secret Service huyaita 'sensitive areas' ndani ya Ikulu..




Inaendelea…



Habib "The Bold" - 0718 096 811 (WhatsApp)
To Infinity and Beyond

Sent using Jamii Forums mobile app
Naendele a kuweka kambi
 
KIDOKEZO

Mwaka jana katika group la Whatsapp niliwahi kuandika na kuchambua kuhusu mgogoro wa Kagame na Museveni uliokuwa unatishia mpaka nchi zao kuingia vitani. Kuna nyaraka fulani nikaweka na masuala fulani nikagusia kuna watu wakaniuliza umejuaje haya... wengine wakauliza "unataka kutuaminisha wewe unajua kuliko taasisi fulani.!"
Nategemea pia kuambiwa sentensi kama hizo kwenye uzi huu ninaouweka.. hivyo mapema kabisa kabla sijajichimbia kwenye hoja mezani nijieleze kwa kidokezo hiki.

Mwaka 2003 kulitokea tukio ambalo lilikuja kuzua mzozo wa kimataifa mkubwa sana. Kuna sheikh mmoja hivi ambaye alikuwa ni imamu wa msikiti kwenye jiji la Milan huko nchini Italia alitekwa na CIA kwa kushirikiaa na SISMI (hii ni idara ya intelijensia kwenye jeshi la Italia). Sheikh huyu jina lake anaitwa Abu Omar (hili ndio jina watu wengi wanalolijua lakini sheikh huyu jina lake halisi hasa anaitwa Hassan Mustafa Osama Nasr). Huyu imamu alikuwa anaishi hapo Italia baada ya kupatiwa ‘political asylum’ akitokea nchini Misri na alitekwa kwa kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Kabla ya kuja kuishi hapo Italia, Abu Omar kule kwao Misri alikuwa ni moja ya wahubiri mashuhuri sana wa kiislamu na alikuwa mwanachama wa kikundi cha harakati kinaitwa al-Gama’a al-islamiyya. Kikundi hiki bado kingalipo hata sasa na harakati yake kubwa ni kutaka kuigeuza Misri kuwa dola ya kiislamu japo hawa wanafanya harakati hii kwa njia za amani tofauti na wenzao wale wa Islamic State. Japo kuna tetesi kwamba pia walishirikiana na kikundi cha Egyptian Islamic Jihad kumuua Rais Anwar Sadat mwaka 1981. Lakini kwa muda mrefu kikundi cha al-Gama-a al-Islamiyya wamekuwa wakijihusisha na harakati za amani nchini Misri.

Sasa huyu Hassan Mustafa naweza kumfananisha na kama mzee wetu sheikh Ponda… huyu bwana ni mtu mwenye misisimamo mikali mno dhidi ya serikali. Kutokana na misimamo yake hii mikali ukafika wakati akawa tishio hasa kwa serikali na akaanza kusakamwa mno na serikali kumuweka kwenye kundi la ‘magaidi’ hatari nchini humo. Alisakamwa mno mpaka kufikia hatua ya kutishia maisha yake. Ndipo hapa ambapo aliamua kuondoka Misri na kukimbilia nchini Italia. Kule Italia alipokelewa kama mkimbizi wa kisiasa na akapewa asylum. Waweza kujiuliza ni kwa nini wazungu wale wampokee ‘gaidi’ ambaye hata nchi yake walikuwa wanamuhofu na kumsaka.

Nimesema pale mwanzo kwamba huyu bwana Abu omar majina yake halisi ni Hassan Mustafa Osama Nasr. Sasa kipindi hicho (kabla ya kukamatwa na CIA) hakuna ambaye alikuwa anajua kwamba huyu bwana Hassan Mustafa ndiye Abu Omar. Yaani kwamba katika ulimwengu wa ujasusi na intelijensia walikuwa wanafahamu kwamba kuna mtu anaitwa Abu Omar ambaye anajihusisha na shughuli za kigaidi kwenye ukanda wa Kaskazini mwa Afrika lakini walikuwa hawajui huyu Abu Omar ni nani (hawakujua kwamba Abu Omar ndiye Hassan Mustafa Nasr).

Mtu anaweza kujiuliza hii yawezekanaje? Umjue mtu mpaka jina na papo papo usimjue ni nani… hii ni kawaida sana kwenye ulimwengu wa ujasusi. Waweza kupata taarifa ya uhakika kabisa kwa asilimia mia moja na papo hapo usijue namna gani inanyumbulika. Mfano mdogo, mwishoni mwa mwaka jana (yaani mwaka 2018, niliweka kwenye group mwaka jana) mpaka miezi ya mwanzo ya mwaka huu (kwa hiyo 2019) hapa Dar es Salaam kulikuwa na taarifa ya uhakika kabisa kwamba kulikuwa na mpango wa kufanyika shambulio la kigaidi katika moja wapo ya maeneo maarufu sana ambako watu wanapenda kutembelea kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali pamoja na kupumzika kwenye migahawa yake mwanana (tuhifadhi jina la sehemu). Hii illikuwa ni taarifa ya uhakika kabisa kwamba kuna shambulio lilikuwa linapangwa kufanyika hapo. Hata kwenye moja ya kambi za jeshi ambazo iko karibu na eneo hilo ninalolizungumzia walianza kutengeneza sehemu za dharura kwa ajili ya kuhifadhi majeruhi kama ikitokea shambulio limetokea. Lakini vyombo vyetu vya usalama hawakuwa wanajua ni lini shambulio hilo litafanyika au labda kuwa hata na list ya ‘potential suspects’. Twapaswa kuwapongeza idara zetu za intelijensia (hasa vipepeo na military intelligence) kwa kuweza kudhibiti hatari hiyo na mpaka sasa jiji liko shwari kabisa…

Nilikuwa naweka mkazo pale nilipoeleza kwamba huyu Hassana Mustafa idara za ujasusi duniani hawakujua kuwa yeye huyu ndiye Abu Omar ambaye wanamsaka. Tuko sawa sawa hapo?

Sitaki kutumia muda mwingi sana au kuandika paragraph nyingi sana kueleza kidokezo hiki… lakini naona ulazima wa kufafanua kidogo juu ya mnyumbuko wa taarifa na vipawa vya kuichambua.

Sasa baada ya kuhamia Italia akaendelea na shughuli zake za harakati za kiislamu na akawa imamu wa msikiti mkuu wa Milan. Sasa mwaka huo 2003 idara za ujasusi zinakapata taarifa kwamba kulikuwa na mpango wa kulipua ubalozi wa Marekani na shule ya msingi ambayo watoto wa wanadiplomasia wengi wa ulaya na Marekani walikuwa wanasoma hapo Milan. Na intelijensia hii ilitanabaisha kwamba mratibu wa shambulio hilo linalopangwa alikuwa ni Abu Omar na zaidi ya hapo intelijensia hiyo ilieleza kwamba Abu Omar pia alikuwa ndiye anaratibu mipango ya kusafirisha vijana kutoka kaskazini mwa Afrika kwenda Afghanistan kujiunga na al-qaida.
Lakini idara za intelijensia hawakuwa wanajua Abu Omar ni nani au anafananje.

Sasa,
Kuna kijana mmoja hivi anaitwa Federico Ilario mhitimu wa chuo kikuu cha Milan ambako alisoma masuala ya Diplomasia. Alikuwa ni kijana mdogo tu wa miaka ishirini na sita. Katika kipindi kile kwa karibia miaka miwili alikuwa anafanya utafiti kwa ajili ya kitabu ambacho alikuwa anakiandika kuhusu ugaidi na namna gani ambavyo kwa mtazamo wake alihisi mataifa ya magharibi yalikuwa na mbinu dhaifu katika ukusanyaji wa intelijensia dhidiya ugaidi.
Tufahamu kwamba huyu alikuwa ni raia wa kawaida, sio afisa usalama wala hakuwahi kuwa mwanajeshi na wala hakuwahi kuandika kitabu hapo kabla, kwa hiyo hakupata hata publisher wa kuchapa kitabu chake na hii ikampasa kufanye ile twaita ‘self-publishing’. Akagharamia kila kitu yeye mwenyewe kuchapa kitabu chake… akachapa kama nakala elfu kumi tu. Yes, nakala elfu kumi tu ambazo kwenye ulimwengu wa publishing ni kama punje ya mchanga kwenye pwani, ni chache mno.

Shughuli yake hii ya kitabu alikuwa anaifanya kienyeji sana kutokana na kukosa publisher, kwa hiyo, siku ambayo alitoka kuchukua mzigo wake wa vitabu kutoka mahala alikovichapa na kurejea navyo nyumbani kwake ili kesho yake aanze kuvisambaza kwa wenye maduka ya vitabu ambao watakubali kuviuza alipata ugeni adhimu kabisa kutoka kwa moja wa maafisa wa CIA aliyetoka stesheni ya CIA ya hapo Millan.

Afisa huyu wa CIA alikuwa na matakwa mawili kutoka kwa Ilario… moja alikuwa anataka kununua nakala zote elfu kumi alizozichapa. Hilo lilikuwa la kwanza. La pili aliomba kupewa ufafanuzi wa mojawapo ya sentensi ambayo iko kwenye kitabu… kitabu kile kilikuwa kimeandikwa kiitaliano na kwa tafsiri isiyo rasmi naweza kuitafasiri kwamba, Ilario aliandika kwamba “….hii ndio sababu ya Abu Omar kukimbia kambi zake huko kwao na kuichagua Milan kama kambi yake mpya…”
Idara za ujasusi na mahususi kabisa CIA walikuwa wanajua uwepo wa mtu anayeitwa Abu Omar lakini hawakuwa wanajua ni nani… lakini kijana huyu kupitia kitabu chake alikuwa ameandika kwamba kuna sababu fulani ambayo imemfanya Abu Omar kuhamishia makazi yake Milan. Kwanza amejuaje kuhusu uwepo wa mtu anayeitwa Abu omar? Hii ilikuwa ni taarifa classified mno…. Pili kijana huyu anapoandika kwamba Abu Omar amehamishia makazi Milan, ina maana kwamba yeye anamjua Abu Omar ni nani mpaka ajue kwamba sasa yupo Milan?


Nifupishe tu… suala lile ambalo kijana Ilario aliliandika kwenye kitabu chake, kwamba “….hii ndio sababu ya Abu Omar kukimbia kambi zake huko kwao na kuichagua Milan kama kambi yake mpya…” baada ya CIA kujadiliana naye kwa makini kijana yule aliwaeleza ni kwa namna gani katika tafiti zake za kuandika kitabu chake alikuja kung’amua juu ya uwepo wa mtu anayeitwa Abu Omar na baadae kuunganisha nukta kuwa Abu Omar ni Hassan Mustafa Nasr Osama ambaye ndiye imam wa msikiti mkuu wa Milan.

Siku ya tarehe 17 mwezi wa pili mwaka 2003, Imam Hassan Mustafa Osama Nasr alikuwa anatembea kwa mguu katika jiji la Milan mida ya mchana kweupe kama saa saba kasoro hivi. Alikuwa anaelekea msikitini kwa ajili ya swala ya dhuhr. Mita chache kabla ya kufika msikitini ilitokea gari ikiwa kwenye mwendo wa kasi mno… kwa kasi sana wakashuka watu wawili na kumsukumia iman Hassan Mustafa ndani ya gari na kuondoka naye. Kutoka hapo akasafirishwa mpaka kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ya Aviano Air Base. Kutoka hapo akasafirishwa mpaka Ujerumani kwenye kambi ya nyingine ya kijeshi ya Marekani ya Remstein Air Base. Na baada ya hapo akasafirishwa mpaka kwenye jela za siri za Marekani nchini Misri ambako kwa muda wa miaka minne Hassan Mustafa Osama Nasr (Abu Omar) alihojiwa kwa kuteswa huku ulimwengu mzima ukiwa haujui ni wapi alipo Imam wa msikiti mkuu wa Milan.

Kwa nini nimesimulia kisa hiki ili kujielezea nafsi yangu… nataka tuone kitu kimoja hapa… CIA ambayo ndio idara yenye rasilimali nyingi zaidi na weledi wa kutukuka wakisaidiwa na majasusi wa SISMI ya Italia kwa miaka kadhaa walikuwa wanajitahidi kumtambua Abu Omar ni nani bila mafanikio. Lakini kijana mmoja, Federico Ilario… kijana ambaye hajawahi hata kuchapa kitabu maishani mwake, kijana ambaye hajawahi kuwa hata mwanajeshi au kupitia mafunzo ya ujasusi, aliweza kuchimba taarifa, aliweza kuunganisha nukta, aliweza kuutafuna mfupa ambao CIA na SISMI uliwashinda licha ya weledi na rasilimali walizonazo.


Nimeanza na kidokezo hiki kwa makusudi kabisa kujibu hoja ya wale watakaosema… "kwa hiyo wewe Bold ndio wajiona wajua zaidi chanzo cha Corona kuliko taasisi za Dunia.."
Jibi ni hapana… sijui kuliko taasisi yeyote. Lakini makusihi, usidharau taarifa.. soma, take notes. Kuna jambo adhimu sana italipata kwenye andishi hili.

Karibuni.

COVID-19 & DEEP STATE: NINI MAANA YA UHANDISI JAMII UNAOTOKEA DUNIANI.!?


"Deception is a state of mind-and the mind of the state.."
James Angleton - CIA Chief of CI

Kama ni msomaji wangu wa muda mrefu basi hii si mara ya kwanza kuona nautumia msemo huu niliouweka hapo juu.. "Deception is a stste of mind-and the mind of the state".
Msemo huu kwa mara ya kwanza ulitamkwa na nguli anayeitwa James Jesus Angleton. Angleton ni aina ya watu ambao wanazaliwa mara moja tu kwenye kizazi.

Sidhani kama dunia imewahi kushuhudia nguli wa Counterintelligence kumzidi James Angleton. Mbinu na stadi nyingi za Counterintelligence tuzitumiazo sasa duniani kote kwenye idara mbali mbali za intelijensia zimeasisiwa na huyu mtabe.
Nguli huyu hakuwahi kushika wadhifa wa Ukurugenzi wa CIA lakini ana mchango mkubwa wa kuifinyanga CIA kuwa namna ilivyo leo hii. Ukiniuliza watu watatu ambao wana mchango mkubwa zaidi wa kuifanya CIA kuwa idara adhimu zaidi ya intelijensia duniani basi nitakwambia mmoja wa watu hao watatu ni huyu James Angleton.
Mtabe huyu namuweka daraja moja na mtu kama akina Allen Dulles na DCI Horbes.

Kama umewahi kusikia kuhusu Operation CHAOS ambayo twaiweka kama moja ya Oparesheni muhimu zaidi ya kiintelijesia kwenye historia ya Marekani, sasa huyu James Angleton ndiye alikuwa kichwa kilichokuwa nyima ya pazia ya Oparesheni hiyo.

Nimeanza makala hii mpya na nukuu ya shushushu huyu jasusi sababu pia ni mtu adhimu sana kwenye uasisi wa masuala ya "uhandisi jamii" (social engeneering).
Ni James Angleton ambaye alisimamia oparesheni hii ambayo ilikuwa na lengo la ku-manipulate fikra, mitazamo na maoni ya jamii kuhusi masuala yao ya nchi kwa CIA kutumia mbinu za kishushushu kuhakikisha ni habari wazitakazo tu zinatokea kwenye vyombo vya habari. Hii ilikuwa moja ya oparesheni adhimu zaidi ya CIA ambayo ilidumu kwa zaidi ya miaka ishirini na ikileta matunda makubwa.

Hivyo kama kuna mtu anafahamu kuhusu namna akili za wananchi wa kawaida zinachezewa na kuwa 'manipulated' pasipo kujua, basi ni huyu nguli James Jesus Angleton.

Kwenye siku zake za mwisho za utumishi na baada ya kustaafu, nguli huyu hakuwahi kuandika kitabu kama wenzake wengine wala kufanya mahojiano na ya televisheni au kutoa midahalo. Moja ya namna pekee aliyotaka kutuacha nayo ili tufahamu walau kiduchu ulimwengu alioishi tangu akiwa kijana, ulimwengu wa ujasusi.. akatuachia kauli hii kwamba ulimwengu wetu huu umejaa hadaa na hata serikali zetu kote duniani zinatumia hadaa hizi kuendelea kutawala.

Mimi binafsi yangu ni mtu mgumu mno kuamini jambo lolote hata liwe dogo kiasi gani, labda pengine ni asili ya kabila letu ubishi… lakini kwa asili huwa mgumu sana kuamini jambo kwa urahisi. Na ni sababu hii pengine huwa inanifanya siamini 'conspiracy theories' nyingi au sizipi daraja la uhalali wa moja kwa moja zaidi ya kuzifanya kama mstari wa kuchochea mjadala mpya juu ya jambo husika.

Kwa mfano, kwenye makala ya "Behind The Curtain" ilikuwa makala ndefu mno lakini mwishoni nilikataa kutoa 'conclusion' ya kwamba ni nani alihusika hasa na tukio lile la 9/11. Ukisoma maoni ya watu mwishoni mwa ule uzi utaona watu wengi walipenda na kuhoji kwa nini nimekataa kueleza kwamba Israel ilihusika… wengine wakalaumu kwa nini sikubainisha kwamba CIA walihusika.

Sikutaka kufanya hivyo sababu ni ngumu kwetu kunyoosha kidole na kuwa na hakika asilimia mia moja kwamba nani amehusika. Kitu pekee tunachoweza kufanya ni kuchambua dalili za kuonyesha nani alihusika na ndicho ambacho nilikifanya na mwishoni mwa makala ile nilimaliza kwa kutoa hitimisho la falsafa mbili ya uhusika…nilihitimisha kwa kuchambua falsafa ya LIHOP (Let it Happen On Purpose) na MIHOP (Make It Happen On Purpose).


Lakini…

Licha ya kutokuwa mwepesi kuamini vitu vingi lakini kipo kitu ambacho nakiamini kwa hakika kabisa.. kwamba dunia yetu hii na namna ambavyo inaendeshwa imejawa na hadaa nyingi sana.
Mambo mengi hayako vile namna ambavyo tunayaona. Kama miaka mitano hivi iliyopita nilipata bahati ya kusoma kitabu cha Andy Grove aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Intel. Moja ya vitu ambavyo nilivipenda sana kwenye kitabu chake ni hitimisho lake la kimtazamo anaposema "..only the paranoid survive.!"


Huu ulimwengu wetu namna ulivyo kwa sasa, ni hatari mno kuamini moja kwa moja kila kinachoshadadiwa na vyombo vya habari.
Nyakati hizi ni zile za kuishi kwa moto ya "believe nothing, question everything.!"

Kuna mambo mengi sana ambayo yanatokea yakionekana kama ya bahati mbaya lakini uhalisia wake ni masuala ambayo yamepangwa kwa ustadi mkubwa na kwa malengo mahususi kabisa.

Katika kipindi kifupi kilichopita dunia imepita kwenye mtikisiko mkubwa sana.
Mwishoni mwa mwaka jana kuliibuka tishio la mlipuko wa vita kuu ya tatu ya dunia. Na baada ya mwaka kugeuka, mwaka huu mpya tumeanza na moja ya balaa kubwa zaidi kuwahi kuikumba dunia kwenye historia ya karibuni.. mlipuko wa maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Kwa mara ya kwanza kabisa baada ya karne kadhaa kupita tunashuhudia nchi zikifunga mipaka yake. Kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya karne moja kupita tunaona Marekani kuna kila dalili ya Rais wao kutangaza utekelezwaji wa Martial Law. Mwaka 2017 kwenye simulizi yangu ya "The Other Half" (fiction story) niliandika kuhusu Rais wa Marekani kutangaza Martial Law kutokana na kuibuka kwa balaa la miji kukumbwa na hali ya ajabu ya watu kupotea na kubadilika hali yao ya ubinadamu baada ya kudhuliwa na watu waliopata "maambukizi" yatokanayo na "kirusi" kilichookotwa bahati mbaya kwenye chupa baharini uko nchini Maldives.

Riwaya ile niliyoandika ni kama inaelekea kutokea kwa uhalisia endapo kama Rais Trump atatangaza Martial Law kutokana na mlipuko wa virusi vya COVID-19.
Na mpaka muda huu ninapoongea tayari Magavana kwenye majimbo Kumi na tano ya Marekani wametangaza amri ya "Stay at Home" na kuamuru biashara zote zifungwe.

Tumebakisha hatua moja tu kwenda kwenye Martial Law.. National Guard wamwagwe mtaani, na Martial Law ianze kutekelezwa.

Nchi kama Italy wao ni kama tayari wameshaingia kwenye Martial Law japo serikali haijatangaza rasmi.

Kwenye historia ya karibuni, hatujawahi kuona dunia ikipitia kipindi kama hiki.

Papa Francis ametoa wito kwa madhehebu yote duniani kufanya maombi maalumu siku ya leo March 25 ili "muujiza" utokee tuepukwe na baa kubwa linalokuja sababu ya COVID-19.
Juzi Imam aliyekuwa anasalisha pale Mecca amelia kilio baada ya kuona Kaaba ikiwa tupu bila waumini kitu ambacho hakijawahi kutokea kabla.
Msikiti wa Mtume Muhammad (S.A.W) Al Masjid an Nabawi juzi umefungwa kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya karne 14 kuepuka waumini kusambaza maambukizi ya Corona.

Ni nini kinatokea Duniani? Na hatma yake ni nini hasa.!?

Kumekuwa na maneno mengi yakisemwa kuhusu kinachoendelea. Maafisa waandamizi wa serikali ya Uchina na kiongozi Mkuu wa Iran wakiwashutumu Marekani kwamba wamekitengeneza kirusi hicho kama silaha, huku Wamarekani wakiwalaumu Wachina kwa Uzembe wa kudhibiti kirusi hicho.
Huku watu adhimu kama Mhandishi, Mbunifu wa teknolojia na Mfanyabiashara mshuhuri Elon Musk akionyesha wasiwasi wake dhahiri kwamba nyuma ya pazia kuna "sinema" tunachezeshwa juu ya baa hili la COVID-19.

Wako pia watu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Ungereza, Mbunge Tobias Elliwood akishutumu kwamba jeshi la Uchina lichunguzwe ili kung'amua asili ya kirusi hicho.

Papo hapo shirika la afya duniani WHO wakijikanyaga kila uchwao juu ya kauli zao.. juzi tu january 14 walitoa waraka kwa vyombo vya habari wakisema kwamba wataalamu wao wamekichunguza kirusi hiki kipya na kubaini kuwa hakina uwezo wa kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.. lakini leo hii dunia nzima inahaha na hao hao WHO wameramba matapishi yao wakituasa kujikinga dhidi ya virusi hivyo.

Ni nini kinaendelea Duniani?


Kwa namna yeyote hakuna ambaye anaweza kuandika andiko na kututaulia vitendawili vyote kuhusu suala hili… tunachoweza kufanya ni kukusanya ushahidi na kuunganisha nukta ili hatimaye tuweze kujenga hoja.
Hivyo makala hii naiandika kwa dhumuni kuu la kuchochea mjadala ili hatimaye tusugue mbongo na kupata majawabu ya mafumbo tunayofumbwa.

Dunia yetu hii imejaa hadaa sana… dunia hii kuna watu wameiweka mkononi wakituchezesha sinema namna watakavyo.

Baada ya tafakari, kufuatilia, kukusanya 'nukta' na ushahidi.. basi nami nikawiwa nitie wino kalamu niyaandike haya kuhusu Deep State na 'Coronavirus'.


OCTOBER, MWAKA 2017 - MAREKANI

Pale Marekani yuko bwana mmoja anaitwa Richard H. Ebright. Bw. Ebright ni mbobezi wa masuala ya Molecular Biology.
Ebright amehitumu shahada ya kwanza ya biolojia kutoka chuo kikuu cha Havard akipata daraja la juu kabisa kwa _summa cum laude_ (highest distinction).

Pia Ebright amehitimu shahada ya Uzamivu kwenye Microbiology na Molecular Genetics toka chuo hicho hicho cha Havard. Sasa hivi Ebright ni profesa katika chuo kikuu cha Rutgers University akifundusha Chemical Biology na pia ni Mkurugenzi Mkuu katika Maabara za Utafiti za Waksman Institute of Microbiology.

Mwaka 2017 Ebright alitoa moja ya rai muhimu zaidi ambayo kwa muda ule kwa kuwa hakuna ambaye alijua nini kitakuja kutokea tulipuuza.
Ebright aliandika chapisho la kisayansi akionya juu ya mwenendo wa maabara ya WIV (Wuhan Institute of Virology).
Maabara hii iko kwenye jimbo la Wuhan, wilaya ya Jiangxia eneo la Hubei. Kituo hiki kinaongozwa na Mkurugenzi Mkuu mwanamama msomi na mwanasiasa Dr. Wang Yanyi ambaye ni mbobezi wa masuala ya Cell Biology.
Mwanamama huyu amesomea shahada yake ya kwanza Peking University huku shahada ya Uzamili na Uzamivu akizipatia nchini Marekani chuo Kikuu cha Colorado.

Licha ya kuwa mtafiti wa sayansi, mwanamama huyu pia ni mwanasiasa akiwa ndiye Mkurugenzi Msaidizi wa Chama cha China Zhi Gong Party.

Sasa, kituo hiki cha Wuhan Institute of Virology awali kilikuwa kundi la BSL-2 lakini mwaka huo ikapanuliwa na kupandishwa hadhi kuwa maabara ya kwanza nchini Uchina kuwa na hadhi ya Biosafety Level 4 (BSL-4).
Chapisho lake hilo la kutoa tahadhari hakugusia hasa nini kilikuwa kinafanyika ndani ya kituo cha Wuhan Institute of Virology, bali alikuwa anatoa tahadhari juu ya upanuzi na upandishaji hadhi huu unaweza kuwa kiashiria ya jambo la hatari linaloweza kuwa linaendelea ndani yake.

Labda tuelewe kwa ufasaha maana ya hadhi hii ya BSL-4 na kwa nini Dr. Ebright alipata wasiwasi baada ya kuona kituo hiki kimepandishwa hadhi hii na kisha kutoa tahadhari ambayo hakuna aliyeitilia maanani kipindi hicho.

Ziko maabara za kibaolojia ambazo zenyewe wanajihusisha na kurutubisha, kutafiti na kuunda 'biological agents'.
Biological agents ni aina za bacteria, virusi, protozoa, parasite, au fungus ambao wanaweza kuundwa kwa dhumuni la kuwa silaha ya kibaolojia. Pia ziko aina ya pathogens, toxins na biotoxins ambazo pia zinatumika kama biological agents.


Sasa kwenye maabara hizi ambazo zinahusika na kurutubisha, kutafiti na kuundaji hizi 'biological agents' kuna tahadhari ambazo zimewekwa kimataifa zinazopaswa kufuatwa. Tahadhali hizi za kibaolojia kwa umombo twaita 'Biocontainment Precautions' ambazo zapaswa kufuatwa katika uhifadhi wa hizo biological agents ndani ya maabara.
Hivyo maabara hizi zenye kujihusisha na uundaji na matumizi wa biological agents zinawekwa kwenye makundi kutokana na aina ya hizo 'precautions' wanazopaswa kufuata kulingana na biological agents wanazounda. Makundi haya ndio hayo yaitwa Biosafety Levels, na level hizo ziko nne.

Maabara ambazo ziko kwenye level ya kwanza (BSL-1) maana yake ni kwamba maabara hiyo inaunda/wanatumia biological agents ambazo haziwezi kuleta madhara kwenye mwili wa binadamu mwenye afya au madhara yake ni madogo mno yenye uwezo wa kudhibitika.

Maabara ambazo wako level ya pili yaani BSL-2 hii ni sawa kwa kila kitu na BSL-1 isipokuwa kunakuwa na pathogenic agents mahususi ambayo maabara hiyo wanahusika nayo, na pia 'access' ya maabara inakuwa 'limited' kwa wataalamu wachache ambao wanahusika na kinachoendelea humo.

Maabara ambazo ziko kwenye BSL-3 zenyewe zinahusika kuunda na utumiaji wa biological agents ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu na mara nyingi kusababisha kifo.

Level ya juu kabisa ni BSL-4 ambazo zenyewe hizi ni maabara zenye kuhifadhi, kuunda au kutumia biological agents ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa binadamu na kifo na pia madhara hayo (au ugonjwa) ni mpya na hivyo hayana chanjo au matibabu hivyo hayawezi kudhibitika.
Kwa lugha nyingine, maabara zilizo kundi la BSL-4 wanatafiti na kuunda biological agents mpya (bacteri, virusi vipya) vinavyoweza kutumika kama silaha lakini kutokana na upya wake bacteria au virusi hivyo havina chanjo au tiba na huwezi kudhibiti.


Sasa hiki kituo cha Wuhan Institute of Virology (WIV)awali ilikuwa iko kwenye BSL-2 lakini mwaka huo 2017 ilipanuliwa na kupandishwa hadhi kuwa BSL-4.

Kwa hiyo, Dr. Ebright aliandika chapisho kutahadhalisha jamii ya wanasayansi kuhoji na kuwabana Uchina waeleze ni nini hasa kinafanyika hapo WIV.
Ifahamike kwamba china wana haki ya kuwa na vituo vya namna hii, lakini zimewahi kutokea 'incidents' kadhaa miaka iliyopita za pathogenic agents kuvuja toka kwenye maabara zao na kuingia kwenye jamii na wasiwasi wa Dr. Ebright ukawa hapo.

Niwarejeshe tena nyuma zaidi.


LAHORE, PAKISTAN - MWAKA 2011

Hii ilikuwa ni mwezi January tarehe 28 mwaka 2011ambapo Polisi wa kituo kikuu cha eneo la Mozang Chungi jimboni Lahore siku hiyo walikuwa katika siku yao ya pili wakifanya mahojiano na mtuhumiwa ambaye mpaka muda huo hawakuwa wanajua hata kama jina lake lilikuwa ni halisi. Kwenye chumba kingine walikuwa wamewekwa mashahidi karibia watano wakieleza kile walichokiona siku moja iliyopita.
Maelezo ambayo mashahidi hawa walikuwa wanayatoa yalikuwa yanarandana lakini yakipingana na maelezo ambayo mshitakiwa alikuwa anayatoa.

Mashahidi walikuwa wanaeleza kwamba kwenye eneo la makutano ya barabara ya Qurtaba ambako kuna mataa ya kuongoza magari walimshuhudia mshukiwa huyo akitoa bastola na kuwapiga risasi watu wawili ambao walikuwa kwenye pikipiki pembeni ya gari. Baada ya kuwapiga risasi alitoka nje ya gari na kuwapiga picha watu hao ambao walikuwa chini tayari wamepoteza maisha na kisha akarejea kwenye gari yake na kuondoka.

Lakini mshitakiwa mwenyewe alikuwa anadai kwamba alitoka nyumbani kwake na kupita kwenye ATM kutoa fedha. Akiwa anaondoka, alipofika makutano ya barabara ya Qurtaba walitokea watu wawili kwenye pikipiki ambao mmoja akatoa bastola wakataka kumpora. Kwenye kujitetea, naye akatoa bastola na kufanikiwa kuwatandika risasi wote wawili.

Suala hili lilikuwa limeanza kuleta mtafaruku wa kidiplomasia sababu mshukiwa huyo alikuwa ni raia wa Marekani huku watu hao wawili waliouwawa walikuwa ni Wapakistani.

Maelezo yake haya yalikuwa na mantiki lakini yalikuwa na mashaka makubwa.
Mashaka hayo yalitokana masuala matatu makubwa.
Mosi; mtu huyo alikutwa na bastola ambayo ilikuwa haijasajiliwa.
Pili; mtu huyu kitambulisho chache kilikuwa kinaonyesha kwamba jina lake alikuwa anaitwa Raymond Allen akiwa ni mwajiriwa wa kampuni inayoitwa Hyperion Protective Consultants. Lakini walipofuatilia anuani ya Kampuni hiyo ambayo ilikuwa inaonyesha ipo Orlando, Marekani walipewa taarifa na ubalozi wao wa kule Marekani kwamba jengo hilo liko tupu na hiyo kampuni haipo

Jambo la tatu ambalo liliwashitua zaidi ilikuwa ni simu yake. Ndani ya simu yake walikuta picha za maeneo ambayo hayaruhusiwa raia kufika wala kupiga picha.. kulikuwa na maeneo kadhaa lakini mojawapo ya maeneo hayo ambayo yaliwashitua zaidi ilikuwa ni "installation" za kijeshi zilizoko mpakani na India.

Sasa,jambo ambalo mara ya kwanza siku ile Polisi wa Kituo kikuu cha Mozang Chungi hawakuking'amua ni kwamba kampuni ile ya Hyperion Protective Consultants ambayo ilikuwa imeandikwa kwenye kitambulishi cha Raymond Allen ilikuwa ni kampuni hewa (shell) inayomilikiwa na Kampuni mama ya Blackwater Worldwide. Hawa Blackwater Worldwide ni moja ya 'contractors'wakuu wa CIA…


Nawakaribisha twende sambasamba na makala hii mpya..


Kesho mchana nitaweka sehemu ya Pili.


Habibu B. Ang "The Bold" - 0718 096 811
To Infinity and Beyond



SEHEMU YA PILI POST # 66

Mkuu hizi nondo weka kwenye maandishi. Hutalala njaa mjini, hata kama sio leo. Ipo siku zitakuwa lulu kwenye ulimwengu wetu huu ambao mambo hayaishi kubadilika.
 
Mkuu Habibu hongera sana kwa kazi nzuri, nikuombe tu pamoja na kuwa unachelewa sana muendelezo wake sio mbaya labda kwa sababu ya maandalizi na muda wa kuandika.
Sambamba na hilo nina ombi moja tu kwako ya kua hii tafadhari ifikike mwisho na kama unahisi hutaifikisha mwisho kama zile zingine mfano The Other Half, Vipepeo weusi n k basi sema mapema kwamba na hii itakua kama zile zingine.
NAWASILISHA.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom