Daktari wa China amsaidia mwanafunzi wa Zanzibar, kupona na kurejea shuleni

Daktari wa China amsaidia mwanafunzi wa Zanzibar, kupona na kurejea shuleni

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
4865b8efb8b942308cd4508b15c60d05.png


Ashfaina Omari Ali, mwenye umri wa miaka tisa na nusu, aliingia katika Shule ya Msingi Sebleni kwenye kisiwa cha Unguja, Zanzibar, akiwa anajiamini upya.

Kwa Ashfaina, kurejea shuleni ilikuwa zaidi ya kuanza kwa siku nyingine ya masomo. Ilikuwa ishara kwamba maisha yalikuwa yakirejea katika hali ya kawaida baada ya ugonjwa mbaya wa sikio kutishia afya yake na kuvuruga masomo yake.

Baba yake, Omari Ali Omari, fundi ujenzi anayeishi Sebleni, aliiambia Xinhua kuwa awali aliogopa kwamba binti yake asingeweza tena kufurahia maisha ya kawaida ya watoto wa umri wake. Sasa, hofu ya Omari imekwisha kabisa.

Kupona kwa Ashfaina kulitokana na upasuaji tata uliofanywa katika Hospitali ya Mkoa ya Lumumba, Zanzibar, na timu ya madaktari kutoka China ikiongozwa na Li Li, daktari kutoka timu ya 35 ya madaktari wa China waliopo Zanzibar.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka tisa alikuwa akisumbuliwa na kifafa na homa za mara kwa mara kwa siku kadhaa. Mwanzoni alipata matibabu ya kawaida ya kupunguza uvimbe katika kituo cha afya cha eneo analoishi, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Alipohamishiwa Hospitali ya Lumumba, Li na timu yake walimpiga xray na kugundua tatizo la uvimbe wa sikio la kati hali mbaya inayohusisha ukuaji usio wa kawaida wa ngozi ya ndani ya sikio la kati.

"Ugonjwa huo ulikuwa umesababisha uharibifu mkubwa; mchanganyiko wa matatizo ya ndani na nje ya fuvu la kichwa ulifanya hali hiyo kuwa hatari zaidi," Li alieleza.

Ashfaina aliendelea kusumbuliwa na homa kali. Kama hali hiyo ingeachwa bila kudhibitiwa, ingeweza kuhatarisha maisha yake. Baada ya maandalizi mfululizo ya kabla ya upasuaji na majadiliano ya kina na familia ya Ashfaina, timu hiyo ilitathmini kwa makini hatari zilizopo na kuandaa mpango maalum wa matibabu kabla ya kuendelea na upasuaji. Upasuaji ulifanikiwa. Ashfaina alipona kabisa na hatimaye kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Upasuaji huo ulichukua saa nne. Uliondoa vyanzo vya maambukizi na hatimaye kupunguza hatari ya ugonjwa huo kusambaa hadi kwenye fuvu la kichwa na mfumo wa damu.

Hata hivyo, kwa baba yake, kipimo muhimu zaidi cha mafanikio hakikupatikana katika ripoti ya matibabu au chumba cha upasuaji. Kilikuwa ni kumuona binti yake akijiandaa kwenda shule tena baada ya kupumzika nyumbani kwa muda mrefu.

Safari ya mtoto aliyekuwa akiugua sana na kukabiliwa na hali iliyotishia maisha yake, hadi kuwa mwanafunzi anayeingia darasani kwa kujiamini, inaonesha matokeo chanya ya huduma maalum za matibabu kwa maisha ya watu.

Kwa mujibu wa timu ya madaktari wa China, kufanikiwa kutibu tatizo la kiafya la Ashfaina kuliziba pengo la eneo hilo katika nyanja ya utambuzi na matibabu ya magonjwa tata na makali ya masikio.

Hata hivyo, jukumu la timu hiyo linavuka mipaka ya kuwatibu wagonjwa binafsi pekee; ugonjwa wa Ashfaina pia ulikuwa fursa muhimu ya kujifunza kwa wataalamu wa afya wa Zanzibar.

Bao Zengtao, kiongozi wa timu ya 35 ya madaktari wa China visiwani Zanzibar, alisema kuwa tangu walipowasili, timu hiyo imesisitiza uhaulishaji wa maarifa matibabu, ujuzi, na teknolojia kwa wahudumu wazawa wa afya ili kuimarisha uwezo wa muda mrefu wa sekta ya afya Zanzibar.

Kwa familia kama ile ya Ashfaina, ushirikiano wa namna hii hupimwa zaidi kupitia matukio yanayogusa hisia za ndani kabisa: mtoto kupona ugonjwa mbaya na mzazi kurejeshewa matumaini.

"Sijui niwashukuru vipi madaktari wa China," alisema Omari. "Wamemrudishia binti yangu uhai."
 
Back
Top Bottom