Part two of the story:
Mume kama ana uhusiano wa kimapenzi na msichana wa kazi, ikitokea mke amesafiri ni nafasi kubwa sana kwao kujiachia.
Ni katika kipindi hicho, hausigeli ataweza kuingizwa hadi chumbani na kulala. Tena wengine hujiachia vibaya, kwani hata akiamka asubuhi anaweza kuacha khanga yake ikiwa imeandikwa; Paka Akitoka Panya Hutawala.
Sasa mke utaijuaje tabia hii? Ni rahisi sana, ukiwa safarini utashangaa ukimpigia simu mumeo saa kumi na mbili jioni na kumuuliza aliko atakujibu nyumbani wakati kawaida yake hurudi saa nne mpaka tano usiku.
Asubuhi, kama kawaida yake kwenda kazini ni saa moja utashangaa kumsikia mpaka saa mbili kasoro hajaondoka na sababu anazokupa hazina maana.
Wakati mwingine pia, ukimpigia simu usiku atachelewa kupokea au akipokea maongezi yake yanaashiria kutaka mmalize haraka. Ni kwa sababu yupo na msichana wa kazi pembeni.
Mapenzi ya aina hii yakifikia hapa, mke ndani ya nyumba anakuwa anaishi katika hatari kubwa ya talaka au ugomvi wa mara kwa mara. Na kama msichana huyo wa kazi amejaaliwa uzuri, hakika ndoa hupinduka na yeye kuchukua nafasi.
Wapo wanawake kibao mitaani ambao ndoa zao zilipinduliwa na wasichana wa kazi. Hufika mahali akitaka kwenda kuwaona watoto anakuwa mwizi, anafikia nyumba ya jirani na kuwaita.
Nakupa mfano mmoja; huu ulitokea wilayani Korogwe, Tanga. Dada mmoja (jina ninalo) aliolewa na kubahatika kuzaa watoto wawili wa kiume.
Lakini alichokosea ndani ya nyumba yake, alimwachia msichana wa kazi kuendesha kila kitu. Mume akirudi anakumbana na huduma kutoka kwa dada, asubuhi akitaka kwenda kazini anakumbana na huduma za hausigeli, mwishowe wakajenga uhusiano wa kimapenzi.
Imekwenda, mke hajui, ikafika mahali mume akamrudisha mke kwao kwa kisa kidogo tu, alimjibu jeuri. Akiwa nyumbani kwao, mke akapata habari kwamba, mumewe amefunga ndoa na msichana wa kazi tena akiwa mjamzito.
Ikawa mke huyo akienda kuwaona watoto wake anakaribishwa na msichana wake wa kazi, anamuandalia chumba cha kulala ambacho awali alikuwa akilala yeye. Mama akawa hana chake.
Haya yote ni madhara ya kuwaachia wasichana wa kazi wafanye kila kitu kwa waume ndani ya nyumba. Ni hatari kuliko inavyofikiriwa.