Damu ya Elvino na mauaji ya huko Msumbiji

SteveMollel

JF-Expert Member
Joined
Jul 12, 2015
Posts
8,797
Reaction score
25,177
Huu haukuwa usiku wa kawaida.



Katikati ya jiji la Maputo, siku ya Ijumaa ya Oktoba 18 , majira ya usiku unaokaribiana kuwa Jumamosi, kulikuwa na kikao kisichokuwa rasmi katika baa moja jijini humo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na watu wanne ila watu watatu ndo' walikuwa wanafahamika;

Mmoja ni wakili msomi, Elvino Dias, wa pili ni msemaji wa chama cha upinzani, Paulo Guambe, na watatu ni mwanamke mmoja aitwaye Adacia.



Mtu wa nne katika kikao hiki, alikuwa hafahamiki.

Hakuwa anajulikana na yoyote yule na wala hakualikwa kabisa katika eneo hili.

Mtu huyu hakuchagamana na wenzake kwenye meza moja. Alijitenga. Alikaa mbali, gizani, akishiriki kikao hichi kwa macho tu.

Kwani kilichomleta hapa haikuwa maongezi bali misheni maalum.

Misheni ya mauaji.

Ikumbukwe kabla ya kikao hiki, tayari kulishatokea matukio mawili makubwa.

Tukio la kwanza, uchaguzi wa serikali za mtaa. Hili lilishamaliza mwaka mzima tangu lilipotokea huko Oktoba 2023.

Kwenye tukio hio, wakili Elvino Dias aliishitaki Tume ya uchaguzi kwa udanganyifu mkubwa uliofanyika kwenye uchaguzi huo.



Alisema kulikuwepo wa masanduku yaliyojazwa kura nyingi feki.

Kura za chama tawala.

Aliambatanisha makaratasi yenye matokeo ya kupangwa, yakiwa na idadi tofauti kabisa na kura halisi zilizopigwa na wananchi vituoni.

Matokeo yake kesi nyingi ziliishia na ushindi upande wake.

Wapinzani wakashika madaraka.

Akaitwa shujaa wa haki.

Tukio la Pili lilikuwa ni la uchaguzi mkuu.

Hili ndo' kwanza lilikuwa linamaliza siku ya kumi tangu lilipojiri Oktoba 9 mwaka huu.

Kwenye tukio hili, kama lile la kwanza, wakili Elvino alionyesha tena nia yake ya kukabiliana na tume ya uchaguzi.

Aliandaa shauri la kupinga matokeo ya awali yaliyowasilishwa na tume hiyo kwenye gazeti la serikali yakimtangaza Daniel Chapo, mgombea wa FRELIMO, kama mshindi kwa zaidi ya kura 70% huku mpinzani, Venancio Mondlane, akiambulia 20% pekee.

Alidhamiria kuanza mchakato huo wiki ijayo, wiki inayoanzia Jumatatu, akiwa tayari ana ushahidi wa kutosha mkononi.

Namna tume hiyo inavyoshirikiana na chama tawala kuwaibia wapinzani, haswa mgombea binafsi aliyekuwa anaungwa mkono na chama cha upinzani cha PODEMUS, bwana Venancio Mondlane.

Matukio haya mawili ndo' yalimfanya mgeni huyu wa siri kufika eneo hili kwa kazi yake maalum.

Kilichomleta hapa ni mithili ya kile alichotoka kukifanya siku mbili nyuma, tarehe 17 ya Oktoba.

Siku hiyo aliyekuwa katika mahesabu yake alikuwa kijana barobaro aitwaye Rachide ambaye ni mnazi mkubwa wa kiongozi wa upinzani nchini.



Alimteka kijana huyo mchana kweupe, akatoroka naye akitumia gari aina ya Toyota Runx.

Alikompeleka, haijulikani mpaka hivi sasa.

Leo hii mahesabu yake yapo kwa wakili Elvino.

Lengo la hapa ni moja, bwana huyo asifike wiki aliyoadhimia kwenda mahakamani.

Na mkakati wa hapa ni mkubwa, tofauti na ule mkakati wa awali.

Yalipofika majira ya saa saba usiku, wakili Elvino pamoja na wenzake wawili waliona sasa inatosha. Muda umeshaenda.

Walitoka baa wakaingia kwenye gari la wakili, BMW SUV rangi ya grey.

Elvino alikalia kwenye usukani, Paulo alikaa pembeni yake huku Adacia akiketi viti vya nyuma peke yake, wakashika barabara ya Joacqim Chassano tayari kusaka maskani zao wakajipumzishe.

Muda si mrefu, gari mbili aina ya Mazda-bt, ziliwasha engine nazo zikaingia katika barabara hiyohiyo.



Ulekeo wake ulikuwa mmoja.

Kufuata lile gari la wakili.

Gari hizo zilitembea wa kasi sana. Ndani ya muda mfupi, waliifikia gari ya wakili, gari moja likapita kwa mbele na nyingine likabaki kwa nyuma.

Gari ya wakili ikawa katikati.

Kufumba na kufumbua gari hizo zilisimama ghafla.

Wanaume wawili waliobebelea bunduki, mmoja akitokea gari la mbele na mwingine gari la nyuma, walirukia chini na kuanza kushusha mvua ya risasi kwenye gari la wakili.

Walishusha vyuma bila ya huruma.

Wakili Elvino akafia papo hapo.

Kazi alopewa yule mgeni ikawa imekamilika kwa asilimia zote.



Wauaji walirudi kwenye magari yao wakatimka kwa kasi kubwa!

Mwendo wa ngiri.

Zoezi lote hili halikudumu hata kwa dakika tano. Ilikuwa ni kama filamu ya maharamia ama zile za mapigano tunazotazama kwenye sinema.

Watu walioshuhudia, walitoa taarifa polisi, ndani ya muda mfupi, polisi wakaitikia wito kufika eneo la tukio.

Walipofika waliwazuia mashuhuda wote kuchukua video na picha yoyote ile.

Na wale ambao tayari washarekodi, baadhi yao walipokonywa simu wakiamrishwa wafute kila kitu.

Gari la wagonjwa liliwasili wakati huo hali ya Paulo na Adacia ikiwa mbaya sana, haswa Paulo ambaye alikuwa anahema kwa mbali mno.



Walipakiwa kwenye gari upesi lakini wakashindwa kuwahi hospitali sababu ya njia kuzuiwa na gari ya polisi.

Hatimaye Paulo naye akafia eneo hilo.



Ni Adacia peke yake ndiye alibahatika kufika hospitali akiwa na pumzi yake.

Ndani ya muda mfupi, gari la wakili liliondolewa barabarani, yani laiti kusingekuwa na madoa ya damu na mabaki machache ya vioo vilivyovunjika, mtu asingelidhania kulitokea kitu eneo hilo.




Palipokucha, habari zilimfikia kila mtu katika jiji la Maputo.

Haikuwa siri.

Haya yalikuwa ni mauaji ya kisiasa (political assassination) na kila mtu aliamini hivyo isipokuwa jeshi la polisi pekee.

Wao walikuwa na maelezo tofauti kabisa.

Afisa Leonel Muchida, msemaji wa jeshi la polisi jijini Maputo, alijitokeza na kutoa neno akisema mauaji ya Elvino sababu yake ni wivu wa mapenzi.



Alisema Elvino na Paulo walienda bar na huko wakagombana na wanaume wenzao sababu ya mwanamke.

Mwanamke mwenyewe ndo' yule Adacia.

Wanaume hao ndo' wakawafuatilia kwa nyuma na kwenda kuwapiga risasi huko mbele kisha kutoweka.

Haikujulikana uchunguzi huu wa jeshi la polisi ulifanyika muda gani na ulitumia ushahidi upi.

Lakini kilichokuja kujulikana hapo mbeleni ni shida ambayo pengine polisi hawakuipigia mahesabu.

Baada ya vifo hivyo, mkakati wa wapinzani kupambana na serikali na tume yake ya uchaguzi ulichukua sura mpya.

Hapo mwanzo, baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi kutoka, bwana Venancio Mondlane akiungwa mkono na wakili Elvino Dias, walihamasisha wananchi kuyakataa matokeo hayo kwa kutumia 'Paralysis Approach'.

Hamna watu kwenda makazini. Hamna kufungua maduka. Hamna kushiriki kwenye shughuli zozote za kiuchumi mpaka pale sauti ya umma itakapoheshimiwa.

Lakini baada ya vifo hivi, wapinzani waliamua kufuata mkakati mpya.

Hamna tena kukaa ndani. Fungua mlango uende nje kupaza sauti.

Sema FRELIMO inatosha. Hatutaki tena.

Mkakati huo ulianza kwa amani na ulianza maramoja.



Ni baada ya siku moja tu tangu mauaji yalipotokea, yaani Jumatatu ya tarehe 21 Oktoba, bwana Venancio aliongoza maandamano ya kwanza ya kitaifa.

Makutano yao yalikuwa palepale walipouawa wakina Elvino.

Wakati maandamano hayo yanaendelea, Venancio alifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari, ikiwemo vile vya kimataifa.



Lakini akiwa anazungumza, polisi walifyatua bomu la machozi katikati ya Venancio na waandishi habari.

Bomu lilifuka moshi wake unaowasha mithili ya pilipili kichaa, kila mtu akakimbia kujinusuru.

Na huo ndo' ukawa mwisho wa maandamano.

Lakini pia mwisho wa bwana Venancio kuonekana tena hadharani.

Tangu siku hiyo, hamna aliyekuwa anajua bwana huyo anaishi wapi ndani ya nchi ya Msumbiji.

Siku tatu mbele, tarehe 24 ya Oktoba, matokeo rasmi ya uchaguzi yalitolewa, na kama ilivyotarajiwa, FRELIMO walishinda kwa kishindo.

Sio tu kwenye urais, hadi huko kwenye ubunge. Walifanikiwa kunyakua viti 190 kati ya viti 250.

Matokeo haya yalizidi kutia chumvi kwenye kidonda kibichi.

Sasa 'mbwai ilikuwa mbwai'.

Venancio aliibuka kwenye akaunti yake ya Facebook akiwa amesimama katikati ya bendera mbili za Msumbiji, amevalia kizibao cheusi na nywele zake ndefu zilizonawiri, akalihutubia taifa.



Alitangaza maandamano ya siku saba mfululizo (seven-day protest) yaliyoanzia Ijumaa ya tarehe 1 Novemba.

Huo ndo'ukawa mwanzo wa maandamano yenye mafuriko ya watu.

Maandamano yaliyoendana na 'Vandalism approach'.

Watu walivunja maduka. Walivamia vituo vya polisi. Walivamia ofisi za FRELIMO. Waliua polisi na wao pia waliuawa.



Maandamano yalisambaa kama mafua ya ndege, kuanzia jimbo la Maputo, Nampula mpaka Zambezia.

Shughuli zilisimama.

Matairi yaliwaka barabarani.



Watu waliwakimbiza polisi na polisi waliwakimbiza watu.

Siku ya kwanza, mchaka mchaka. Siku ya pili, heka heka.

Siku ya tatu, wakati vurugu inaendelea kupamba moto huko Msumbiji, Venancio alishangaa kuupokea ugeni asioutarajia.

Pengine wakati wote alipokuwa mafichoni, alidhania yu salama; yeye, mkewe na binti yake, lakini siku hiyo ndo' alijua alikuwa anajidanganya.

Watu walikuwa wanamtafuta usiku na mchana, hatimaye wakafahamu anapoishi.

'Wageni' wakatumwa kwenda kumsabahi huko kwenye viunga vya Sandton, Johannesburg, nchi ya Afrika ya kusini.



Ulikuwa ni usiku wa Jumapili, Novemba 3.

Venancio aliona watu asiowafahamu malangoni pake, akapata hisia za hatari na hakutaka kupuuzia 'machale' yaliyomcheza.

Alimkusanya mkewe na mwanaye wakapitia mlango wa nyuma, wakaruka ukuta na kukimbilia mtaani kujinusuru.

Baada ya hapo alihamisha makazi yake. Hakutaka kubakia Afrika kabisa. Alikimbilia Ulaya anapojihifadhi mpaka hivi sasa.

Kama kawaida, aliendelea kuhutubia wafuasi wake kupitia mitandao ya kijamii akiwahamasisha waendelee na maandamano.

Novemba 7, maandamano ya siku saba, yalifikia kilele chake nchini Msumbiji.

Ilikuwa ni siku ya kihistoria.

Maandamano yalikuwa makubwa mno kuwahi kutokea nchini. Watu maelfu waliingia barabarani, vyombo vya usalama vikaelemewa.



Kwenye baadhi ya maeneo, ilibidi polisi na wanajeshi wakimbie kujiokoa na hasira za wananchi.

Mwezi uliofuata, mambo yalindelea kuwa magumu zaidi.

Mahakama kuu ilihalalisha ushindi wa Daniel Chapo wa FRELIMO kama Rais anayetakiwa kuapishwa tarehe 15 January mwaka huu.



Maamuzi hayo yalimuibua tena Venancio kupitia akaunti yake ya Facebook; akaunti yenye mamilioni ya wafuasi, akatangaza UFUFUO wa maandamano.

Muda huu aliyaita TURBO V8.

Maandamano hayo yaliambatana na uharibifu mkubwa. Gereza la Maputo Central lilivunjwa na zaidi ya wafungwa 1,500 walitoroka, baadhi yao wakipora silaha za maaskari na kutokomea nazo kusikojulikana.



Sasa polisi walijikuta wana majukumu mapya, wakipambana na waandamanaji lukuki na huku wakiwatafuta wafungwa hatarishi waloingia mtaani.

Wakati huo Venancio naye ametangaza, katika tarehe ileile 15 ya Januari, kama ilivyopangwa na mahakama kuu, ataapishwa kuwa Rais wa nchi ya Msumbiji.

Ataapishwa na nani? Ataapishiwa wapi na kwa namna gani?

Ni yeye ndo' anajua.

 

Attachments

  • 20dfb1264f2ab8247c88f94d4169e3c4.png
    241.2 KB · Views: 3
Kama Tundu Lisu walivyomiminia risasi za kutosha.
Hawanaga mbinu za kuua bila kuacha ushahidi mpaka wamvizie mtu wammiminie risasi na kuleta hofu na taharuki kwa raia..

Au ndio onyo kwa wengine.
 
uasi ktk nchi huwa unaanza kama hivi hivi.
 
Afrika Kuna watu wachache wanaona kwamba wao ndio wenye hatimiliki ya utawala wa nchi. Iwe itakavyokua wanaona wanatakiwa kuwepo madarakani. Kwa faida ya nani..... haifahamiki
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…