Mvutano kati ya bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote dhidi ya Boss wa mamlaka ya usimamizi wa bidhaa za petrol Nigeria bwana Farouk ndio mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii wiki hii.
Kwakifupi sana, Dangote anamshutumu Farouk kuhujumu sera za nchi ya Nigeria kukuza uzalishaji wa ndani wa bidhaa za petrol kwa kutoa vibali vya kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi. Jambo ambalo Dangote anadhani bwana Farouk analifanya katika mazingira ya rushwa.
Kwa upande wake bwana Farouk amedai kuwa utoaji wa vibali ni kwa maslahi ya umma, kuiwezesha nchi yake kuwa na mafuta ya kutosha na amemtuhumu Dangote kuwa anataka upendeleo wa kiwanda chake cha kusafisha mafuta.
Ni katika mazingira haya Dangote amewasilisha madai yake kuwa bwana Farouk amesomesha watoto wake wanne elimu ya sekondali nchini Uswiz kwa zaidi ya dola za kimarekani milioni 5, sawa na zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 13. Dangote amezitaka mamlaka zinazoaimamia maadili ya viongozi nchini Nigeria zimhoji Farouk amepata wapi fedha hizo?
Ni kama bwana Farouk kaona mambo yasiwe mengi, amejiudhuru na Rais Tinubu ameteua boss mpya wa mamlaka ya usimamizi wa bidhaa za petrol.
Ukikitazama kisa hiki kinafanana sana na mzozo wa vibali vya kuagiza Sukari hapa nchini kwetu ambapo siku zote kumekuwa na mvutano kati ya wenye viwanda vya kuzalisha sukari nchini, wafanyabiashara wanaotaka kuagiza sukari kutoka nje na serikali inayotoa vibali vya kuagiza sukari.
Ingawa hapa kwetu hatujawaona wenye viwanda kuchukua hatua kama za Dangote, lakini ni wazi swala hili limeshawagharimu mawaziri kadhaa nafasi zao. Ni imani yangu kuwa kisa hiki cha Farouk na Dangote kinaweza kuamsha ari ya wenye viwanda kupaza sauti zao kutetea uwekezaji wao dhidi ya watendaji wasiowaaminifu wanaofanya maamuzi ya kuumiza nchi kwa maslahi yao binafsi.