Ikulu yathibitisha kifo cha Balali
Shadrack Sagati
Daily News; Wednesday,May 21, 2008 @17:01
Ikulu imekiri kupokea taarifa za kifo cha aliyekuwa gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali. "Rais amesikitishwa na taarifa hizo za kifo cha Ballali, tunaandaa rambirambi tutazituma baadaye," alisema mwandishi habari msaidizi wa Rais, Premi Kibanga.
Hata hivyo, Premi alisema Ikulu haiwezi kutoa taarifa za kifo hicho badala yake wenye jukumu la kufanya hivyo ni ndugu zake marehemu, "Ikulu haihusiki na kutoa taarifa tafuteni ndugu zake waseme habari za hicho kifo."
Habari nyingine kutoka katika ofisi za Benki Kuu ambako Ballali hadi anaondoka kwenda kutibiwa alikuwa mtumishi wa taasisi hiyo, zilithibitisha kutokea kwa kifo hicho. Ofisa Habari wa BoT, Emmanuel Mwero alisema walipokea taarifa za kifo hicho kutoka kwa mke wa Ballali, Anna Muganda.
Mwero alisema Anna ametuma ujumbe kwa wafanyakazi wa BoT usiku wa kuamkia leo akiwajulisha kuwa mume wake alifariki dunia Ijumaa iliyopita mjini Boston, Marekani. "Ni kweli tumepokea ujumbe kutoka kwa mke wake kututaarifu kifo cha mzee Ballali," alisema Mwero.
Hata hivyo, hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo akisema kuwa ujumbe uliotumwa hapo ni kwa ajili ya wafanyakazi kujulishwa kwa vile waliwahi kufanya naye kazi. "Unajua Ballali siyo tena mfanyakazi wa BoT, kwa hiyo kutoa taarifa rasmi itakuwa ni vigumu," alisema ofisa huyo.
Tetesi za kifo cha Ballali zilianza kuvuma tangu Jumapili iliyopita kupitia katika mtandao wa Jamiiforums. "Ballali hatunaye tena," ulikuwa ujumbe uliotawala katika tovuti hiyo tangu Jumapili huku wasomaji wengine wa mtandao huku wakihoji ukweli juu ya taarifa hizo.
Hata hivyo ilikuwa vigumu kuthibitisha habari hizo kutokana na usiri uliogubika kifo hicho. Hata Ikulu Dar es Salaam leo haikuwa tayari kusema ni lini imepokea taarifa hizo za kifo cha Ballali. Hadi jana hakuna ndugu ambaye alitoa taarifa za kifo hicho.
Nyumbani kwa Ballali mtaa wa Mahandu kitalu namba 347 Masaki, Dar es Salaam hakukuwa na dalili zozote za msiba. Gazeti hili lilifika nyumbani hapo na kumkuta kijana aliyejitambulisha kwa jina la Hassan, akieleza kuwa hajui chochote juu ya kifo cha bosi wake.
"Mimi kwa kweli sijui lolote, ni vyema mwende kule alikokuwa anafanyia kazi wanaweza kuwa na taarifa rasmi," alisema Hassan na kuongeza kuwa yupo peke yake na mlinzi na hakukuwa na mtu mwingine ndani.
Mama yake Ballali ameelezwa kuwa anaishi Boko, lakini gazeti hili lilishindwa kufahamu nyumbani anakokaa. Lakini baadhi ya watu wanaamini kuwa yawezekana pia hakuwa na taarifa juu ya kifo cha mwanawe.
Rais Kikwete alitengua uteuzi wa Ballali Januari 9 mwaka huu baada ya kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kugundua Sh bilioni 133 kuchotwa kutoka katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyoko BoT.
Ufisadi huo ulifanywa na watu mbalimbali kupitia kampuni 22 ambazo zilitumia nyaraka za bandia kuchota mabilioni hayo ya fedha. Baada ya kumtimua Ballali, Rais aliunda tume iliyoko chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na wote wanaohusika wakamatwe na wachukuliwe katika vyombo vya sheria.
Kabla ya Ballali kutimuliwa aliondoka nchini kwenda Marekani ambako ilielezwa alikwenda kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake baada ya kudorora kwa muda mrefu. Hali hiyo ya afya iliwafanya hata ndugu zake kutoa malalamiko kuwa yawezekana alikuwa amelishwa sumu.
Akiwa huko aliwahi kuomba ajiuzulu kutokana na matatizo ya afya, lakini Ikulu ilikataa ombi hilo hadi kusubiri ripoti ya EPA ambayo ilimkasirisha Rais Kikwete hadi akaamua kumtimua kazi.
Wakati Ballali akiwa amelazwa Marekani, Gavana wa sasa wa BoT, Benno Ndulu alikiri walikuwa wanamlipia nusu ya matibabu kwa vile aliondoka nchini akiwa mtumishi wa benki hiyo. Hata hivyo Profesa Ndulu hakuwahi kutaja hospitali ambako Ballali alikuwa amelazwa na hadi kifo chake hakuna taarifa rasmi ya kulazwa kwake hospitalini.
Amekufa zikiwa zimebaki siku chache tume ya Rais ikamilishe kazi ya uchunguzi wa ufisadi uliofanywa kupitia akaunti ya EPA. Wasifu wa Ballali unaonyesha kuwa wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mwaka 1967-1976 alikuwa mtumishi katika BoT na alishika nyadhifa mbalimbali. Mwaka 1979 -1984 alifanya kazi Ghana akiwa mtumishi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kama mchumi. Mwaka 1984-1986 akiwa IMF alihamishiwa Zimbabwe katika nafasi hiyo ya mchumi.
1986-1997 aliongoza timu ya IMF kwa ajili ya majadiliano na usimamizi wa sera ya mageuzi ya uchumi. 1997-1998 aliteuliwa kuwa mshauri wa Rais wa mambo ya uchumi na mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Gavana wa BoT, wadhifa aliodumu nao hadi Januari mwaka huu.
Lakini wakati akiwa gavana, IMF ilimteua tena mwaka 2006-2008 kuwa mjumbe wa bodi za magavana akitokea Tanzania. Pia mwaka 2006 alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato (TRA).