DC TEMEKE APOKEA RASMI WANAFUNZI KIDATO 1 Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Jokate Mwegelo leo Januari 17, 2022 amewapokea rasmi wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2022 wanaotarajiwa kutumia madarasa mapya yaliyojengwa kutokana na fedha za mpango wa maendeleo kwa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya mapokezi hayo, Mhe. Jokate ameendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa alonayo juu ya utoaji wa fedha hizo zilizosaidia kuondoa changamoto ya madarasa, huku zikisaidia wanafunzi hao kuanza masomo yao wakiwa katika mazingira safi yanayorahisisha upatikanaji vizuri wa elimu utakaosaidia ufaulu wa masomo yao.
"Tumewaona vijana wetu wamejitokeza kwa wingi siku ya kwanza kuanza masomo yao rasmi, sisi kama Manispaa na Wilaya tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais kwa vitendo, tutaendelea kuhakikisha watoto wetu hawa, wanajifunza yale masomo na stadi zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa". alisema Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hayo Mhe. Jokate ameonesha kufurahishwa kwa kukamilika kwa maono ya Mhe. Rais juu ya ujenzi wa madarasa huku akitoa wito kwa wazazi kuendelea kuunga juhudi za viongozi wao kwa kuwahimiza vijana wao kwenda shule na kuwasimamia katika masomo yao kwa nguvu zote.
"Kikubwa leo hii ni kuwaonesha Watanzania kwamba yale maono ya Mhe. Rais aliyokuwanayo yametimia, kilichobaki ni kuendelea kuwahimiza wazazi kuwalea vijana wetu hawa na kuwasisitizia umuhimu wa kupenda kujifunza na kujiendeleza" alisema Mhe. Jokate
Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kwamba Manispaa na Wilaya wanamikakati ya kuboresha mazingira ya kujifunza, kwa kujenga majengo ya kompyuta, maabara, kuongeza matundu ya vyoo na kubadili mitazamo ya wanafunzi, walimu na wazazi juu ya maisha yao na Taifa letu kwa ujumla.
Ikumbukwe leo 17/01/2022 ni siku ya kufunguliwa kwa shule zote za Msingi na Sekondari nchini huku tukishuhudia shule zikiwapokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuyatumia madarasa mapya yaliyojengwa kuboresha mazingira ya shule za sekondari na kukuza sekta ya elimu nchini.