Dear mama....

Magulumangu

JF-Expert Member
Joined
Jan 7, 2010
Posts
3,051
Reaction score
461
kamwe sijekuchelewa,kwako mama ninasema,
miezi tisa kulelewa,na wewe tumboni mama,
maneno ulirushiwa,mbele na ulitizama,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

Wengi waliyasema,ni utazaa jambazi,
Jibu kwao hukusema,maneno yako ni tenzi,
Ulienda kwa neema,ukayaacha mapenzi,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

Najua mama ulipo,umelala kwa salama,
Muumba daima na yupo,zake mbawa dhahama,
watoto wako na wapo,kukukosa we daima,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

najua nawahi mama,kukwambia siku yako,
kumbuka we ulisema,kuwahi chelewa mwiko,
ulienda kwa heshima,zote mpaka na uliko,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

sina zaidi kukupa,mpaka siku tuwe wote,
ila kwako ulinipa,mapenzi wakati wote,
miezi tisa ulinipa,tumboni wakati wote,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

maua nimeyaweka,tayari siku ifike,
ulipo kuyatandika,harufu kwako ifike,
siku pia nitafika,mungu na anialike,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

Nakumbuka lipotoka,chozi lilitiririka,
miaka kupukutika,kichwani nakukumbuka,
tabasamu nakumbuka,kabla haujatoka,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,

Chozi laanza nitoka,anifuta malaika,
hata yeye akumbuka,siku ulipong'atuka,
mafuta alikupaka,kwa heri hutafufuka,
Hii ndio siku yako,ishiri sita wa tano,
 


Pole sana Magulumangu
yuko maahali pema na pa zuri
yuko nyumbani
 
I LOVE MY MUMY SO MUCH! Mungu Akupe Maisha marefu!
 
Magulu umesikika kilio chako kwa mama..
Hakika atafurahi kuona umesimama..
Bila wasiwasi anajua alivyo kwako maana..
Pole jamani pole kumpoteza mama!

Miezi tisa tumboni alikuona baraka...
Na wale walioponda akawaona viraka..
Naweza kumtetea kukuacha hakutaka..
Pole jamani pole kumpoteza mama!

Futa machozi machoni useme mama asante..
Fuata yake mafunzo furaha moyoni apate..
Kuona waendelea na mezani hukosi mkate..
Japo kakutangulia siku moja utamwona!
 

Lizzy kwa maishair azid kunikosha
Ninachoweza kukushauri...

Aaah mi nimeshindwa bana lizzy hahaha
 
Mwenyez Mungu akulaze mahali pema mama. Nakupenda na na kukushukuru kwa yote mama yangu uliyofanya kwangu.

Amen!
 
Malenga Magulumangu, Pokea zangu salamu,
Wewe kama ndugu yangu, Najua unafahamu,
Alichokipanga Mungu, Hakiwezi mwanadamu,
Mungu amlaze pema, daima milele yote.

Hakuna tena kabisa, alokuwa kama mama,
Kwa zamani mpaka sasa, hata mwisho wa kiama,
Mama huwa hana visa, wala hana uhasama
Mungu amlaze pema, daima milele yote.

Tulioko duniani, lazima tutapotea,
Tutazikwa aridhini, peponi kujongelea,
Na tuishi kwa makini, tusije kuhangamia
Mungu amlaze pema, daima milele yote.

Alale pema amina, Amina tena amina,
Amina nasema tena, Tena na tena amina,
Tuje tumuone tena, Tuseme naye amina,
Amina tena amina, tena na tena Amina.

Na: Big Braza ODM a.k.a Asprini (Babu)
Kaunta ya Juu, Etiennes
Boko Basihaya
Dsm

Dedicated to: Malenga Magulumangu
JF Malenga Wetu
MMU.
 
Lizzy kwa maishair azid kunikosha
Ninachoweza kukushauri...

Aaah mi nimeshindwa bana lizzy hahaha

Hahahaha ungemalizia bwana maana ulikua umeanza vizuri kweli!

Pole na wewe mpendwa!!
 
Pole yaliyokufika, e ndugu magulumangu
Hujafa hujaumbika, hiyo kazi ya mungu
Acha kusikitika, najua una machungu
Mola atamrehemu,alale pema peponi

Dunia ni ya kupita,yeye ametangulia
Na sisi tutafuata, punguza ndugu kulia
Ya mema atayapata,mola atamjaalia
Mola atamrehemu, alale pema peponi

Busara alokwachia, hilo la kujivunia
Fuata yake tabia, pepo utakuja ingia
Sifuate ya dunia, hofu yatakupatia
Mola atamrehemu, alale pema peponi

Futa machozi machoni, mama amepumzika
usiwe mwenye huzuni, najua wataabika
tumuombee kaburini,aishi ka malaika
Mola atamrehemu, alale pema peponi


 

Pole malenga wetu, kwa msiba wa mama
Amlaze mola wetu, mahala palipo pema
Subira ibaki kwetu, kifo cha mama chauma
Huu ndio mwisho wetu, hakuna wa daima

Pole mkuu magulumangu, RIP mama

DEDICATED TO ALL MAMAZ
Ewe mama mpenzi, shairi nakutungia
Yako mema malezi, sina cha kukulipia
Daima nitakuenzi , hadi mwisho wa dunia
Ewe wangu mzazi, zawadi yangu pokea

Miezi tisa tumboni, mwako ulivumilia
Chakula hukutamani, udongo ulijilia
Usiku ni hamkani , usingizi ulipotea
Umbo lako la thamani, shepu ilikupotea

Ladha hukujionea, ukila ulitapika
Homa za kujirudia, hakika uliteseka
Miezi tisa katimia, uchungu nikakutwika
Ulichukia dunia , wakati mimi natoka

Mara ulifurahia, kwa mimi kunipakata
Wala hukujutia, jina zuri uliniita
Nikaanza na kulia, usingizi hukupata
Uliacha ya dunia , huduma niweze pata

Malezi ukayatunza, maisha niyakabili
Mengi uliyonifunza, sasa nimeyakubali
Nina mengi kueleza, muda haunikubali
Mama sitotelekeza, wosia wako ni mali

Kaditamati wa tama, kalamu naweka chini
Tuwaenzi wetu mama, hima hima jamani
Hata akiwa rikwama, walisema wa zamani
Vibaya wakitusema, basi tumo laanani
 

Ndugu yangu klorokwini, Yote umeshayasema,
Kote hapa duniani, hakunaye kama mama,
Wamama nawaenzini, siku zote na daima,
Huyu mama huyu mama, mwacheni aitwe mama.

Bila mama duniani, Wapi pangeli kalika?
Mama ndiye namba wani, hilo halina mashaka,
Ndiye bingwa wa amani, upendo pia hakika
Huyu mama huyu mama, mwacheni aitwe mama!
 

Tukiamua kueleza , mateso alopitia
Kurasa tutamaliza, wala hatutoishia
Mama hana mwenza, aspirin nakwambia
Naiona miujiza, kwa yote alovumilia

Wakwangu nae pia, akhera katangulia
Magulu kakumbushia, namimi namalizia
Dua ninamuombea, daima taendelea
Urithi aloniachia , bado ninajivunia
 


Hili bandiko limenikumbusha mbali sana. Limenikumbusha the most painful tears of my life. How i wish could be able to turn back the hands of time. Ohhh dear
 
NA HAKUNA KAMA MAMA

Malenga mmeandika, mama kumuelezea
Na mimi najumuika, machache kuongezea
Hakika twafarijika, malezi waliotugea
Na hakuna kama mama, mama ndiye namba wani

Na hakuna kama mama, malenga twakubalia
wapata nyingi dhahama, usiku twawalilia
Hawastahili lawama, mengi wametupatia
Na hakuna kama mama, mama ndiye namba wani

Bila mama duniani, tungepata shida nyingi
Leo tupo furahani, sababu wao msingi
Mama yangu natamani, uone miaka mingi
Na hakuna kama mama, mama ndiye namba wani

Mama umejaaliwa, wema uliozidia
Nahisi changanyikiwa,roho itapokimbia
Nitageuka mfiwa, milele takulilia
Na hakuna kama mama, mama ndiye namba wani
 
We loved u mum and dady bt the almighty loved you the most,we couldn't think tht u will leave us in only three months time and that this would be life turn-out. We P,Y,J,H,H,S AND M,YOUR GRANDCHILDREN R. AND F. we remember u both so much and we love u so much. You left us by the time we need you the most.inshaallah M.MUNGU awarehemu na awaweke moingoni mwa waja wake wema. AMINA
 

Asnte nami natoa,kamwe siwe mbanifu,
ni yeye aliyetoa,kachuka kwa ubunifu,
maombi mie natoa,kila siku yakinifu,
kila moja wetu hapa,atayaonja mauti,
 


Ntakujibu jamani,acha kwanza nitulie,
Wewe ni wangu vitani,kuchana wote tulie,
upo juu kilimani,kwa vina pia misilie,
Nitakujibu mkuu,acha moyo utulie,
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…