Deni la serikali ya Tanzania limeongezeka na kufikia trilioni 76 mpaka Januari 2023 kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania, hi ikiwa ni ongezeko la trilioni 4 toka Septemba 2022. Takribani asilimia 65.2 ya deni hili ni deni la nje huku asilimia 34.7 ikiwa ni deni la ndani ambalo ni jumla ya trilioni 26.4.
Kwa kuendesha miradi mikubwa mikubwa kwa pamoja, ambapo sehemu kubwa miradi hiyo imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha za kigeni, Tanzania imejikuta katika shinikizo kubwa la kutafuta mikopo ili kuweza kufidia mapungufu katika bajeti yake.
Madhara ya mtikisiko katika anga ya kimataifa pia yameongeza makali, hii ni kutokana na Tanzania kuhitaji fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa kuliko fedha zinazoingia kupitia mauzo ya nje.
Mijadala mikali imekua ikiendelea nchini juu ya deni la taifa, juu ya ustahimilivu wake. Kwa kutumia ripoti ya tathmini inayofanywa na Benki ya Dunia, IMF a serikali ya Tanzania, serikali ya Tanzania imekua ikieleza kuwa bado deni la serikali ni stahimilivu.
Hata hivyo wadau wa uwajibikaji wamekuwa wakitaka maboresho zaidi kwenye mfumo wa ukopaji, ikiwemo kuongeza wadau katika Kamati ya Madeni ya Taifa ambapo kwa sasa inaongozwa a Wizara ya Fedha kupitia Katibu wake. Wadau wanaopendekezwa kuongezwa ni Bunge la Tanzania, kama uwakilishi wa wananchi.
Wadau kama Muunganiko wa Azaki Katika Mikopo na Maendeleo (TCDD) wamekua wakishauri kuwepo na mfumo wa kikomo cha kukopa (debt celieng), katika mtiririko mzima wa ukopaji Tanzania.
Chanzo: The Chanzo