kwa maneno rahisi Dira ni mwongozo wa kule tunakokusudia kuelekea,wakati sera ni tofauti kidogo na hilo. Ebu fuatana nami katika uchambuzi niliowahi kuufanya kuhusu Sera ya Elimu nchini Tanzania (usichoke kusoma tafadhali)
UCHAMBUZI WA SERA YA ELIMU YA TANZANIA na
WITO WA MJADALA WA KITAIFA KUHUSU MFUMO WA ELIMU TANZANIA
Ifuatayo ni sehemu yaliyomo katika mada kuu iliyotumika kuzindua mjadala wa elimu kitaifa kama ilivyotolewa na Mwl. George Kahangwa, mkufunzi wa shirika la elimu ya sheria Tanzania (TANLET), katika maadhimisho ya Nyerere day Oktoba 2006, ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni; Dar es Salaam
Utangulizi
Watanzania katika ujumla wetu tunayo masuala yetu ya ndani ambayo yamevurugika sana na kutukosesha maendeleo. Nguvu zetu na ushirikiano wetu ndio pekee utakaotusaidia kuyaweka sawa na kutupeleka kule tunakotaka. Tokea miaka ya mwanzo ya Uhuru wa nchi yetu, Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere alitutaka tushirikiane na tutumie nguvu za pamoja kupigana vita dhidi ya maadui wetu ujinga, maradhi na umaskini. Miaka 45 sasa, tukiwa katika vita hivyo hatujaweza kumshinda angalau adui mmoja kati ya hao watatu. Hapana shaka tuna udhaifu mkubwa sana katika mapambano yetu, na udhaifu upo hasahasa katika sekta ya Elimu nchini.
Kama elimu yetu isingekuwa na matatizo mbona tungeushinda ujinga, kwa Elimu tukaushinda umaskini na maradhi; kwa Elimu tukafikia kiwango kizuri cha maendeleo kama tulivyoshuhudia katika nchi za wenzetu (mathalani Japan na nchi za Scandinavia) waliotumia raslimaliwatu vizuri, wakawekeza katika elimu na sasa wako mbali sana kimaendeleo.
Tumekosea sana katika elimu kuanzia nini tunachokiamini, na tunachokitekeleza kupitia sera zetu na mipango mbalimbali ya elimu. Tumeshindwa kuwathamini askari wa mstari wa mbele katika vita vyetu (Walimu). Tumeendelea kutenga kiasi kidogo sana cha fedha kwa ajili ya sekta hii. Tumechezea mitaala na kuiyumbishayumbisha kana kwamba taifa hili halina dira wala mwelekeo. Taifa limegeuzwa kichwa cha mwendawazimu kwa kufanyiwa majaribio ya mara kwa mara ya nadharia za sera na mipango ya elimu isiyo endelevu na sera zisizoendana na ukweli wa kiutafiti ambazo mara zote zimefanya ubora wa elimu uzidi kuporomoka. Kwa mtindo huo taifa linaangamia kwa kupelekwa hatua moja mbele kisha hatua mbili nyuma ilihali ulimwengu wa utandawazi unasonga mbele kwa kasi, hautungojei.
Yatosha sasa tulivyozunguka mlima wa matatizo, turejee katika mstari sahihi. Tujitathmini sisi wenyewe, tutambue madhaifu yetu, tujirekebishe, tukubaliane njia sahihi za kutupeleka mahali sahihi tena kwa haraka. Hakika tunahitaji kwanza kujadiliana kwa pamoja, tuangalie pamoja na mambo mengine, lile ambalo wadau mbalimbali wa elimu wametoa wito tulifanye, yaani Mjadala wa kitaifa kuhusu elimu mjadala wetu uangalie ni nini tulipanga kufanya kama nchi, kitu gani kinatekelezwa katika sekta ya elimu na ni kipi kilicho bora zaidi ambacho tungepaswa kufanya. Kwa maana hiyo mjadala huu uwe sehemu ya kutathmini mipango na utekelezaji wake kisha uibue mapendekezo yatakayoliokoa taifa.
Ili tuweze kuijadili vizuri mfumo wa elimu yetu hatuna budi kuangalia kwanza sera ya elimu inatotumika hapa nchini. Tuanze kwa tutafakari nini maana ya neno sera.
Sera yaweza kuwa ni mpango wa yatakayotendwa katika sekta fulani au ni maelezo ya malengo na njia ya utendaji iliyochaguliwa kuyafikia malengo hayo. Sera huwekwa katika maandishi ili iwe ndio kiongozi cha maamuzi ya nini kifanyike.
Sera zaweza kuainishwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngazi zake mbili. Katika ngazi ya kwanza sera hubainisha masuala muhimu ya sekta fulani na kufafanua nia ya kisiasa ya kurekebisha au kuboresha vipengele mbalimbali vya mfumo wa sekta fulani. (Substantive policies)
Katika ngazi ya pili sera huweka wazi utaratibu au namna ya utekelezaji wa kilichobainishwa katika masuala muhimu: nani mtekelezaji; utekelezaji ufanyikaje; kipindi cha utekelezaji; na ni raslimali gani zitumike. (Procedural policies) Hivyo sera ya elimu iliyokamilika na inayotekelezeka lazima iwe na ngazi zote mbili yaani sera bainishi na sera namna. Haya ni mabawa mawili yanayotegemeana. Sera nyingi zimekua dhaifu na zisizotekelezeka kwa kukosa bawa la pili; sera namna.
Aidha yapo mambo kadhaa yanayofanya sera ifanikiwe. Miongoni mwa mambo hayo ni ushirikishaji kamilifu wa wadau wote wa sekta husika kuanzia hatua za mwanzo za uandaaji wa sera yenyewe, utekelezaji wake na kuifanyia tathmini sera hiyo.
Elimu (kama sekta) inao wadau ambao ni pamoja na serikali kuu na serikali za mitaa, wamiliki wa Taasisi za Elimu za umma na binafsi, wazazi, walimu, wataalam wa elimu, wanafunzi, asasi zisizo za kiserikali, vyama vya siasa, jumuiya ya wafadhili, na wananchi kwa ujumla.
Hapana shaka mjadala kuhusu elimu utakuwa haujakamilika kama utapuuza kuwashirikisha kikamilifu wadau wote hao. Hakika sera iitwayo ya Taifa na mipango yoyote isiyozingatia ushirikishwaji wa kundi fulani la wadau, kwa vyovyote vile ina walakini.
Sera ya elimu inayotumika nchini Tanzania kwa sasa ni Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995.
Yanayojiri nchini katika sekta ya elimu
Katika kipindi cha takribani mwaka mmoja sasa tangu serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Wizara dada zinazohusika na utoaji wa Elimu nchini; yaani Wizara ya Elimu na Mafunzo chini ya Mheshimiwa waziri Magreth Simwanza Sitta na Wizara ya Sayansi Teknolojia na Elimu ya juu inayoongozwa kwa sasa na Mheshimiwa Waziri Profesa Peter Msolla; zimetenda mambo kadhaa ambayo yamemgusa kila mtanzania anayejali maendeleo ya taifa letu. Yaliyotendwa ni pamoja na jinsi wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu ilivyolishughika suala la mikopo ya wanafunzi wa Tanzania wanaosoma stashahada na shahada mbalimbali katika vyuo vikuu vya umma na vya binafsi nchini na nje ya nchi. Awali karibu na uchaguzi mkuu wa mwaka jana (2005) Serikali iliutangazia umma wa Watanzania kwamba fedha za mikopo zipo nyingi sana ila wakopaji ni wachache. Lakini mwaka huu (2006) Waziri wa sasa katika wizara husika akaliambia Bunge mjini Dodoma kwamba sasa mikopo ingetolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya umma tu. Hilo nalo likatenguliwa kwa uamuzi mwingine kwamba wanaostahili ni wavulana wa daraja la kwanza na wasichana wa daraja la kwanza na la pili la kidato cha sita. Kutokana na maamuzi hayo,watanzania kadhaa wakashindwa kujiunga na elimu ya juu wakiwemo yatima na maskini.
Kwa kweli maamuzi hayo ya wizara kwa niaba ya serikali si tu yalipunguza fursa za watanzania kupata elimu bali yalienda kinyume na sera ya Taifa ya elimu na mafunzo. Wakati sera katika kipengele chake cha 8.6, inaeleza nia ya serikali kuongeza udahili katika elimu ya juu, matamko ya wizara yalisigina nia hii njema ya kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanapata elimu ya juu kwa ajili ya kuiendeleza nchi yetu.
Vilevile katika kipengele cha 3.3 cha sera hiyo, inaelezwa kuwa serikali itasaidia jamii zisizobahatika (yatima, maskini na wengine) ziweze kupata fursa nyingi za elimu. Maamuzi ya wizara yaliweka kando hilo na kuamua kutumia madaraja ya kufaulu hata kama kuna maskini na yatima anastahili kuingia chuo kikuu lakini hana hilo daraja. Ama kwa hakika kusaidia hawa wasio na uwezo ndilo lengo hasa la kuundwa kwa Bodi ya Mikopo na kuwepo kwa mikopo yenyewe.
Aidha wakati kipengele cha 3 cha sera ya elimu kinazingatia kanuni ya fursa sawa kwa wote, maamuzi ya serikali yalikuwa na chembe za ubaguzi wa kitabaka, kijinsia, kinasaba, kidini, kikanda na kimaumbile. (Ubaguzi huu umeongeza manunguniko miongoni mwa waliokwisha shiriki mikutano ya mjadala huu, hata baadhi ya watu wakadhani ndio ajenda kuu ya mjadala)
Vigezo hivyo vya utoaji wa mikopo kwa daraja la kwanza na la pili vimewekwa kwa namna ambayo inaonesha wazi kuwa serikali imeingilia mamlaka ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi, kinyume cha sheria namba 9 ya mwaka 1994 iliyounda Bodi hiyo ya Mikopo. Sheria hiyo sehemu ya 17(d) na kanuni ya Bodi ya mikopo ya 2004 pia nayo inaeleza kuwa kipaumbele kitatolewa kwa yatima, wenye ulemavu,wanawake katika masomo ya sayansi au uandisi na teknolojia. Kwa kutozingatia vigezo hivyo, maamuzi ya serikali yalikuwa yanakinzana si tu na sera, bali hata sheria ya Bodi ya Mikopo na katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania. Kwa ufupi suala la mikopo limetuonyesha kwamba, ubora wa sera na mipango si tu maandishi yake bali ni pamoja na uwezo wa watekelezaji kuielewa, kuizingatia na kuitekeleza kwa umakini.
Utekelezaji unaoendelea sasa umewaumiza wanyonge na umeifanya elimu ya juu nchini iendelee kuwa ya wateule wachache (elite). Wachache hao kamwe peke yao hawataweza kutupeleka kwenye kiwango cha maendeleo tunachokitaka. Ili nchi yetu iweze angalau kufikia hatua ya awali ya maendeleo kitekinolojia sharti asilimia 25% ya wanaoingia elimu ya msingi nchini waweze kudahiliwa katika elimu ya juu. Tanzania hadi kufikia mwaka 2001 tulikuwa kwenye asilimia 0.37%, katika hali yetu mahututi kiasi hicho bado tunawanyima watu mikopo ya kusoma!
Kwa utendaji huo wa kuliangamiza taifa, watendaji yamkini wana agenda ya siri ya kujenga kwa maksudi taifa lenye wasomi kichele na alaiki ya mambumbumbu wasio na uwezo wa kushiriki masuala ya uchumi na siasa za nchi yao; wasioweza kuhoji utendaji wa viongozi wao na kuwawajibisha, wasioweza kukataa kuporwa kwa raslimali za nchi kwa njia ya mikataba inayonuka rushwa na ufisadi mwingine; wasioweza kushika nafasi za uongozi ili uongozi na utajiri ubaki mikononi mwa familia chache teule.
Wizara ya elimu na mfunzo kwa upande wake imeishafanya mengi ikiwa ni pamoja na kuzingatia sera katika kipengele cha 6.2.5 kwa kurejesha masomo yaliyofutwa na waziri wa zamani, kipengele kinaweka wazi kuzingatiwa kwa masomo hayo katika mfumo mzima wa elimu. Kumbe tofauti ya mawaziri hawa ni kiwango chao cha kutekeleza au kutotekeleza sera na mipango ipasavyo.
Aidha wizara ya elimu katika kile kinachodaiwa ni kukabili upungufu wa walimu, imeamua kuwapeleka vijana waliomaliza kidato cha sita katika mafunzo ya mwezi mmoja ili wawe walimu wa sekondari na kuwaahidi shahada za chuo kikuu huria. Hatua hiyo ni kinyume na sera ya Elimu hususan kipengele chake namba 5.4.4 kinachoweka sharti kwamba, kiwango cha chini kabisa cha taaluma ya mwalimu wa sekondari iwe ya umma au ya binafsi kitakuwa Diploma ya Elimu tena iliyotolewa na chuo kinachotambulika. Kadhalika utendaji huo wa wizara unapingana na sera katika masuala ya ubora wa elimu na hitaji letu la kuwa na walimu mahiri, kama sera yenyewe inavyosema. Kibaya zaidi chuo kikuu uria cha Tanzania nacho kimenasa katika mtego usiokuwa wa kwake kwa kuandaa mpango huitwao clash program wa kuwasomesha watanzania shahada ya ualimu kwa miaka miwili ilihali kinajua wapo walimu waliosoma shahada hiyo kwa miaka minne tena kwa kozi ya kuishi chuoni. Ni dhahiri hiyo haitakuwa shahada, kwa mujibu wa sera ni diploma.
Mafunzo ya mwezi mmoja yameudhalilisha ualimu. Ualimu ni taaluma (Profession) haiwezi kufunzwa katika siku thelathini. Mwalimu ndiye mpiganaji wa mstari wa mbele katika vita yetu dhidi ya ujinga. Iwapo askari wa mgambo hawezi kufundishwa kwata tu akaambiwa nenda kasaidie angalau kikosi cha mstari wa akiba vitani kabla hajafunzwa shabaha, inakuwaje yanachukuliwa maamuzi ya namna hii katika taaluma nyeti ya ualimu na sekta ya elimu kwa ujumla. Ama kwa mfano mwingine, taifa letu lina uhaba wa madakitari hadi serikali inaamua kuwaita kazini waliostaafu, basi tuwapeleke vijana waliomaliza kidato cha sita wakasomee udakitari kwa mwezi mmoja. Kuna taaluma tatu zinazofanana kwa jinsi zinavyogusa moja kwa moja nafsi ya mtu; ukasisi unaoshughulika na roho; udaktari unaushughulikia mwili na ualimu unaoshughulikia akili. Zote tatu hazipaswi kuchezewa hata kidogo, hafundishwi Padri au Shehe kwa siku therathini. Mara nyingi mwalimu shuleni amefanya yote matatu.kumlea mtoto kiakili, kiroho na kimwili, iweje leo tumpe mtu mwenye wajibu mzito kiasi hicho mafunzo ya zimamoto. Labda tuwaulize hao waliosoma kwa siku 30, ninyi ni wataaluma ipi na mna cheti kipi kinachohalalisha huduma yenu? Jibu ni la wazi, ninyi sio walimu ondokeni mara moja mashuleni kama mnalipenda taifa letu, acheni kucheza na akili za watoto wa watanzania wasio na hatia.
Kwa nini serikali haijifunzi kutokana na makosa yaliyofanyika wakati wa utekelezaji wa mpango wa UPE miaka ya 1970 na 80. Alizolewa yeyote akapewa ualimu, madhara yake yanaliandama taifa hadi leo. Wakati umefika wa Tanzania kuwa taifa linalojifunza kutokana na wengine au makosa yetu wenyewe. Iweje hadi leo hatupendi kushugulikia mzizi wa tatizo tunakimbilia kuchukua maamuzi ya ilmradi. Tunapuuza kabisa sababu zinazowafanya walimu wenye sifa waikimbie taaluma yao kila siku iendayo kwa Mungu. Matharani, siku kadhaa zilizopita iliripotiwa kutoka mkoani Mara kwamba walimu wa shule kadhaa za sekondari mkoani humo wamekimbia, kisa serikali tangia iwaajiri hawakuwahi kulipwa mishahara yao. Badala ya kushughulikia chanzo cha tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi tunakurupuka kuajiri wasio na sifa za ualimu eti kujaza nafasi.
Wakati tulionao si wa kuharibu zaidi. Ni wazi sasa kwamba ipo haja ya kujadili sera na mipango ya Elimu na mafunzo ili tukubaliane namna ya kudhibiti yanayotekelezwa katika sekta ya elimu yasiendelee kuliangamiza taifa.
Mfumo wa elimu
Watanzania tunatofautiana sana kifikira kuhusu mfumo wa elimu unaoifaa nchi yetu. Tofauti hizo zimejidhihirisha zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, ambapo kila chama kina mtizamo wake kuhusu elimu. Ikitokea vyama hivi vya siasa vikapishana mara kwa mara katika utawala wa nchi, na vyote hivi vina sera tofauti tofauti za elimu, balaa kubwa litaisibu sekta hii nyeti ya ELIMU.
Tunavyo vyama vya siasa 18 vyenye usajili wa kudumu na takribani vitatu vyenye usajiri wa muda. Hivyo, zipo sera tofauti zaidi ya 18 kuhusu elimu. Je sera ya elimu ya taifa imejumuisha kwa kiasi gani michango kutoka sera za vyama vyote hivi ili kujenga mwafaka wa kitaifa kuhusu jambo hili nyeti? Ni wazi kuwa taifa linahitaji sera moja isiyoyumbayumba, inayokubalika kwa wadau wote wa elimu ili labda tofauti zetu zibaki katika mbinu za utekelezaji. Mjadala wa kitaifa ndio pekee waweza kutufikisha katika muafaka huo.
Tuchukulie mfano wa kilichomo katika ilani za uchaguzi za vyama kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Tutaona wazi kuwa elimu iko hatarini, kama hatutajadiliana, kuelewana na kukubaliana. Yapo maeneo ambayo ilani za vyama fulanifulani vinakubaliana na mengine vinatofautiana.maeneo hayo ni pamoja na Mfumo wa miaka ya elimu, Lugha ya kufundishia na namna ya Kugharimia elimu. Vyama kadhaa viliweka bayana katika ilani zake nia ya kuimarisha elimu ya awali katika maeneo yote nchini. Lakini kwenye suala la mfumo wa elimu, vyama vinatofautiana sana. Wakati vipo vyama vinayoshikiria mfumo wa miaka 2-7-4-2-3+, vingine vinaona bora miaka 2-8-4-2-3+, vingine miaka 2-11-1-3+
Elimu ya msingi na suala la ajira
Sera ya elimu inayotumika nchini inaeleza kuwa baada ya elimu ya msingi, mhitimu aweza kuingia katika ulimwengu wa kazi (kuajiriwa/kujiajiri). Tujiulize, elimu yetu ya msingi tuliyonayo sasa nchini na mitaala yake ilivyo, kweli yatosha kwa mtoto anapomaliza darasa la saba kuingia katika ajira, ajira ipi (ufanyakazi za ndani, uchangudoa, upigadebe na unyoka katika machimbo ya madini, ukuli au umachinga?); na je ni ajira katika umri upi na si kinyume na sheria za kazi za shirika la kimataifa (ILO) zinazozuia watoto wasiajiriwe/wasitumikishwe? Sera haielezi kama wahitimu wa elimu ya msingi wanao ujuzi wowote wa kuwawezesha kuingia katika soko huria lenye changamoto za utandawazi, sayansi na tekinolojia ya kisasa.
Mitaala ya elimu nchini
Nchi yetu imekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala karibu kila wizara ya elimu ilipopata uungozi mpya. Wizara ya Elimu imepata kuongozwa kwa vipindi tofauti na mawaziri ambao idadi yao sasa inafikia 16. Kila mmoja wa hawa aliingia madarakani na mikakati yake tofauti na wenzake. Tofauti hizo badala ya kuleta tija zimeikosesha sekta ya Elimu mwendelezo (continuity) na kuchangia uduni tunaouona leo katika elimu ya taifa. Kwa mfano ni wazi kuwa tofauti kati ya Waziri Jackson Makwetta na Waziri Joseph Mungai na sasa tofauti kati ya Mungai na Waziri Magreth Sitta imeyumbisha mno ubora wa mitaala ya elimu ya nchini.
Bila mitaala mizuri na imara hakuna elimu bora. Laiti kila waziri angefuata msimamo wa sera ya kitaifa, elimu yetu isingekuwa duni kama tunayoijua leo. Kwa kuzingatia unyeti wa suala la mitaala, mnamo mwaka 1996 wadau wa elimu nchi waliwahi kuishauri serikali kutengeneza sera rasmi ya pekee kuhusu mitaala. Leo hii miaka kumi baadaye, watanzania hawajasikia lolote kuhusiana na kuzinduliwa kwa sera ya mitaala. Mjadala huu utusaidie ili serikali ilifanye hilo kwa maslahi ya taifa. Hakika tunahitaji mitaala isiyoyumbayumba tena iliyo sahihi.
Bajeti na kugharimia elimu
Watanzania hatuna budi kutafakari kwa kina mwelekeo wetu wa namna tunavyogharimia elimu kuanzia ya msingi hadi chuo kikuu. Jinsi elimu inavyogharimiwa kwa sasa ni mashaka matupu, ambapo bajeti ya serikali kwa ajili ya elimu imeedelea kuwa ndogo na matumaini ya watanzania maskini kupata elimu bora yanazidi kufifia. Matharani,suala la mikopo ya chuo kikuu linavyoshughulikiwa.
Aidha tukirejea katika sera ya elimu nchini, miongoni mwa madhaifu ya sera hiyo ni kuwa na mambo yanayotofautiana au yanayopingana hususan kuhusu ni vipi tugharimie elimu na kwa maslahi ya nani. Mathalani wakati sera katika sura ya 3 inazungumzia upatikanaji wa elimu na fursa sawa (Access and equity) ikilenga kuwainua maskini, yatima na makundi mengine ya wasiobahatika, kwa upande mwingine inaweka upinzani kwa hilo katika sura ya 10 kipengele 10.2 inaposisitiza uchangiaji wa gharama za elimu bila kuonesha makundi ya wasioweza yataponea wapi.
. Tujiulize swali jingine katika mjadala huu, kwamba Wizara ya Elimu ilipofuta ada ya UPE iliweka njia gani mbadala kwa ajili ya kupata fedha za kugharimia elimu ya msingi nchini?
Na je tulipofuta ada ya UPE, huku bado tunazitaka halmashauri (kwa mujibu wa sera kipengele cha 10.2.12) zianzishe kodi maalum ya elimu kwa ajili ya kupata fedha za kuendesha elimu ya msingi, huku sio kujikanganya? Ukweli ni kwamba halmashauri nchini hadi sasa hazina kodi hiyo zimebaki kuwa tegemezi kwa serikali kuu na kwa fedha ya wafadhili.
Sera pia inataja nia ya serikali kuboresha mgawo wa bajeti yake ya kila mwaka kwa ajili ya sekta ya elimu (kipengele 10.2.11). Lakini katika utekelezaji, bajeti ya elimu inapanda na kushuka mwaka hadi mwaka. Mathalani, mwaka ilipoandikwa sera (95/96), Elimu ilipata asilimia 15.3% ya bajeti, ikashuka hadi asilimia 10.5% mwaka 97/98. Ikaja kupanda hadi 22.1% mwaka 2001/02 lakini ikaporomoka tena hadi 15.1% mwaka 2004/05 Kuyumbayumba huku hakuendani na sera hata kidogo na kunaonesha jinsi ambavyo serikali imeshindwa kuweka kipaumbele na msimamo katika elimu. Wapo wadau wa elimu wanaopendekeza asilimia ya bajeti kwa ajili ya elimu ifikie 30% na zaidi. Kwa sasa ugharimiaji wa elimu nchini unategemea sana misaada toka nchi wafadhili na mikopo ya Benki ya Dunia. Ni vema tunavyosaidiwa, lakini watanzania tunapaswa kutafuta namna tutakavyo ongeza fedha za kugharimia elimu tusitegemee misaada siku zote.
Kwa upande wa vyama vya siasa nchini, navyo vinatofautiana sanaa kuhusu namna ya kugharimia elimu. Matharani, wakati chama fulani msimamo wake ni serikali kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, kingine kinasema mwanafunzi atachangia elimu, kwa kufuata mpango wa kadri mwanafunzi atakavyofaulu vizuri zaidi ndivyo atakavyozidi kulipia gharama kidogo zaidi kwa ajili ya elimu
Suala ubinafsishaji katika elimu
Hivi karibuni nchi yetu iliingia katika ubinafsishaji ambao uliikumba pia sekta ya elimu. Hivi leo watu binafsi wanamiliki na kuendesha shule za awali, msingi, sekondari na vyuo Sera ya elimu itumikayo nchini inaunga mkono ubinafsishaji huu katika vipengele vingine mbalimbali,lakini Katika sura ya 3 sera hiyo hiyo inasisitiza dhana ya usawa katika kuwapatia watu wote elimu bora. Swali la kujiuliza ni, kwa kiasi gani tofauti za kitabaka zimeongezwa na kasi ya ongezeko la shule binafsi za gharama ya juu zenye mvuto wa kimaslahi na mazingira bora ya kazi kwa walimu, ilihali shule za umma hazina walimu. Ni dhahiri katika hili ubinafsishaji unamaanisha kutoweka kwa matumaini ya wanyonge. Naam, asiye na hela akaandikishe watoto wake katika shule zisizo na walimu, mtoto apate daraja la chini akose mkopo wa elimu ya juu, umaskini uzidi kushamiri katika familia yake. Yule mwenye pesa akasomeshe wanawe kwenye shule zenye walimu wa kutosha na wa akiba ili azidi kufaulu na kuneemeka.
Tulipoamua kubinafsisha elimu, tungeona mbali ili kuepusha kupanuka kwa wigo wa matabaka katika jamii. Leo hii mshahara wa mwalimu mwenye shahada anayeanza kazi serikalini ni wastani wa sh. 230,000/=, wakati katika baadhi ya shule binafsi mwalimu mwenye sifa kama hizo ana mshahara mara mbili ya huo, ingawa naye mazingira yake ya kazi hayajawa mazuri. Serikali katika hali hiyo ya tofauti kubwa kimaslahi, isitegemee shule za umma zitakuwa na walimu bora. Lakini kwa kuwa Serikali inao uwezo kuliko wamiliki wa shule binafsi, muda umefika imheshimu mwalimu na kumboreshea maslahi yake. Ubinafsishaji ulipaswa kuzingatia haki ya kila mtoto wa kitanzania kufundishwa na mwalimu bora.
Matatizo ya walimu
Suala la matatizo ya walimu nchini limekuwa wimbo wa muda mrefu bila ufumbuzi wake. Hatupaswi kuendelea na wimbo huu tena. Sharti ufumbuzi upatikane sasa.
Sera ya elimu katika ukurasa wa 31 inaorodhesha matatizo hayo ya walimu, ikiwa ni pamoja na mishahara midogo, uhaba wa nyumba za walimu, hadhi ya chini ya taaluma ya ualimu na ukosefu wa nafasi za walimu kujiendeleza. Hatua zinazopendekezwa ndani ya sera kwa ajili ya kuondoa matatizo hayo ni za kiujumla sana. Kushindwa kwa sera kubainisha mikakati mahususi ya kuondoa kero zinazowakabili waalimu kumechangia kwa kiasi kikubwa usugu wa kero hizo ambazo zinaendelea kuwepo hadi leo. Ingefaa matatizo yanayawapata walimu wetu, yatafutiwe ufumbuzi wa kudumu haraka sana.
Aidha kuhusu taaluma yenyewe, kipengele cha 5.3.6 kinasisitiza kwamba taaluma ya chini ya mwalimu wa shule ya msingi itakuwa ni cheti cha ualimu daraja la kwanza. Kipengele kinakwepa kusema hali hiyo itakuwa imefikiwa ifikapo lini. Hivi leo miaka kumi na moja baada ya kuzinduliwa kwa sera hiyo, katika mikoa kadhaa, kwa mfano mkoa wa Lindi asilimia 44.3% bado ni walimu wa daraja B/C.
Kwa upande wa ujuzi wa walimu wanaofundisha mashuleni, Taifa mwaka huu lina jumla ya walimu 47,536 ambao taaluma yao ni chini ya daraja A, wataendelezwa lini hawa? Inaelekea jitihada zinafanyika Dar es Salaam ambako asilimia 13.1% tu ndio wa daraja la B/C. Wakati huo huo tunaimba wimbo wa haki ya watanzania wote kupata maisha bora bila kuwa na shule bora, walimu wenye taaluma ya kutosha na kwa usawa. Dar es Salaam ina walimu 238 wenye shahada ya chuo kikuu walioko elimu ya msingi, wakati kwenye hiyohiyo, Lindi, Kagera, Mtwara, Mwanza, na Singida hawana hata mmoja! Huu si umakini hata kidogo katika matumizi ya raslimali watu.
Sera ya elimu inatambua kwamba mwalimu wa daraja la A ni yule aliyehitimu kidato cha nne na kupata mafunzo ya miaka miwili katika chuo cha ualimu, leo tunao waliopata mafunzo hayo kwa mwaka mmoja, hawa nao ni wa daraja gani?
Wakati sera kwa kipengele namba 5.4.4 inasema kwamba kiwango cha chini cha taaluma ya mwalimu wa sekondari kitakuwa Diploma (bila kutaja ifikapo lini) Shule za sekondari za serikali mwaka huu (2006) zina walimu 1860 ambao ama hawana taaluma ya ualimu au wana cheti daraja la B/C; wapo pia walimu 196 wa cheti daraja A tu wanaofundisha katika shule za sekondari nchini.
Sera katika ukurasa wa 41 inazitupia lawama shule binafsi kwa kuendekeza ajira kwa walimu wasio na sifa (lakini hao wanaofundishwa kwa siku 30 wanaenda shule za serikali). Ukweli ni kwamba walimu wengi wenye shahada na walio mahiri wako katika shule za binafsi kwa sababu zinathamini ubinadamu wao na taaluma yao.
Sera katika ukurasa wa 46 inataja hitaji la haraka la kufundishwa walimu wengi zaidi, lakini leo hii idadi ya walimu tarajari wa cheti daraja A wanaojiunga na vyuo vya ualimu nchini inazidi kupungua, wakufunzi vyuoni wanapungua, vyuo vya ualimu vimepungua na fungu la bajeti ya serikali kwa ajili ya vyuo vya ualimu imeporomoka kutoka asilimia 2.6% mwaka 1997/98 hadi 1.1% mwaka huu 2006/07.
Wakufunzi wa vyuo vya ualimu kwa mujibu wa sera wanatakiwa wawe na elimu si chini ya shahada inayotambulika ya chuo kikuu (kipengele 5.5.5). Takwimu za mwaka huu zinaonesha kati ya wakufunzi 799 wa vyuo vya ualimu vya serikali ni 286 tu ndio wana shahada. Inakuwa ni jambo linaloshangaza sana, kwamba vyuo vya serikali vina wakufunzi 24 ambao hawana hata cheti cha daraja A (hao wanamfundisha nani, nini) wakati huo kuna walimu zaidi ya 200 wenye shahada ya chuo kikuu wako shule za msingi. Huo ni ushahidi mwingine wa matumizi mabaya ya rasilimali watu yanayoendekezwa na wizara husika.
Lugha ya kufundishia
Eneo jingine tunalopaswa kujadili na kukubaliana ni suala la lugha ya kufundishia. Kwa muda mrefu sasa hapa nchini kumekuwa na mabishano ya lugha gani itumike kufundishia mashuleni..Japo tafiti mbalimbali zimethibitisha kwamba Kiswahili kingeweza kuboresha elimu yetu ya sekondari hadi vyuo, bado tumeendelea kungangania lugha ya mkoloni. Seraya elimu (ukurasa wa 52) inataja sababu za Tanzania kuendelea kutumia lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia katika shule za sekondari. Sababu hizo ni kuwawezesha watanzania kupata (to access) ujuzi na maarifa, sayansi na teknolojia na kuwasiliana na mataifa mengine. Tujiulize katika mjadala huu iwapo hayo hayawezi kupatikana kwa Kiswahili chetu na hivyo tuendelee kungangania kiingereza ambacho wapo wanaopata shida katika kufundisha au kujifunza kwa kiingereza. Hatuna mfano wa nchi yoyote katika ulimwengu wa kwanza iliyopata maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa kutumia lugha ya kigeni.
Aidha kipengele namba 5.5.8 cha sera kunasema kwamba lugha ya Kiswahili itakuwa somo la lazima kwa wanaosomea ualimu daraja A, diploma na shahada, Hili ni jambo jema lakini haliendani na ukweli kwamba katika vyuo vyetu vikuu wanafunzi wa shahada ya ualimu hawana kozi ya Kiswahili kama somo la lazima isipokuwa wale tu wanaochagua wenyewe kusoma Kiswahili.
Kwa upande wa siasa, vipo vyama vya siasa nchini ambavyo vikiingia madarakani (si ajabu 2010) lugha ya kufundishia kuanzia chekechea hadi chuo kikuu itakuwa Kiswahili tu. Lakini vipo pia vyama ambavyo vikiingia madarakani vitataka lugha ya kufundishia iwe kiingereza tu. Ni wazi kuwa tusipojenga mwafaka wa taifa kuhusu masuala nyeti kama haya, ipo siku taifa litaingia katika matatizo makubwa. Mjadala huu utusaidie tupate suluhu ya suala hili pia.
Mitihani na malengo yake
Tunaitaji pia kuafikiana juu ya usahihi wa malengo ya mitiani itolewayo katika mfumo wetu wa elimu. Mingi imeonekana ikilenga kuchuja na kutupa waliowengi nje kusikojulikana na mingi inapima tu uwezo wa wanafunzi kukariri na kukumbuka kiasi kwamba nyanja nyingine za maarifa hususan ujuzi na stadi zimepuuzwa.
Matharani, katika ukurasa wa 58 wa sera kuna maelezo kwamba mtihani wa darasa la IV lengo lake ni kupima uwezo wa wanafunzi katika kusoma, kuandika na kuhesabu (K3) na kuamua wandelee darasa la V au wakariri (warudie) darasa la IV. Ni heri tungepima K3 katika kiwango cha chekechea na sio darasa la juu kiasi hiki (la IV). Upungufu mwingine ni kwamba, sera haitaji mwanafunzi aruhusiwe kurudia mara ngapi darasa la nne na baada ya hapo iweje?
Mzazi mmoja ambaye mwanae alijikuta akirudia darasa la nne mara ya pili, alimfuata mwalimu mkuu shuleni na kumwambia hivi;
Mwalimu, unarudisharudisha tu mtoto bila kufikiria mimi mzazi nabeba mzigo gani? Sasa mimi nahesabu mwanangu yuko darasa la sita na mwakani anamaliza, miaka itayoongezeka hapo sare na madaftari utanunua wewe.
Nafasi ya tafiti na tathmini katika elimu
Sera nzuri za elimu au za sekta iwayo yoyote hazina budi kutungwa kutokana na ugunduzi wa tafiti za kina na hatimaye kutathminiwa mara kwa mara. Kipengele cha 6.4 cha sera ya Elimu na mafunzo kinazungumzia utafiti katika elimu na tathmini ya sera. Kipengele hiki kinazitupia lawama tafiti zinazofanyika nchini, kwamba hazina mwelekeo wa kusaidia kuunda sera na hazina mtazamo wa kiutendaji. Kipengele kinaendelea kulalama kwamba, watendaji katika vitengo husika vya tafiti wanaondoka na waliobaki wana utaalamu finyu katika masuala ya tafiti za elimu. Ni dhahiri katika hali hiyo sera zinazotungwa nchini zimetungwa kisiasa zaidi na zinatekelezwa kisiasa kwa lengo la kutafuta umaarufu wa gharama ndogo miongoni mwa wapiga kura badala ya kujali ukweli uliothibitishwa kisayansi (ki-utafiti).
Kuna ukweli kwamba sera za elimu Tanzania hazina uhusiano na yale ambayo watafiti wameyathibitisha kupitia tafiti mbalimbali. Mfano ni sera ya kuifanya elimu ya msingi kuwa bure (kufutwa kwa ada ya UPE). Uamuzi huo ulipingana na tafiti zilizoonesha kwamba baadhi ya wazazi wa kitanzania (wengi) walikuwa na uwezo wa kulipa ada hiyo na wala ada ya UPE haikuwa miongoni mwa sababu kuu za watoto wa kitanzania kutoandikishwa au kutoendelea na shule. Sababu kuu za wazazi wa kitanzania kutowapeleka shule watoto wao ni pamoja na mchango wa watoto hao katika pato la familia kupitia kazi wanazotumikishwa kinyume cha sheria wasipoenda shule. Sababu nyingine ni utamaduni uliojengeka miongoni mwa jamii kadhaa za kitanzania kwamba mtoto wa kike hana haja ya kusoma shule .
Aidha inashangaza kuona kwamba wanasiasa wanaohubiri kujitegemea na kuchangia gharama za huduma za jamii wanachukua uamuzi wa kufuta kabisa mchango huo wa wazazi na kuwatangazia watanzania kwamba elimu ya msingi ni bure (japo elimu toka enzi ya mkoloni haijawahi kuwa bure). Wakati huo huo wanalibebesha taifa mzigo wa deni la dola za kimarekani milioni 150 (sawa na fedha za kitanzania bilioni 202,na milioni500) kutoka Benki ya Dunia kwa ajili mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM). Yamkini, si vibaya kukopa kwa ajili ya maendeleo. Lakini Wataalam wa masuala ya sera, wanaonya kuwa, ili sera ifanikiwe, pamoja na mambo mengine isiwe na shinikizo au mkono mkubwa wa kutoka nje ya nchi.
Mjadala huu utusaiidie kujiuliza, hivi Benki ya Dunia imetupatia mkopo huo ili tujitegemee au tuzidi kuwa tegemezi. Kama mkopo huu, tutaulipa kwa kodi zetu, tunashindwaje leo kutumia kodi hizo hizo maalum kugharamia elimu.
Kwa ujumla, Sera za elimu nchini petu zimeghubikwa na tatizo la kukosa uhusiano kati ya ufafanuzi wa sera kisiasa na utekelezaji wa sera hizo. Kumekuwa na maelezo ya kinadharia na ya kialinacha ambayo hayatekelezeki. Mathalani Falsafa ya elimu ya kujitegemea ilitafsiriwa na kuekelezwa visivyo kisera na kisha Watanzania wakabakia kutupiana lawama kwa kutokuwa makini.
Viongozi wetu wamekuwa na tabia ya kuibua sera mpya na kuanza kuzitekeleza bila utafiti wa kutosha. Matokeo ya tabia hii yamekuwa ni kufuta sera hii leo kisha kuirejesha kesho bila tahadhari wala maelezo ya kuridhisha. Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995 inaonekana kula matapishi maana imerejea kanuni ya zamani ya wazazi kulipa karo na kuruhusu watu binafsi kuendesha shule.
Huduma za Maktaba
Sera katika kipengele cha 6.5 inataja matatizo ya Bodi ya Huduma za Maktaba nchini. Matatizo hayo ni pamoja na ukosefu wa vitabu vinavyoendana na wakati, uhaba wa wakhutubi wenye ujuzi, maktaba kukosa mawasiliano na taasisi mbalimbali, na watanzania kutokuwa na utamaduni wa kujisomea. Katika kipengele 6.5.1 badala ya sera kutaja ufumbuzi wa matatizo hayo inashikilia tu msimamo kwamba Bodi ya Maktaba itaendelea na huduma zake.
Elimu maalum kwa wenye vipaji
Ama kuhusu suala la watoto wenye vipaji linalotajwa na sera katika kipengele namba 3.2.15, utekelazaji wake ni dhaifu mno kwani hadi sasa kigezo pekee kinachotumiwa kuamua mtoto mwenye kipaji ni alama alizopata kwenye mtihani wa mwisho. Kimsingi kuwa mwenye kipaji ni pamoja kudhihirisha uwezo usio wa kawaida kiakili, katika ubunifu, uongozi wa wengine, usanii na kipaji cha michezo.Je, wote wenye vipaji hivi Tanzania tumewatambua na kuwaweka katika shule maalum?
Aidha shule wanazopelekwa watoto hao hazina chochote cha umaalum cha kuvilea vipaji ipasavyo. Ni afadhali tu wangesoma katika shule za kawaida ili kuheshimu kanuni ya kusoma pamoja (inclusion) na kujiepusha na kiini macho cha shule maalum. Shule maalum za wenye vipaji zinaweza zisiwe muafaka kwa Tanzania kutokana na hali yetu kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kama kweli tuko makini na suala hili, sera isingetaja tu kwamba kutakuwa na chombo cha kuwatambua na kuwaendeleza watoto wenye vipaji, bali ingezitaka shule zote nchini kuwa na utaratibu wa kitaalam wa kuwatambua. Kwa jinsi hii, kila shule ingelazimika kutumia vigezo vya kitaaluma vya utambuzi wa vipaji.
Falsafa ya elimu ya kujitegemea
Sera ya elimu pamoja na mambo mengine, imegusia falsafa ya elimu ya kujitegemea na suala la maadili katika elimu (values). Yafaa pia katika mjadala huu tutafakari mambo hayo pia. Sera inaitaja falsafa hii katika utangulizi, ukurasa wa ii na ix sera inapozungumzia Elimu na Maendeleo na inataja wazi kuwa elimu ya kujitegemea itaendelea kuwa ndio falsafa yetu ya elimu.
Tunafahamu kwamba elimu ya kujitegemea ni falsafa ilivyoasisiwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, miaka ya mwanzoni ya uhuru wa taifa letu. Falsafa hii iliweza kuendana na malengo ya elimu ya wakati wa kujenga ujamaa na kujitegemea hapa nchini. Kulingana na wakati tulio nao, mengi katika falsafa hiyo yanaonekana kusukumwa kando kwa sababu hasa za uchumi wa dunia ya leo, na si watanzania wote leo hii wanaamini bado katika ujamaa. Hivyo, tunahitaji ama kuiboresha falsafa hii au ipatikane falsafa mbadala kabisa ambayo inaweza kuendana vema na zama hizi za utandawazi, soko huria, ushindani na hata siasa za vyama vingi.
Falsafa ya elimu ya kujitegemea ililenga kutatua matatizo yaliyosababishwa na elimu ya kikoloni. Ililenga pia kujenga jamii ya kitanzania na wasomi wanaoweza kulitumikia taifa hili kulingana na mazingira yetu ya ndani ya miaka ya mwanzo ya kujitawala. Wahitimu wa elimu walitarajiwa wapende kazi za mikono hususan katika sekta ya kilimo, ambayo inadaiwa kuwa ndio uti wa mgongo wa taifa.
Changamoto tuliyonayo sasa ni kwamba, kama tuliweza kuondoa mapungufu katika elimu ya mkoloni, tusione aibu kuondoa mapungufu ya elimu ya kujitegemea labda kama hatuyaoni. Vile vile tujiulize tena, kwa sasa tunataka kujenga jamii ya namna gani. Elimu ya kujitegemea ni mtoto wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Kadri muda unavyokwenda ndivyo wahubiri wa itikadi hiyo hapa nchini wanavyoiweka kando, hivyo wanayaweka kando pia malengo ya elimu ya kujitegemea.
Tujiulize kama matumizi ya jembe au zana za kale za uzalishaji wa mahitaji ya binadamu tuliyonoyo hadi leo yalikuwa ndio tafsiri sahihi cha falsafa yenyewe ya kujitegemea hasa ilipozungumzia suala la watanzania kupenda kazi za mikono. Tujiulize sasa kama taifa lisilo na tekinolojia, uwezo wala mwelekeo wa kuzalisha mahitaji yake lenyewe litafikia malengo ya dira ya 2025. Ni dhahiri tunahitaji tekinolojia ya kisasa katika uzalishaji wa kila sekta na ni dhahiri pia kuwa uchumi za taifa utaimarika tu pale tutakapojijengea uwezo wetu wenyewe wa kuzalisha mahitaji yetu badala ya kutegemea kuagiza mahitaji hayo nchi za nje.
Ingawa EK ilikuwa na malengo mazuri haionekani kama ilifanikiwa. EK ilitakiwa iboreshe uchumi wa vijijini na iwatayarishe wasomi kwa ajili ya maisha ya kijijini. Lakini leo hii miaka 39 tokea EK ianzishwe, vijiji vingi Tanzania vimebakia kuwa mahali pasipofaa kukaa si kwa wasomi wa elimu ya juu tu bali hata wahitimu wa elimu ya msingi wanazidi kupakimbia na kugeuka wamachinga mijini. EK imeshindwa kuinua maisha ya vijijini.
Kwa ujumla malengo ya EK yalipangwa vizuri sana kinadharia, lakini ilivyokuja kwenye utendaji wahusika ni kama vile hawakujua wafanye nini. Kwa wengi EK ilimaanisha tu kuwa na miradi ya bustani shuleni, mifugo na duka la shule hata kama wanafunzi hawajifunzi chochote kutokana na miradi hiyo. Ndio maana leo hii tusishangae miradi hiyo uongozi wa shule kadhaa nchini umeamua kuiendesha kwa mtindo wa ubinafsishaji.
Aidha EK hapa nchini imekumbwa na jeraha jingine la mauti tokea kuanzishwa kwa shule binafsi za msingi, sekondari na vyuo. EK iliweza kuzungumzika vizuri wakati serikali inahodhi umiliki wa shule, ni jinsi gani utamshawishi mmiliki wa English Medium Academy (ambako ni kimbilio la wenye uwezo wa kifedha) kwamba EK ifundishwe kwa jembe la mkono bustanini na si kompyuta kwenye mahabara.
Wakati umefika ambao hatuna budi kuwa na falsafa ya elimu ambayo inalenga kuwafanya wahitimu wetu wa shule wawe raia wanaomudu kuzikabili changamoto za ulimwengu wa sasa. Enzi hizi, tunapozungumzia na kuingia katika ushirikiano wa kiuchumi na nchi mbalimbali, ambamo nguvu kazi imekuwa huru kuhama toka nchi moja hadi nyingine.wahitimu wetu sharti wawe wameandaliwa kumudu ushindani huo katika soko la kimataifa la ajira ili wasije kufanywa vibarua ndani ya nchi yao, na wengine waweze kwenda nchi jirani na kukubalika kwa uwezo wao. Mathalani watanzania tunahitaji kufanana na wenzetu wa Kenya na Uganda katika utaalamu na stadi tunazozimudu, tunapoelekea kwenye shirikisho la Afrika Mashariki.
Ikumbukwe kwamba, falsafa ya elimu ndio inatakiwa iwe chimbuko la nini kiwe katika mitaala ya elimu na mafunzo. Falsafa hiyo pia ndio hutumika kutathmini na kukosoa malengo ya elimu Hivyo iwapo kilichomo katika mitaala yetu hakiendeni na falsafa tunayoiamini basi mitaala hiyo ni potofu. Na kama mitaala inaendana na mahitaji ya wakati wa sasa na wa baadaye ila inatofautiana na falsafa, hatuwezi kusema tuko makini.
Maadili katika Elimu
Kipengele 2.3.2 cha sera kinataja haja ya elimu kuinua maadili na utamaduni wetu. Tatizo la maadili katika elimu lina uhusiano wa karibu na tatizo la falsafa. Kwa jinsi itikadi ya ujamaa ilivyoamua falsafa ya elimu, ndivyo itikadi hiyo ilivyoelekeza yapi yawe maadili ya elimu. Wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, maadili ya elimu yalikuwa ya kijamaa, ndio maana watoto walikariri mashuleni pamoja na mambo mengine kwamba ujamaa na kujitegemea ndio njia ya pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru. Aidha watoto walikariri ahadi za mwana TANU, sijui kwa nini watoto hao ukubwani walio wengi wamesaliti yote hayo. Leo hii ujamaa tunao tu kwenye Katiba ya Jamuhuri ya muungano lakini hata Baba wa Taifa alifariki akijua umekwisha toweshwa nchini.
Tatizo la maadili linajitokeza ifuatavyo;
Kwamba chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ambako karibu kila wafuasi wa chama fulani wana itikadi yao, ni dhahiri haieleweki ni maadili gani ambayo tumeyaweka wazi katika mitaala ili yaendane na mfumo wa kisiasa uliopo.
Kwamba japo kinachoendelea katika uchumi wetu ni cha itikadi za kiliberali bado sera ya elimu haioneshi au iko kimya iwapo maadili ya kiliberali yanapaswa kuwemo katika mitaala au la. Kuna tofauti kubwa kati ya hali halisi kiuchumi na maadili yafundishwayo mashuleni hivi leo.
Kwamba walimu wetu, wako katika mkanganyiko wa ama wafundishe ujamaa na maadili yake au wajiunge na upepo wa sasa wawafundishe watoto mitizamo ya kiliberali. Mjadala utusaidie tujue moja.
Tuzingatie kwamba uliberali umeyafungulia milango maadili ya kigeni (kizungu) kuingia nchini kwa kasi (mengine mazuri mengine mabaya) na kuwa maadili hayo yamewateka vijana wetu na jamii kwa ujumla. Maadili hayo tunaona yakiambatana na utumiaji wa madawa ya kulevya, ushoga, uzuraraji, kuzungumzia mambo ya kujamiiana hadharani hata mbele ya watoto, itikadi kali na mmomonyoko wa maadili kwa ujumla. Hivyo sera haitaji/haibainishi njia sahihi za kutumika nchini kwa ajili ya kufundisha maadili mema na utamaduni wetu mashuleni, tunaishia kuiga tu wanachofanya wenzetu ambao jamii zao zimeharibika zaidi kimaadili bila kujiuliza wanakosea wapi (wapo wanaoamini kwamba mmomonyoko wa maadili ni kwa sababu kadhaa ikiwemo kuwatesa walimu wetu kimaslahi na kupiga marufuku viboko mashuleni)
Eneo jingine linaloifanya sera hii istahili kujadiliwa au kutathminiwa, ni kusheheni kwake takwimu na taarifa za zamani ambazo nyingine zimepitwa na wakati. Ni jambo muafaka kwamba sera hii iandikwe upya (revised edition) na mjadala huu utupeleke hapo.
MAPENDEKEZO
Kwa kuwa matatizo ya elimu nchini ni lukuki, majadiliano yetu yaangalie si yale tu yatajwayo katika mada hii bali elimu kwa ujumla wake, ili hatima ya mjadala iwe kuibuliwa kwa sera ya elimu na mafunzo yenye ubora wa kipekee, tunayoikubali wote tena inayotekelezeka.
Tutumie fursa ya mjadala huu kuwataka watekelezaji katika sekta ya Elimu wazingatie dira yetu inayobainishwa katika sera zilizo rasmi na iwe mwiko kuchukua maamuzi yanayoliondoa taifa katika mwelekeo unaokubalika na ulio sahihi.
Vile vile tuzingatie katika kujadili kwetu kwamba ni kazi bure kuongelea elimu bora bila mitaala bora tena inayozingatia wakati tulionao na ujao.
Mjadala huu pia, utupeleke mahali ambapo tunaweza kusema kumdhalilisha mwalimu na taaluma ya ualimu sasa basi. Mathalani, tuwe na sheria inayouhesabu ucheleweshaji wa mishahara na maslahi mengine ya walimu kwamba ni udhalilishaji, ni kunyume cha haki za binadamu na ni kosa la jinai (kumtesa mtu). Pia tuwe na utaratibu unaompa heshima ya pekee mwalimu. Kama tunadiriki kuwaambia walimu kila mara kwamba kazi yao ni ya wito, basi tusione taabu kuwapa heshima ileile ya kijamii wanayopewa watumishi wengine wa wito, matharani viongozi na watumishi wa dini.
Kuhusu suala la ukosefu wa nyumba za walimu, iwe marufuku kufungua shule mpya ambayo haina nyumba za walimu, nyumba zenye hadhi tena kwa idadi inayoendana na ikama itakiwayo. Aidha iwe haki ya mwalimu kupewa nyumba ya kuishi na mwajiri (entitled) Na mwalimu asipelekwe katika shule fulani bila mwajiri kumhakikishia nyumba ya kuishi na familia yake.
Katika kumwendeleza mwalimu kitaaluma, uwe wajibu wa mwajiri (serikali au binafsi) ndani ya mkataba wa kazi kumwendeleza mwalimu kila baada ya muda uliotajwa wazi, kupitia njia ya mafunzo kazini na nyinginezo.
Kuhusiana na tatizo linalojitokeza la matumizi mabaya ya raslimali watu, mjadala wa kitaifa utusaidie tuwapange walimu wetu (askari wetu dhidi ya ujinga) katika mstari wanapostahili kuwa.
Vile vile tujadiliane tupate ufumbuzi ambao ungefaa kwa matatizo ya makitaba na wananchi kutopenda kujisomea. Suluhu yaweza kuwa ni pamoja na kuwafundisha walimu hata wa shule za msingi ukhutubi ili waboreshe huduma za maktaba kwa wanafunzi mashuleni. Hili liendane pamoja na kuzitaka mamlaka husika kuhakikisha kila shule ina maktaba.
Aidha ingefaa maktaba za umma ziwe wazi siku na saa ambazo watu hawako katika shughuli za kujipatia riziki, maktaba zitafaa sana kama zitakuwa kama sehemu ya watu kuburudisha akili zao baada ya uchovu wa kazi yaani ziwe na vivutio vya burudani, na ziwe wazi siku za mapumziko na watanzania wafahamishwe hilo.
Falsafa ya elimu tunayoihitaji sasa ni ile itakayomwezesha mtanzania kuwaza kama raia wa ulimwengu mzima wakati huohuo akiweza kutenda kazi kulingana na mazingira ya nyumbani. Falsafa ya elimu imwezeshayo mtu kumudu maisha wakati wote mahali popote katika uso wa dunia yetu
Ingefaa tuwe na sera ya elimu inayotaja bayana maadili ya kufundishwa kupitia elimu. Na isiishie tu kuyataja bali itaje na njia za kuyafundisha. Wataalamu wanataja njia tano za ufundishaji maadili ambazo tunaweza kuziingiza katika sera yetu na kuwafundisha walimu wetu kuzitumia (inculcation-kufunda, moral development-kukuza mwenendo, analysis-kuchambua, value clarification-kufafanua maadili na action learning-mafunzo vitendo)
Kwa maoni yangu, kupitia masomo ya uraia, michezo, muziki na sanaa mbalimbali akili za watoto wetu tuzijengee maadili ya kidemokrasia, uaminifu kwa matendo, mawazo na maneno, uzalendo, uwajibikaji, utawala bora wa mali binafsi na za umma, uchapakazi, utunzaji mazingira, kujiamini, kujisimamia, kusaidiana, heshima, kujali, haki, usawa,uvumilivu,ustaarabu na mengine. Wanafunzi wafundwe maadili haya si katika nadharia tu kama ilivyozoeleka bali waingizwe katika vitendo halisi na waone mfano bora kutoka kwa viongozi na jamii yote inayowazunguka.
Inatubidi tambue umuhimu wa kupanua elimu ya lazima kwa kila mtanzania iwe si chini ya kidato cha nne ili kulipatia taifa watu wenye ujuzi na uwezo kushiriki barabara katika miradi ya kuondoa umaskini na maradhi na wenye uwezo wa kuhoji na kuwajibisha viongozi. Pasipo kupanua elimu ya lazima (ya msingi) tutajikuta hatuna uwezo wa kupanua elimu ya juu na hivyo hatutapata nguvu kazi ya kutosha yenye taaluma za kati na za juu kitekinolojia. Vivyo hivyo, ikiwa tunasita kuwekeza ipasavyo katika elimu ya juu kwa kuwapa mikopo wahitimu wote wenye sifa za kudahiliwa, maendeleo ya taifa letu yatabaki kuwa ndoto ya mchana. Hatuna budi kusahihisha makosa yote tuliyoyafanya katika sekta ya elimu, vinginevyo tusilie tukiona kuwa soko la ajira la Jumuiya ya Afrika Mashariki linatawaliwa na Wakenya, Waganda, Warundi na Wanyarwanda walioamua kuelewa nini maana ya kuwapa elimu bora raia wote, tusilalamike iwapo tutalazimika kuambulia kazi za kilalahoi tu katika shirikisho la Afrika Mashariki lijalo.
Zaidi ya yote tutumie akili zetu na tafiti za wataalamu wetu kutafuta na kutumia ipasavyo vyanzo vyote vya fedha vinavyowezekana kwa ajili ya kugharimia elimu. Vinginevyo mipango yetu itaendelea kupendeza kwenye karatasi na elimu bora itabaki njozi. Miongoni mwa vyanzo vinavyoweza kufaa ni fungu kubwa zaidi kutoka bajeti ya serikali, kodi maalum ya elimu, ushuru maalum matharani katika vinywaji vikali, michango ya kila mwezi ya makampuni au mashirika yanayozalisha faida kubwa na kadhalika,
HITIMISHO
Wakati umekwisha wa kuendelea kuwa mashuhuda wa kudidimia kwa sekta ya elimu nchini bila kufanya jitihada za maksudi tena madhubuti sote kwa pamoja kuliokoa taifa letu Tanzania.
Hatuna budi kutafuta haraka ufumbuzi wa matatizo yote ya elimu kama tunalitakia taifa letu mema. Tujadiliane kwa nia njema, tuitathmini sera yetu ya elimu kwa kina. Tuangalie wapi tunakosea, wapi tunafanikiwa, nini kinatukwamisha na nini tufanye. Hatimaye tuibuke na dira moja madhubuti itakayotuhakikishia kufika salama kwenye bandari ya maendeleo tunayoyatamani.
Inapatikana pia
www.georgekahangwa.blogspot.com