Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Rais Mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera leo Aprili 10 amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya vyama vya siasa na watendaji wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa vyama alivyokutana navyo ni CHADEMA kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti John Heche, aliyeongoza jopo la viongozi wa chama hicho.
Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, Mwanasheria Mkuu wa Chama Rugemeleza Nshala, Mwenyekiti wa Bazecha Taifa Susan Lyimo na rafiki wa Chadema Jenerali Twaha Ulimwengu.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho leo imesema, katika kikao hicho, Dk Chakwera amepokea taarifa ya msimamo wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
"Aidha, amepewa maelezo ya kina kuhusu matukio yaliyotokea kabla na baada ya tarehe 29 Oktoba, ikiwemo kukamatwa kwa Mwenyekiti wa chama, Mheshimiwa Tundu Lissu, pamoja na wimbi kubwa la utekaji, mauaji ya raia, na kuzuiwa kwa shughuli halali za kisiasa za chama.
"Vilevile, Dk Chakwera amepokea ombi rasmi kutoka CHADEMA la kuruhusiwa kwenda kumuona Mheshimiwa Tundu Lissu akiwa gerezani, ili kujionea hali halisi na kupata taarifa za moja kwa moja," imesema taarifa hiyo.
Mbali na CHADEMA, Dk Chakwera amekutana pia na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Ndugu Dorothy Semu katika ofisi ndogo za uwakilishi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.Katika kikao hicho, Semu aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa chama Zanzibar, Ndugu Ismail Jussa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Ndugu Isihaka Mchinjita pamoja na Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje, Ndugu Mwanaisha Mndeme.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na chama hicho leo, chama kimeeleza kuwa matukio ya Oktoba 29, 2025 yaliambatana na ghasia, vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, hali iliyodhoofisha imani ya wananchi katika mfumo wa kidemokrasia.
ACT Wazalendo imedai kuwa kulikuwa na dosari mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya matokeo ya kura, ukosefu wa uwazi katika takwimu za wapiga kura na kuzuiwa kwa mawakala wao kushiriki kikamilifu katika vituo vya kupigia kura. Pia imeeleza kuwa vyombo vya dola vilihusika katika vitendo vilivyokiuka haki za binadamu wakati na baada ya uchaguzi.
Chama hicho kimesisitiza kuwa hali ya kisiasa nchini imeathiriwa na kile ilichokiita “mazingira ya hofu na ukandamizaji,” kikidai kuwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kushiriki siasa umeendelea kudidimia.
Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imependekeza hatua kadhaa, ikiwemo kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, kuanzishwa kwa mchakato wa mageuzi ya uchaguzi na katiba, pamoja na kuwajibishwa kwa wote watakaobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Dk Chakwera pia alikutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Lazarus Chakwera jijini Dar Es Salaam Aprili 09, 2026.
Mjumbe Maalum huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo atakutana na wadau mbalimbali jijini Dar Es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
Wakati wa ziara hiyo ambayo itahimishwa Aprili 16, 2026. Mhe. Chakwera amepangiwa miadi ya kukutana na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na viongozi wastaafu.
Chakwera aliwasili nchini Aprili 08, 2026 na kupokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe na alianza ratiba yake kwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo Aprili 09, 2026 jijini Dar EsSalaam.