Dkt. Akwilapo atolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi

Dkt. Akwilapo atolea ufafanuzi malalamiko ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi

Wizara ya Ardhi

Govt Institution
Joined
May 14, 2024
Posts
306
Reaction score
165
Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ametolea ufafanuzi malalamiko yanayohusu migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, huku akisisitiza wananchi kuzingatia sheria na taratibu za umiliki na matumizi ya ardhi ili kuepuka migogoro na hasara zinazoweza kujitokeza.

Mhe. Dkt. Akwilapo amesema hayo Agosti 26, 2026, ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, alipokutana na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu kuvunjiwa maendelezo waliyoyafanya kwenye maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kumekuwa na malalamiko mengine yanayohusu matumizi na umiliki wa baadhi ya maeneo ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umebaini kuwa baadhi ya wananchi wanaowasilisha malalamiko hayo hawatoi taarifa sahihi kuhusu uhalisia wa masuala yao, huku wengine wakitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutafuta huruma ya jamii.

Akitoa mifano ya baadhi ya matukio hayo, Mhe. Dkt. Akwilapo ametaja tukio la Agosti 18, 2026, linalomhusisha Bi. Rahel Suda dhidi ya Bi. Adelaida Mkoko kuhusu umiliki wa Kiwanja Na. 42, Kitalu B, kilichopo Kikuyu Extension jijini Dodoma, ambapo Wizara tayari imeshatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo baada ya kupata maelezo ya kina.

“Maeneo mengine yenye malalamiko ni yale yanayohusu utekelezaji wa hatua za mamlaka zenye wajibu wa kisheria wa kusimamia hifadhi za umeme au reli katika maeneo ya Tegeta kwa Ndevu, Mavurunza na Kilungule, mkoani Dar es Salaam,” amesema Mhe. Dkt. Akwilapo.

Ameongeza kuwa Wizara inatambua umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kufikisha taarifa na malalamiko ya wananchi serikalini, lakini akabainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiitumia kutoa taarifa zisizo sahihi, licha ya kufahamu kuwa masuala yao tayari yameshughulikiwa kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama au hatua za kisheria zilizochukuliwa na Serikali.

“Napenda kutoa rai kwa wananchi kuzingatia taratibu za kisheria katika kupata ardhi na kufanya ujenzi mijini na vijijini ili kuepuka kupata hasara kutokana na kubomolewa kwa maendelezo yaliyofanyika kinyume cha sheria,” amesema Dkt. Akwilapo.

Migogoro ya ardhi ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kufuatilia malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na viongozi wake kufanya ziara katika maeneo yenye migogoro kujionea hali halisi na kutafuta ufumbuzi.

--------------mwisho------
 

Attachments

  • IMG-20260827-WA0041(1).jpg
    IMG-20260827-WA0041(1).jpg
    95.1 KB · Views: 10
Back
Top Bottom