UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Wakati mradi wa maji wa Shilingi bilioni 4, Kata ya Mkwajuni, Wilayani Songwe ukisubiriwa kwa hamu kubwa kuanza kufanya kazi, hofu ya kiafya inazidi kuongezeka miongoni mwa wananchi wa Kata hiyo.
Wananchi wanabainisha kuwa maji wanayolazimika kuyatumia hivi sasa kwa matumizi ya nyumbani si safi wala salama, jambo linaloweka maisha yao katika hatari kubwa ya kukumbwa na milipuko ya magonjwa hatari kama vile kipindupindu, homa ya matumbo (typhoid), na magonjwa ya kichocho.
Kama ilivyoelezwa hapo awali, maji hayo yanachotwa moja kwa moja kutoka kwenye makolongo ya asili ya Lulongo na Kalungo. Katika maeneo hayo, akina mama wanalazimika kufukua visima vifupi vya muda kwenye mchanga, huku wengine wakichota maji kwenye visima vilivyochimbwa kienyeji ambavyo vingi havijafunikwa wala kulindwa dhidi ya uchafuzi. Hali hii inafanya vyanzo hivyo kuwa wazi kwa vumbi, majani yaliyooza, na kinyesi cha wanyama, jambo linalohatarisha zaidi usalama wa afya zao.
Viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Uhalisia wa Mkwajuni
Kulingana na viwango na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), vyanzo vya maji vinavyotumiwa na binadamu vinapaswa kulindwa kwa ukamilifu dhidi ya uchafuzi wowote unaotokana na wanyama au shughuli za kibinadamu. Hii ni hatua ya msingi kabisa katika kuzuia maambukizi ya vijidudu vya magonjwa kuelekea kwa watumiaji.
Hata hivyo, uhalisia uliopo Mkwajuni unakinzana kabisa na miongozo hii. Benedicto Kalolo, mkazi wa Kitongoji cha Kikuyuni na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Kitongoji hicho, anafichua kuwa mnamo mwaka 2023, kata hiyo ilikumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa kipindupindu. Mlipuko huo uliathiri kaya nyingi na kusababisha taharuki kubwa katika wilaya nzima.
"Sisi mto huu mkubwa ambao tunautegemea ni mto huu wa Lulongo na Kalungo. Yale maji, pamoja na kwamba tunayatumia, si salama kabisa. Mwaka juzi hapa Kikuyuni, kipindupindu kilidumu karibu miezi minane. Kile kipindi cha kiangazi tulihaha sana sisi wananchi. Lakini pia mifugo inakufa; ng'ombe zaidi ya mia moja na kitu walikufa baada ya kunywa maji yaliyachafuliwa na kemikali za migodi ya dhahabu kule milimani." — Benedicto Kalolo.
Mwingiliano wa Uchimbaji Madini na Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji
Uchimbaji wa madini ya dhahabu mkoani Songwe umekuwa nguzo kuu ya uchumi, lakini umekuja na gharama kubwa ya mazingira.
Maelezo ya Benedicto Kalolo yanathibitisha ukiukwaji mkubwa wa Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019, kinachokataza mtu yeyote au shughuli yoyote kuchafua vyanzo vya maji kwa namna inayoweza kuhatarisha afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira.
Maji ya mvua yanaponyesha milimani, yanabeba mabaki ya sumu (kama vile zebaki na sianidi) yanayotumiwa na wachimbaji wadogo wa dhahabu na kuyatandaza kwenye mabonde ambako ndiko wananchi wanakochoa maji. Hali hii inafanya maji ya mito hiyo kuwa na rangi ya udongo na yenye ladha ya metali, jambo linalothibitisha uwepo wa sumu.
Elimu ya Afya na Matumizi ya Vidonge vya Water Guard
Kutokana na ukweli kwamba mradi wa bilioni 4 bado haujakamilika kikamilifu, Idara ya Afya ya Wilaya ya Songwe imelazimika kuchukua hatua za dharura za kutoa elimu ya afya kwa jamii.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Dr. Kevin Mwasha, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za haraka wanapotumia maji kutoka kwenye vyanzo hivyo visivyo salama ili kujilinda na vifo, amebainisha kuwa, kwa sasa, wananchi wanashauriwa kufanya mambo mawili makuu:
Chemsha Maji: Chemsha maji yote ya kunywa hadi yachemke kabisa ili kuua vijidudu vya magonjwa.
Vidonge vya Kusafisha Maji (Water Guard): Tumia kidonge kimoja cha Water Guard kwenye dumu la lita 20 la maji, na uyaache maji hayo yatulie kwa dakika 30 kabla ya kuanza kuyatumia.
"Kimsingi maji yanayopatikana huko yanatakiwa yachemshwe au wananchi watumie dawa ya Water Guard. Kidonge kimoja kinawekwa kwenye ndoo ya lita 20, baada ya nusu saa maji yanakuwa salama. Tumesambaza hivi vidonge kwenye maduka yote ya dawa muhimu na bei yake ni nafuu sana, vidonge 120 vinauzwa kwa Shilingi 1,000 tu, ili wananchi wamudu kujilinda na kipindupindu na magonjwa ya kuhara." anasema Dr. Kevin Mwasha.
Mbali na mapambano ya maji, mkoa wa Songwe na Wilaya ya Chunya kwa ujumla inakabiliwa na uharibifu wa misitu unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Katika hotuba yake iliyotolewa jijini Mbeya, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, ameweka wazi kuwa matumizi ya nishati mbadala ni sehemu ya mpango mkubwa wa kitaifa.
Mhandisi Zena ameshauri kuwa, ili wananchi waache kukata miti, ni lazima wafundishwe mbinu mbadala za usimamizi wa fedha zao za kila siku. Amependekeza kuwa, ikiwa mwananchi alikuwa na uwezo wa kununua mkaa wa Shilingi 1,000 au 2,000 kila siku, anaweza kubadili mtindo huo na kuweka fedha hizo kwenye kibubu maalumu cha akiba. Ndani ya mwezi mmoja, akiba hiyo itamsaidia kununua au kujaza mtungi wa gesi pindi unapoisha, na hivyo kumwondoa kabisa kwenye matumizi ya kuni.
Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna vikwazo vya kisaikolojia na kiuchumi vinavyowafanya wananchi waone gesi ni ya gharama kubwa, jambo linalohitaji elimu endelevu ili kuwatoa wananchi kwenye tabia ya sasa ya kuharibu mazingira.
Hitimisho
Kilio cha maji na uharibifu wa mazingira mkoani Songwe na Chunya ni changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Maji haina budi kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakamilika kwa wakati, na miundombinu hiyo inalindwa dhidi ya uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu. Kupitia upatikanaji wa maji safi na nishati mbadala, afya na ustawi wa wananchi unaweza kuimarishwa.
ANDIKO LA: Heneliko Malo
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS