Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,618
- 9,611
Waziri Mpango alitoa kauli hiyo juzi jijini hapa, wakati akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari kuhusu ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2019.
Dk Mpango alisema hivi karibuni wameibuka wahujumu uchumi, ambao wanaharibu na kuhatarisha uchumi wa nchi, si watu wazuri, lakini ingekuwa amri yake angetoa adhabu kubwa zaidi.
Alisema Wananchi wanapoona fedha bandia, wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa noti hizo. Aliwataka wananchi kuwa makini na kutambua alama za noti halali ili wajue kutofautisha na noti bandia.
Waziri Mpango alisema anawapongeza viongozi, watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) na vyombo vya usalama, taasisi na wananchi wazalendo kwa kutoa taarifa za kubaini noti na mtandao wa watengeneza noti hizo.
Alisema serikali itaendelea kuwafuatilia kwa karibu wale wote wanaojihusisha na uhujumu uchumi huo ambao ni hatati kwa maendeleo ya nchi.
Dk Mpango alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Anange Saimon kwa kuisaidia serikali kunasa mtandao wa utengenezaji na usambazaji fedha bandia.
Waziri Mpango alionya mitandao ya simu Tigopesa, Halo-pesa, M-Pesa, TPesa, Airtel Money na Easy Pesa, ambayo inatumia miamala mbalimbali kupokea na kutoa pesa kwa wananchi, kuwa makini na fedha bandia kutumika, hasa nyakati za usiku.
Dk Mpango alisema wenye mitandao hiyo, wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu wanaotengeneza na kusambaza fedha bandia, ili watiwe nguvuni na kupata cha moto wa volkano.
Alisema serikali haitakuwa na huruma, kwa mtu yeyote atakayeshikwa na fedha bandia, kwani atahesabika ni mhujumu uchumi, na itaendelea kuwasaka na kuwakamata.
Alisema serikali itawachukulia hatua kali. kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 1984.
Dk Mpango aliiagiza BoT kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, kutambua na kujua alama mbalimbali za fedha halali ili wasije kupewa fedha haramu bila kujua. Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Florens Luoga alisema benki hiyo imejipanga kudhibiti uingizaji noti bandia katika benki na kwenye mzunguko wa fedha nchini.
Profesa Luoga alisema inatumia watalaamu kubaini fedha bandia, kabla hazijaingia katika mzunguko au kwenye benki.
Profesa Luoga alisema benki hiyo, imeandaa utaratibu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kanda mbalimbali nchini ili waelewe alama muhimu kwenye noti halali.
Habari Leo