Mwanamwana
Platinum Member
- Aug 1, 2011
- 9,604
- 22,722
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetuma onyo kali kwa waliokuwa wanachama wao, Saidi Issa Mohamed na Ahmed Rashid, kikitaka wajiandae kukilipa chama hicho mamilioni ya fedha kama fidia ya hasara waliyosababisha kufuatia mfululizo wa kesi wanazofungua mahakamani.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Juni 15, 2026, na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala, akizungumza na waandishi wa habari kwenye viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, ambapo shauri jipya lililofunguliwa na wawili hao dhidi ya Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama hicho lilitajwa.
-----Namnukuu Mwanasheria mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala
Leo tarehe 15 ya mwezi huu wa sita mwaka 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, tulikuwa na kesi ya Said Issa Mohamed na mwenzake mmoja, Hamed Rashid, pamoja dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Ikiwa ni kesi ambayo ni baada ya ile ya kwanza ya 83/23 mwaka 2025 iliyokuwa kwa Jaji Mwanga na baadae kuhamishiwa kwa Jaji Ngonyani, kwa hiyo imefukuzwa au imeondolewa.
Sasa, hawa Said Issa na mwenzake wameamua tena kurudi mahakamani, wamewasilisha maombi yao. Hati yao ya mashtaka iliwasilishwa kwetu sisi tarehe 11 mwezi wa sita mwaka 2025. Na kwa kuwa tuna siku 21 za kuweza kuwajibu, tumeweza kuitaarifu mahakama kwamba tuko ndani ya muda ule wa kuweza kuwajibu.
Na majibu yetu tutayawasilisha sisi tarehe 1 mwezi wa 7 mwaka 2026, na ndani mambo mengi yataweza kuwekwa wazi. Said Issa Mohamed na mwenzake Ahmed Rashid nasema tu ujumbe ambao nilionao kwenu ni kwamba, 'mwana kulitafuta, mwana kulipata'.
Ile, ile huruma ambayo tulikuwa nayo, kama tulikuwa nayo, katika kesi iliyopita, safari hii haitakuwepo. Mjiandae kukilipa Chama cha Demokrasia na Maendeleo fedha nyingi sana.
Madai yao ni kama ile kesi ya kwanza kwa msingi tu, ambayo hayupo hapa sasa ni Mama Maulida Anna Komu ambaye yeye ametangulia mbele ya haki.
Wao wanadai kwamba kuna ubaguzi katika chama chetu, kwamba hatuna, hatujajenga ofisi Zanzibar, kwamba ofisi ziko tu Bara, na kwa hiyo Zanzibar inabaguliwa. Ajira kwa wafanyakazi kule Zanzibar kunabaguliwa.
Kwa hiyo, safari hii wamekuja kusema kwamba madai yao yameanza mwaka 2021 na mpaka mwaka 2024. Tumeyaona ni yale yale.
Lakini na sisi mnafahamu hasara tuliyoipata ndugu zangu. Tumekaa chama kimefungiwa kwa siku 309, magari yameharibika, ofisi zimeharibika, wafanyakazi wengi wamepoteza ajira zao kwa sababu ya hawa watu.
Kwa hiyo, tutawasaidia kuweza kujua maana ya mtu ambaye anakuwa kidomi-domi ni kitu gani ambacho atakipata.
Kwamba sasa huwezi ukasababisha, ukasababishia chama hiki hasara kubwa alafu tukakuacha hivi hivi. Kuna fedha nyingi sana ambazo tumezikosa, tumekosa ruzuku kutokana na zuio lao, tumekosa fedha ambazo ufadhili ambao tulikuwa tumepewa, fedha zimebidi kurudishwa nje kwa wale wafadhili wetu.
Tutaisaidia mahakama kuweza kujua hasara ambayo hawa watu wametusababishia, na wao tutawaomba waweze kutulipa. Na wao tunataka kujua anwani yao hapa Dar es Salaam ni ipi, kuweza kupambana vizuri.