Imetayarishwa na Màgidd Mjengwa
Nyumba Aliyoishi RC Wa Iringa Dr Kleruu Inavyoonekana Hii Leo..
Ndugu zangu,
Hii ni nyumba ama iliyokuwa Ikulu Ndogo alikoishi RC wa Iringa Dr Kleruu. Aliondoka asubuhi kutoka nyumbani kwake Jumapili ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Dr. Kleruu hakurudi tena. Aliuawa kwa kupigwa risasi na Mkulima Mwamwindi.
Picha hiyo niliipiga mwaka jana. Nilipata nafasi ya kuingia ndani ya nyumba hiyo ambayo, baada ya kuawa kwa Dr Kleruu, hakuna RC mwingine aliyeingia humo. RC aliyechukua nafasi ya Dr Kleruu aliitwa Mohammed Kissoky. Wakati Dr Kleruu alikuwa na Phd, inasemwa Kada wa TANU Mohammed Kissoky alipata tabu hata kwenye kuandika.
Maswali: Kwanini Julius Nyerere alimteua Mohammed Kissoky kuwa RC Iringa? Nini ilikuwa tofauti kwenye leadership style kati ya RC Dr. Kleruu na RC Mohammed Kissoky? Je, Wana- Iringa walimpokeaje RC Kissoky?
Maswali haya na mengine yatajibiwa kwenye simulizi hii ya kitafiti inayotafuta jibu la swali la msingi, la Kwanini Mkulima Mwamwindi Alimpiga Risasi RC Dr Kleruu?
Ndugu zangu,
NIKO mgahawa wa Neema Craft mjini Iringa. Ni mwaka 2011. Mzee David Butinini na mimi tumepanga tukutane mahali hapa kwa chakula cha mchana.
Ni fursa pia ya kuendeleza mazungumzo yetu kuhusiana na alichokishuhudia Mzee Butinini miaka takribani 40 iliyopita. Inahusu tukio la mkulima Said Mwamwindi kumpiga risasi na kumuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya kutimu saa saba mchana tuliyoahidiana kukutana, namwona Mzee Butinini
( Pichani kulia) akipandisha ngazi za mgahawa ulio ghorofani. Pamoja na umri wake mkubwa, Mzee Butinini bado anaonekana kuwa na mwili wa kiuanamichezo .
Kwa wasiomjua, kwenye miaka ya sitini na wakati akiwa kwenye jeshi la Polisi, Mzee Butinini alipata pia kuchezea klabu ya soka ya Ushirika ya Mwanza wakati huo ikijulikana zaidi kama Mwanza-Coop. Huyu ndiye pia baba wa wanamichezo waliopata kuwa mahiri hapa nchini; marehemu Duncan Butinini kwenye soka na marehemu Jane Butinini kwenye mpira wa pete.
Namwuliza Mzee Butinini; Dk. Kleruu alipata kuwatamkia watu wa Iringa, kuwa kama hawamjui wawaulize watu wa Mtwara. Na wewe unasema ulikuwa naye Mtwara kabla hajahamishimiwa Iringa, je, Dk Kleruu uliyemfahamu wewe ni mtu wa namna gani?
“ Sikumfahamu sana Dk. Kleruu . Hakuwa rafiki yangu, bali. Kumfahamu kwangu ni kikazi zaidi. Nilikuwa namwona zaidi kikazi. Maana, kikazi mimi nilianzia Masasi, Mtwara. Nakumbuka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Kleruu alifika Masasi na kuzungumza na wananchi kwenye Mkutano wa hadhara.
Nilimwona pia Newala. Ni kweli, hata kule Mtwara Dk. Kleruu alionekana kuwa ni kiongozi mkali na mwenye kuhimiza mambo kwa nguvu.
Lakini pia ieleweke hapa, kuwa maeneo kama Newala na sehemu nyingine za Mtwara yalikuwa ni maeneo ya Vita. Itakumbukwa tulikuwa kwenye kuwasaidia ndugu zetu wa Msumbiji hususan Frelimo kwenye mapambano yao ya ukombozi kutoka kwenye utawala wa Wareno. Sasa labda hali kule Mtwara ilikuwa ni tofauti na ilimtaka mtu kama Dk. Kleruu.” Anasema Mzee Butinini.
Swali: Umesema kuwa Kleruu alipohamishimiwa Iringa nawe ukahamishiwa Iringa pia. Je, Dk. Kleruu uliyemwona Mtwara alikuwa na tofauti gani na Dk. Kleruu uliyekutana nae Iringa?
” Niliripoti Iringa kunako mwezi Machi mwaka ule wa 1971. Nami nilikuwa mgeni pia na mkoa huu wa Iringa. Nilikuwa askari kijana sana . Kule Mtwara Dk. Kleruu nilimwona kwenye kuhimiza wananchi kwenye masuala ya maendeleo lakini zaidi kwenye hali ya kijeshi ikiwamo mambo ya kuchimba mahandaki kutokana na hali ya kivita niliyoielezea hapo awali. Watu wa Mtwara walikuwa katika hali duni sana kimaendeleo. Kule Mtwara Dk. Kleruu hakukumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi, ni kama hakukuwa na upinzani kabisa.
Sasa nadhani hapa Iringa Dk. Kleruu alikutana na hali tofauti. Kwa mawazo yangu, nadhani Dk. Kleruu kama Mkuu wa Mkoa alipaswa kujiandaa na zaidi kujifunza juu ya mila na desturi za watu wa Iringa. Maana, watu wa Iringa ni watu wa Iringa. ” Anasema Mzee Butini, kisha anaendelea kusema..
”Kwa kweli Dk. Kleruu alikuwa kijana mdogo sana kwenye macho ya wazee wa mji huu wa Iringa. Na mji huu wa Iringa ulikuwa na kundi dogo la wakulima wazawa waliokuwa na kipato kikubwa. Ndio waliokuwa wakiijenga Iringa. Walikuwa wanamiliki mashamba makubwa sana. Walikuwa wanamiliki magari, malori na matrekta ya kulimia. Walianzisha pia Umoja wao. Mmoja wa wakulima hao ndiye huyu mkulima Said Mwamwindi.”
Swali: Mzee Butinini, umeaniambia huko nyuma kuwa mara baada ya kupigwa risasi na kuawa kwa Dk. Kleruu kuna wakulima hapa mjini Iringa waliokamatwa na kutiwa nguvuni. Je, inakuwaje wakulima waishi mjini?
” Unajua Maggid, Iringa ilikuwa tofauti sana. Wakulima wakubwa wa Iringa walikuwa na mashamba yao pale Isimani. Ni umbali wa kilomita arobaini hivi kutoka hapa. Sasa kule shamba walijenga nyumba za kufikia tu wakati wa msimu. Lakini makazi yao haswa ya kudumu ilikuwa hapa mjini. Kuna wakulima waliokwenda shamba asubuhi na usafiri wao , na jioni walirudi Iringa Mjini. Na kuna ambao mjini hapa walikuwa wamewekeza kwenye shughuli nyingine. Hawa watu walikuwa matajiri hata kwa kiwango cha wakati ule. Walikuwa ni watu wenye ushawishi pia. Walisikilizwa na watu, waliheshimiwa”
Swali: Mzee Butinini, Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na natarajia nitakutana nae kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili na ambaye alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Je, unafikiri ataniambia nini kuhusu kilichotokea?
” Bwana Maggid, Mzee Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. Amevalia pama lake kichwani. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue, kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya yaliyomkuta.
Maana, usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia, alikimbia makazi yake. Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadae akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi akakuta nyumba na kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Kuna mifano mingine ya watu kama mkulima Pesambili .” Anasema Mzee Butinini. Anavuta pumzi na kunywa juisi iliyokuwa mezani. Kisha anaendelea kusimulia..
UKIMWONA kwenye mitaa ya Iringa bado anatembea kwa hatua za kijeshi.
Ni David Butinini ( Pichani kulia).
David Butinini ni kachero mstaafu wa jeshi la polisi . Butinini alishuhudia kwa macho yake, siku Mkulima Said Mwamwindi alipofika kituo cha Polisi Iringa akiwa na mwili wa marehemu Dk. Kleruu kwenye gari aliloendesha.
Dk. Kleruu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeuawa na Mwamwindi kwa kupigwa risasi. David Butinini alikuwa pia mmoja wa mashahidi kwenye kesi ya mauaji iliyomkabili marehemu Mwamwindi.
Mzee David Butinini ni rafiki yangu wa muda mrefu. Jioni ya Jumapili moja, 2011 tunakutana Soko Kuu Iringa. Namuuliza juu ya kumbukumbu zake ya kilichotokea miaka 40 iliyopita.
Tunazungumza huku kwa pamoja tukikiangalia kituo cha polisi kilicho mbele yetu na ambapo David Butinini alifanya kazi kama Polisi miaka 40 iliyopita.
“Unasikia
maggid, nilishuhudia kwa macho yangu. Nilikuwa bado kijana enzi hizo. Nilikuwa mwanamichezo pia. Nilikuwa kwenye kikosi cha polisi cha mpira wa miguu. Nakumbuka ilikuwa jioni ya Jumapili ya Krismasi . Ni kwenye saa kumi na moja hivi.
Tulikuwa kama askari watatu tumevalia kiraia. Tulisimama pale nje ya kituo,” David Butinini ananieleza huku akionionyesha kwa mkono mahali hapo.
Kelele za makuli wabeba mizigo sokoni zinatufanya mimi na Mzee Butinini tusisikilazane vema. Wote tunajikuta tunasogea mbele kidogo na kusimama kando ya kibanda cha rafiki yangu Mwarami. Kijana anayeuza matunda Soko Kuu la Iringa.
“Unajua
maggid, Iringa ya wakati huo ilikuwa na watu wachache sana hapa katikati ya mji. Magari nayo yalikuwa ya kuhesabika. Jumapili ile ya Krismasi ilikuwa tulivu kupita kiasi. Ghafla tukasikia muungurumo wa motokaa kama tulivyokuwa tukiyaita magari enzi hizo.
“Mita mia tano mbele yetu tukaliona gari likitokea kwenye mtaa huu tuliosimama. Ni Mtaa wa Jamatini wengine wanauita Uhindini. Na kama ilivyo sasa, na enzi hizo pia barabara hii ni one way. Gari zinakwenda njia moja tu.
Zinashuka Kusini, hazipandi Kaskazini.
Swali: Je, ni wakati gani mlibaini kuwa ni gari la mkuu wa mkoa? Namwuliza Mzee Butinini.
“Kwanza kama askari tukabaki tukijiuliza; kwa nini dereva wa gari linalokuja anavunja taratibu za barabarani? Lakini, gari lilipokaribia tukabaini haraka kuwa ni Peugeot 404 rangi ya buluu. Ni gari la mkuu wa mkoa. Pembeni mlangoni lilikuwa na maandishi ’ RC-Iringa’. Sikumbuki namba za usajili wa gari lile.
Tukahisi kuwa mkuu wa mkoa amekuwa na dharura iliyomfanya avunje taratibu za barabarani,” Anasema Mzee Butinini anayeonekana kuwa na kumbukumbu nzuri ya tukio kana kwamba lilitokea juzi tu.
Swali: Unasema mlihisi mkuu wa mkoa alikuwa na dharura fulani. Je, gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo gani na dereva wa gari alifunga wapi breki ya kwanza? Mbele ya kituo? Nyuma ya kituo au kando ya kituo? Namuuliza Mzee Butinini.
“Kwa kweli hata mwendo haukuwa wa kasi sana. Ni wa kawaida tu. Dereva alipunguza mwendo baada ya kupita kituo cha polisi. Akakata kulia na kufunga breki kando ya kituo pale kwenye ule mnara wa kumbukumbu ya askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia,” anajibu.
Swali: Nini kikatokea?
“Tukamuona mtu ambaye hakuwa mkuu wa mkoa akifungua mlango na kuelekea mlango wa mapokezi. Alikuwa mtu mrefu, mnene kiasi na nakumbuka alikuwa na sharubu kiasi.”
Namkatisha Mzee Butinini kwa kumwuliza; kwa vile mlifahamu kuwa gari lilikuwa la mkuu wa mkoa na dereva hakuwa mkuu wa mkoa wala dereva wake, hamkuona kuwa ni jambo la kushangaza? Mlichukua hatua gani kabla dereva huyo hajafika ‘kaunta’ ya mapokezi pale polisi?
“Bwana Maggid, kila kitu kilikuwa cha kushangaza na kilikwenda haraka sana. Maana, yule Bwana Mwamwindi alikwenda moja kwa moja kaunta na pale alikutana na afande Mbete.
Nakumbuka afande Mbete alikuwa kijana wa Zanzibar. Mara tukamwona akitoka tena na kurudi kwenye gari. Akachukua bunduki na kuja nayo tena kaunta ya polisi. Alikwenda ‘kuisarenda’ kwa maana ya kuikabidhi,” anasema Mzee Butinini.
Swali: Je, nyinyi askari mliokuwa nje mlibaki hapo hapo na umesema mlivaa kiraia. Je, mlikuwa makachero?
“Kazi ya uaskari ni kazi ya ukachero pia, lakini kwamba tulivaa kiraia siku ile ni kwa vile ilikuwa Jumapili na tena siku ya Krisimas. Na kwa kweli hatukuwa na pa kwenda. Tulikuwa tukijiandaa kusafiri kwenda Moshi kesho yake. Nilikuwa kwenye kikosi cha mpira na tulikuwa na mashindano ya polisi kule Moshi.
Kwa sisi askari vijana kituo cha polisi ilikuwa ni kama kijiwe pia cha kukutania na kupiga stori tukiwa nje. Si unaona hata sasa hivi kuna askari vijana pale kituoni wamevalia kiraia wanapiga gumzo. Na sisi ilikuwa hivyo hivyo enzi zetu,” anasema Mzee Butinini huku akinionyesha askari wale vijana nje ya Kituo cha Polisi Iringa, siku ile ya Jumapili jioni.
Namrudisha tena Mzee Butunini kwenye reli ya mazungumzo kwa kumkumbushia swali langu;
Je, mlifanya nini baada ya kumwona Mwamwindi akiwapita na bunduki kwenda kukabidhi kituoni?
“Ahaa! Tuliingiwa na shauku ya kipolisi ya kutaka kwenda kuichunguza gari ya mkuu wa mkoa. Nakumbuka wakati Mwamwindi akiandikisha maelezo yake tuliizunguka gari ile ya mkuu wa mkoa kugagua kilicho ndani.
“Mimi nilikuwa wa kwanza kumtambua Mkuu wa Mkoa, Dk. Kleruu aliyekuwa amelazwa kiti cha nyuma akiwa amevalia overall nyeusi na miwani machoni. Nikasema jamani huyu ni RC Kleruu!” Mzee David anaelezea picha yake ya kwanza ya kifo cha Dk. Kleruu.
Swali: Kipi kikatokea baada ya hapo?
“Kwa kweli mambo yalikwenda haraka sana. Nakumbuka kulikuwa na pilikapilika nyingi pale kituoni. Mimi nilikuwa mtaalamu wa chumba cha mawasiliano tukiita signals. Taarifa zilianza kusambazwa kupitia chumba cha signals nilikofanyia kazi.
Ilikuwa mshikemshike. Tarumbeta la polisi likapulizwa. Askari wakakusanyika. Tukatangaziwa rasmi kifo cha mkuu wa mkoa. Kuna askari waliotumwa hospitalini kwenda kuchukua kitanda cha magurudumu cha kumlaza Dk. Kleruu na kumpeleka kumuhifadhi chumba cha maiti.
“Gari la mkuu wa mkoa likazungushwa na kuingizwa uani kwenye kituo cha polisi.
Wanamichezo tuliokuwa tukijiandaa na safari ya Moshi kesho yake tukaambiwa tuendelee na mipango ya safari. Tuliondoka asubuhi yake na basi la Relwe.
“Nyuma yetu tuliacha vumbi kubwa. Msako mkali wa kipolisi ulianza usiku ule ule wa kuamkia safari yetu ya Moshi. Iringa ilitikisika na ikaendelea kutisikika kwa wiki kadhaa.
“Kuna jamaa wa mjini na ambao walikuwa ni wakulima na walimchukia sana Dk. Kleruu. Baadhi nawakumbuka kwa majina. Jamaa hawa walipopata habari ya kifo cha Dk. Kleruu, basi, mmoja wao alinunua kreti za bia na kuanza kunywa na wenzake kusheherekea. Kati ya watu wa kwanza kunaswa kwenye msako wa kipolisi ni jamaa hawa.
Swali: Je, nini kilitokea kwenye majuma ya mshikemshike na kamatakamata?
Inaendelea kesho...
maggid. anajibu.
Swali: Nini kikatokea?
KWENYE mazungumzo yangu na Mzee David Butinini mtakumbuka nilimuuliza; Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na nilitarajia ningekutana naye kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili . Nilimwuliza Butinini, anadhani Mzee Pesambili angesema nini?
Naam, Pesambili alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Pesambili ana taarifa nyingi, ndio maana nikaona umuhimu wa kumtafuta.
Vinginevyo, taarifa za kamata kamata kwa baadhi ya wakulima wakubwa bado ziko kwenye kumbukumbu za baadhi ya wenyeji wa Iringa.
Kuna taarifa pia za baadhi ya wenyeji wa Iringa kuonyesha wazi hisia zao za kuchukukizwa na uongozi wa Dk. Kleruu na hivyo kuwa tayari kusimama upande wa mkulima Mwamwindi.
Aidha, kuna taarifa za kuwapo kwa wakulima waliochangishana fedha kwa madhumuni ya kukodi wakili kutoka Uingereza aje kumtetea Mwamwindi kwenye kesi hiyo.
Inasemekana vyombo vya usalama viliinasa orodha ya majina ya waliochangisha fedha na iliitumia orodha hiyo katika zoezi la kumkamata mmoja baada ya mwingine miongoni mwa wachangiaji.
Kwenye Jamhuri, kuawa kwa RC na raia lazima ardhi itikisike na vumbi litimke. Hali ilikuwa ni ya shaka sana.
Kuna wakati, wanafunzi wa Chuo cha Ualimu waliambiwa waandamane kupinga kitendo cha mauaji kilichofanywa na mkulima Mwamwindi. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho waliokuwepo wakati huo, ananiambia, kuwa mandamano hayo ilibidi wayatawanye wenyewe mara walipoingia mitaa ya mji wa Iringa, maana, walikutana na sura nyingi za wenyeji wa Iringa walioonyeshwa kukerwa na kitendo kile cha wanafunzi kuandamana.
” Tulihofia tusije tukapigwa mishale, tukatawanyika wenyewe kurudi chuoni,” ananiambia mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambacho baadaye kikaja kujulikana kama Chuo Cha Ualimu Cha Kleruu”.
Hakika, tukio lile la Mkuu wa Mkoa kupigwa risasi na Mkulima Mwamwindi halikutikisa Iringa tu, bali nchi nzima. Na kwenye maeneo mengine ya nchi hii watu wa kabila la Wahehe walihofiwa kwa kudhaniwa ni wenye hulka ya kuua kama Mwamwindi. Ikafika wakati, nje ya Iringa, mwanamume wa Kihehe akiingia kwenye baa, kuna wenyeji wa sehemu hizo waliotania kwa kusema; ameingia Mwamwindi!
Taarifa juu ya siku ile ya tukio la mauji zimekuwa zikiwachanganya wengi hadi hii leo. Simulizi hii ya kitafiti ni jaribio la kuusaka ukweli wa nini hasa kilitokea.
Mathalan, mbali ya Kachero mstaafu , David Butinini, utafiti wangu umenifikisha kwa kachero mwingine mstaafu aitwaye Mushi .
Kachero Mushi kwa sasa anaishi Moshi akiendesha kampuni ya ulinzi . Kwenye mazungumzo yetu ananiambia haya;
" Bwana Maggid, mimi nilikuwa kaunta siku ile ya tukio; Jumapili ya Krismasi, Desema 25, 1971. Bwana Butunini uliyeongea naye tulikuwa naye pale polisi Iringa. Siku ile ya tukio, asubuhi kabisa Dk. Kleruu alifika pale polisi baada ya kutoka kwa RPC Aboubakar.
Kleruu na mimi tulikuwa marafiki baada ya mimi kumsaidia kwenye upepelezi wa wizi uliotokea nyumbani kwake na nikafanikiwa kupata vitu vyake karibu vyote vilivyoibwa nyumbani kwake.
Ukweli ulikuwa wizi wa ajabu maana nyumba ya Mkuu wa Mkoa ilikuwa inalindwa,” ananiambia Mushi. Kisha anaendelea kunisimulia;
Tangu hapo mimi na RC Kleruu tukawa na uhusiano wa kirafiki. Nakumbuka siku ile ya tukio alipofika pale kituoni aliniaga kwa kuniambia anaenda Nyang’olo kwenye mambo ya kilimo. Kisha akanikaribisha jioni hiyo niende nyumbani kwake nikale Krismasi. Basi, baadaye tukajua kuwa afande RPC Aboubakar alimwambia ampe walinzi wa kwenda nao, lakini Kleruu alikataa.”
Basi, jioni ile ndio tukaona gari lake likingiia kituoni. Aliyeliendesha hakuwa Dk. Kleruu. Mimi ndiye niliyepokea bunduki aliyoikabidhi Mwamwindi. Ilikuwa ya midomo miwili. Hata gari la Mkuu wa Mkoa ndiye mimi niliyeliendesha kulizungusha kule uani polisi baada ya mwili wa marehemu kutolewa,” ananiambia Kachero mstaafu Mushi.
Maelezo haya yanathibitisha kitendawili kigumu juu ya kilichotokea siku hiyo.
Naamua kumtafuta mwanawe Mkulima Said Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi. Naye hafanyi kitendawili cha Desemba 25 kuwa rahisi. Nikiwa nyumbani kwake Mlandege, tukiwa wawili sebuleni, Amani Mwamwindi, mbali ya mambo mengine ananiambia;
” Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua kutokula Krismasi. Alivaa kofia yake ya pama. Kleruu akaendesha mwenyewe gari lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu.
Katika orodha yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Rashid Juma wa Nyang’olo. Nambari mbili ni marehemu baba yangu. Namba tatu simjui.
Swali: Kwanini baba yako, Said Mwamwindi hakuwa target namba moja wala tatu? Nini kilimtokea target namba moja, Rashid Juma? Na je, uliziona ishara gani za kilichotokea kabla ya kutokea kwa maana ya mahusiano ya Mkulima Mwamwindi na RC Dr Kleruu?
Itaendelea kesho.. anajibu.
Swali: Nini kikatokea?
TUNAENDELEA NA JAHAZI LETU
Nimekaa sebuleni na Bw. Amani Mwamwindi. Ni nyumbani kwake, Mlandege, Iringa, mwaka 2011.
Amani ni mwana wa Mkulima Saidi Mwamwindi . Amani amepata pia kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa.
Swali: Unayakumbuka yepi kwenye siku ya tukio, Jumapili, Desemba 25, 1971, siku ya Krismasi.
“Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia.
“Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa ni siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi ili kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo, mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka;
” Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae”.
Nikaongea na Mzee.
“Niliweza kuongea na Mzee na kupata picha ya kilichotokea. Niliondoka kurudi nyumbani. Habari zilishasambaa. Hali haikuwa nzuri. Mji wa Iringa ulitulia sana. Halafu ukaja mtikisiko mkubwa. Wazee wengi walioishi mjini na waliokuwa wakilima na Mzee kule Isimani walisombwa na vyombo vya usalama.”
Swali: Je, ni kina nani hao waliosombwa?
“Mzee kama Ibrahim Khalili, Mursali na wengine. Watu kama 30 hivi walisombwa na kupelekwa sehemu mbalimbali za nchi. Kuna waliopelekwa Mwanza, Shinyanga hata Zanzibar. Kwa namna fulani walitenganishwa katika sehemu hizo.”
Swali: Je, na wewe ulikumbwa na msukosuko huo?
“Ndio, hata mimi nilihojiwa ingawa niliachwa niendelee na kazi zangu. Kumbuka nilikuwa kijana wa miaka 21 tu, na siku ya tukio nilikuwa shambani kwangu Ifunda. Hapa nyumbani kwangu kulikuwa na askari wa FFU muda wote. Katika kuhojiwa kwangu maswali mengine yalikuwa hayana msingi.
Kwa mfano, niliulizwa;
Mzee alipokuja hapa kwako kutoka Isimani siku ya tukio alitaka kukwambia nini? Sasa, mimi hakunikuta nyumbani na hatukuongea, nitajuaje alichotaka kuniambia siku hiyo? Anaeleza Amani Mwamwindi, akionyesha kushangaa, hata hii leo.
Swali: Je, kwa wakati huo, wewe na familia yenu mlihisi kutengwa na jamii kutokana na kitendo alichofanya Mzee Mwamwindi?
Namwona Amani Mwamwindi akionyesha kuguswa sana na swali hili.
“Tulikuwa na wakati mgumu sana kama familia. Kibaya zaidi kwetu ilikuwa ni kuingia kwenye uhasama na ndugu wa jamaa ambao wazee wao walisombwa na vyombo vya usalama na kwenda kusikojulikana.
“Kwao waliamini kama isingekuwa Mzee wetu Mwamwindi kufanya tendo lile, basi, wazee wao wangebaki salama na kuendelea na shughuli zao za kilimo. Hivyo basi tulisakamwa na wengine ambao ni ndugu zetu.”
Swali: Mlifanyaje kuikabiili hali hiyo?
“Tulifikia uamuzi mimi niende Dodoma kwenye gereza alikokuwa Mzee Mwamwindi. Niende nikamjulishe baba juu ya hali iliyotokea huku nyumbani. Kwamba tuna uhasama na jamaa wa waliosombwa na vyombo vya dola.
Nilipata kibali cha DC hapa Iringa. Kibali cha kwenda kumwona Mzee kule Dodoma. Nilipofika Dodoma nikaonana naye. Tukazungumza. Nikamwambia shida ya nyumbani. Mzee alisikitika sana.
Akaniuliza; “Sasa tufanyeje?”. Nikamshauri aandike barua kwenda kwa Nyerere kumwomba atusaidie. Baba aliandika barua siku hiyo hiyo. Alimwandikia Nyerere kumwambia na kumhakikishia kuwa ni yeye Said Mwamwindi na si mtu mwingine yeyote aliyehusika na tendo alilofanya; kumpiga risasi na kumuua Kleruu.
Barua ile ilifika kwa Nyerere, na haukupita muda mrefu, wazee wale wakulima wa Isimani waliachiwa huru na kurudishwa Iringa. ”
Swali: Je, hali ya uhusiano na waliowachukia ilibadilika na kuwa njema baada ya wazee hao kurudi Iringa?
“Ndio, kabisa. Hali ikawa shwari.
Swali: Je, wazee wale wakulima wa Isimani walirudi na kuendelea na kazi zao za kilimo?
“Niseme kuwa walirudi Iringa wakiwa wameathirika kisaikolojia. Kuna ambao hawakutaka kabisa kurudi tena Isimani. Baadhi yao hawakuishi muda mrefu, walifariki. Sijui nini kiliwatokea.”
Swali: Je, unafikiri Iringa ingekuwaje kama tukio lile la siku ya Krismasi mwaka 1971 lisingetokea?
“Naamini kabisa, Iringa isingekuwa kama ilivyo sasa. Ingeendelea sana. Unajua kulikuwa hakuna mahala pengine katika nchi hii ambapo kulikuwa kunazalishwa mahindi kushinda Isimani.
“Mzee na wenzake walilima ekari nyingi sana. Naamini wangelima zaidi. Walianza kujijenga na hata waliunda ushirika wao. Tukio lile lilisimamisha kasi ya kilimo Isimani. Ni kama laana fulani vile, maana, tangu wakati ule mvua zimekuwa za taabu Isimani,” anasema Mzee Amani Mwamwindi.
Swali: Nilifika pale nyumbani kwenu. Mkungugu, Isimani, nikaona mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu, kwanza nilifikiri ni kumbukumbu ya Mwamwindi. Je, unajisikiaje kuona nyumbani kwenu kuna mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu na si ya baba yenu?
“Mimi naona ni sawa kabisa kwa mnara ule kuwa pale”. Ananijibu Mzee Amani Mwamwindi huku akionyesha kuchangamka. Anaendelea.
“Unajua hata Nyerere alipofika Isimani wakati fulani aliuliza; ” Hivi huu mnara ni wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu au Said Mwamwindi?” Nyerere alikuwa na maana yake.” Ananiambia Mzee Amani Mwamwindi. Kuna kitu anataka kufafanua, anasita. Namwacha aendelee kutafakari.
Kisha Amani Mwamwindi ananiuliza mimi swali gumu. Nabaini ni mara ya kwanza katika mazungumzo yetu ameamua kunirushia swali. Kwa mtazamo wangu ni swali la kifalsafa. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza;
“Bwana Mjengwa, mche unaochipua ardhini unahitaji kumwagiliwa maji ili uendelee kuchipua. Ukisimama vema unauacha ukue wenyewe. Na je, ukishakua na kukomaa unaufanyaje?”. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza huku akinitazama usoni.
Jibu langu kwa swali hili gumu linachochea moto wa mazungumzo yangu na Amani Mwamwindi. Ni pamoja pia na majibu ya maswali yangu ya msingi ikiwamo kwanini RC Dr Kleruu hakuanza na Said Mwamwindi siku ile ya Jumapili ya Krismasi, 1971.
Itaendelea kesho..
maggid.
Ndugu zangu,
Naendelea na mazungumzo yangu na Mzee Omary Nzowa anayeonekana pichani.
Swali: Je, unafikiri ni kwanini Dk. Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa Iringa?
” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza ubwana na kuwadharau wananchi.
Hakika, wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alipata tabu sana na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka ,Tanzania kama nchi ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.
”Nikwambie Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji.
Hawa hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia.
”Ni kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi. Naamini hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.
”Sisi tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu.
Ndiyo, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”
Swali: Unasema ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je, Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia?
”Huo ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika chama (TANU) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya uanachama wa TANU niliikatia Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba ikaja ya kwangu.
”Hata leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini , akafikia mpaka cheo cha ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa siku nyingi.
”Sasa nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi? Kwa kweli si mara moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake.
”Kwamba ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao. Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.
Swali: Turudi kwenye kilichotokea kijijini Mkungugu, siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya Dk.Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?
” Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku, basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango usirudi tena kitandani kwako!”
Swali: Hivi Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka?
” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana. Wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”.
Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Mzee Nzowa anapekua kabati lake huku akinismulia kisa cha vijana wa mjini Iringa wakati huo, waliotaka kumwonyesha Julius Nyerere, kuwa RC wake aliyemleta Iringa ana mambo ya hovyo.
Kwa vile RC Kleruu alikuwa pia ni mtu wa moja moto moja baridi, basi, jioni moja vijana wa mjini wakamtafutia RC mtego wa wasichana warembo wa mjini kunywa nae.
Kilichotokea , asubuhi RC hakuonekana Ikulu Ndogo. Katika tafuta tafuta ya RC, akaonekana asubuhi hiyo, chini ya gari lake, eneo la Mshindo, Iringa. Ananisimulia Mzee Omary Nzowa.
Mzee Nzowa ananiambia, jaribio hilo lilikuwa njia ya kumshinikiza Julius Nyerere amuondoe RC Dr Kleruu, mkoani kwao.
Narudi tena kwa Amani Mwamwindi anayenieleza alichoambiwa na baba yake Said Mwamwindi, mara ile Mkulima Said Mwamwindi alipotoka kwenye mkutano kati ya RC Dr Kleruu na wakulima uliofanyika ukumbi wa Welfare, Iringa.
Ni siku chache kabla ya tukio la Desemba 25, 1971.
Itaendelea kesho...