Nadharia Njama (Consipirancy Theory) ni hali ya kuamini kwamba kuna taasisi au watu fulani wanahusika kufanya jambo fulani la siri kwa faida yao. Lakini pia inawezekana ikawa ni hoja fikirishi ya kutungwa dhidi ya kitu fulani lakini hoja yenyewe isiwe ya kweli.
Siku moja miaka ya themanini (1987) kulitokea habari kwamba kwenye eneo fulani kule Buguruni kuna mtu kageuka nyoka. Zama zile kulikuwa hakuna mitandao ya kijamii wala teknolojia ya kusafirisha habari kama ilivyo hivi sasa, lakini habari hiyo ilisambaa kwenye mji wa Dar es salaam kwa kasi ya ajabu sana. Ghafla mji mzima ukashikwa na taharuki na kukawa na heka heka kubwa sana ya watu kuelekea Kituo cha Polisi Buguruni kwenda kumuona huyo mtu aliyegeuka kuwa nyoka.
Habari hii haikuwa mwisho wa habari kama hizo kutokea katika taifa letu. Na aghalabu habari zenyewe huja wakati kama Taifa huwa tunakuwa kwenye hali fulani inayohitaji mjadala wa Kitaifa. Kwa waliosoma kwenye shule za umma za Dar es salaam miaka ya sabini na themanini, watakumbuka vurumai za wanafunzi kutimua mbio kisa wameambiwa kuna Mumiani au majini yanakuja kwenye shule yao. Kuna wakati shule hadi zililazimika kufungwa kwa kuwa waalimu hawakuwa na amani kwenda shule kufundisha na wazazi nao ,walikuwa na hofu ya watoto wao kunyonywa damu ama na Majini au Mumiani.
Lakini hebu tujiulize, hivi ile habari ya "Rama mla watu" iliishaje? Ilikuwaje Taifa zima likasombwa kwenda Samunge kwa Babu? Nani anajiuliza dalali alikubalije kuziuza nyumba za Lugumi kwa kuambiwa tu kuwa "mia tisa itapendeza zaidi" na Dokta Shika?
Au hizi habari huwa zinazushwa ili kutupumbaza tusijali na kujadili mambo ya msingi kwa Taifa letu??