Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema chama chake hakitakubali kura za maoni za Katiba mpya kufanyika bila ya kuboreshwa daftari la Wapiga kura.
Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwendakulima wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Chadema haitakuwa tayari kuingia katika kura za maoni za katiba mpya bila daftari la wapiga kura kuboreshwa kwa kisingizio cha gharama na ukubwa wa nchi, alisema.
Dk. Slaa alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haipaswi kuogopa gharama za kufanya maboresho hayo kwani demokrasia yenyewe ndiyo gharama na suala hilo ni sheria siyo hisani.
Alisema Daftari la Wapiga kura linapaswa kufanyiwa marekebisho mara mbili katika kipindi cha kumalizika uchaguzi mkuu na kuingia uchaguzi mkuu mwingine kama sheria inavyoelezwa.
Dk. Slaa alisema anafahamu kinachoendelea katika suala la uboreshaji wa daftari la wapiga kura na kwamba kauli za tume kudai haina fedha za kufanya maboresho hayo siyo za kweli bali zinatokana na kuwapo kwa mvutano wa baina ya serikali pamoja na tume.
Serikali inajua Daftari hili likiandikwa upya vijana wengi wataandikishwa na kupata fursa ya kupiga kura hivyo CCM itashindwa katika uchaguzi mkuu ujao, alisema.
Alitoa mfano kuwa katika chaguzi mbalimbali mfano ule wa Arumeru Mashariki jumla ya vijana 14,000 walishindwa kupiga kura kutokana na kutokuandikishwa katika daftari la wapiga kura.
Dk. Slaa amemaliza ziara yake katika mikoa ya Shinyanga, Kigoma na sasa anaendelea katika mkoa wa Tabora kabla ya kuingia mkoa wa Singida.
CHANZO: NIPASHE