Dowans bado kaa la moto Send to a friend Wednesday, 23 February 2011 21:00 0diggsdigg
NAFASI ZA AJIRA KWA VIGOGO ZATANGAZWA
Ramadhan Semtawa na Exuper Kachenje
KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini jana ilichukua zaidi ya saa tano kukutana na uongozi wa Tanesco kujadili na kutafuta ufumbuzi kuhusu mgawo wa umeme unaoendelea, huku taarifa zikionyesha kuwepo mvutano mkubwa baina ya pande hizo na Tanesco kukataa kujadili suala la Dowans.
Hali hiyo inaonyesha kuwa Dowans bado ni kaa la moto kwa Tanesco na Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na January Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumbuli.
Awali akizungumza katika utambulisho, Makamba alisema dhumuni la ziara ya kamati yake pamoja na mambo mengine ni kutaka kujua mgawo wa umeme utaisha lini na wao kusaidia mawazo katika kutatua tatizo hilo.
"...Tunataka kujua mgawo wa umeme utaisha lini na utaishaje? Na katika hili muwe wazi na sisi tuweze kusaidia mawazo yetu kuondoa tatizo, pia tujue mnaendeshaje Tanesco, matatizo ili tusaidie kwa manufaa ya Watanzania," alisema Makamba.
Mvutano ndani ya kikao
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa ulizuka mvutano mkubwa baina ya wabunge na viongozi wa Tanesco huku ikielezwa kwamba shirika hilo limeshindwa kutoa kwa kamati hiyo mikakati yake ya kumaliza mgawo wa umeme.
Tanesco pia ilidaiwa kukataa kuzungumzia suala la Dowans nje ya Mahakama na kuwashwa kwa mitambo hiyo ili itoe megawati100 za umeme kwa lengo la kupunguza makali ya mgawo wa umeme unaondelea sasa.
"Mvutano mkubwa humo ndani, moto unawaka, Tanesco hawataki hata kuzungumzia suala la Dowans, mvutano unaendelea. Nimechoka maana huku ni kupoteza muda, hatuelewani ili kutatua tatizo," alisema mmoja wa wabunge ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na kuongeza:
"Tumeomba mikakati yao (Tanesco) katika kumaliza mgawo wameshindwa, wamesema eti bado ipo katika Bodi yao ya Wakurugenzi".
Tanesco wakaa faragha
Ujumbe wa Tanesco ulitoka nje ya ukumbi wa mkutano saa 8:51 mchana na kufanya kikao cha faragha huku baadhi ya wajumbe wake wakionekana kuhaha kuweka sawa mambo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Makamba alikiri kugawanyika kwa pande hizo, lakini akasema kulifuata kanuni.
"Kutoka nje si tatizo, sisi tumefanya kikao kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, inaruhusiwa na imetokana na mwenendo wa mjadala," Makamba alisema.
Alisema kamati yake imepokea taarifa ya Tanesco na kwamba wao wamejikita katika hatua za dharura.
Kuhusu Dowans, alisema kama taarifa zilizokuwepo, wamiliki wa Dowans walikuwepo nchini na wameanza mazungumzo na Tanesco ambapo mazungumzo na taratibu zinaendelea bila kuathiri kesi iliyo mahakamani ili mitambo hiyo itumike.
Hata hivyo, alikiri kuwapo kwa mvutano katika suala hilo na kwamba kazi ya kamati yake ni kushauri hatua za haraka kumaliza mgawo, pia kuishauri Tanesco waingie biashara ya kuwasha umeme na siyo kuzima.
Alisema Jumatatu ijayo kamati yake itakuwa na taarifa na mapendekezo ya kumaliza mgao wa umeme.
Majumuisho ya Kamati
Jana jioni, Makamba alizungumzia majumuisho ya kikao hicho ambapo alisema kuwa wameihimiza Tanesco waharakishe utekelezaji wa miradi ya umeme.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa wa megawati 260 kwa njia ya gesi unaotakiwa kukamilika Juni mwaka huu na mingine ambapo alisema tayari Tanesco imeipa kamati hatua zilizofikiwa na wadau wa miradi husika.
Makamba alisema kazi ya kamati yake sasa ni kuisukuma Serikali itoe fedha haraka kukamilisha miradi iliyopo kwenye hatua nzuri ili iweze kukamilika katika muda uliopangwa na kuondoa kabisa tatizo la umeme.
Kuhusu Dowans, Makamba alisema Kamati yake imeiagiza Tanesco kuhakikisha hakuna utata wowote wa kisheria na kwamba iwapo wataingia mkataba na kampuni hiyo basi mkataba huo uwe mfupi na usivuke mwezi Juni mwaka huu.
Nafasi za vigogo wazi
Wakati hayo yakiendelea shirika hilo la umma linajipanga kuwabadili wakuu wote wa vitengo vinavyounda menejimenti yake.
Uamuzi huo wa kuifumua Tanesco pamoja na mambo mengine, umekuja kipindi ambacho shirika hilo limepigwa mawimbi mazito huku wimbi la Dowans, likionekana kutikisa zaidi.
Katika tangazo lake lililotolewa jana kwenye vyombo vya habari, lenye Kichwa cha habari, '' Ajira kwa Nafasi Nyeti za Uongozi,'' Tanesco imeweka bayana kuwa nafasi zote za wakuu wa vitengo ziko wazi na zinahitaji kujazwa.
Nafasi hizo ni pamoja na Meneja Rasilimali Watu, Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati, Meneja Mwandamizi wa Utafiti na Meneja Mwandamizi wa Miradi.
Nafasi zingine zilizotangazwa katika tangazo hilo ni Meneja Mwandamizi wa Uangalizi wa Mfumo na Meneja Mwandamizi Mfumo wa Usambazaji.
Zingine ni Meneja wa Uzalishaji Umeme kwa kutumia Maji, Meneja Mwandamizi Uzalishaji Nishati na Meneja wa Mauzo na Masoko.
Pia anatafutwa mtu wa kujaza nafasi ya Meneja Mwandamizi Usambazaji, na nafasi ya Meneja Uhusiano wa shirika hilo.Mwisho wa kutuma maombi ya kujaza nafasi hizo ni Machi 8, mwaka huu 2011.
Tanesco imekuwa ikitajwa kukabiliwa na matatizo ya menejimenti kwa muda mrefu, hali inayotajwa kama moja ya chanzo cha kuzorota kwa utendaji wa shirika hilo nyeti la umma.
Matatizo mengine yanayoikabili Tanesco ni mikataba mibovu kama ule ulioingiwa kati yake na Richmond ambao baadaye ulirithiwa na Dowans Tanzania Ltd, ambayo sasa inaidai Tanesco Sh94 bilioni kwa kukatisha mkataba kinyume cha taratibu.
Jana Makamba alisema ukaimu wa nafasi mbalimbali ndani ya Shirika hilo kuwa moja ya tatizo la kiutendaji linaloliyumbisha.Makamba alitoa kauli hiyo katika utambulisho wakati kamati yake ilipofanya ziara Makao Makuu ya Tanesco, Ubungo Dar es Salaam."Kaimu wengi, inawezekana hili ni moja ya matatizo,"alisema Makamba.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Nishati na Madini, alijikuta akitoa kauli hiyo ghafla baada ya mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando, kujitambulisha na kutoa nafasi kwa ujumbe wake kujitambulisha.
Katika utambulisho huo zaidi ya nusu ya wakuu wa idara na vitengo vya Tanesco, walijitambulisha kuwa ni makaimu.
Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Last Updated on Thursday, 24 February 2011 09:02
Comments
0
#11 issa moshi 2011-02-24 11:11 sisi tunaomba mkuu wa police kumkamata huyu adawi afikiswe mahakamani awataje wenzie kwa makosa ya kuhujumu nchi huyu si muoman ni mtanzania anae tumia pasport ya oman huyu adawi anatumiwa na baadhi ya watu nchini
Quote
0
#10 Honorable 2011-02-24 10:48 Hapa kuna ujanja makamba anaucheza wa kiintejensia, anataka kuliingiza Bunge kubarika ufisadi wa Dowans, napenda kuwaonya wabunge walioko kwenye kamati ya makamba, wawe makini hasa wabunge wa Upinzani rasmi Bungeni wasikubali ukuwadi wa makamba wa kutaka mitambo ya dowans iwashwe, Dowans ni wahujumu uchumi, tuwaacheni watanzania tukae gizani hata kwa mwaka mzima lakini tupiganie heshima yetu, na wabunge wetu tafuteni utatuzi endelevu wa maswala ya umeme nchini, nampogeza ztto kabwe kwa kuanza kujadili suluhisho endelevu la umeme, na kuachana na kujadili wahalifu dowans! Kwani Dowans ina uchumi kuliko Tanzania? Hiyo mitambo ya Dowans inagarama kiasi gani kiasi kwamba Tanzania kama nchi haiwezi kumiliki? Kwanini Makamba hujadili umiliki wa Mitambo yetu hata kwa dharura, kwanini unajadili Dowans kila wakati au ndo ulivyo tumwa na chama chako? Hatutaki kusikia mitambo ya Dowans imewashwa! Heri tukae gizani kipindi chote cha utawala wa Kikwete na CCM, kwani ni miaka 5 imebaki! Tutoe hukumu yetu kwenu kwa hasira!
Quote
0
#9 TZA. HATUWAJIBIKI 2011-02-24 10:39 Pigo la TANESCO lina liza umma mzima.
pigo la ATCL lina liza umma mzima.
pigo la Rites RELI lina liza umma mzima.
Looh wenzangu tumebakia na nini? vishindo vilviyo enea humu ni ufisadi mtupu. sioni laa maana kabisa kama kunakuwajibka. Makosa ya poor GOVERNESS.
Je wenzangu hamuoni kuwa tunahujumiwa na nchi jirani? maana kila tukinyanyua kichwa tuna kandamizwa na kila tukianza shughuli/miradi tunazi zoretesha au kupoteza dira na hatimaye kufiya mbali. WHATs going on??
Quote
0
#8 Wakudata 2011-02-24 10:25 Dowans SA wameishitaki Tanesco, kwa kuvunja mkataba kutokana na hiyo mitambo ya Dowans. Ni ajabu na kweli Kamati ya Bunge chini ya January Makamba Mbunge kupitia CCM wanailazimisha Tanesco kuwasha mitambo ya Dowans, Tanesco ndiyo watakaolipa deni hilo la Dowans pesa ya walipakodi ndiyo maana gharama za nishati ya umeme imepanda ili kufidia hasara. Hiyo mitambo isiwashwe hadi kesi imekwisha. Je kuna kibali chochote cha kutoka mahakamani kinachoruhusu kuwashwa mitambo hiyo. Je ni nani anapaswa kukiomba ni Tanesco au Kamati ya Bunge. Tunajua Makamba anapigania maamuzi yaliyopitishwa na Kamati kuu ya CCM kulipwa kwa Dowans SA, ndiyo maana anaipigia debe ili kuihalalisha kiujanja ili baadaye waseme Bunge ndilo limehalalisha uhalali wa Dowans. Sisi Watanzania tunasema hakuna kuwasha mitambo hiyo hadi kieleweke.
Quote
+1
#7 MKWELI 2011-02-24 10:10 Ndugu GILLIARD tATIZO LA UONGOZI WA TANESCO ULIKUWA UNAINGILIWA SANA NA MAFISADI WENGI WAO WALIPEWA HIZO KAZI KWA VIMEMI. HAWAKUAJILI WATU KULINGANA NA SIFA NDIO MAANA UNAYUMBA, HAWAKUWA HURU KUFANYA KAZI ZAO. VIGOGO WALIWAPA KAZI WATU WAO ILI KUHUJUMU NCHI NA LEO NDIO HAPO TULIPOFIKA. USIONE WAMETOA NAFASI ZA KAZI KWA MKUPUO ILI NI KWA AJILI TU MAFISADI ISWAKUTE KASHFA KWANI AJIRA ZA UONGOZI WA TANESCO ULIJAA MIZENGWE SIKU NYINGI. WA KULAUMIWA NI MAFISADI AMBAO WANAJULIKANA.Quoting GILLIARD:
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete acha kuwa Rais Bubu hatujakuchagua uwe kivuli Ikulu.
Vunjilia mbali uongozi mzima wa Tanesco ndio unahujumu uchumi wa Taifa.Anzia Tanesco makao makuu hadi mikoani.Uchumi wa nchi ukiharibika kwa ajili ya uongozi mbovu wa Tanesco wananchi wanajua wewe ndio umeshindwa uongozi.Fumba macho tumia fyagio la chuma.
Quote
+1
#6 BENSON 2011-02-24 10:09 HIVI, IMEKUWAJE HATA KUFIKIA HAPO? BADO MIMI HAIINGII AKILINI KWA NINI SERIKALI IMESHINDWA KUNUNUA MITAMBO YAKE YENYEWE. KAMATI YA MAKAMBA WALISEMEE NA HILI. TUMECHOSHWA NA HADITHI ZISIZOISHA ZA DOWANS. LEO ANAFIKA MAHALI ATI ANATAKA KUTUWEKEA MASHARTI, SASA HII NI NCHI YENYE RAIS WAKE AU NI KAMPUNI YA [NENO BAYA] FULANI TU? TUTADHALILIKA HIVI MPAKA LINI?
MIAKA NENDA RUDI TUNAHANGAIKA NA VINA VYA MAJI NA MGAO WA UMEME, HIVI NI KWA NINI SERIKALI IMESHINDWA KULIMALIZA HILI? HILI LIPO KILA MWAKA KILA KIANGAZI, TUNASHINDWAJE KULIMALIZA? WAKO WAPI WASOMI WA NCHI HII? HEBU TUFIKE MAHALI TUACHE HUU U[NENO BAYA] UNAOITWA SIASA, UMEPITWA NA WAKATI. TUNAKUWA KAMA HATUAMINI KUWA TULIKWISHA PATA UHURU, TUNATAKA WENGINE WATUSAIDIE HATA PALE AMBAPO UWEZO TUNAO? HESHIMA YETU IKO WAPI?
Quote
+1
#5 JOHN 2011-02-24 09:49 Sikirizeni bwana mm naona hapa kuna sumu hata hawa Tanesco wamelishwa na yawezekana ikawa wanamjua mmiliki halisi wa mitambo hiyo ndio maana hawakutaka kuzungumzia hizo habari wakihofia kufukuzwa kazi mm naiomba hiyo kamati ya nishati ya bunge itafute njia mbadala yakuweza kafanya kazi zake vizuri kwa manufaa ya watanzania,tofa uti na hivyo hawatafanikisha lolote.
Quote
-1
#4 Zanzibari Mtanzania 2011-02-24 09:35 Ukeli umejulikana na haki isemwe wazi
Maoni mengi jana tuliyasikia na kusoma kwa kumsakama Mwarabu/mOmani eeti alikuwa anafuata nini. Ngoma ipo kwa wanaSIASA kutuuza bei ndogo. Huyu mmiliki wa DOWANZ anafuatilia kazi na miliki yake kama alivyo ahidi huko alipozitoa ULAYA/UMERKANI/SINGAPORE /popte, wenye mali wamemuamrisha kufuata malipo na hatma ya mitambo, sivyo tunavyo dhania Watanzania. Ikiwa humu ndani Tunatapeliwa na wana Siasa wetu au Viongozi mafisadi. Basi ujuwe mwarabu naye kesha chapwa vibaya, Ndiyo maana ameamua kujitosa na kugaragara hapa na kutupiwa lawama na kupigwa chenga za Wabongo. Sura yote utaielewa hivi sii punde.
Quote
+1
#3 Modern Day 2011-02-24 09:22 Shukrani Kwa Gzti.Mwananchi kutuletea habri nzito na moto za Dowans. Ukweli umejulikana kuwa kuna mvutano baina ya Kamati v/s Utendaji. yaani kwa kifupi baina ya siasa na uongzi.Ukitafakari utaona kuwa kuna uhondo wa mambo wenye lengo la kuhujumu uchumi na uzalishaji nchini, Kwani yote hayo tuna shuhudia upungufu mkubwa kapata umeme kukimu kazi na maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati. Je Wa Tanzania hamuoni hapo kuna utata fulani, Wapo tayari kuzorotesha uchumi wetu humu ili mambo (agenda) zao zipite na kusambaza mali na biashara zao zichanganye faida na sisi watuachie Siasa na malumbano baina yetu WaTZA.(hiyo ni sabotage ndogo tu).Nina Amini kuna watu wanalipwa na nchi jirani.(pelelezni kuna payroll kwa kundi moja).
La pili inafahamika sasa kuwa " Wahusika wana uza TIME ".
hayo utayajua kama una miliki mradi au kazi,Biashara,h ata workshop ndogo tu utaona taathira zake na hasara zake.
Quote
-2
#2 GILLIARD 2011-02-24 09:16 Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete acha kuwa Rais Bubu hatujakuchagua uwe kivuli Ikulu.
Vunjilia mbali uongozi mzima wa Tanesco ndio unahujumu uchumi wa Taifa.Anzia Tanesco makao makuu hadi mikoani.Uchumi wa nchi ukiharibika kwa ajili ya uongozi mbovu wa Tanesco wananchi wanajua wewe ndio umeshindwa uongozi.Fumba macho tumia fyagio la chuma.
Quote
0
#1 MKWELI 2011-02-24 09:11 NAWAPONGEZA TANESCO KWA KUKATAA MAADHIMIO YA MAFISADI, HAIWEZEKANI WEWE TANESCO UMEFIKISHWA MAHAKAMANI KAMA MUHARIFU. KWA HIYO USIKUBARI KUJADILI NJE YA MAHAKAMA, HUYO MAKAMBA ANATUMIWA TU!. HIYO NIJANJA YAO MAFISADI KUTUCHINJA KIMYAKIMYA. TANESCO MKISHINDWA TUAMBIENI WANANCHI!
Quote