Geofrey Nyangoro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeteketeza azma yake ya kumwekea pingamizi mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa zimeeleza kuwa chama hicho kiliwasilisha pingamizi hilo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini jana saa 7:30 mchana.
Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika, ndiye aliyewasilisha pingamizi hilo.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa alipoulizwa hakutaka kukubali au kukataa kuliona pingamizi hilo na akasema atazungumzia suala hilo leo.
Awali Chadema ilipanga kuweka pingamizi hilo la kutaka Kikwete azuiwe kugombea urais, Agosti 27 mwaka huu, lakini, ilisitisha kwa kile ilichoeleza kuwa inasubiri mambo mengi zaidi ambayo wangeyaingiza kwenye pingamizi hilo.
Chama hicho awali kilitaka kuweka pingamizi hilo kwa kile kilichoeleza kuwa Rais Kikwete amekiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa kutangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi kwenye kampeni.
"Tulishindwa kupeleka pingamizi hilo jana kwa sababu tumesikia kwamba huku anakoendelea na kampeni zake, mgombea huyo ameendelea kufanya makosa mengine ambayo tutataka tuyaingize kwenye pingamizi hilo," alisema Mnyika mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na gazeti hili jana muda mfupi baada ya kuwasilisha pingamizi hilo, Mnyika alibainisha kuwa mambo mengine mapya yaliyoingizwa kwenye pingamizi hilo ni mgombea huyo wa CCM kuahidi kukilipia Chama cha Ushirika cha Nyanza deni la Sh 5 bilioni na kuahidi kununua meli kwa ajili ya watu wa mikoa ya Kagera na Mwanza.
Mnyika alisema tayari Chadema imewasilisha pingamizi hilo jana lakini, ina mashaka kama ofisi ya msajili itawatendea haki.
Sisi tumeshawasilisha pingamizi letu kwa msajili wa vyama vya siasa kama Sheria ya Gharama za Uchaguzi zinavyoelekeza, lakini, tuna tumaini lenye shaka ndani yake kama tutatendewa haki,alisema Mnyika na kuongeza.
Mheshimiwa Kikwete wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi, moja kwa moja akitumia nafasi yake kama rais, ameongeza na /au kuahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kwa kupandisha kima cha chini kutoka Sh130,000 hadi Sh235,000,inasema sehemu ya kwanza ya pingamizi hilo lenye sehemu tatu.
Katika pingamizi hilo, Chadema pia ilieleza kuwa mgombea huyo wa CCM, ameahidi kutoa Sh5 bilioni kwa chama cha Ushirika cha Nyanza ili kilipe madeni yake mbalimbali na kuahidi kuwa serikali itachukua madeni yote ya vyama vya ushirika.
Chadema pia imesema katika sehemu ya tatu ya pingamizi hilo kuwa mgombea Kikwete alitumia nafasi yake kwa kuwaahidi watu wa mkoa wa Kagera kuwa atawanunulia Meli mpya, kubwa na ya kisasa.
"Ahadi hizo ni sehemu ya mambo yaliyokatazwa kwa mujibu wa kifungu cha 21 (1) (a) na (e) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010," imeendelea sehemu ya pingamizi hilo.
Mnyika alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, vitendo hivyo vilikuwa na nia ya kushawishi wapigakura wampigie kura mgombea huyo wa CCM.
Kuhusu ahadi ya kuchukua madeni ya Chama cha Ushirika cha Nyanza, alisema kitendo hicho nacho kililenga kuwashawishi wananchi wa Mkoa wa Mwanza kumpigia kura.
Nyongeza ya mishahara, ahadi ya Sh5 bilioni na ahadi ya meli kutumika kama hongo/rushwa kwa hao wote wahusika ili wampigie kura Kikwete," alisema Mnyika na kueleza kifungu kinachozuia mambo hayo kuwa kinasema:
"Mgombea yeyote ambaye yeye mwenyewe, wakala wake au chama chake kitafanya kitendo ambacho kimekatazwa na kama ilivyoelezwa katika sehemu hii, atakuwa, au, kitakuwa kimepoteza sifa za kushiriki katika mchakato wa uteuzi na uchaguzi.
Wakati huo huo, mgombea urais wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amemshukia Meneja wa Kamati ya Kampeni CCM, Abdulrahman Kinana na kumtaka anyamaze kwani katika orodha ya uchafu wa watuhumiwa wa ufisadi nchini hatoki.
Juzi Kinana aliwaambia waandishi wa habari kwamba, Dk Slaa anawadanganya wananchi kuhusu suala la ufisadi na kumtaka aache kufanya hivyo na anadi sera zake.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara katika Jimbo la Mikumi Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro jana, Dk Slaa alisema fisadi ni fisadi tu na hana njia nyingine ya kumpamba kwa maneno mazuri mtu anayeiba mali za umma.
Namuonya Kinana anyamaze, nisije nikamshukia kwa sababu katika orodha ya wana-CCM waliofanya uchafu hatoki kupitia kampuni zake, alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alimgeukia Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo kwamba pamoja na cheo chake cha uwaziri na ubunge katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, lakini wilaya yake ni moja kati ya tano zilizopata orodha chafu sana .
Dk Slaa anaendelea ziara zake za kampeni na leo anatarajia kufanya mikutano kadhaa katika mkoa wa Dodoma kwa kutumia usafiri wa helikopta.
Source: Mwananchi.
Ulitaka source hiyo!!!!