Kesi ya mauaji ya Dr Victoria Mutiso imeingia katika sintofahamu mpya baada ya Timu ya Mawakili waliokuwa wakiwakilisha Rose Mbithe Mulwa na watoto wake wawili, Chris na Angela Mulwa, kujiondoa ghafla mbele ya Mahakama Kuu ya Milimani.
Mawakili hao, akiwemo Cliff Ombeta, Danstan Omari, Martina Swiga, Samson Nyaberi na Shadrack Wambui, waliambia Jaji Alexander Muteti kwamba hawawezi kuendelea na uwakilishi kwa sababu walidai wateja wao walikuwa wanafanya baadhi ya maombi Mahakamani bila kuwashirikisha.
Ombeta alieleza kwamba kulikuwa na hali ya “kutovutana upande mmoja”, akisema Rose na watoto wake walikuwa wakichukua hatua ambazo hazikushirikisha Timu hiyo ya Mawakili.
Mzozo huo ulijitokeza wazi baada ya Mahakama kufahamishwa kuhusu ombi la dhamana ambalo Rose na watoto wake walikuwa wamewasilisha bila kuwashirikisha Mawakili wao. Wakili Joel Kyatha Mbaluka aliingia kuwasimamia katika hatua hiyo.
Rose hakuficha masikitiko yake kuhusu kuondoka kwa Mawakili hao, akisema yeye na watoto wake wameachwa bila msaada wa kisheria wakati ambao wanauhitaji zaidi. Aidha Rose alisema kuwa baadhi ya Mawakili hawakuwa wamewahi kuwatembelea gerezani ili kupata maelekezo yao moja kwa moja.
Isitoshe, Rose na wanawe waliwasilisha madai kuhusu namna walivyoshughulikiwa wakiwa kizuizini, wakidai kuwa waliteswa na kubaguliwa katika kipindi cha takriban siku 60 chini ya ulinzi wa Polisi. Madai hayo bado hayajathibitishwa na Mahakama na Jaji Muteti aliagiza upande wa mashtaka kuwasilisha majibu ndani ya siku 3. Mahakama pia iliagiza mawakili wapya wa washtakiwa hao kuwasilisha nyaraka za ziada kabla ya kusikilizwa kwa ombi la dhamana.
Lakini kesi yenyewe ina historia nzito:
Rose Mbithe, watoto wake Chris na Angela, Police Constable Elijah Kimoi na Maritim Kimutai wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Dr Victoria Mutiso na wote wamekana mashtaka hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi zilizoripotiwa, kesi hiyo imehusishwa na mzozo wa muda mrefu kuhusu mali unaohusisha familia ya Dr Mutiso na Rose Mbithe. Rose, hata hivyo, amekana kwamba kesi yake inatokana na mauaji hayo, akihusisha mashtaka na mzozo wa mali unaoendelea mahakamani kuhusu ardhi ya Mlolongo.
Sasa, wiki ijayo Oktoba 6 ndiyo siku iliyowekwa kusikilizwa kwa maombi ya dhamana. Kwa hiyo, hatua inayofuata si tu kuhusu kama watatu hao watapata dhamana bali pia Mahakama itakabiliana vipi na madai ya utetezi kuhusu namna uchunguzi na kizuizini vilivyoshughulikiwa, huku upande wa mashtaka ukisisitiza kuwa una ushahidi wa kutosha kuhusisha washtakiwa na mauaji hayo.