Dah! Inabidi kukaa pembeni na kutazama kwa macho, itachukua muda sana mimi kumwelewa Magufuli anachojaribu kufanya au malengo yake, maana kila uchao anaibuka na jipya, hujui kesho atakuja na lipi. Halafu anathubutu chochote bila breki. Juzi ametangaza kuwafuta wote wenye vyeti feki nikamsifia, leo ameibuka na hili la kuzuia magazeti kusomwa redioni...khaa!
Labda ndani ya miaka mitano tutamwelewa, labda huyu ndiye aina ya rais Afrika inahitaji au ndiye wa kukaa mbali naye. Labda Afrika hatuhitaji uhuru wa maoni, magazeti wala demokrasia za wazungu vitu ambavyo naona Magufuli anaviminya, au labda atakua anafanya makosa makubwa sana. Tusubiri tuone experiments zake hizi kama zitafua dafu.
Akipewa kipaaza sauti na kuanza kutoa hotuba, yeye huzungumza kilicho moyoni, wala harembi au kupaka kwa mgongo wa chupa. Anasema tu liwalo na liwe, juzi kawaambia watu wa Kilimanjaro amewasamehe kwa kupigia kura upinzani, kwanza kule Kagera ndio katema cheche wakati wa janga la tetemeko la ardhi. Halafu keshasema hapangiwi na wala asijaribiwe na mtu....hehehehe!!
Haya Magufuli yetu macho mzee, labda wewe ndiye kiongozi wa kuigwa na utainyanyua Tanzania iwe kwenye level mpya kiuchumi na kimaendeleo kwa kuzuia makelele na maneno mengi ya Waswahili na kuwaburuza kwa pua ili wafanye kazi na kuacha soga au labda wewe ndiye utaipiga chini nchi kwa kutotaka ushauri wala nini.
Nafikiri kinachomfanya Magufuli awe hivi ni kwa sababu ya upinzani. Wapinzani wa Kiafrika hawajui kukosoa kwa nia njema, wao hupinga chochote kwa vyovyote na kwa nguvu zote, hawana lolote njema wala cha kusifia, hapo inabidi rais kujitoa ufahamu na kufanya yake ili atimize malengo yake.