Meli ya hospitali ya Jeshi la maji la China, "Peace Ark" inayotekeleza jukumu la “Operesheni ya Masikilizano mwaka 2024”, hivi karibuni ilihitimisha ziara yake ya urafiki na huduma za matibabu nchini Djibouti, na kuelekea kituo chake kijacho nchini Sri Lanka. Hii inamaanisha kumalizika kwa safari ya meli hii ya hospitali barani Afrika kwa mafanikio. Katika siku 161 za safari, meli hii ilitembelea nchi 12 za Afrika na kutoa huduma za afya kwa watu wapatao 78,000. Ustadi wa hali ya juu wa madaktari wa kijeshi wa China pamoja na huduma zao bora zimefisiwa sana na watu wa Afrika. Meli hiyo ya hospitali kwa mara nyingine tena imeonyesha jinsi jeshi la China linavyotekeleza ahadi yake ya kutetea amani duniani.
Tangu kuanza rasmi huduma zake mwaka 2008, meli ya hospitali “Peace Ark” imefanikiwa kutekeleza majukumu ya “Operesheni ya Masikilizano” mara 10, ikitembelea nchi na maeneo 45 na kutoa huduma za matibabu za kibinadamu kwa malaki ya watu. Kati ya ziara hizo, tatu zilizofanyika mwaka 2010, 2017, na 2024, zimelenga Afrika katika kutoa huduma za matibabu, zikinufaisha zaidi ya watu laki moja wa bara hilo. Mwaka huu, ambao China na Tanzania zimeadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi, meli hiyo ilitembelea Tanzania mwezi Julai kwa mara ya tatu. Wakati wa ziara hiyo, watu zaidi ya 8,000 walipatiwa huduma za matibabu, zaidi ya upasuaji 80 ulifanyika, na mtoto wa kwanza alizaliwa kwenye jukumu la “Operesheni ya Masikilizano mwaka 2024” ambaye pia ni mtoto wa kwanza wa “amani” wa Tanzania. Kama ilivyoelezwa na gazeti la Daily News la Tanzania, huduma za matibabu za kibinadamu zinazotolewa na "Peace Ark" zinaonyesha upendo wa watu na jeshi la China kwa amani na heshima yao kwa maisha.
Wahenga wa China wamesema “dunia ni ya watu wote, hii ndio haki.” Kama sehemu ya jeshi la maji la China, “Peace Ark” siyo tu ni meli ya kawaida ya hospitali, bali inawakilisha amani na moyo wa kibinadamu wa watu wa China kwenye jukwaa la kimataifa, na pia inabeba mchango wa China katika kukuza azma ya binadamu wote kwa amani na maendeleo.
Hata hivyo, kinachostahiki kutajwa ni kwamba wakati meli hiyo ya hospitali ya China inapata sifa kubwa kwenye jumuiya ya kimataifa, nchi chache za Magharibi kama Marekani zina mtazamo tata. Kwa upande mmoja, hazina budi kutambua mchango mzuri wa juhudi za China katika kuinua viwango vya afya duniani, lakini kwa upande mwingine, zinahofia kwamba operesheni hiyo itapunguza ushawishi wao, hasa katika nchi zinazoendelea kama za Afrika. Ni kweli kwamba, katika mazingira ya sasa ya kimataifa yenye changamoto nyingi, majeshi ya nchi za Magharibi yamejikita zaidi katika vita, lakini meli ya hospitali ya China haibebi makombora wala mizinga; badala yake, imejaa tamaa ya China ya amani na heshima kwa maisha ya binadamu.
Kuanzia Bahari ya Hindi hadi Atlantiki, safari tatu za meli ya "Peace Ark barani Afrika zimeandika hadithi za kuvutia katika kujenga kwa pamoja jumuiya yenye mustakabli wa pamoja kati ya China na Afrika. Meli hii imevuka mipaka ya taifa, rangi, na tamaduni, na kuleta matumaini kwa dunia nzima. Tunatarajia kwamba meli hiyo ya hospitali itaamsha nchi nyingine kushiriki katika kuendeleza amani ya dunia na maendeleo ya huduma za afya, kuleta matumaini na msaada kwa wale wanaohitaji msaada na kujitahidi kujenga dunia yenye amani, afya, na ustawi zaidi.