SoC01 Dunia ya Sasa na Malezi ya Watoto

SoC01 Dunia ya Sasa na Malezi ya Watoto

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Dunia ya sasa ni tofauti kabisa na ile ya zamani, simaanishi hizi ni dunia mbili hapana! Dunia ni ile ile isipokua mambo yanayojiri duniani hubadilika, kama ambavyo mazingira au sura ya dunia yalivyobadilika. Mabadiliko hayo ya dunia yameathiri sana maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa katika kila eneo. Miongoni mwa mambo ambayo yameathiriwa mno na mabadiliko ya dunia ni hili la ulezi wa watoto.

Kulelewa katika mazingira salama, tulivu, yenye amani na upendo ni miongoni mwa haki za msingi za watoto. Ninaposema mtoto hapa namaanisha mwanadamu aliye na umri chini ya miaka kumi na nane; na zaidi wanaoguswa na mada yangu hasa ni wale walio chini ya miaka saba ambao kwa umri huo wanahitaji sana malezi ya wazazi kuliko mtu mwingine yeyote.

Tangu zamani jukumu la ulezi wa watoto ni la wazazi, yaani baba na mama, hasa mama. Na endapo mmoja wao akikosekana kwa sababu zisizozuilika kama vile kifo basi ndugu wa karibu huingilia kati na kubeba jukumu hilo. Hivyo mtoto akalelewa katika malezi mema kuanzia kuzaliwa kwake mpaka anafikia umri wa eye kujitegemea mwenyewe.

Tabia ya mtu huathiriwa kwa asilimia kubwa kutokana na aina ya malezi aliyopatiwa akiwa mdogo. Pia aina ya mtu aliyekulea nayo huathiri tabia ya mtu. Kwa mfano mtu aliyelelewa na wazazi wake wa pili yaani bibi na babu huwa tofauti sana katika tabia, silika, utashi, na hata hisia na mtu aliyelelewa na wazazi wake wawili baba na mama. Aliyelelewa na mzazi mmoja hutofautiana na aliyelelewa na wazazi wote wawili. Na hivi ndivyo ilivyo kila wanapotofautiana walezi.

Kutokana na uduni wa dunia ya kale, wazazi walilea watoto wao mpaka walipofikia umri mkubwa sana na wakati mwingine wazazi ndio walikua wanajukumu la kumtafutia mchumba mtoto wao. Hivyo wanahakikisha mtoto wao wanamuoza kwa mume waliyemtafuta wao au kumtafuta binti atakayeolewa na mtoto wao na watahakikisha wanamgharamia kila kitu katika ndoa yake, hapo ndipoo panakuwa maagano ya wao na mtoto wao aende akajitegemee na kuishi kivyake. Hapa nakusudia kwamba suala la malezi hapo zamani lilikua limepewa kipaumbele kiasi mtoto alikua analelewa na wazazi wake hata akiwa ameshafikia umri wa kwenda kujitegemea bado aliendelea kuhudumiwa nyumbani. Na hii ni kutokana na aina ya dunia waliyokuwa wakiishi wakati huo. Hali hii ilibadilika kila siku zilivyozidi kusonga mbele.

Kutokana na kuendelea kwa dunia na mambo kuchukua sura mpya, mambo sasa hayapo kama zamani. Kutokana na mahitaji ya dunia leo hii ulezi wa watoto umekua mgumu sana kusimamiwa na wazazi. Dunia ya leo wazazi wameshugulishwa na shuguli za kuijenga dunia jambo linalowasababishia kukosa muda wa kulea watoto wao, hivyo ili watoto waendelee kupata malezi wazazi wakaamua kumtafuta mlezi wa kando. Kukapatikana walezi binafsi wa nyumbani ambao wengi wa maisha ya kati huwatumia wadada wa kazi kulea watoto wao, na wale wa maisha ya juu wakawapeleka watoto wao katika vituoa vya kulelea watoto. Na wenzetu wa maisha duni watoto wao hujiingiza kwenye shuguli za kujikimu kimaisha wakiwa na umri mdogo sana na ndio hawa hulelewa na ulimwengu.

Jambo la wazazi kushindwa kulea watoto wao na kutafuta walezi ili wawalelee watoto wao limepelekea yafuatayo;-

  1. Kuongezeka kwa idadi ya watu (vizazi)

    Kwa kuwa wazazi hawana muda wa kutosha wa kuishi na watoto wao, imewalazimu wawaachishe kunyonya mapema ili wasipoteze muda mwingi pamoja na watoto wao, wakakosa muda wa kufanya shuguli za kujenga dunia. Hili hupelekea wazazi kupoteza ile hali ya upendo kwa watoto wao mapema na kutamani kuwa na watoto wengine, au kwa kuwa wazazi wametengeka na watoto wao hujikuta wapweke na ule upweke hupelekea mama kushika ujauzito mapema.
    Zamani ilikua baba na mama wanamlea mtoto wao mpaka anafikia umri mkubwa kisha ndio wanapata mtoto mwingine. Ile hali ya kuwa karibu na mtoto iliwazuia wao kuwaza kuwa na mtoto mwingine. Mwisho wa siku ndani ya muda mfupi dunia imekuwa na watu wengi kiasi cha kufanya rasilimali zilizopo zisitoshe kukidhi mahitajio yao.

  2. Kukosekana kwa maadili na malezi mema

    Kila mtu mwenye weledi na utashi atakubaliana na mimi kwamba wadada wa kazi za nyumbani sio walezi wazuri. Hata hivyo kwa kuwa wao ndio hukaa na watoto wetu kwa muda mrefu wamekuwa ndio walezi wa watoto huko nyumbani wakati wazazi wakiwa katika mishuguliko ya dunia. Hivyo watoto huiga tabia na mienendo ya walezi wao hao wadada wa kazi ambao wengi wao hukosa maadili mema kutokana na wao hawakupata muda wa kulelewa na wazazi wao.

  3. Kukosekana kwa mapenzi ya kweli na upendo

    Suala la dunia kukosa upendo na mapenzi ya kweli ni matokeo ya wazazi kutotimiza jukumu lao la ulezi kwa watoto wao. Na ndio maana tunashuhudia leo hii watoto hawawapendi wazazi wao kama ilivyo kwa wazazi wahawapendi watoto wao. Na hili huwa mpaka kwa ndugu wengine wa karibu katika familia au ukoo. Matokeo yake hata hao watoto wakikua wazazi wao wanaonekana ni kero kwao ikafika wakati kukaanzishwa vituo maalumu vya kulea wazee. Yaani mtoto ambae wewe ulimpeleka kwenye kituo cha kulea watoto wakati wa uzee wako na yeye anakupeleka ukalelewe kwenye kituo cha kulea wazee. Huku ni kukosekana kwa mapenzi na upendo wa kweli.
    Matukio tunayoyasikia ya mauaji wazazi kuuwa watoto wao, na watoto kutukana, kwadhalilisha na pengine kuwaua wazazi wao ni matokeo ya kukosekana kwa malezi ya wazazi.

  4. Kupotea na kutoweka kwa tamaduni na asili

    Mambo ya kiutamaduni kama vile miiko, desturi na jadi hurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kwa kizazi kingine. Na wazazi ndio wadau wakuu wa uhamisho huo wa tamaduni kutoka kwa mababu kuja kwa watoto. Kwa kuwa muda wa kukaa na watoto haupo kwa wazazi, leo tamaduni na mambo ya jadi yamepotea na hayapo tena. Watoto wetu hawana wakijuacho kuhusu mambo yao ya kiutamaduni. Huko kwenye vituo vya kulelea watoto wanafundishwa utamaduni mpya wenye mchanganyiko, matokeo yake hata lugha zetu za asili leo hii hazizungumzwi na watoto wetu. Hata hao wanaolelewa na wadada wa kazi za nyumbani hawana wakijuacho kuhusu tamaduni zao. Kubwa zaidi hata inapofika wakati wa likizo za shule wazazi hawafikirii kuwapeleka watoto wao kijijini kwao angalau wakajifunze mambo ya asili yao. kinyume chake huo ndio muda hutumiwa kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani na wa nje katika maeneo mbalimbali ya kuvutia.
Matokeo hasi ya hili tunaloendanalo ni mengi, nikiendelea kuyataja nitajaza kurasa na maneno yasitoshe kuelezea. Lakini kwa ufupi ni kwamba dunia ilipofikia sasa imetukwaza sisi wazazi tukawa hatuna namna isipokuwa tuishi hivi ili tuendane na kasi ya dunia, kwani hakuna wa kutukwamua.

NINI KIFANYIKE

Ni wazi kwamba leo dunia imetushugulisha sana, na endapo tutaacha kushugulika na kung’ang’ana na malezi ya watoto basi tutajikuta tunalea watoto wasio na afya, watoto wenye utapia mlo kwa kukosa chakula cha kutosha. Hivyo hatunabudi isipokua kuchakalika na dunia na wakati huo huo ni wajibu wetu sisi wazazi kuhakikisha watoto wetu wanapata malezi yetu bora.

Kwa mtazamo wangu wa karibu, kwa kuwa kulea hasa yale malezi mubashara yanapatikana kwa mwanamke/mama pekee, na huu ndio ukweli usiopingika. Na ndio maana linapofika suala la kutafuta mtu wa kulea watoto nyumbani anafikiriwa dada wa kazi na sio kaka wa kazi. Na kwa dunia ya sasa mambo yalivyoingiliana na dunia inavyoenda kasi imekua ngumu mama kubakia nyumbani kulea naonelea kufanya zamu (shift) katika malezi.

Baba na mama wapangiane siku za mmoja wao kubakia nyumbani kuhakikisha malezi na makuzi mazuri ya watoto wao pamoja na uwepo wa hao wadada wa kazi. Baba akienda kuchakalika huko duniani mama abakie na watoto na siku mama akienda kujihangaisha baba abaki nyumbani kuhakiki malezi mema ya watoto. Ingawa kuna changamoto nyingine hapo kwa baba siku za yeye kubakia nyumbani na dada wa kazi. Lakini kwa wazazi wenye kufahamu malengo yao na nini wamekusudia katika kufanyiana zamu hizo hili angalau litapunguza maafa ya watoto kukosa malezi ya wazazi. Kwani jukumu la malezi ni la wazazi wote, baba na mama.



DustBin
 
Upvote 7
Back
Top Bottom