MATUKIO YA WIKI NCHINI.
Matukio makubwa ya kutisha yaliyotokea nchini wiki hii ni pamoja na Mauaji ya kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Vurugu za Mbagala na Uchaguzi wa CCM.
Tuangalie uchaguzi wa CCM.
Niwakumbushe wasomaji kuhusu haya tuliyoyaandika katika mabandiko yetu hapa duru za matukio siku za nyuma:
Makongoro Nyerere ambaye ni maarufu kwa 'kule site' wanasema mafisadi..... naye ni victim. Tofauti na wenzake yeye ana ngao ya jina kubwa na huenda kumwacha nje ya sytem kunaweza kuzua makubwa. Wamiliki wa CC na NEC kwasasa hapendi arudi katika uongozi, wakati huo huo wapo wanaotaka jina hilo libaki kama heshima kwa Nyerere. Ni kazi nzito kumuengua kwa mizengwe lakini tayari jitihada zinaendelea ili aenguliwe mapema huko Musoma kabla hajafika NEC au CC kukwepa lawama
Matokeo ya uchaguzi mkoa wa Mara kwa mujibu wa taarifa,Makongoro Nyerere ameangushwa katika uenyekiti wa mkoa. Kama taarifa hizo ni kama tulivyozipokea basi tuliyosema sasa yanatimia. Kuondolewa kwa Makongoro hakutokani na kundi la Mtandao bali ni kundi ndani ya chama linaloongozwa na wakubwa wa chama wa kutaka aondoke kwasababu ya misimamo yake ndani ya NEC.
Njia ya 'kisayansi' ni kuhakikisha anamalizwa huko huko ili kuosha mikono mapema.
Mkoa wa Dar es Salaam umeshuhudia mabaliko ambako Ramadhani Madabida amemuengua Joh John Guninita.
Madabida amekuwa mwanachama wa NEC kwa muda mrefu.
Madabida anaungwa mkono na kundi linalojulikana kama wazawa wa Dar es Salaam likiwashirikisha akina Idd Simba,Sophia Simba, Sykes n.k.Ni dhahiri kuwa ipo nguvu ya ziada nyuma yake.
Ikumbukwe, Guninita alichukua wadhifa huo kutoka kwa mzee Hemed Mkali ambaye pia alikuwa mwanachama wa kundi la wazawa. Kuingia kwa Guninita kulikuwa na Chapuo la juu ambalo safari hii halikufanya kazi.
Hii pia inaonyesha ni jinsi gani siasa za chama zinavyobadilika kutoka katika sera na kuegemea makundi.
Adam Kimbisa aliyewahi kuwa Meya wa jiji naye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkoa wa Dodoma.
Matokeo yanayoendelea yanaonyesha wazi kuwa ndani ya NEC kuna upungufu w kundi la mtandao ukilinganisha na siku za nyuma. Katika makundi ya kuelekea 2015 kundi la Sitta linaonekana kupata nguvu huku kundi la Lowasa likiwa na majeraha mkubwa.
Hata hivyo kwa uzooefu wa siasa za mitandano, kundi la Lowasa haliwezi kuondolewa katika mbio kwasababu lina uwezo mkubwa wa kucheza karata za kisiasa. Sasa hivi kuna jitihada za makusudi zinaendelea ili kurikruti wanachama wapya wa NEC kwa kutumia gharama kubwa.
Vurugu za Mbagala:
Tukio hilo limesababishwa na watoto wawili wenye umri wa miaka 12 na 14. Ni tukio la kukojolea kitabu kitakatifu cha Kurani. Inasemwa kuwa baada ya tukio hilo wazazi wa pande mbili waliyamaliza kama wazazi, lakini pia hatua zikachukuliwa kwenda katika vyombo vya sheria.
Kilichotokea ni Ijumaa iliyopita waamuni kuvamia kituo cha polisi ili kumtoa mtoto huyo na kumwadhibu huenda kukatisha maisha yake. Baada ya jaribio hilo kushindwa ndipo waumini wakavamia makanisa na kuanza kufanya uhalifu.
Duru za matukio zina amini kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuishi kwa kuhesimu kile mwingine anachokikubali au kukikataa.
Imani ni jambo nyeti sana katika jamii hasa jamii zetu ambazo ufahamu wa mambo ni tatizo.
Ni vema wazazi wakaanza kuwalea watoto kutambua umuhimu wa kuishi kwa utangamano katika jamii moja.
Duru matukio inaamini kuwa umri wa miaka 12 na 14 ni mdogo kuweza kuchambua madhara ya jambo fulani.
Nakumbuka nikiwa katika umri wa miaka hiyo niliwahi kufanya michezo ya kuchezea mahindi yaliyokuwa katika stoo. Furaha yangu ilikuwa kuwasha kiberiti ili 'nywele; za mhindi ziungue na hapo nilijisikia raha.
Matokeo ya hili yalikuwa kuchoma ghala zima na kusababisha hasara kubwa.
Umri wa miaka hiyo ni umri wa majaribio ya kila jambo ikiwa ni pamoja na kuchungulia watu wakioga, kufuatilia sauti zisizo za kawaida vyumbani, kukimbilia katika matukio kama ya watu kuuawa n.k.
Ni umri unaosikia na kuona lakini hauna uwezo wa kupambanua zuri na baya.
Ni kwa ukweli huo sheria nyingi kama upigaji kura, kujamiiana n.k. zinalitenga kundi hili.
Inafanyika hivyo kwa kuelewa kuwa ni umri unaojua aina ya vyama, bendera za vyama na wapi sanduku la kura lilipo, lakini haujui ni kwanini wamachague kiongozi A na siyo B.
Hatukabali kwa namna yoyote tabia mbaya na wala si vema kutoa excuse kwa tabia chafu kwa kisingizo chochote tukielewa kuwa hayo yaweza kuwa matatizo ya ulezi, jamii n.k.
Kinachosikitisha ni pale watu wazima wanapokuwa na uelewa mdogo katika kupambanua mambo na hoja.
Sidhani kuwa mtoto alyefanya hivyo alitumwa na kundi lolote la jamii. Siamani hivyo!
Na kama nitaamini hivyo basi itanibidi niami kuwa kibaka aliyeiba nyumbani kwangu naye alitumwa na wazazi au familia. Itabidi niende mbali ili kufahamu jina la kibaka huyo na kama ni Mohamed basi atakuwa ametumwa na Waislam, kama ni Chiristian basi atakuwa ametumwa na Wakristo.
Nitakwama endapo jina la kibaka wangu ni Gugutioh Mwanoga maana halina kiashiria cha dini.
Ni ujinga wa hali ya juu kuchukua jina na kulifanya dini. Hili ndilo tatizo tulilorithishwa Waafrika.
Tunadhani kuwa jina peke yake linamfanya mtu kuwa mcha mungu.Vitabu vitakatifu havisemi ukiitwa John Samson Jacob basi automatic wewe ni mtu wa ufalme wa mungu.
Wala havisemi kuwa ukiitwa Abdul Mohamed Hussein wewe ni mtu wa peponi.
Sijui ni kigezo gani kilitumika kutambua kuwa kijana aliyetenda kosa hilo ni muumini wa dini fulani. Sijui ni kigezo gani kilitumika kujua kuwa ametumwa kufanya uhalifu huo na dini yake. Na sijui ni kigezo gani kilitumika kujua kuwa yeye au wazazi wake ni wafuasi wa dini fulani.
Matokeo ya kutokuwa na majibu ya maswali hayo achilia mbali kujiuliza ndiyo yamepelekea watu kuvamia na kuchoma makanisa moto. Hakika hiki ni kitendo cha uovu kilichokosa busara kabisa.
Hata kwa kutumia busara za kawaida tu hili lisingefika lilipofikia. Ni suala ambalo lingezungumzwa na kufikia tamati bila kuwa na mikwaruzo au vurugu. Hakukuwa na busara ya aina yoyote katika kuvamia sehemu nyingine na kuleta uharibifu.
Kinachoonekana hapa ni uwepo wa matatizo mengine yanayosubiri sababu, lakini tatizo lililokuwepo halikuwa katika kiwango kilichotokea. Lazima tukiri kuwa kuna watu wameachwa katika jamii yetu kujenga chuki baina ya watu na watu, dini na dini na pengien kabila na kabila.
Tumelikemea sana hapa JF pale mijadala iliyolenga kuleta vuru ilipoletwa. Nakumbuka Mohamed Said ambaye ni kinara wa chuki hizi za jamii aliposema, 'tuangalie tusijejikuta AU, EU wanakuja kutusuluhisha'.
Hoja ya namna hiyo ililenga kuleta chuki na nadhani ni wakati Mohamed Said ajitokeze na kueleza furaha yake kwa kupandikiza chuki hizi.
Kinachosikitisha sana ni kuona watu wenye nia mbaya ya kulichonganisha taifa na jamii wamepewa fursa ya kufanya hivyo hadi tumefikia hapa. Hapa tulipo ni mahali pa baya kwasababu inapotokea mtu anaamua kwenda kuchoma moto nyumba za dini nyingine bila kujua kwanini anafanya hivyo inatisha.
Duru matukio inalaani dhihaka za imani na pia inalaani matumizi ya nguvu yasiyozingatia weledi au busara.
Two wrongs never make one right.
Iko wapi Tanzania niliyoishi nikiwa na marafiki wengi wa imani tofauti na yangu, marafiki wengi wa makabila yasiyokaribiana na langu?
Ukweli usemwe, kuogopa kusema ni kulea tatizo.
Tusemezane