Wasalaam,
Nimepokea Mail hii Toka kwa Mnyika:
Eric,
Naomba uliweke tamko hili Jamboforum/TEF. Waeleze nimeshindwa kuingia kuliweka. Forum inakataa jina na password yangu. Naomba moderator anitumie maelekezo kwenye
mnyika@yahoo.com. Waeleze kuwa hoja zilizoelekezwa kwangu kuhusu elimu nitazijibu baada ya hii kama nilivyoahidi.
JJ
Nami nawasilisha:
TAMKO KUHUSU UCHAGUZI WA BUNGE LA AFRIKA YA MASHARIKI
UTANGULIZI
Tamko hili linatoa taarifa ya timu ya kampeni ya mgombea ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kuhusu mapungufu, mafanikio, mapendekezo na mwelekeo kuhusiana na mchakato wa uchaguzi husika.
Novemba pili mwaka 2006 wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walichagua kwa niaba ya watanzania wabunge wa kuiwakilisha nchi yetu kwenye bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki.
Mchakato wa uchaguzi huu ulianza rasmi mapema mwezi Septemba baada ya katibu wa bunge kutangaza nafasi kuwa wazi na kupeleka barua kwa vyama kuteua wagombea.
CHADEMA kilishiriki katika uchaguzi huo toka mwanzo mpaka mwisho wa mchakato wa uchaguzi huu.
CHADEMA ilianza kwa kutangaza kwa uwazi kwa wanachama wake katika ngazi mbalimbali kujitokeza kugombea nafasi za ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA. Wanachama mbalimbali walijitokeza kuomba na kamati kuu iliketi Oktoba 27 mwaka huu kufanya uteuzi wa wagombea ambapo wagombea wawili waliteuliwa mmoja katika kundi la wanawake na mmoja katika kundi la vyama vya upinzani. Mgombea wa kundi la wanawake alijitoa katika hatua za awali kabla ya jina lake kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi.
Hivyo CHADEMA iliwasilisha jina la mgombea mmoja katika kundi C la vyama vya upinzani Profesa Mwesiga Baregu. Timu ya kampeni iliundwa kwa ajili ya kuratibu kampeni za mgombea wa CHADEMA katika uchaguzi huo.
Lifuatalo ni tamko la timu ya kampeni za mgombea wa Afrika ya Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA kuhusu uchaguzi huo.
MAPUNGUFU:
Uchaguzi wa Bunge la Afrika ya Mashariki 2006 HAUKUWA HURU WALA WA HAKI kutokana na mapungufu yafuatayo ya msingi:
1. UFISADI NA SHINIKIZO/MAELEKEZO KWA WAPIGA KURA: Kampeni zilitawaliwa na mapungufu mawili makubwa: Mosi, palikuwa na ufisadi katika kampeni hususani katika makundi yaliyogombewa na wagombea wa Chama cha Mapinduzi(CCM) pekee. Katika lugha rahisi ufisadi unaweza kutafsiriwa kama uozo wa kimaadili ambao unajumuisha rushwa ya fedha, matumizi mabaya ya madaraka nakadhalika. Katika kundi hili la wagombea yalisikika malalamiko toka kwa wagombea mbalimbali kwamba wapo waliokuwa wakitumia rushwa ya fedha, wengine wakitumia sababu za kuwa na ndugu zao ama watu wa karibu yao walioko katika utawala na hivyo kampeni kujikita katika siasa za makundi na kambi mbalimbali. Takribani nusu ya wagombea walioshinda wana undugu na watu mbalimbali katika utawala ama baba, kaka, wanandoa nakadhalika.
Pia palikuwa na malalamiko ya kuwepo kwa kampeni za kuchafuana hususani kupitia jumbe za simu za mkono.(SMS). Lakini katika hali ya kushangaza na pengine yenye kuleta hisia za kulindana wagombea hao hao walihutubia na kutangaza kwamba mchakato mzima ulikuwa wa kidemokrasia. Kwa upande wa kundi C la upinzani hali ilikuwa mbaya zaidi, kwa ujumla wapiga kura ambao pia ni wabunge wa jamhuri ya Muungano wengi wao walipiga kura kwa shinikizo na maelekezo. Usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura wabunge wa CCM walikutana kama kamati ya chama chao(party caucus). Vyanzo vya kuaminika vimedokeza kwamba kupitia kikao hicho aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikao Mheshimiwa Edward Lowasa ambaye pia ni Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwamba imeamuliwa kura zote za wabunge wa CCM apewe mgombea wa UDP Dk. Fortunatus Masha.
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa hoja hii ilizua mjadala huku wachache wakiipinga waziwazi lakini mwisho shinikizo na maelekezo hayo yalibadili upepo wa uchaguzi. Sababu za kufikia uamuzi huu zilizotolewa ni pamoja na hisia kwamba Profesa Baregu angekuwa na msimamo usiyoyumbishwa katika masuala fulani fulani na kwa upande mwingine hofu kwamba kumpa fursa hiyo ingekuwa ni kama kuijenga CHADEMA kisiasa. Kwa ujumla ufisadi na shinikizo vilifanya wengi ya wabunge wapige kura si kwa kuzingatia zaidi uwezo wa wagombea na maslahi ya taifa na hivyo kufanya uchaguzi kutokuwa huru na wa haki hususani katika kundi la vyama vya upinzani.
2. UKIUKWAJI WA KANUNI NA TARATIBU ZA UCHAGUZI:Kuanzia mchakato wa uchaguzi wa bunge la Afrika ya mashariki kwa upande wa Tanzania ulipotangazwa CHADEMA ilimuandikia barua spika katika hatua mbalimbali kutaka ufafanuzi ama kulalamikia baadhi ya taratibu. Masuala mengi ambayo CHADEMA ilipendekeza yazingatiwe katika uchaguzi huu hayakuzingatiwa. Lakini kwa upande mwingine ofisi ya spika ilitoa ufafanuzi kwamba vyama vya upinzani vinayoruhusa ya kusimamisha wagombea katika makundi mbalimbali katika uchaguzi huu zaidi ya kundi C ambalo limetengwa mahususi kwa vyama vya upinzani.
Barua hii ndio ilikuwa msingi wa matangazo ya mwito kwa wanachama kujitokeza kugombea na hata mchakato wa kuteua wagombea uliofanywa na kikao cha kamati kuu ya CHADEMA. Ufafanuzi huu uliendana pia na hukumu iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi wa kipindi kilichopita ambaye alikuwa katibu wa bunge kipindi hicho Bwana Musa Kipenka ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu. Katika hoja zake alizotumia kutupilia mbali pingamizi dhidi ya mgombea mmoja wapo wa TLP wakati huo aliweka bayana kuwa vyama vya upinzani vinahaki ya kugombea katika makundi mbalimbali ya uchaguzi huo. Lakini hali ilikuwa tofauti katika hatua za mwisho za uchaguzi wa mwaka huu ambapo spika wa bunge aliamua ama kwa kutokujua au kwa makusudi kupindisha kanuni na tafsiri yake. Baadhi ya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni na taratibu ni pamoja na: Mosi, uhuru wa mawazo na haki ya kujitetea iliminywa hususani katika hatua za awali za msingi. Kuanzia katika utangulizi wake spika alionyesha kuwa hayuko tayari kwa majadiliano huku akisisitiza kwamba mwongozo wa spika ni wa mwisho na kwamba yoyote mwenye dukuduku awasilishe malalamiko yake katika kamati inayohusika na kwamba maamuzi ya kamati yatatolewa baada ya uchaguzi na yatakuwa ni kwa ajili ya kumbukumbu tu.
Pamoja na kwamba kanuni za sasa zinampa mamlaka haya spika kwa vyovyote vile kwa nia ya kuondoa mashaka na madukuduku tulitegemea spika angepanua wigo wa majadiliano na maridhiano kwa mamlaka hayo hayo aliyopewa. Pili, Spika alimnyima mathalani mgombea wa CUF Mohamed Abrahaman Dedes haki yake ya kugombea kundi la Zanzibar. Na mbaya zaidi spika alimhamishia kundi la upinzani ambalo silo alilotaka kugombea. Hii ni sawa na mtu aliyewasilisha fomu za kugombea ubunge Ubungo ajikute tume ya uchaguzi imempeleka kugombea Ilala. Kwa vyovyote vile mgombea aliyefanyiwa hivi anao uhalali wa kisheria wa kubatilisha uchaguzi kutokana na kunyimwa haki yake ya kushiriki.
Tatu, spika alimua kutumia mamlaka aliyopewa kuteua maofisa wa ofisi yake kuwa mawakala wa kuhesabu kura badala ya mawakala kupendekezwa na wagombea au vyama vyao ama kambi mbili za bunge(ingawa baadaye aliruhusu wagombea kushuhudia izingatiwe kuwa katika mazingira ya uchaguzi mara nyingi mgombea mwenyewe hushindwa kuwa wakala, ndio maana katika uchaguzi unaofuata misingi ya demokrasia mgombea hupewa fursa ya kuteua wakala wa kumwakilisha). Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi uliopita spika wa wakati huo, Pius Msekwa aliteua mawakala wawili miongoni mwa wabunge mmoja akiwakilisha chama tawala na mwingine akiwakilisha kambi ya upinzani.
MAFANIKIO:
a) TUMEENDESHA KAMPENI ZENYE UFANISI NA KUWEKA MBELE MASLAHI YA TAIFA: Timu ya kampeni ya CHADEMA ilifanikiwa kuendeleza utamaduni wa kuendesha kampeni zenye ufanisi zilizojikita katika ajenda, uwezo wa mgombea na kutanguliza mbele maslahi ya taifa. Mgombea wa CHADEMA Profesa Mwesiga Baregu aliongoza kwa kuweka bayana ajenda zake kuhusu Afrika ya Mashariki na kumfanya kukubalika na kuheshimika. Alibainisha vyema dira(vision) yake ya kuona Afrika ya Mashariki yenye watu wenye ustawi ambayo imeungana kiuchumi na yenye umoja wa kisiasa ikiongoza mwendo kuelekea jumuia ya kiuchumi ya afrika na Umoja wa Afrika wenye kukabiliana na chagamoto zo utandawazi. Nia na sababu zilizomfanya agombee pamoja na malengo yake ya kufanya kama angechaguliwa kuiwakilisha nchi katika bunge hilo kwa pamoja viliibua majadiliano.
Baadhi ya masuala yaliyoibuka ni pamoja na: haja ya Tanzania kuwa nchi ongozi katika mchakato wa Afrika ya Mashariki kutokana na uzoefu wake katika Muungano, idadi ya watu, uwingi wa raslimali na kadhalika; kulinda maslahi ya Tanzania katika muktadha wa maslahi ya pamoja yanayohusiana baina ya nchi za afrika ya mashariki; nafasi ya jumuia katika kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi wanachama na pendekezo la wabunge wa Afrika Mashariki kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi ama kupanua mfumo wa uwakilishi na uchaguzi. Kwa ujumla wasifu wa Profesa Baregu kama msomi anayeshimika katika masuala ya siasa na mahusiano ya kimataifa pamoja na mchango wake katika kamati mbalimbali za kiserikali (chini ya wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa) za michakato ya amani ya katika eneo la maziwa makuu na usalama wa Afrika ya Mashariki vilifanya watu wengi kumpa nafasi kubwa ya kushinda katika