SoC04 Elimu ni safari

SoC04 Elimu ni safari

Tanzania Tuitakayo competition threads

Gyda

New Member
Joined
Aug 8, 2022
Posts
2
Reaction score
2
Nilipokuwa mdogo wazazi wangu hawakuacha kunisisitiza nizingatie masomo kwani elimu ni ufunguo wa maisha. Wazazi waliamini wakitupeleka shule nzuri na kutupatia elimu bora basi maisha yetu yatakuwa ya kujitosheleza kuliko yao. Kipindi cha likizo wakati wanafunzi wengine wakiwa nyumbani sisi tulipelekwa shule kwenye masomo ya ziada jambo ambalo lilitukwaza kwa kuwa tuliamini tuna haki ya kupumzika kama watoto wengine.

Ilipofika jioni wazazi wetu walikagua daftari zetu, walihakikisha tumefanya mazoezi tuliyopewa kabla ya siku iliyofuata na hawakukosa vikao vya shule kujadili maendeleo yetu. Kwa kipindi kile tulikuwa shule ya msingi, hatukuruhusiwa kumiliki simu za mkononi na tuliwekewa muda maalumu wa kutazama runinga yaani muda wa taarifa ya habari. Baada ya kula chakula cha jioni pamoja tuliomba Mungu. Watoto wote tuliambiwa tukalale huku wazazi wakiendelea kutizama vipindi wanavyovipenda.

Ukiacha adhabu za kutofanya vizuri kazi za walimu shuleni, tulikuwa na adhabu kutoka kwa wazazi wetu. Pale tulipofaulu juu ya kiwango tuliporudi nyumbani tulipongezwa. Pongezi hizi zilikuwa ni pamoja na kupikiwa chakula tunachokipenda mfano: Wali wa kuku kwa ajili ya kusherehekea aliyefaulu na siku nyingine tulikula kande za maharagwe au kununuliwa ubuyu kwa ajili ya mtoto aliyefeli. Ingawa tulikula sote; siku tuliyokula vizuri tulifurahi pamoja na kumsifu aliyefaulu na siku tuliyokula chakula ambacho hatukukipenda tulihuzunika na kumuhimiza aliyefeli ajitahidi ili tule vizuri mara kwa mara. Jitihada zote hizi hazikwenda bure; zilileta matokeo chanya kwani tuliweza kushika nafasi za juu darasani na kuibuka vinara katika mitihani mbalimbali.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi nilianza kutafuta shule ya sekondari. Nilichaguliwa kwenye shule ya bweni ambayo wanafunzi wote walikuwa vinara kwenye shule walizotoka. Mwisho wa muhula wa kidato cha kwanza tulifanya mitihani ambapo matokeo yaliwekwa kwenye ubao wa matangazo. Kwenye orodha ya kila kidato kulikuwa na jina kamili la mwanafunzi, wastani wa alama alizopata na nafasi yake darasani. Tulikuwa wanafunzi zaidi ya mia moja kwa kidato cha kwanza. Hii siku wanafunzi walihuzunika saka kwani kila mmoja alizoea kushika nafasi ya kwanza. Hapa kuna waliokuwa ndani ya orodha ya karatasi ya kwanza yaani wa kwanza mpaka wa thelathini, karatasi inayofuata thelathini na moja hadi sitini na wengine kwenye karatasi ya mwisho. Siku zilivyozidi kwenda mara nyingi wa kwanza alibaki kwenye nafasi yake, wengine walijitahidi wakashika nafasi za juu katika orodha na wengine walizidi kushuka chini yaani walishajikatia tamaa. Kipaumbele cha shule kilikuwa shule iwe ya kwanza siku zote na hata wale ambao hawakwenda na kasi hiyo walionekana ni wanafunzi dhaifu na wanarudisha shule nyuma.

Ukiacha mafunzo ya darasani, wanafunzi walikuwa na vipaji mbalimbali lakini kulingana na mfumo wa elimu kadri siku zilivyozidi kwenda dhumuni letu likawa kusoma sana, kufaulu mitihani na kushika nafasi ya kwanza.

Tulipofika kidato cha tatu, wakati wa kuchagua michepuo ulifika. Wanafunzi wengi tulichagua masomo ya sayansi na wachache sana walichagua biashara. Sio kwamba tulikuwa hatupendi masomo ya biashara lakini hali hii ilichangiwa na aina ya walimu. Walimu wa biashara walikuwa wakali sana na tulipowauliza maswali pale ambapo hatukuelewa mwalimu alielekeza kwa kugomba wakati walimu wa masomo ya sayansi walijitoa hata muda wa ziada kutufundisha pale tulipokwama hivyo wanafunzi wengi wakapenda zaidi masomo ya sayansi. Baada ya hali hii kutokea tulipewa mtihani ambao uliamua nani abaki kwenye mchepuo wa sayansi na wengine wakasoma masomo ya biashara.

Baada ya kufaulu kidato cha nne ulifika muda wa kuchagua michepuo na sikujua niende wapi. Kila niliyemuomba ushauri alinishauri niende alipo yeye mfano nisomee biashara kwasababu yeye ni mfanyabiashara au sheria kwasababu anaona kuna uhaba wa wanasheria. Niliendelea na masomo ya sayansi na kufaulu vizuri kidato cha sita.

Shida hii ilijitokeza tena ulipofika muda wa kwenda chuo kikuu na kuchagua taaluma ninayotakiwa kusoma. Kila niliyemuuliza alikosoa upande ambao haupendi na kuelezea kwanini nichague taaluma moja na sio nyingine. Baada ya kufika chuo kikuu na kuanza mwaka wa kwanza nikakutana na wanafunzi wengi ambao wanahisi wanachosomea sio walichotaka kuwa hapo mwanzo. Mfano mmoja alinisimulia jinsi alivyotamani kuwa rubani lakini anasomea udaktari, mwingine aliyetaka kuwa daktari alihamia kwenye masomo ya biashara. Aliyetaka kuwa mbunifu wa mavazi anasomea madini. Hata hivyo nilisoma kwa bidii na kupata alama za juu kama ilivyo kawaida. Baada ya kumaliza chuo kikuu, nilipambana sana kutafuta ajira bila mafanikio nikakumbuka kipaji changu.

Wakati naendelea kuomba nafasi za kazi nilianza kujiendeleza katika kipaji changu. Ingawa watu wengi hawakukubaliana na hali hii, niligundua haya ni maisha yangu na kama kijana siwezi kurudi nyuma hivyo natakiwa kupambana ili nijikwamue kiuchumi na juhudi nilizoweka zisipotee bure.
Hivi sasa nimejiajiri, naendelea kuboresha ujuzi wangu na kumshukuru Mungu kwa kuendelea kunipigania kwani naweza kujitegema kwa mahitaji yangu ya msingi.

MAPENDEKEZO:
Ili kuwa na maendeleo katika nchi yetu ndani ya miaka ijayo:
  1. Serikali na sekta binafsi ziweke mfumo ya ushauri (mentorship) kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu ambayo kwa ushirikiano wa wazazi, wanafunzi na walimu itasaidia kuwapa wanafunzi mwongozo sahihi wa kusoma na hatua za kuchukua kulingana na uwezo na kipaji cha mwanafunzi. Hii itasaidia watanzania kusomea taaluma wanazozipenda na kufanya kazi sehemu wanazozielewa na kuzimudu.​
  2. Mifumo ya elimu ya vitendo ipewe kipaumbele sawasawa na elimu ya nadharia. Mitaala iboreshwe kuendana na mazingira yetu ili kuwapa wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kutatua ukosefu wa ajira nchini.​
  3. Malezi ya wazazi ni muhimu sana katika kuleta kizazi kinachojituma na vijana wanaopambania maendeleo ya nchi yetu. Pamoja na kuwahimiza watoto wasome, wazazi wasiwalazimishe watoto kufanya vitu walivyoshindwa kutimiza wao badala yake wawasaidie kujitambua, kutimiza ndoto zao na kujenga maisha yao.​
  4. Ukali wa walimu hausaidii wanafunzi kuelewa darasani. Walimu walipwe mishahara kwa wakati. Walimu sio adui wa wanafunzi wawatunze kama walezi mbadala wa wazazi.​
  5. Mchakato mzima wa mitihani uangaliwe upya. Usahihishaji wa mitihani uzingatie kuelewa na si kukariri, matokeo yatolewe katika orodha ya nambari bila majina hii itasaidia kutunza afya ya akili ya wanafunzi. Mwanafunzi anapofeli asaidiwe na sio kuhamishiwa kituo kingine cha mtihani ili asiiangushe shule.​
  6. Sheria zinazomlinda mwanafunzi dhidi ya rushwa ya ngono ziangaliwe upya ili kuwasaidia wanafunzi watimize malengo yao hasa katika ngazi ya chuo kikuu.​
  7. Kazi ya ualimu isiwe kwa wale waliofeli kidato cha nne bali kwa watu wenye wito wa kufundisha.​
 
Upvote 0
Back
Top Bottom