Mlenge
R I P
- Oct 31, 2006
- 2,125
- 2,306
Elimu ya Ufundi Katika Utumishi wa Umma
Serikali imeamua kutekeleza kwa vitendo uamuzi wake wa kutokuwa na watu wasio na elimu ya kutosha katika utumishi wa umma. Katika kutekeleza hilo, Serikali imeamua kuwa wale wote wasio na vyeti vya kidato cha nne waondolewe kutoka kutumikia umma kwa vile hawakidhi vigezo, mradi tu wawe ni wale walioajiriwa baada ya Mei 20 2004. Naunga mkono uamuzi wa kuimarisha utumishi wa umma kwa kuzingatia viwango vya elimu. Kwa nyongeza, uamuzi wa Serikali unaweza kuboreshwa zaidi kwa kuzingatia pia elimu ya ufundi katika utumishi wa umma.
Zamani, kusoma elimu ya ufundi kulionekana ni kama njia ya kambo kupatia elimu. Elimu ya ufundi ilionekana kuwa ni kwa wale ambao "hawakupasi" vya kutosha kwenda elimu ya sekondari. Watu hao njia yao ya kujiendeleza kielimu ilikuwa na vipingamizi vingi, njia isiyoeleweka inakoanzia wala inakoishia.
Mtu aliyeingia kwenye mkondo wa elimu ya ufundi, kwa mfano, ilimuwia vigumu kusoma masomo ya shahada ('digirii') kwa vile hakukuwa na masomo ya namna hiyo, walau ya kutosha. Watu hao walipokuwa wakijaribu kutoka kwenye mkondo wa elimu ya ufundi kurudi kwenye mikondo mingine, walijikuta wakikabili vikwazo vingi vilivyofanya ionekane 'haiwezekani' wao kusoma masomo ya shahada.
Kwenye baadhi ya vyuo vya elimu ya juu, palitengwa nafasi chache, za ngama, kwa wale waliopitia elimu ya ufundi ("FTC" au vyeti vinginevyo). Hawa waliingia kama 'Watu Wazima waliochelewa kusoma" (Mature Age Entry) hata kama umri wao ulikuwa sawa tu na wa wenzao waliokuwa wanajiunga. Kisha, kulikuwa na kozi chache tu ambazo waliruhusiwa kuzisoma.
Matokeo ya vikwazo vingi kwenye elimu ya ufundi kulifanya jamii idharau elimu ya ufundi na wengi kuikwepa walipoweza kwani haikuwa na njia zilizoeleweka za kujiendeleza kielimu mpaka elimu ya juu. Elimu ya ufundi ikanyanyapaliwa na kuonekana kana kwamba ni kwa wale "waliofeli" kuingia katika mkondo wa elimu "rasmi" ya masomo ya sekondari na vyuo vinavyotoa "elimu", ikiwa na maana ya vyuo vyote visivyotoa "mafunzo" ya ufundi. Matokeo yake vijana wengi walikwepa kuingia mkondo wa elimu ya ufundi.
Kwa kutambua mapungufu haya, serikali iliamua kubadilisha sera na sheria ili kuwezesha ufundi kuonekana nao pia ni "elimu", na ambao "ni sawa tu" na "elimu ya sekondari" iliyoonekana kana kwamba ndio "elimu ya kweli". Mtu aliyemaliza elimu ya msingi akienda sekondari aweze kujiendeleza mpaka kufika elimu ya juu. Mtu huyohuyo aliyemaliza elimu ya msingi akienda elimu ya ufundi aweze kuwa na njia hukohuko elimu ya ufundi ya kujiendeleza mpaka afike elimu ya juu. Ndipo Bunge letu tukufu lilipotunga sheria za elimu ya ufundi, na kuanzisha baraza la kusimamia elimu ya ufundi (NACTE). Baraza hilo, hata hivyo bado halijazoeleka. Wengi hulichanganya na baraza la mitihani (NECTA). Na hata viwango vya elimu vinavyotambuliwa na NACTE havijakubalika kwenye mfumo wa utumishi wa umma namna vile ya NECTA vilivyokubaliwa.
Mfano halisi na rahisi ni huu wa ulazima wa vyeti vya kidato cha nne kwenye utumishi wa umma. Ni wazo zuri, lakini linalotekelezwa kwa mapungufu. Vyeti vinavyotambuliwa na baadhi ya waajiri wa umma ni vile vya NECTA tu katu si vya NACTE. Huu ni upungufu mkubwa sana. Unarudisha nyuma kwa miongo kadhaa mafanikio ya serikali katika kuboresha elimu ya ufundi. Elimu ya ufundi ni muhimu mno katika kujenga uchumi wa viwanda, sawa tu, na pengine kuzidi elimu isiyo ya ufundi. Kumlazimisha mtu aliyepitia mkondo wa elimu ya ufundi inayotolewa na baraza la NACTE alete cheti cha kidato cha nne kinachotolewa na baraza la NECTA ni sawa na kupima weledi wa samaki kuogelea kwa vigezo vya uwezo wa samaki huyo kukwea minazi.
Watumishi wa umma wenye elimu ya ufundi sawa na kidato cha nne (wengi wao kuzidi) wamesimamishiwa mishahara na wako kwenye taharuki kubwa kutegemea waliajiriwa lini. Wale ambao waliajiriwa zamani wanaonekana wamebakizwa kwenye ajira "kwa hisani tu", kwa vile tu, "bahati yao", waliajiriwa kabla ya Mei 20 ya mwaka 2004. Wale wanafunzi waliojitosa kwenye mafunzo ya ufundi (Vocational Training) mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, kwa malengo wakajiendeleze kwenye utaalamu wao mpaka ngazi za juu za utaalamu, bila shaka sasa wengine wao watakuwa wanajutia uamuzi huo. Wanaona Serikali iliyoahidi kutambua elimu yao hiyo, imewageuka.
Tumerudi zamani, kule ambapo ufundi siyo elimu, walau kwa muonekano, siyo elimu kama vile ile "elimu kweli" ya sekondari. Jionee tofauti. Ukisoma sekondari unapata "elimu ya sekondari". Ukisoma ufundi unapata "mafunzo ya ufundi". Hapa ndipo tatizo linapoanzia.
Mapendekezo
Serikali isitishe utekelezaji wa kuwaondoa wasio na mafunzo ya kidato cha nne kutoka kwenye utumishi wa umma, mpaka pale itakapowianisha vizuri mafunzo ya sekondari na elimu ya ufundi. Kwa mfano, kumfukuza mtumishi mwenye mafunzo ya ufundi (National Technical Awards) kutoka Chuo kinachotambuliwa na NACTE au mamlaka ya elimu ya ufundi (VETA), kwa vile tu hana "D" mbili za kumpatia "divisheni 4" ya mafunzo sekondari ya NECTA ni kupoteza nguvukazi ya taifa bila ulazima.
Serikali itambue na kutamka bayana elimu za ufundi katika miundo ya utumishi wa umma sawa na vile inavyotambua mafunzo ya sekondari katika utumishi wa umma.
Serikali iangalie namna ya kukabiliana na sintofahamu iliyoko kwenye kada za ufundi kutokana na miundo mbalimbali ya utumishi wa umma na ya udahili elimu ya juu kutotambua ipasavyo elimu ya ufundi.
HITIMISHO
Mwelekeo wa siku hizi duniani ni kuimarisha elimu ya ufundi, na kuimarisha mafunzo yanayoegemea weledi (Competence-based) zaidi kuliko nadharia.
Manufacturing boom: Trade school enrollment soars
Now is the time to forsake that liberal arts degree for skilled labor
Vocational Education Is Out; Career and Technical Education Is In | EdSurge News
Waajiri wakubwa kwa wadogo, siku hizi wameacha kuangalia vyeti, na badala yake waangalia ujuzi wa mtu, kwani vipo vyeti ambavyo huonekana si lolote si chochote.
Bill Gates And His Foundation: Employers Should Focus On Skills, NOT College Degrees
Uni degree? You don’t need one
Employers value skills over college degrees, workers say
Waajiri sasa hutafuta vipaji (aptitude) na weledi kwa watumishi; makaratasi ya vyeti yakiwa ni kutimiza mradi tu.
A Funny Book about Worthless Degrees | Minding The Campus
The 10 Skills Employers Most Want In 20-Something Employees
Google & 14 More Companies That No Longer Require a Degree
--------------