Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
Ni jambo la kusikitisha na linaloumiza moyo kuona hali ya
miundombinu ya barabara na daraja katika
Kata ya Bunamhala, iliyopo
Wilaya ya Bariadi Mjini. Mbunge wetu,
Mhe. Kundo Andrea Mathew, tunaomba utupie macho hali hii inayotishia uhai wetu.
Kama unavyoona kwenye picha na video, hapa ndipo mahali ambapo:
- Watumishi wa umma hulazimika kupita kila siku kwenda kutoa huduma kwa jamii.
- Wanafunzi na wagonjwa (ikiwemo akina mama wajawazito) wanahatarisha maisha yao kuvuka maji haya ya kasi.
- Wananchi na watumishi wenzetu wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji wakijaribu kutafuta riziki na kulitumikia taifa.
Hatuwezi kuendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa na wapendwa wetu kwa sababu ya daraja na barabara isiyopitika wakati wa mvua.
Tunaiomba mamlaka husika (TARURA) na uongozi wa wilaya ya Bariadi Mjini kuchukua hatua za haraka kabla maisha mengine hayajapotea.