Date::11/15/2008
DPP: EPA bado mbichi, aagiza uchunguzi baadhi ya majadala
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
SIKU chache baada ya kutanda ukimya wa kufikishwa mahakamani watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), Eliazer Feleshi, amesema sakata hilo bado bichi.
Kauli ya DPP Feleshi imekuja siku chache baada ya watu wa kada mbalimbali, kuanza kuhoji kama idadi ya wanaotuhumiwa kwa wizi huo imekamilika baada ya jumla ya watu 20 kupandishwa kizimbani katika muda wa wiki mbili.
Swali kubwa la msingi ni kwamba, kati ya watu maarufu wanaotajwa kwenye sakata hilo la EPA, hadi sasa ni mfanyabiashara Jeetu Patel pekee, ambaye anaonekana kuwa kigogo kati ya wafanyabiashara hao 20.
Hata hivyo, DPP, katika kauli mpya ambayo aliitoa jijini Dares Salaam jana, ameongeza shinikizo la damu kwa baadhi ya watuhumiwa wa EPA akiashiria kuwepo uwezekano wa vigogo wengine, akiwemo waziri mmoja wa serikali ya awamu ya tatu, kutinga mahakamani.
Akivunja ukimya baada ya siku nne za hisia na mawazo tofauti, DPP Feleshi alisema hadi sasa kuna majalada ambayo bado yanafanyiwa uchunguzi.
Alifafanua kwamba hatua ya kuendelea kufanyiwa uchunguzi kwa baadhi ya majadala ni katika kuhakikisha ushahidi wa kutosha unapatikana.
Mkurugenzi huyo, ambaye ofisi yake kwa sasa inaangaliwa na umma kwa umakini, alisema hadi sasa majalada yote ambayo yako kwake yanafanyiwa kazi.
"Kwa majalada ambayo yanahitaji uchunguzi zaidi, yanaendelea kufanyiwa kazi kama nilivyoelekeza vyombo vya uchunguzi vifanye," alisema Feleshi kuthibitisha ubichi wa sakata la EPA.
Alisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ni ya umma inayofanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu au mamlaka yeyote.
"Majalada yote yanayohusiana na EPA yanaendelea kufanyiwa kazi. Kama mnavyoshuhudia, baadhi ya watuhumiwa wamepelekwa mahakamani," alisisitiza.
"Ni kwa misingi hiyo, ninawaomba wananchi kuwa na subira na kuiacha ofisi kufanya kazi yake kwa kwa mujibu wa sheria."
Hadi sasa watuhumiwa 20 tayari wamekwishafikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa EPA, wakiwemo vigogo wanne wa BoT.
Hata hivyo, matarajio zaidi ni kuona vigogo zaidi ambao baadhi yao ni wafanyabiashara wakubwa.
Ufisadi huo wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi wa Kampuni ya Deloitte&Touche ya Afrika Kusini, ambayo ghafla ilisitishwa kazi na BoT bila sababu za msingi baada ya kubaini ufisadi wa sh 40 bilioni zilizochotwa na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.
Hata hivyo, baadaye serikali mwaka jana ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni ya kimataifa, kufanya ukaguzi huo kubaini ukweli.
Ofisi ya CAG iliteua Kampuni ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi wa fedha hizo zaidi ya sh 133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.
Makampuni 13 yalijichotea sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD of Tanzania.
Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.
Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota sh 42.6 ni pamoja na G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.
Makampuni mengine mawili ambayo ni Rashtas (T) na G&T International LTD, kumbukumbu zake ikiwemo nyaraka za usajili katika daftari la Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.
Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na kisha baadaye, deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.
Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.
EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.
Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana.