Siri nzito EPA (Tanzania Daima)
na Salehe Mohamed
SIRI ya kufichuka kwa wizi uliokuwa ukifanyika kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kubainika.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili limezipata kutoka vyanzo vya kuaminika ndani na nje ya serikali, zinaeleza kuwa kubainika kwa siri hiyo kulitokana na hatua ya mfanyabiashara mmoja Mtanzania mwenye asili ya Kiasia, kuamua kulipiza kwa kutoa siri za wizi huo uliofanywa na mfanyabiashara mwenzake mwenye asili ya Kiasia, ambaye alimdhulumu kiasi kikubwa cha fedha.
Habari hizo zinaeleza kuwa wafanyabiashara hao, ambao (majina yao tunayo) walikuwa marafiki wa karibu na walikuwa wakifanya udanganyifu huo kwa pamoja huku wakishirikiana na wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye hivi sasa yuko rumande baada ya kupewa masharti magumu ya dhamana katika kesi inayowakabili, ndiye anayetajwa kumdhulumu mwenzake baada ya kuona amekamilisha nyaraka zote muhimu zilizokuwa zikitakiwa katika kuiba fedha kutoka EPA.
Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya maofisa wa BoT zinaeleza kuwa mpango wa wizi huo uliowafanya wafanyabiashara hao kutengana ulikuwa ni wa zaidi ya sh bilioni 20, ulioandaliwa kwa muda mrefu na kwa umakini wa hali ya juu na wafanyabiashara hao kabla hawajadhulumiana, kama wafanyavyo majasusi mbalimbali duniani.
Mfanyabiashara anayesota rumande hivi sasa ndiye aliyedakia ‘dili' ya mwenzake ambaye alikuwa katika hatua za mwisho za kuzungumza na wafanyakazi wa BoT ili wamsaidie kufanikisha wizi huo.
Inaelezwa kwamba, katika hali isiyo ya kawaida, Mfanyabiashara huyo aliye rumande alipata nyaraka hizo na kuwakalisha kitako wafanyakazi wa BoT ambao waliingia katika mtego wake na kuidhinisha kiasi hicho cha fedha.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hasira za mfanyabiashara aliyezungukwa na kudhulumiwa na mwenzake zilikuwa kubwa baada ya kubaini kuwa amezungukwa na fedha alizokuwa akitegemea kuzipata kutoka BoT zimekwisha kuchukuliwa na kuingizwa katika akaunti za kampuni za aliyemdhulumu zilizo ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya watu walio karibu na wafanyabiashara hao, wameleeza kuwa njama za wizi huo zilifichuka kutokana na hasira ya kuzungukwa aliyokuwa nayo mfanyabiashara aliyedhulumiwa.
Kwa mara ya kwanza mpango wa wizi huo uliwasilishwa kwa mbunge mmoja ambaye anasifika ndani na nje ya Bunge kwa kulipua hoja nzito, anapokuwa akichangia mijadala mbalimbali katika vikao vya Bunge.
Walieleza kuwa tofauti na matarajio ya mfanyabiashara huyo, mbunge huyo aliwasiliana na watendaji wa juu wa BoT na anadaiwa kuwa ili kuhahakisha suala hilo halilipuliwi bungeni, yalifanyika mazungumzo ambayo mpaka sasa yamekuwa siri.
Mmoja wa maofisa wa BoT aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini, alieleza kuwa baadaye taarifa za wizi huo zilisambazwa na mfanyabiashara huyo katika mtandao wa ‘internet' na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) pamoja na wahisani mbalimbali nao walitaarifiwa kuhusu wizi huo.
Kusambazwa kwa taarifa hizo, mtandaoni, kuliwafanya baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), kuzidaka na kutinga nazo bungeni, ambako alilivalia njuga suala hilo na kutaka ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo huku akilitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa hakuna taarifa sahihi za moja kwa moja mwanzoni mwa sakata hilo, na ndiyo maana alipotaka kiasi cha fedha kilichoibwa katika akaunti hiyo alisema ni sh bilioni 800, lakini baadaye ilielezwa na mbunge mmoja anayedaiwa kulijua kwa undani sakata hilo kuwa kiasi kilichoibwa ni sh bilioni 133.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji, alisema taarifa hizo za Dk. Slaa, si sahihi na analidanganya Bunge.
Aliongeza kuwa serikali haifanyi kazi kupitia taarifa za kwenye mitandao ambazo hazina ukweli wowote.
Dk. Slaa, alionyesha nia ya kutaka kutoa hoja binafsi lakini hakufanikiwa, kwani alizimwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliyemwambia nchi haiwezi kuendeshwa kwa kutegemea taarifa za kwenye mtandao.
Fukuto la EPA lilizidi kushika kasi hasa pale wafadhili walipotishia kufunga misaada yao kwa Tanzania mpaka ufanyike uchunguzi katika akaunti ya EPA na hatimaye serikali ilisalimu amri na kuipa jukumu Kampuni ya Ernst & Young kufanya ukaguzi.
Kampuni hiyo iligundua kampuni 22 zilijichotea kiasi cha sh bilioni 133 na kuwasilisha ripoti yake serikalini ambapo Rais Jakaya Kikwete aliamua kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali, aliyekuwa nchini Marekani kwa matibabu.
Pamoja na kutengua uteuzi wa Balali, Rais Kikwete, aliunda timu ya kufuatilia suala hilo iliyokuwa ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, ambayo ilitoa taarifa na kupendekeza wote waliohusika katika wizi warejeshe fedha.
Aidha, timu hiyo iliomba iongezewe muda kutafuta taarifa za kampuni tisa ambazo mpaka sasa hazijaweza kujulikana zilipo.
Rais Kikwete, alikubalina na mapendekezo hayo ya timu hiyo na kutoa muda mpaka Novemba mosi kwa wezi wa EPA wawe wamerejesha fedha hizo la sivyo atawaburuza mahakamani.
Muda alioutoa Rais Kikwete, ulimalizika na baadhi ya wezi walishindwa kurejesha fedha. Hivyo, Rais Kikwete, alimwagiza Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) Elieza Feleshi, kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika kwenye wizi huo.
Feleshi, alianza kulitekeleza jukumu hilo, ambapo mpaka sasa watuhumiwa 20 wameshafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kampuni 22 zilizovuna mabilioni ya EPA ni Bencon International Ltd of Tanzania, VB & Associates Ltd, Bina Resorts Ltd, Venus Hotels Ltd, Njake Hotels Ltd and Tours Ltd, Maltan Mining Company na Money Planers and Consult, Bora Hotels and Apartment Ltd na BV holdings Ltd.
Nyingine ni Ndovu Soaps Ltd, Navy Cuts Tobaco Ltd, Changanyikeni Residential Complex, Kagoda Agriculture Ltd, G&T International Ltd, Mibale Farm Liquidity Sevices Ltd, Clyton Marketing Ltt, M/s Rastash, Malegesi Law Chambers, Kiloloma and Bothers na Karnel Ltd.
Hadi sasa jumla ya washitakiwa 20 wa EPA wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma zinazowakabili kuhusiana na wizi huo.