Bosi wa Tanroads aitunishia serikali msuli
Na Restuta James
13th November 2009
Awabandua wakurugenzi watatu
Wamo mameneja watatu
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Ephraem Mrema, ameitunishia misuli bodi ya wakurugenzi ya taasisi hiyo na Wizara ya Miundombinu kwa kupuuza maagizo halali yaliyotolewa kwake.
Kinyume cha maelekezo ya wakuu wake kwamba asiwafukuze kazi wakurugenzi na mameneja wa mikoa bila kufuata taratibu za utumishi serikalini, Mrema ambaye awali alitii agizo hilo na kusitisha uamuzi wake, baadaye aligeuka tena na kuendelea na maamuzi yake ambayo sasa yameamsha taharuki kubwa ndani ya taasisi hiyo yenye dhima ya kujenga na kusimamia matunzo ya barabara kuu nchini.
Sakata hili ambalo sasa linaonekana kama ni mapambano ya kimamlaka kati ya Mrema, Bodi ya Tanroads na Wizara mama, lilianza Oktoba 30, mwaka huu, baada ya kiongozi huyo kuitisha kikao cha wafanyakazi na kutangaza kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji waandamizi ambao ni Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara, Thomas Mosso; Mkurugenzi wa Mipango, Jason Rwiza na mameneja wa mikoa mitatu ya Dodoma, Gerson Lwenge; Morogoro, Charles Madinda na wa Ruvuma, Abraham Kissimbo. Pia kwenye orodha hiyo yupo William Shilla ambaye ni mhandisi makao makuu Tanroads.
Habari zilisema kwamba watendaji hao waandamizi walionyesha wazi kukataa kukubaliana na hatua hizo kwa sababu zilikuwa ni kinyume cha taratibu na hivyo wakakata rufaa wizarani.
Baada ya mamlaka hizo kupata kilio cha watendaji hao, zilitengua maamuzi ya Mrema kwa kuwa hayakuzingatia taratibu za Tanroads.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mrema juu ya suala hilo ambazo Nipashe imeziona, kiongozi huyo
Novemba 6, mwaka huu aliwaandikia wafanyakazi wote waraka wa kutangaza kusitisha utekelezaji wa tangazo la kikao chake na wafanyakazi cha Oktoba 30, 2009 kwa kuwa alikuwa amepata maagizo kutoka Serikalini ya kusitisha tangazo lake.
"Napenda kuwajulisheni kwamba nimepata agizo la Serikali kwamba uteuzi wa wakurugenzi na viongozi wengine wa Tanroads umesitishwa, aidha," sehemu ya waraka huo inasomeka na kuongea kuwa:
"Serikali imeagiza kuwa mchakato wa uteuzi wa viongozi hao utatakiwa kufuata kanuni za ‘Executive agencies' kwa kuzingatia usawa, uwazi na ushindani…kutokana na hayo, napenda kukujulisheni kwamba mawasiliano hivi sasa yanaendelea na mamlaka husika jinsi ya kutekeleza agizo hili kulingana na muundo wa Tanroads ulioidhinishwa."
Hata hivyo, siku tatu baadaye yaani Novemba 9, Mrema aliandika waraka mwingine wa kutengua ule wa Novemba 6, akidai kuwa ulikuwa umesambazwa kwa wafanyakazi kimakosa ijapokuwa ulikuwa na saini yake.
Badala yake alisema kwamba maofisa waandamizi waliokuwa wamefutwa kazi maamuzi yake yanaendelea kama alivyokuwa ameamua na kutangaza kwa wafanyakazi wote Oktoba 30, mwaka huu, kwani alikuwa amepata baraka za mamlaka za juu.
"Nasikitika kuwajulisheni kwamba taarifa ya kusitisha utekelezaji wa waraka wa terehe 30 Oktoba 2009 ilitumwa kwenu kimakosa kabla ya kupata kibali cha mtendaji mkuu kwa hiyo waraka huu unafuta waraka wa kusitisha utekelezaji wa waraka wa Mtendaji Mkuu wa Novemba 6 na unawajulisha kwamba uteuzi wa uongozi uliotajwa Oktoba 30 umeanza kazi rasmi Novemba 1, 2009 na umepelekwa katika ngazi husika kupata baraka za mwisho," alisema Mrema katika waraka huo.
Katika waraka huo, Mrema alitangaza kusitisha mikataba ya wahandisi waandamizi sita, yaani Mosso, Rwiza, Shilla, Lwenge, Madinda na Kissimbo.
Kwa mujibu wa waraka huo, tayari nafasi za mameneja hao zinashikiliwa na wahandisi wengine ambapo Mkoa wa Dodoma unashikiliwa na Dorothy Mtenga; Morogoro, Obrien Machange, wakati Yusuph Mazana amepelekwa Ruvuma.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinaonyesha kuwa mikataba ya wahandisi waliofukuzwa kazi ilikuwa haijamalizika wala hawakuwa wametimiza umri wa kustaafu.
Wafanyakazi ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, waliliambia gazeti hili kuwa Mrema amekuwa akitamba kwa wafanyakazi kuwa mabadiliko yote anayofanya ndani ya wakala huo ni utekelezaji wa ahadi yake alipokuwa akipewa ajira.
Walisema awali, kila baada ya miezi mitatu, wakuu wa idara na mameneja wa Tanroads wa mikoa walikuwa na utaratibu wa kukutana katika vikao kwa ajili ya kuangalia utendaji wa wakala huo, lakini Mtendaji huyo aliufuta utaratibu huo na kueleza kuwa Tanroads haiwezi kuendeshwa kwa vikao.
Mfanyakazi mmoja wa wakala huo alidokeza kuwa kwa miaka miwili mfululizo, Mrema amekuwa akifanya mabadiliko makubwa ndani ya Tanroads na anapoulizwa anasema anadhani huo ndio utendaji bora.
Mwandishi wa habari hizi alipoomba kukutana na Mrema jana, alielezwa kuwa yupo kwenye kikao nje ya ofisi na kwamba asingeweza kurudi ofisini mapema.
Gazeti hili lilipomtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Tanroads, Abel Mwaisumo, ili kuzungumzia madai hayo, lilielezwa kuwa yupo nje ya nchi kwa matitabu.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Samwel Nyantahe, alithibitisha kuwa na taarifa ya Mrema kupindisha maagizo ya bodi na kusema kuwa bodi na Wizara zinakutana leo jijini Dar es Salaam kujadili suala hilo.
"Bodi imekwishapokea ‘allegations' (madai) yote kutoka kwa wafanyakazi na sisi tunayafanyia kazi, tulikutana Jumatatu tulijadiliana na kesho (leo) tutakutana tena, hii yote ni kuhakikisha kuwa tunayapatia ufumbuzi matatizo haya," alisema Dk. Nyantahe.
CHANZO: NIPASHE
http://www.ippmedia.com/frontend/index.php?l=9728