Tunarukaruka kama Manyani hatujui ni mti gani tunaupenda tukabangaize! Thread nzima imekosa mwelekeo maana hakuna kinachoeleweka kinaendelea.
Nitachangia kwa mtazamo wangu kutokana na kauli ya Mbunge na mitazamo ya wachangiaji hapa.
1. Mbunge kahoji; Jinsi Mrema alivyopata kazi kwa mlango wa nyuma huku hakuwa kwenye Semi Fainali ya Usaili. Hili ni halali na muhimu kujua ni vipi Mrema aliweza kuletwa na kupewa kazi. Je kuna kumbukumbu za kuonyesha ni jinsi gani mchakato wa kutafuta CEO mpya ulivyofanyika? Je kuna provision gani za kuruhusu late applicants kama Mrema aliwasilisha CV yake wakati usaili umeanza? Je Alichaguliwa kwa Merits zipi na lile jopo lililomchagua yeye na si wengine?
2. Mbunge kahoji; Mshahara na marupurupu ya Mrema ni ya Kifisadi. Hili halina nguvu na tena lawezakuwa Mbunge alitumia hoja hii ili kulazimisha hoja yake ya Kwanza na ya tatu (kutishia wafanyakazi) zipate nguvu.
Kama Mghana aliyekuwepo alikuwa analipwa mshahara na marupurupu hayo hayo, kwa nini Mtanzania asilipwe hivyo hivyo? Kwa nini Mtanzania aendelee kuwa Daraja la Tatu lakini wengine wabebwe na kulipwa First Class? Je Mbunge na hata Wachangiaji wengine humu tumesahau kuwa tumelia kwa muda mrefu kuhusu Mishahara midogo na kupuuzwa? Je tunasahau katika mfumo wetu mpya wa Uchumi ambao umeachana na Ujamaa, ni kuwa mishahara si maamuzi ya Kamati kuu bali ni uwezo wa ushawishi wa anayetaka kazi kutaka alipwe mshahara unaolingana na Elimu, Uzoefu, Ufanisi na Utendaji (track record)? Kuna mwana JF katoa maoni kuwa akiwa Mtanzania alipwe Shilingi kwa kufuata viwango vya mishahara ya Serikali, lakini akiwa ni Mgeni asiye Mtanzania, basi tumlipe ki-ulaya ulaya, this does not make any sense. Kwa nini ajira ya kazi hiyo hiyo iwe na mishahara ya kiubaguzi?
3. Mbunge kahoji; Mrema alitishia ajira za mfanyakazi aliyefuata sheria. Hili ni haki na halali kuhoji kwa nini Mrema atishie maslahi ya mwingine kisa mfanyakazi kufuata kanuni? Hili pia linahitaji uthibitisho, maana mpaka sasa limekaa ki-umbea umbea na Mbunge sidhani kama amewasilisha vielelezo ikiwa ni pamoja na mfanyakazi kuandika barua ya kulalamika kwa Bodi ya Tanroads au kwenda Idara ya Kazi kuwasilisha malalamishi. Ikiwa itabainika Mrema ni kweli alitumia vitisho kupindisha kanuni, je ni hatua gani zichukuliwe kutokana na mwongozo wa kiutendaji (employee hand book)wa Tanroads?
4. JF inahoji; Wasifu wa Mrema. Kuna wanaosema ni mchumi wa ujenzi, project management, kafanya kazi katika mashirika mbali mbali ndani na ya imataifa katika masuala ya miuondo mbinu. Swali linarudi kwa wana JF, je ni lazima CEO wa Tanroads awe Mhandisi wa Ujenzi? what about Chemical Engineer, Electrical Engineer, Geologist, Architect, Lawyer, Economist, Accountant, Agro Economist, Nuclear Phycist?
Je kwa kuwa kazi ni kujenga barabara ni lazima awe ni mhandisi wa ujenzi (civil engineer) au kuwa na shahada ya Uhandisi wa Ujenzi ni added value na bonus?
Kazi ya CEO ni nini? ni kuchukua supatu, sululu, jembe, kisu, wrench, boiler na kuingia kazini au ni kusimamia uendeshaji mzima wa Taasisi kuhakikisha malengo ya Taasisi na kazi zake zinafanyika kwa Ufanisi? Je si kuna Wataalamu wa Research, Archirtect, Soil composition, Surveyors, Construction design, Civil Engineereing, Chemical Engineering, Accountants, Marketing, Environmental studies na fani nyingine ambao wamo katika Idara za Tanroads na wajibu wao ni kufanya kazi za kitaaluma kutumia Utaalamu wao kuhakikisha kila kitu ni sawa?
Hivyo basi kama track record ya Mrema ni mbovu na hana uwezo wa kutuonyesha alichofanya iwe Tanzania au kwingineko, basi si suala la Elimu yake bali ni ukosefu wa Ufanisi ambao tupigie kelele na kuhoji kwa nini kapewa majukumu makubwa wakati uwezo hana. Lakini kama kuna proven track record ya kazi alizosimamia na mashirika aliyofanya kazi, basi kulalama kuhusu CV yake ni waste of time.
5. JF na Ukabila; Badala ya kuangalia merits za mtu, tumeangalia ni kabila gani na ni yapi ambayo tunadhania kwa hisia kayafanya kwa Upendeleo wa Kikabila. Mzee Mwanakijiji kaanzisha mada nzuri sana inayoshibana na suala la Ukabila, Udini na kauliza kama 58% au 68% ya Kamati kuu ya CCM ni Waislamu, je ni sawa kudai CCM ina Udini?
Swali ni hili, jee Mrema alipofika Tanroads, ni Wataaalamu wangapi na Wakandarasi wangapi ambao ni mahiri ni Wachaga? Ikiwa 75% ya Wafanyakazi wataalamu wa Tanroads na Contractors ni Wachaga, tutamlaumuje Mrema kuwa yeye ni Mkabila? Je mnaodai ana ukabila, mna vithibitisho gani kuwa anafanya kazi kwa kutumia Ukabila na kutoa Upendeleo wa Mikataba kutokana na Ukabila?
5. Hisia na Upembuzo Yakinifu wa JF; Hapa JF ni Jungu Kuu ambalo lina watu kutoka makabila mbali mbali, fani mbalimbali na upeo tofauti. Kuna walioko Tanzania na walioko Ughaibuni.
Niaanza kwa kuzungumzia Ufanisi na Elimu. Suala la Tanroads na CEO wake si la kwanza kutuvuruga JF. Watanzania tunachanganya sana suala la Usomi na Uwezo wa kufanya kazi. Elimu ni nyenzo ya kufanya kazi, inasaidia kufanya kazi, lakini elimu haina maana mtu atakuwa mahiri na mwenye ufanisi, muadilifu au mnyenyekevu. Sisi tumejenga Tafsiri na kasumba potofu kuwa Ukiwa na Shahada na Udakitari, basi wewe ni bingwa. Kipimo cha Ufanisi wa mtu si Elimu na Shahada alizonazo, bali ni matendo yake, uwezo wake wa kuelewa mambo, Uwezo wa kuwa Mbunifu.
Kwa Tanzania ya sasa tunatafuta Malaika maana tumekulia na kuiva kutokana na watu wazembe, wavivu, wasio na tija na waliokosa motisha. Je kuwa na PHD ndio solution? hapana. Tanzania itaanza kuwa fanisi pale siku watu watyakapoamua kujipa motisha wa kuamka na kwendha kuchapa kazi, kutumia juhudi na maarifa waliyonayo.
Tanzania itapata maendeleo katika Utendaji wa mashirika,Serikali, Taasisi, Watu binafsi, Wafanyakazi na Wakulima , tukiamua kuachana na visingizio na visababu visivyo na msingi na focus yetu kuwa kuzalisha mali kwa bidii, ufanisi, ubora, tukiwa wabunifu, wenye tija na kuchochea motisha.
Tunalilia mishahara mikubwa, lakini hatuzalishi vya kutosha ili kukidhi matumizi ya uzalishaji na mishahara ya wafanyakazi. Je tutawezaje kupiga hatua? Ni vipi Mzungu, Mhindi, Mkenya, Mwarabu, Mchina wakija Tanzania wanakuwa na Ufanisi na Juhudi za kuchapa kazi lakini tukipewa hatamu sisi wenyewe tunashindwa kujiongoza na kujiendesha?
La mwisho ni kupotea kwa Watanzania katika mfumo wa Uzalishaji mali na Uchumi. Tumekomaa sana katika Ujamaa, mawazo yetu bado yako katika Ujamaa wa kulazimisha kuwa kuishi kimaskini ndio fahari ya Mtanzania. Tunaona "ubepari" kuwa ni unyama na kuwa na mishahara mikubwa ni Ubepari na Unyonyaji. Tunaona kuishi katika Ufukara ndio Utu, sawa, haki na thawabu, na labda pia ni kutokana na mapokeo yetu potofu ya Imani zetu hasa Ukristo kuwa ni Rahisi kwa masikini kuingia Mbinguni kuliko Tajiri ambaye ni sawa na Ngamia kupita tundu la sindano!
Ni mentality hii ambayo inatufanya tuone ni halali kwa Odhiambo, Montgomerry, Olatunde, Zhang, Iqbal na Al Muneiz walipwe mishahara ya Kimataifa wanapofanya kazi Serikalini mwetu au kwenye Mashirika yetu. Tunahalalisha wao kuwa Mabepari na Wanyonyaji bila hata kuwa na kinyongo zaidi ya kulalamika kuwa mbona sisi mishahara yetu ni kiduchu. Mbaya zaidi, ikiwa hawa Wageni wakazi ndio wenye makampuni yao na yanafanyakazi Tanzanzia, ufanisi wetu huwa marudufu ya Watanzania wenzetu wanaofanya kazi katika mashirika ya umma na Serikali.
Lakini tukisikia Masauni, Mallya, Mutakyamirwa, Bundala, Ngonyani, Ole Saibul, Marwa, Mchafukazi na wengine ambao ni Wazawa na wanalipwa fedha nono, huwa tunajenga chuki na kuanza kuwalaumu kutumia dini, ukabila na hata kuhoji elimu zao.
Badala ya kudai kwa Serikali na Waajiri wetu kuwa viwango vya mishahara yetu havitoshi na ni vidogo kulingana na kazi na ujuzi na hata kukidhi ukali wa maisha, tunawasakama wale wachache ambao wameweza kupata upenyo kuvunja mfumo mbovu wa Kiuchumi na Kiitikadi.
Najua tutaka kujua Mattaka, Idrisa, Kimei, Ndulu na ma CEO wengine wote tujue mishahara yao, ili tupime nini? Ufanisi au ni kulalama bila kuwa na mwelekeo?
Suala la Mrema, kama kuna yaliyosemwa na Mbunge yatathibitika kuwa ni kweli, basi hatua za kinidhamu zichukuliwe. Jiandaeni kuangua kilio mkidai afukuzwe mkakuta kuwa katika mkataba wake wa ajira kuna kipengele cha kulipwa fedha bwelele akifukuzwa kazi!