JUMLA ya vocha za pembejeo za kilimo 1,114 zenye thamani ya zaidi Sh 21 milioni kati ya vocha 34100 zilizogawiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro zimepotea katika mazingira mbalimbali kwa mawakala wa kata tatu za Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, ofisa kilimo, mifugo na ushirika, Dk Issack Khama alisema Januari 14 mwaka huu, ofisa mtendaji wa mtaa wa Lukobe kata ya Kihonda, Salma Mbandu alitoa taarifa juu ya kupotea kwa vocha 300 ambazo alikabidhiwa.
Alisema katika taarifa ya ofisa mtendaji huyo juu ya upotevu wa vocha hizo alidai kuwa baada ya kukabidhiwa vocha hizo akiwa njiani kwenda katika ofisi yake kuendelea na ugawaji wa vocha , alitumia usafiri wa pikipiki ambapo alizifunga nyuma ya pikipiki vocha hizo ambapo zilidondoka njiani na yeye kutoziona wakati zilipoanguka
Dk Khama alimtaja wakala mwingine kuwa ni ofisa mtendaji wa Ngerengere Mkangwa ambaye aliibiwa vocha 300 katika mtaa huo, baada ya kuziacha ofisini Januari 22 na aliporejea ofisini Januari 25 hakuzikuta na katika mtaa wa Mindu, zilipotea vocha 514 baada ya Mwenyekiti wa kamati za vocha za mtaa, Iddi Kassimu kuzihifadhi nyumbani kwake na kuvunjiwa nyumba na hivyo kuibiwa vitu mbalimbali zikiwemo vocha hizo.
Hata hivyo Dk Khama alisema baada ya kupokea taarifa za wizi huo, ofisi yake iliripoti kwenye vyombo husika ikiwemo ofisi ya katibu tawala wa mkoa, kamati ya vocha ya wilaya ambayo inasimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambapo mawakala hao walitoa taarifa polisi ambapo uchunguzi zaidi kuhusu upotevu huo unaendelea.
Dk Khama alisema kati ya vocha hizo zilizogawiwa, vocha 1,114 ziliibiwa ambazo ni 361 za mahindi aina ya chotara, 375 za mbolea ya kupandia na 378 za mbolea ya kukuzia aina ya urea ambapo Januari 14 mwaka huu ofisa mtendaji wa mtaa wa Lukobe kata ya Kihonda Salma Mbandu alitoa taarifa juu ya kupotea kwa vocha 300 ambazo alikabidhiwa.
Alisema kuwa awali halmashauri ilipokea vocha 10,500 za mbolea za kukuzia 10100 za kupandia 10,500 za mahindi aina ya chotara, za mahindi mchanganyiko 2000 na za mbegu za mpunga 1000 ambapo ofisi hiyo ilizigawa kwa wenyeviti wa kamati za mitaa, maafisa watendaji wa mitaa hiyo mitatu ndio walihusika katika kusaini na kupokea vocha hizo.