BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Kuongezeka kwa biashara ya mafuta ya kupikia kunaweza kuwa na manufaa kwa uchumi wa nchi, lakini kufanya biashara hiyo katika mazingira ya wazi, ni hatari kwa afya ya watumiaji.
Uuzaji wa mafuta ya kupikia kwenye maeneo ya wazi hukaribisha uwezekano wa athari za oksaidi, ambazo zinaweza kusababisha harufu ya uozo ambayo ina athari kwa walaji.
Athari za oksaidi husababisha kuundwa kwa viini vinavyoharibu mafuta ya kupikia na bidhaa nyingine za vyakula.
Ripoti ya mwaka 2020 ya ‘Health Implications of Rancid Fats and Oils’ iliyochapishwa na Taasisi ya Olive Wellness, inaonyesha ulaji wa mafuta hayo unaweza kupunguza thamani ya lishe ya chakula kwa kuharibu vitamini muhimu, zikiwamo za A na E.
“Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuoza kwa bidhaa zinazozalishwa na mafuta ya oksidi kunaweza kuwa na madhara kwa afya. Hii imehusishwa na maendeleo ya hali ya kuharibika kwa nyurolojia inayosababisha magonjwa ya Alzheimer’s na Parkinson,” inasoma sehemu ya ripoti hiyo.
Tanzania yachukua hatua
Hatari hizo za kiafya zimelifanya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na wadau wa mafuta ya alizeti nchini, kutangaza msako mkali dhidi ya mafuta ya kupikia yanayouzwa katika mazingira ya wazi, hususan katika mikoa ya kati ya Tanzania.
Wanachama wa Chama cha Wasindikaji wa Alizeti Tanzania (Tasupa) waliohudhuria mkutano uliowakutanisha wadau kadhaa hivi karibuni, waliliambia gazeti hili bila kutaja majina yao kuwa uuzaji wa mafuta kwa mtindo huo ulisababisha matatizo kadhaa ya kiafya.
“Ni pamoja na watoto waliodumaa, aina tofauti za saratani, shinikizo la damu, ongezeko la viwango vya lehemu na gundi kwenye mishipa ya damu na kusababisha upungufu wa nguvu za kiume,” alisema mwanachama mmoja.
Alisema wafanyabiashara wengi wa mafuta ya alizeti si wasindikaji, bali wamechapisha lebo zinazofanana na zile zinazotumiwa na wasindikaji halisi na kuzitumia bila ridhaa na ujuzi wao.
Kulingana na chanzo hicho, wafanyabiashara wengi hawajapata mafunzo kuhusu njia za kuzalisha bidhaa na mbinu bora za uhifadhi.
“Baadhi yao hutumia vifungashio vilivyotumika kuuza bidhaa hiyo kando ya barabara kuu na nje ya maduka. Wachache wanaomiliki viwanda vya usindikaji, wanazingatia mahitaji ya usafi,” imeelezwa.
Hata hivyo, mmoja wa wamiliki wa viwanda vya kusindika alizeti, George Njela alisema baadhi ya wasindikaji hawana utaalamu wa usindikaji wa mafuta ya alizeti.
Alisema wengine wanatuhumiwa kwa kuchakachua, bidhaa iliyochakatwa huchanganywa na vitu vingine kama vile mafuta ya transfoma.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tasupa, Ringo Iringo alisema kikao hicho kilichoitishwa Oktoba 19, mwaka huu, kiliazimia mafuta ya alizeti yanayouzwa kwenye mazingira ya wazi yakamatwe na kuharibiwa ili kulinda afya ya mlaji.
“Uamuzi huo umefikiwa baada ya TBS kueleza wasiwasi wake juu ya madhara yanayoweza kutokea kiafya, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kusababisha magonjwa hatari kama saratani, moyo na mishipa kutokana na ongezeko la korestro kwenye mishipa ya damu, magonjwa ya tumbo, koo, kuhara na matatizo ya ngozi,” alisema.
Iringo alisema TBS ilisisitiza haja ya kuuza mafuta ya kupikia na vyakula vingine katika maeneo yenye vivuli na joto la kawaida.
Alisema Tasupa na wanachama wake wanawajibika kuhakikisha usalama wa afya kwa wananchi kwa kushirikiana na TBS, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) na watendaji wa afya.
“Tunaiunga mkono TBS katika uamuzi huo wa kuhakikisha bidhaa hiyo inaondolewa kwenye soko la kanda ya kati na kuelimisha jamii kuachana na matumizi ya bidhaa hizo,” alisema.
Alisema kwa kushirikiana na wadau wengine, wakiwamo Mennonite Economic Development Associates (Meda) Tanzania, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (Usaid), BusinetAfrica na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), wamekuwa wakitoa elimu na kutoa mafunzo kwa jamii.
Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka, alisema mafuta ya kupikia na vifaa vingine vya matumizi vinapaswa kuuzwa katika mazingira ya halijoto linalopendekezwa ili kulinda ubora wake. Alisema TBS imeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya biashara ya bidhaa za chakula katika mazingira ya wazi, hivyo kusababisha changamoto za kiafya kwa walaji.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tasupa, Daudi Mwasantaja alisema wafanyabiashara wa alizeti wanapaswa kufuata maelekezo ya afya na kuepuka kuweka mazao kwenye mazingira ya wazi.
“Watanzania wachangamkie kila fursa bila kuumiza afya za wananchi. Tuna magonjwa makubwa siku hizi, watoto chini ya miaka 18 wanaweza kugundulika kuwa na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi au matatizo ya moyo na mishipa,” alisema.
MWANANCHI