Mkuu Marire, Habari za Jiji la "Rock City"?
Pamoja na baadhi ya michango iliyopo kwenye uzi huu, jaribu kutafuta Uzi wenye Kichwa cha Habari "Ifahamu VSLa (Village Saving and Loan Association)/VICOBA". Uzi huo uko kwenye Jukwaa la Ujasiriamali na ulianzishwa tarehe 18/04/2012. Uzi huo utakuelewesha baadhi ya mambo muhimu unayotakiwa kuyafahamu kuhusu Mfumo wa Hisa (VICOBA).
Naomba sasa nikusemeshe machache. Kwanza ni vizuri kuwa tayari wewe na Wafanyabiashara wenzako mmeanzisha, kwa nia nzuri kabisa, "mchezo". Huo ni mwanzo mzuri. Hata hivyo ninadhani kuo "mchezo" wenu haustahili kuitwa "upatu". "Upatu" ni kitu hatari, na kukitekeleza ni kuvunja Sheria za Nchi (usiniulize Sheria namba ngapi, ya mwaka gani, n.k. - sijui). Ila ukiona kitu kinaitwa "Upatu" kimbia mbio kama Bolt - ni janga!
"Mchezo", kama huo wa kwenu, una mazuri kadhaa. Hata hivyo wingi wa mapungufu yake unazidi hayo wazuri machache. Kuokoa muda, sitataja mazuri. Ninakutajia baadhi tu ya mapungufu ya "mchezo" wenu: 1. Pesa yenu (mitaji) itabaki pale pale, haitakuwa wala kuongezeka, kama ulivyosema. Leo ni tarehe 20/03/2014. Tuseme "mcheze" kwa miaka mitatu mfululizo, tarehe kama ya leo baada ya miaka hiyo mitatu, mchango wako kwenye Kikundi chenu utakuwa palepale, yaani Sh. 50,000/= bila kujali anguko/ongezeko la thamani ya Shilingi ndani ya muda huo 2. "Mchezo" hauna dhamana. Kwa mfano, mmecheza hadi mtu wa saba halafu inatokea mmoja anapata tatizo linalopelekea kushindwa kuchanga kama kifo, ajari, kuugua, n.k., inakula pande yenu hasa pande ya wale ambao zamu yao inakuwa haijafika 3. "Mchezo" kama huo wenu unamfanya Mwanakikundi atarajie kiasi fulani cha pesa kwa muda fulani, hakuna mabadiliko 4. "Mchezo" unamlazimisha Mwanakikundi achukue/apokee fedha, Sh. 500,000/=, zamu ikifika hata kama haihitaji kiasi hicho siku hiyo 5. "Mchezo" ni jela ya aina yake. Yaani mnapoanza mzunguko, Mwanakikundi anakuwa hana uhuru wa kutoa mchango pungufu, au kutotoa kabisa, hata kama mambo yake ni magumu. Sio kila siku zinalingana. Hii inaweza kumsababishia Mwanakikundi huyo Msongo wa Mawazo na hivyo kusababisha matatizo makubwa zaidi 6. "Mchezo" mara nyingi hauna fungu la pembeni la kusaidiana inapotokea Mwanakikundi amepata dharura kama kuugua, kuuguliwa, kufiwa, kufa, kupeleka mtoto Shule, n.k.
Nia yako ya kubadilika kutoka kwenye "mchezo" kwenda kwenye Mfumo wa Hisa/VICOBA ni nia endelevu. Ni kweli, mngepata Mtaalamu hapo Mwanza atakayewapa Darasa na kisha kuwasimamia kwa kipindi hadi mtakapo komaa, ni wazo zuri sana. Miaka kama minne iliyopita nilishuhudia Vikundi vya Mwanza vinalipa Wataalamu wa Hisa/VICOBA kati ya Sh. 50,000/= - 100,000/= kwa kila siku anayokuja kufundisha Kikundi! Sifahamu kama hilo bado lipo. Jaribuni kuongea na Mashirika mbalimbali kama CARE na CRS, wako Isamilo, ili waweze kuwasaidia. Jaribu vilevile kwenye Halmashauri ya Jiji, Idara ya Maendeleo ya Jamii, unaweza pata msaada wa Wataalamu, lakini sio kwa bei hiyo niliyoitaja - huo ni wizi!
Hebu sasa tupige hesabu ya kawaida tu ya Kikundi chenu kama kitabadilika kutoka "analogia" (Mchezo) kwenda "dijitali" (Mfumo wa Hisa/VICOBA)
Tuseme: 1. Hisa moja iwe Sh. 10,000/= 2. Ratiba ya kukutana Kikundi chenu, ili kununua Hisa (kuweka Akiba) ibaki siku moja kwa Wiki kama mnavyofanya sasa hivi 3. Kila Mwanakikundi akaendelea kujiwekea kiasi kilekile kama sasa yaani Sh. 50,000/= kwa wiki, yaani Hisa 5 (Sh. 10,000/= X Hisa 5 = Sh. 50,000/=) 4. Idadi ya Wanachama ikabaki ile ile ya Watu 10 mliopo; Ina maana jumla ya Mtaji wenu kama Kikundi kwa Wiki, utakaotokana na Akiba/Hisa zenu, utakuwa: Sh. 50,000/= x Wanachama 10 = Sh. 500,000/=. Kwa mwezi itakuwa: Sh. 500,000/= x Wiki 4 = Sh. 2,000,000/=. Kwa Mwaka mtakuwa na Mtaji wa: Sh. 2,000,000/= x Miezi 12 = Sh. 24,000,000/=. Katika kiasi hicho, wewe Mkuu Marire, kama utakuwa na nidhamu ya kujiwekea Akiba/Kununua Hisa 5 (yaani Sh. 50,000/=) kila wiki kwa Mwaka mzima, Jumla ya Sh. 2,400,000/= taslimu zitakuwa ni za kwako - mgawo wako bila chenga!
Mwaka ukifikia mwisho, yaani mkifikia mwisho wa Mzunguko, mnaweza kufanya maamuzi ama 1. kugawa Akiba/Hisa kwa kadri ya kila Mwanakikundi alivyoweza kujiwekea 2. kugawana sehemu ya Akiba/Hisa hiyo ili kinachobaki kiweze kuendeleza Mtaji wa kukopeshana au 3. kutogawana kabisa na fedha hiyo ikaendelea kukopeshana kwa Wanakikundi.
Uzoefu wangu kwa Jiji la "Rock City", Jiji Safi kuzidi yote hapa Afrika ya Mashariki, Jiji la Sato, Sangara na Mumi, kiasi cha Sh. 2,400,000/= unaweza kulipia Karo za Watoto wawili wa Shule ya Msingi katika Shule za "International - Bongo" zinazofundisha kwa "yes" na "no", unaweza kununua bonge la kiwanja Luchelele, Igoma, Kiseke, n.k. au hata kulipia Mahari toto zuri kabisa la Kisukuma (na bado chenji ikabaki)! Unaweza vile vile kuirudisha kwenye Biashara yako ili kupanua Mtaji! N.k.
Hesabu iliyoko hapo juu imeongelea Akiba/Hisa zenu tu mlizojiwekea kwenye Kikundi. Kikundi cha Hisa/VICOBA ni Kikundi cha Kuweka (Akiba) na Kukopeshana. Fedha ya kukopeshana, kwa masharti nafuu, inatokana na Akiba/Hisa zenu Wanakikundi mnazojiwekea kwenye Kikundi chenu. Tunaposema "kukopeshana kwa masharti nafuu" ni pamoja na Rida/Ziada ya Mkopo unaotolewa kwa Mwanakikundi kuwa kidogo ikilinganishwa na viwango vinavyotozwa na Taasisi za Fedha yaani Mabenki, SACCOS, n.k. na Wakopeshaji wa Mitaani (Loan Sharks). Vilevile Masharti nafuu ni pamoja na muda unaotolewa kwa Mwanakikundi "kuzungusha" huo Mkopo kwenye Biashara/Shughuli yake kabla ya kurejesha. Kiwango cha Riba/Ziada ya Mkopo inayopendekezwa, mara nyingi, ni 10% na muda ambao Mwanakikundi anaruhusiwa "kuzungusha" Mkopo wake kwenye Biashara zake mara nyingi ni miezi mitatu.
Ina maana, Mkuu Marire, ukikopeshwa leo, tarehe 21/03/2014, Sh. 1,000,000/= unaruhusiwa kurejesha Mkopo huo tarehe 21/06/2014! Kati ya leo, unapokopeshwa na Kikundi, hadi siku ya kurejesha, utatakiwa uwe unalipa Riba/Ziada ya Mkopo kila Mwezi kutegemea na Katiba yenu. Mfano kama Katiba yenu inasema Riba/Ziada ya Mkopo ni 10%. Hivyo tarehe 21/04/2014 utalipa Riba/Ziada ya Mkopo ya Sh. 100,000/=, utalipa tena Riba/Ziada ya Mkopo ya sh. 100,000/= tarehe 21/05/2014 na tarehe 21/06/2014 utalipa Mkopo yaani Sh. 1,000,000/= kujumlisha Riba/Ziada ya Mkopo ya mwezi huo wa tatu ya Sh. 100,000/=.
Fahamu kuwa Riba/Ziada ya Mikopo kwa Mikopo yote inayotolewa na Kikundi kwa Wanakikundi, inapolipwa inalipwa kwenye Kikundi na inachanganywa na Hisa/Akiba za Wanakikundi na hivyo kupanua Mtaji wa kikundi kukopesha mikopo zaidi kwa Wanakikundi.
Hivyo kiasi cha fedha kinachogawanwa na Wanakikundi mwishoni mwa mwaka ni = (Hisa/Akiba za Wanakikundi + Riba/Ziada ya Mikopo + mapato mengine kama faini, n.k.) Kama Kikundi kikiendesha shughuli zake kwa ufanisi, yaani 1. Wanakikundi wakanunua Hisa/Kuweka Akiba ipasavyo 2. Wanakikundi wakakopa kwa bidii; na 3. Wanakikundi wakarejesha kwa ufanisi na kwa wakati, basi Faida/Ziada itakayopatikana kwa Mwaka mzima ni kati ya 30% - 40%, yaani kila Sh. 1 itazaa kati ya senti 30 hadi senti 40!
Mkuu Marire, tukirudi kwenye hesabu zako hapo juu, yaani Hisa/Akiba yako ya Sh. 2,400,000/= itakuwa "imezaa" kati ya Sh. 720,000/= hadi Sh. 960,000/=! Ina maana, kama mtaamua kugawana na kuanza upya, Mkuu Marire, siku ya kugawana utaondoka na "fuko" la kati ya Sh. 3,120,000/= hadi Sh. 3,360,000/=!
Ni benki gani hapa Duniani inaweza kukukopesha kwa masharti hayo na kisha mwishoni mwa Mwaka kukulipa faida ya Akiba yako kwa kiasi hicho?
Mtu anaweza kuuliza mapungufu ya Mfumo wa Hisa/VICOBA ni yapi. Kusema kweli, kwenye mapungufu ya Mfumo huo mimi huwa ninakuwa kipofu! Ndio, mara moja, katika Kikundi chetu tulichokivunja baada ya kuwa tumekuwa nacho kwa miaka mitatu, tumewahi kupunguza kiasi cha kugawana baada ya baadhi ya Wanakikundi kutokomea na mikopo. Kwa kuwa Kikundi cha Mfumo wa Hisa/VICOBA mara nyingi ni Kikundi kisicho rasmi, yaani hakijaandikishwa popote Kisheria, kuchukua hatua za Kisheria kwa Wanakikundi kama hao ni ngumu sana. Tulipata "hasara" hiyo baada ya kuwa sisi Wanakikundi 1. Tumeacha kusimamia shughuli za kila siku za Kikundi baada ya kuwa tumebweteka na mafanikio makubwa ya miaka miwili mfululizo 2. Tumekaribisha Wanakikundi wasio waaminifu 3. Kikundi kimekuwa kikubwa sana cha Wanachama zaidi ya 35 na hivyo usimamizi ukawa mgumu 4. Mtaji wa Kikundi umekuwa mkubwa sana na hivyo kupelekea Wanakikundi kukopa Mikopo mikubwa iliyowazidi uwezo wa kuisimamia na hivyo kushindwa kurejesha na 5. Kikundi kutokuwa na mbinu za kuwapa Elimu zaidi Wanakikundi ili waweze kumudu Mikopo mikubwa na biashara kubwa zaidi!
Ni hayo tu kwa sasa. Naachia na wengine wenye ufahamu zaidi kwa kuwa ufahamu wangu unatokana na uzoefu zaidi! Wasalimie Jiji la "Rock City", Jiji la Sato, Sangara, Mumi, Nembe na Totoz za Kisukuma! Ciao!