Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakichangishana fedha na kukopeshana kwa mfumo unaoitwa benii za vijijiji (VICOBA).
Kupitia mfumo huo, wanachama waliokubaliana huchanga fedha na lkuziweka kwenye sanduku linalokaa kwa mjumbe mmoja kati yao aliyeteuliwa kukaa na funguo.
Kisha wameweka utaratibu wa kukopeshana, ambapo wanachama wanaotaka mkopo hujaza fomu inayosainiwa na viongozi wa kikundi na kisha kupewa hela na hutakiwa kurejesha ndani ya miezi mitatu ikiwa na riva.
Hata hivyo, palipo na maendeleo hapakosi uhalifu. Hivyo ndivyo baadhi ya vikundi vya VICOBA vilivyojikuta matatani baada ya vikundi vilipojikuta vikiporwa fedha zilizohifadhiwa.
Miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa ni la kikundi cha wanachama VICOBA, waliokuwa wamechangisha wakiwa na matumaini ya kupanua shughuli zao na kulipa madeni, lakini ndoto zao, ziliyeyuka baada ya wahalifu wanaodaiwa kuwa na silaha kutoroka na fedha zao walizokuwa wamekusanya zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100.
Tukio hilo lililoripotiwa na gazeti la The Citizen la Juni 9, 2014 lilitokea Juni 8, 2014 majira ya saa 1:45 usiku wa Jumapili, ambapo watu wasiojulikana walipora shilingi milioni 100.6 zilizokuwa mali ya kikundi cha Ushindi VICOBA chenye makao yake Ugombolwa, Kata ya Segerea, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kikundi cha Ushindi, Grace Katule, alithibitisha kuwa mapema jioni hiyo, wanaume wanne waliokuwa na silaha, ikiwemo bunduki ndogo ya kivita (SMG) na bastol, walivamia nyumba yake na kuondoka na masanduku matatu ya chuma yaliyokuwa na fedha hizo. Masanduku hayo yalikuwa yamehifadhiwa katika chumba kimoja ndani ya nyumba yake.
Wanachama wa kikundi waliokuwa na mshtuko walionekana jana wakipanda daladala kuelekea Kituo cha Polisi Stakishari ili kuripoti tukio hilo na kutafuta ushauri wa kisheria.
Mmoja wa waathirika, Bi Irene Kimario, alisema walikuwa wamepanga kulipa gawio kwa wanachama waliokuwa wameweka akiba kupitia VICOBA kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
Matumizi ya teknolojia yaboresha huduma
Hata hivyo, kutokana na matumizi ya mitandao ya simu, huduma hizo zinawahishwa. Tofauti na zamani ambapo iliwalazimu wanakikundi kukutana, kwa sasa wanawasiliana kupitia mitandao ya jamii kwa simu na kukubaliana na kisha mikopo hutolewa kwa wanachama
Kote Tanzania, matumizi ya teknolojia ya kidijitali yanazidi kuwa kichocheo kikuu cha ujumuishaji wa kifedha. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Desemba 2024, idadi ya usajili wa huduma za fedha kwa simu ilifikia milioni 63.2—karibu sawa na idadi ya watu nchini ya milioni 66.3.
Ripoti ya mwaka 2024, “The Effects of Village Community Banks on Economic Empowerment of Women in Tanzania,” inaonyesha kuwa Tanzania ina takribani vikundi 50,000 vya VICOBA, vinavyohifadhi jumla ya shilingi trilioni 1.5 na kuhudumia wateja wapatao milioni 4.4.
Ripoti ya Ujumuishaji wa Kifedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2023 inaonyesha kuwa asilimia 76 ya watu wazima walitumia huduma rasmi za kifedha kufikia Juni 2023. Tafiti za FinScope 2023 zinaonyesha upatikanaji wa huduma hizo umeimarika, ingawa bado kuna idadi kubwa ya watu waliotengwa, hususan vijijini, wakulima wadogo, vijana na wanawake.
Changamoto
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Social and Economic Development Initiative of Tanzania (SEDIT), mkufunzi na mwanzilishi wa VICOBA nchini, George Sweveta amesema lengo la kuanzisha mfumo huo lilikuwa ni kuwasaidia watu masikini kuwa wazalishaji, hivyo kabla ya kukimbilia kwenye teknolojia lazima msingi wa mfumo huo uzingatiwe kwanza.
“Wakati tunaanzisha VICOBA miaka ya 2000 tuligundua changamoto mbili kwa wananchi, ambazo ni ukosefu wa elimu ya ujasiriamali na ukosefu wa mitaji.
“Benki zinatoa mikopo, lakini ni kwa wale wenye uwezo kulipa na dhamana, je, hawa masikini wanakopeshwa na nani? Ndio tukawaunganisha tukaanzisha VICOBA, ili wachange kidogo kidogo kisha wakopeshane mara tatu ya mtaji alioweka,” amesema.
Kuhusu matumizi ya teknolojia za digitali amesema: “Hawa wanaotumia njia za kiteknolojia ni wenye uwezo wa kifedha na kumiliki simu janja, na sio lazima sana wafuate sana ile misingi ya VICOBA.
“Matumizi ya tekonolojia ni sawa, lakini ni lazima yaendane na lengo la kuondoa umasikini katika jamii.
“Zamani wakati tunaanzisha vikundi tulishauri watu wawe wanaoishi karibu, sasa ikaonekana watu wengi wa Dar es Salaam hawana makazi ya kudumu, wanapanga, kwa hiyo wanaweza kukopa fedha halafu wakahama.
“Kwa hiyo matumizi ya teknolojia za mawasiliano yanawezekana katika hali hiyo, lakini msingi wa kuondoa umasikini lazima uwepo, maana wapo hata watu walioajiriwa lakini hawana elimu ya ujasiriamali, wanaishia kukopa fedha lakini hawazitumii kuzalisha,” amesema.
Sheria
VICOBA zinatambuliwa rasmi kama watoa huduma za fedha wa ngazi ya nne (Tier IV) chini ya Sheria ya Huduma Ndogo za Kifedha ya Taifa ya mwaka 2018, huku usimamizi ukifanywa na mamlaka za serikali za mitaa.
Kutokana na kuongezeka kwa vikundi vinavyohamia mifumo ya kidijitali, Benki kuu ya Tanzania (BoT) inashirikiana na benki, waendeshaji wa huduma za fedha kwa simu, na Chama cha FinTech Tanzania kuunda mfumo wa kitaifa wa uendeshaji wa VICOBA kidijitali—kwa lengo la kulinda watumiaji, kukuza uelewa wa kifedha na kujenga imani.
Kupitia Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo wa Tanzania (TIPS), wanachama wa VICOBA wanaweza kuhamisha fedha mara moja kati ya benki zote na mitandao ya simu kwa gharama nafuu, kupunguza ucheleweshaji na kupanua ujumuishaji wa kifedha kote nchini.