*MFAHAMU KINDA GHALI DUNIA ALIYETUA MADRID*
ANTHONY Martiaaaal. Ndivyo alivyosikika mtangazaji maarufu wa England, John Champion, alipokuwa akilitangaza bao la mchezaji kinda aliyetua Manchester United, Martial ambaye alikuwa ni mchezaji mdogo zaidi kununuliwa kwa bei mbaya Ulaya.
Kilichowavutia United wamsajili Martial kutoka Monaco kwa pauni milioni 36, ni uwezo wake wa kupangua ngome ngumu za wapinzani kwa chenga, mbio na uwezo wa kucheka na nyavu. Baada ya siku chache tu, akapachika bao dhidi ya Liverpool na kuufanya uwanja wa Old Trafford ulipuke kwa shangwe.
Tangu siku hiyo Martial akapendwa sana na mashabiki wa United kabla hajaanza kuandamwa na mkosi wa kushuka kiwango na kukosa raha kama ilivyo kawaida kwa wacheza soka.
Hakutokea tena kinda mwingine aliyevunja rekodi ya bei mbaya, hadi leo amekuja dogo mmoja kutoka Brazil.
Vinicius Junior.
Pauni milioni 38.7 zimetosha kumtoa kinda huyo wa miaka 16 kutoka Flamengo hadi Real Madrid. Amevuruga kila kitu. Amemvurugia Martial na makinda wengine waliowahi kusajiliwa kwa bei mbaya.
Madrid imevutiwa sana na uwezo wake. Anacheza nafasi zote za ushambuliaji. Wanamuita Neymar mpya.
Alianza kuichezea Brazil ya watoto chini ya miaka 15, huku yeye akiwa na miaka 13 tu. Hadi leo ameendelea kuonesha maajabu ya soka. Tayari ameshachukua tuzo bora ya michuano ya vijana chini ya miaka 17 Amerika Kusini mwaka huu, akiwa na jumla ya mabao 12 kwenye mechi 15. Madrid wamelamba karata dume hapa.
Baada ya Vinicius na Martial, ni akina nani walio chini yao na walisajiliwa kwa bei gani, makala haya yamekuorodheshea vizuri.
Lucas Moura
Winga huyo wa Brazil alitua PSG kwa kitita cha pauni milioni 32.5 akitokea Sao Paulo, uhamisho uliomtoa ‘povu’ kocha wa zamani wa Man United, Sir Alex Ferguson, ambaye naye alimhitaji.
Ferguson alidai kuwa PSG walitumia kiasi kikubwa cha fedha kilichomrubuni mchezaji huyo, lakini kwa mabao 45 tu aliyofunga Moura ndani ya mechi 233 PSG, kocha huyo sasa atakuwa anafurahia kumkosa.
Moura ameshapotea kwenye ramani ya soka. Kilichobaki kwa sasa ni kuamua, abaki PSG au atafute timu nyingine ya kulifufua jina lake.
Mario Gotze
Ilikuwa ni taarifa mbaya kwa Dortmund baada ya Gotze mwenyewe kutangaza Bayern Munich wapo mbioni kulipa pauni milioni 31.5 za kuuvunja mkataba wake ili aende Allianz Arena. Kichwa chake kilishafunga hesabu. Aliamua kuiacha Dortmund.
Maisha yake ndani ya klabu ya Bayern yalikuwa na furaha ya mataji, mabao, lakini majeraha yalipoanza kumuandama, akaanza kupotea. Akarudi nyumbani. Akarudi Dortmund. Kwa bahati mbaya zaidi, tangu arudi kule hajacheza mechi za kutosha kwa sababu ile ile, majeruhi.
Luke Shaw
Mtazame Moura, mtazame Gotze halafu urudi kwa Shaw. Pauni milioni 29 zilizotumika kumtoa Shaw kule Southampton hazijarudisha chochote. Beki huyo wa kushoto ameshiriki asilimia ndogo sana ya mafanikio ya United tangu aliposajiliwa hadi leo hii.
Bahati mbaya kwake, alivunjika mguu 2014. Hapo ndipo balaa lilipoanza, ameichezea Southampton mechi nyingi zaidi ya alizocheza kwa Man United. Unafikia kipindi unajiuliza, huyu ni mchezaji wa United kweli?
Renato Sanches
Bayern walivutiwa na kazi ya Sanches kwenye Euro 2016 akiwa na mabingwa Ureno. Wakahesabu pauni milioni 27.5 wakawapa Benfica, halafu wakawaambia, “tupeni mtu wetu”.
Siku zote, kusajili makinda hawa kwa bei mbaya huwa ni kama mchezo wa kamari. Na Bayern waliliwa hapa. Sanches hajacheza mchezo wowote. Ameshindwa kufurukuta mbele ya viumbe wazito, Arturo Vidal na Thiago Alcantara. Amecheza mechi 17 tu, na maisha yake ya soka yapo hatarini.
Gabriel Jesus
Jesus alikuja kuwaokoa Manchester City na ameifanya kazi yake vizuri.
City ilifanikiwa kumnasa Mbrazil huyo kwa dau la pauni milioni 27.2 kutoka Palmeiras, na katika wiki za awali tu ndani ya Ligi Kuu England, mshambuliaji huyo akafanikiwa kuteka hisia za mashabiki wa City kwa kufunga mabao muhimu kabla ya kukumbwa na maumivu ya enka dhidi ya Bournemouth. Akakaa nje kwa wiki kadhaa.
Aliporudi akaendeleza tena kasi yake ile ile. Na ni hatari zaidi akitokea benchi kuliko akianza. Ndani ya mechi 10 tu alizocheza kwenye mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Jesus akafanikiwa kufunga mabao saba na kutengeneza mengine manne. Hela haikupotea bure hapa.
[emoji460][emoji115]