Jioni moja ya mwaka 2003, jijini Cairo nchini Misri kulikuwa na mechi nzito, uwanja ukiwa umetapika kulikuwa na shujaa mmoja aliyekuwa golini akiibeba timu yake ya Simba Sc kwa kupangua mikwaju ya penati na kuivua taji mabingwa watetezi Zamalek. Shujaa huyo si mwingine ni Juma Kaseja. Dunia ikabaki imeduwaa.
Leo 28.04.2023 miaka 20 baadae, Simba ipo tena uarabuni kucheza na bingwa mtetezi ambaye ni Wydad, katika mazingira yaleyale.
Simba atashuka akiwa na mtaji wa goli 1-0 katika mchezo wa kwanza, uliopigwa Tanzania. Je historia kujirudia? Simba ataweza kuivua Wydad ubingwa akiwa kwao kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita pale Zamalek. Sababu wanayo, uwezo wanao nia pia wanayo.
Ni mechi ya kufa au kupona, ewe Mwana Simba uliyepo Ndola, Tanga, Entebbe, Nakuru na maeneo mengine tembea kifua mbele, usiwe mnyonge kwa Simba hii mwarabu atakufa kwao. Je Shujaa atakuwa nani? Baleke, Chama, Inonga au Kiungo punda Mzamiru?
Mechi itakuwa mubashara kuanzia Saa 4:00 Usiku kwa Masaa ya Afrika Mashariki na mchezo utakuwa live kupitia ZBC 2 ya AzamTv, Chaneli 225 ya DStv, Canal Plus na Bein Sports.