SoC01 Fumbo la uaminifu kwa vijana wa Tanzania

SoC01 Fumbo la uaminifu kwa vijana wa Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

From Chugga

New Member
Joined
Aug 22, 2021
Posts
4
Reaction score
9
Akichangia hoja ya Waziri Mkuu kwenye kikao cha 11 cha Bunge la 12 Spika wa Bunge Muheshimiwa Job Ndugai aliwasihi waheshimiwa wabunge kufikiria na kuchangia juu ya tatizo la kupungua kiwango cha uaminifu kwa vijana wa Tanzania na kupendekeza namna ya kutatua tatizo hili. Katika maelezo yake, Muheshimiwa Spika akaeleza kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wakilia kwa hasara wanayopata kwenye miradi au biashara hapa nchini, inayosababishwa na vijana wasio waaminifu.

Tatizo hili ni zito na linahitaji suluhisho la haraka ikizingatiwa kuwa vijana ndio wabeba bendera ya maendeleo ya Taifa, ndio wanaotegemewa kutoa nguvukazi kwa kiasi kikubwa kwenye Nyanja zote za uzalishaji. Endapo kundi hili halitakuwa sawa kuna hatari ya kudumaa kwa mendeleo ya kijamii ya nchi kwa sababu vijana hawatawekeza fikra zao kwenye kukuza weledi na taaluma zao zitakazosaidia kustawisha vitengo wanavyofanyia kazi. Badala yake wataweka fikra zaidi kwenye kunuifaika wao binafsi bila kujali madhara yanayokumba vitengo vyao au kuporomoka kwa miradi waliyoajiriwa kuifanyia kazi.

Kadhalika, vijana ndio chombo cha kusafirisha maadili, desturi, taaluma na stadi kutoka kizazi kimoja hadi kingine, miaka kadhaa ijayo vijana wa sasa ndio watakuwa kwenye rika la watu wazima watakaotegemewa kuongoza jamii na watakaokuwa nyuma yao. Swali ni kuwa watawezaje kuongoza ikiwa wao wenyewe hawana uaminifu na maadili. Kuna ulazima Taifa lichukulie kadhia hii kwa uzito wake ili kurejesha jamii yetu kwenye msitari.

Suala hili si mwiba kwa wawekezaji kutoka nje pekee, pia kuna idadi kubwa ya wazawa wamekuwa ni wahanga wa hili. Takribani kila mtu amewahi kuguswa au anamjua mtu ambaye “amelizwa” kwenye kazi au biashara. Hadithi zinazosimuliwa mitaani zimezoeleka, zimekuwa za kawaida na kuonesha kukata tamaa sasa kumekuwa na usemi “siku hizi usimuamini mtu”.

Imefikia hata kwenye maisha ya kawaida watu wanaogopa kukopeshana pesa, kwa sababu wengi hawalipi; inasababishwa na kupotea kwa uaminifu.

Wahanga wa kwanza wa kadhia hii ni wazawa wanaojitahidi kuwekeza kwenye shughuli tofauti nje ya ajira zao, mfano, kuna vijana wengi waliingia kwenye shughuli za kilimo, walinunua au kukodisha mashamba na kuweka vijana wawasimamie wakati wao wanaendelea na kazi au biashara zao mijini.

Hata hivyo ni wachache sana walioona faida ya uwekezaji wao, wengi wameishia kupoteza muda na fedha walizowekeza. Mashamba waliyokodisha wakayarejesha kwa wenyewe, wengine wakauza mashamba yao waliyokuwa wameyanunua na hata wengine kuyaacha tu mashamba yao kwa kukata tamaa. Sasa hutoa ushuhuda kwa wengine kuwa kuwekeza kwenye kilimo lazima upate mtu wa uhakika sana au usimamie mwenyewe. Hivyo wengi wamerudi nyuma na wengine wanaogopa kabisa kuwekeza kwenye sekta hii kwa sababu hawana wasimamizi waaminifu.

Ubaya wa hapa ni kupoteza fursa ya kukua pamoja, ambapo aliyewekeza angeongeza kasi ya kuyaendea mafanikio na aliyepewa dhamana ya usimamizi angepunguza umasikini kwa kuongeza kipato na ustawi wa maisha. Kwa kukosa uaminifu na kuendeshwa na tamaa wanabaki palepale walipo siku zote ndani ya gurudumu la umasikini.

Hata kwa vijana wa mijini wanaoungana kufungua biashara haichukui muda mrefu kusikia mmoja kamzunguka mwenzie na kumdhulumu. Wengine hata wanadiriki kubadili hadi umiliki wa biashara, mwenzie anakuja kutahamaki amewekwa nje bila kujua hasa kilichotokea. Tatizo likafika hadi kwenye miradi ya mikopo midogomidogo ya halmashauri, wengine wakapotea nayo na kufanya wengine wasipate nafasi ya kukopa.

Ari ya kushirikiana na kusaidiana kama vijana inapotea, inabaki kila mtu afanye mradi wake peke yake na aliye kweye dimbwi la umasikini hasa vijijini atajikwamua kwa jitihada zake mwenyewe. Hili halina mustakabali mzuri kwa jamii kama ya kitanzania ambapo watu wanasifika kuishi kwa kushirikiana bila kujali tofuati zao.

Upande wa pili wa sarafu ndio wenye shimo lililomeza uaminifu wa vijana wa Tanzania. Shimo hili ni msururu wa matukio ya ubadhirifu wa fedha za umma au wizi wa fedha za miradi ambayo yamekuwa yakitokea kwa muda mrefu na jamii haikuwaza kuwa yatakuja kuleta madhara kama haya.

Matukio haya yamekuwa yakiandikwa na vyombo vya habari, jamii wakayasoma na kuyaongelea kama simulizi za “yatokeayo”, hakuna tahadhari inayotolewa juu ya mmomonyoko wa uaminifu na maadili unaoweza kuletwa na matukio haya.

Mmomonyoko uliosababishwa na matukio haya umewakumba vijana wote; wasomi na wasio wasomi, wenye ajira rasmi na zisizo rasmi, mijni na vijijini, imekuwa wote wanaongozwa na tamaa ya manufaa binafsi.

Jamii imefika wakati inaonekana ni jambo la kawaida kusikia “madudu” kwenye miradi ya kimaendeleo, kwa sababu habari zake zimekuwa zikitajwa mara nyingi kwenye vyombo vya habari. Itaonekana ajabu mradi ukamilike kwa muda uliopangwa na kwa kiwango kilichokusudiwa bila kutokea konakona.

Jamii inapotafakari njia ya kuwanusuru vijana kutoka kwenye hali hii ya kukosa uaminifu ikumbuke kuwa vijana wamejifunza kutoka kwa wakubwa na viongozi ambao walipaswa kuwa viigizo vyema badala yake wamekuwa mifano mibaya kwa vijana kwa kesi za kujinufaisha binafsi kutumia nafasi zao.

Baadhi ya matukio yaliyotokea na kuandikwa kwenye vyombo vya habari yanasisimua kusikia kiasi cha fedha kinachotajwa kupotezwa, mfano, kusikia kiongozi wa taasisi ya kukusanya kodi mahakamani kwa kesi ya utakatishaji wa dola za kimarekani milioni sita na Mawaziri wa zamani kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa kuisababishia serekali hasara kwa ya sh bilioni 11. Hizi fedha si haba kwa nchi ambayo uchumi wake ni wa kujikongoja na kukabiliwa na upungufu mkubwa kwenye vitengo vuote vya huduma ya jamii.

Zaidi kuna habari za mikataba mibovu, kusafirishwa kwa twiga na rasilimali zingine, kujilimbikizia mali na ardhi, mawaziri kujichotea fedha kutoka akaunti maalumu na mapungufu yanayobainishwa na ripoti za wakaguzi wa mahesabu ya serekali.

Yote haya kwa ujumla wake yanafundisha kuwa kuna viongozi wanatumia nafasi zao kujinufaisha, hao ndio shimo lililomeza uaminifu wa vijana wa Taifa hili kwa sababu wanafundisha njia za kufanya ili kuwa na maisha ya kifahari kama waliyonayo wao na familia zao bila kujali jamii kubwa inayoteseka.

Inapotokea wanaotajwa hawawajibishwi kulingana na kiasi cha makossa yao au thamani halisi ya hasara waliyosababisha inajenga hisia kuwa “mbuzi atakula alipofungiwa”. Ndipo jamii ilipofikia sasa, kuwa kiongozi akimaliza muda wake bila kujilimbikizia mali anaonekana mjinga na huenda akabezwa.

Imekuwa ni fahari mtu akimaliza muda wake wa uongozi awe na mali nyingi, hata ikiwa kiwango cha mali hizo hakiakisi uhalisia wa kipato chake madarakani. Vijana ni rahisi kuiga kwa sababu hakuna anayependa kuishi katika umasikini.

Miongoni mwa hao waliotajwa kuhusika na matukio hayo, hakuna yeyote amewahi kutamka kuwa anajutia alichofanya na hatamani kuwa mfano mbaya (bad influence) kwa vijana. Wote wanaendelea kuishi maisha ya kifahari na wanatembea vichwa juu na wanaitwa waheshimiwa.

Mwenye akili za kutafakari anajiuliza hawa wanawezaje kuishi na dhamira ya kujirundikia mali kutoka mifuko ya Umma huku kuna wengine wanaishi kwenye umasikini uliopindukia, hata maji ya kutumia wanategemea madimbwi ya maji ya mvua au kuchimba kwenye mchanga wa mtoni.

Jamii na vijana wanaelewa kuwa mchezo unavyokwenda ni kuwa mtu “keshalamba” fedha za kutosha hata akitolewa kwenye nafasi yake ataendelea kuishi kwa jeuri. Huwezi kustaajabu vijana kutokuwa na dhamira na mioyo ya kujihisi vibaya kwa kuchota fedha za miradi ya wawekezaji kwa sababu wanajifunza kutoka kwa wakubwa.

Tamaa imeua mioyo ya vijana, hawana muda wa kutafakari matokeo ya matendo yao wakaendelea kuonesha kwenye mitandao maisha yao ya kifahari bila kujali kuwa jamii wanajua walichofanya. Hapo linarudi swali la dhana ya heshima binafsi (integrity) ambayo wengi wameipoteza.

Kufupisha mada, kuna usemi wa James Baldwin unasema, “Children have never been very good at listening to their elders, but they have never failed to imitate them”. (Watoto hawajawahi kuwa wazuri kuwasikiliza wakubwa wao ila hawajawahi kukosea kuwaigiza) ndio unaweza kutuongoza kwenye suluhisho.

Ikiwa kweli tunataka kurudisha hali ya uaminifu kwa vijana wa Taifa letu basi viongozi waanze wao kufanya kazi zao kwa uaminifu na uadilifu na wengine watawafuata nyayo.

Itakuwa jambo kubwa sana vyombo vya habari vikianza kuandika kuwa Raisi au Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa kazi nzuri baada ya kufanya ziara ya kushitukiza idara Fulani. Tofauti na ilivyo sasa, kuwa, ziara za kushitukiza zimekuwa zikigundua “madudu” tu. Mfano siku za hapo nyuma ziara za Waziri Mkuu mwendokasi, bandarini na benki kuu zote ziliripotiwa kugundulika taarifa zisizopendeza, itokee hizo ziara zifuatiwe na pongezi za kazi nzuri.

Pakiwa na taarifa mbaya jamii inajiuliza wasomi na viongozi kwenye hizo taasisi wanafanya nini na taaluma zao. Hayo “madudu” yapo siku zote na watumishi wengine wanayaona, hadi aje Waziri Mkuu, nao wanajifunza nini kwayo?

Kuna ulazima wa kuhuisha mioyo iwe inahisi aibu kuwatendea wengine yasiyostahili na kurudisha heshima katika utu badala ya kitu. Viongozi waone aibu kutumia nafasi zao kwa maslahi binafsi watekeleze wajibu wao inavyostahili.

Tuwafundishe watoto wetu kuwa urithi wa mali hasa zisizo za halali haudumu muda mrefu kulinganisha na urithi wa heshima (legacy of honour), ambao hubaki kuishi na kusimuliwa kwa vizazi na vizazi, kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa.

Viongozi wawaoneshe vijana kuwa inawezekana kuwa kiongozi na kuishi maisha ya kawaida yanayoakisi kipato na majukumu ya kiongozi wa Umma. Itaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye fikra za vijana na huenda wakasikiliza na kuelewa mahubiri ya kujenga uaminifu na kuheshimu vitu na haki za wengine.

Hayo yakifanyika itaweza kurejesha ushirikiano mzuri wa kazi kati ya vijana na wawekezaji wa ndani na nje. Walioajiriwa mijini wakashirikiana kwenye kilimo na vijana walio vijijini inadumisha ushirikiano wa kijamii, hii ni njia nzuri na ya uhakika ya kustawi pamoja.

Itakuwa ni sifa ya ziada kuwavutia wawekezaji kutoka nje na watakapokuja watakuja na heshima kwa wazawa badala ya kuwatumia wachache kuwakandamiza wengine. Yote yatawezekana kama tutakuwa na viongozi ambao ni “role models” (mifano ya kuigwa) kwa vijana.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom