FURAHA AU AMANI? Mtazamo wa kiteolojia na kijamii

FURAHA AU AMANI? Mtazamo wa kiteolojia na kijamii

Joined
Aug 13, 2026
Posts
6
Reaction score
9
FURAHA AU AMANI : Mtazamo wa Kiteolojia na Kidiplomasia katika Ustawi wa Tanzania

Na Mch Emanuel Malembela (Mchambuzi wa Mambo ya Kijamii Na kiimani)

"Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru" Yn 8:32

Ni nini tofauti ya Furaha na Amani katika Taifa?,Je watawala na watawaliwa kwa sasa Katika Taifa wana Furaha na amani?.Baada ya kutafakari nimeona nitumie taaluma na nafasi yangu katika ujenzi wa taifa kuchambua jambo hili.Furaha ni hisia ya msisimko wa muda mfupi inayotokana na matukio au mambo mazuri yanayotokea nje ya maisha ya mtu kwa mfano kushinda uchaguzi,kupata kazi,kupata rafiki wa kweli n.k. Wakati huo huo, amani ni hali ya utulivu wa ndani wa kudumu na wa kina, unaomwezesha mtu kuwa na mstarehe hata katikati ya changamoto au matatizo makubwa mfano kufiwa na wazazi,kufukuzwa kazi n.k.

Kwa upande mwingine ili kuitwa Dola (State), eneo lazima liwe na idadi ya watu ya kudumu, mipaka inayoeleweka, serikali thabiti, na mamlaka kamili ya kuingia mikataba ya kimataifa. Sifa hizi nne huipa nchi uhuru kamili wa kujitawala na kuwezesha kutambuliwa kwake na mataifa mengine duniani.katika muktadha wa maendeleo ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania, kuna taswira ya kipekee inayojitokeza unapotazama makundi mawili makuu yanayojenga taifa letu: viongozi waliopo madarakani (watawala) na watetezi wa haki, wanasiasa wa upinzani, wanaharakati pamoja na wananchi kwa ujumla. Kwa jicho la haraka, makundi haya yanaonekana kuishi katika Dunia mbili tofauti—mmoja ukiwa umejaa tabasamu, itifaki, na sherehe za mafanikio (furaha), na mwingine ukiwa umejaa mapambano, misukosuko, na misimamo thabiti (amani).

Hata hivyo, kama mchambuzi, ninalitazama jambo hili kupitia miwani ya kiteolojia na kidiplomasia si kama mtengano, bali kama nguzo mbili muhimu zinazotafuta usawa (equilibrium) ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu pendwa Tanzania

Watawala na Furaha ya Majukumu (The Joy of Governance and Stewardship)

Katika nyanja ya kidiplomasia na uongozi wa juu, watawala wamebeba dhamana kubwa ya kitaifa (State Stewardship).Wanaongoza Dola(Taifa) na serikali.Furaha yao inayoonekana wazi kwenye majukwaa inatokana na kuridhika kwa kuona mipango ya kimaendeleo inatekelezeka—kama vile ujenzi wa miundombinu mfano reli ya kisasa,Bwawa la kufua umeme na barabara za kiwango cha lami, utulivu wa kiuchumi, na uwakilishi mzuri wa nchi kimataifa. Hii ni furaha halisi inayotokana na matokeo yanayoonekana (tangible results).

Hata hivyo, kiteolojia na kidiplomasia, nafasi hii inakuja na changamoto kubwa ya kiutendaji inayoweza kutikisa amani ya ndani ya kiongozi:

1. Mzigo wa Maamuzi Magumu:Aliwahi kusikika kiongozi mmoja akisema "Nchi inahitaji viongozi wa kufanya maamuzi magumu". Ni ukweli usiopingika kuwa Kiongozi aliye madarakani analazimika kufanya maamuzi magumu kila siku ili kulinda usalama wa nchi na maslahi ya wengi. Mara nyingi, maamuzi haya ya kiutawala hubeba shinikizo kubwa na upweke wa kimaamuzi, jambo linalohitaji utulivu wa hali ya juu wa kiakili na kiroho.

2. Diplomasia ya Uwiano (The Balancing Act):Taifa limebeba watu wengi wenye makundi yenye mitazamo tofautu. Watawala wanapaswa kusawazisha mitazamo tofauti ya wadau wa ndani na washirika wa kimataifa. Jukumu hili la kutosheleza matarajio ya kila mtu ndilo linalofanya amani yao kuwa ya gharama kubwa, kwani uongozi ni utumishi unaoacha alama kupitia changamoto nyingi.

Kwa watawaliwa,wananchi na Wanaharakati kubeba Amani ya kweli (The Prophetic Peace of Principles)
Kwa upande wa pili, wanaharakati, watetezi wa haki, na wanasiasa wa upinzani wanasukumwa na nguvu ya ushawishi wa kimaadili (soft power). Mazingira yao ya kazi mara nyingi yanawakosesha furaha ya kiitikadi na kiitifaki kwa sababu wako upande wa kuhoji na kusukuma mabadiliko.
Pamoja na kukosa furaha ya kawaida ya kiutawala, wanaonyesha amani kubwa ya ndani inayovushwa na dhana hizi:

1. Wajibu wa Unabii na Ukumbusho (The Prophetic Voice): Kiteolojia, jamii yoyote inahitaji sauti inayokumbusha misingi ya haki, usawa, na utu (Imago Dei). Amani ya wanaharakati inatokana na utambuzi kuwa wanasimamia wajibu wao wa kikatiba na kimaadili wa kusaidia kuboresha mifumo ya jamii.

2. Kujitoa kwa Ajili ya Jamii: Wanapokubali kupitia changamoto na misukosuko kwa ajili ya kile wanachoamini, wanajenga amani thabiti ya ndani inayotokana na dhamiri safi. Hii ni sifa inayotambuliwa hata kidiplomasia kama uwezo wa kusimamia misingi (principled diplomacy) ambayo huongeza thamani ya mijadala ya kitaifa.

Maridhiano njia ya kuleta amani na furaha ya kweli: Mahali Ambapo Furaha na Amani Zinakutana

Tanzania yetu inahitaji nguvu zote mbili. Watawala wanahitaji furaha na uthubutu wa kutekeleza maendeleo, lakini pia wanahitaji sauti za wanaharakati na wapinzani ili kuwapa amani kuwa nchi inakwenda katika mwelekeo sahihi wa kimaadili na wa haki.

Vivyo hivyo, wanaharakati wanahitaji utulivu na utekelezaji unaofanywa na watawala ili misingi wanayoipigania itafsiriwe kuwa maisha bora kwa wananchi.

Kama ifundishavyo diplomasia ya amani, "Maendeleo bila haki ni ujenzi juu ya mchanga, na haki bila utekelezaji ni ndoto isiyofanya kazi." Na kwa lugha ya zaburi za kiteolojia, ustawi wa taifa letu utafikiwa pale tu "Fadhili na kweli zitakapokutana, haki na amani zitakapobusiana." Makundi haya mawili si maadui, bali ni washirika katika pande mbili tofauti za sarafu moja inayoitwa Tanzania.

Tanzania ya Amani na furaha inaweza kurejeshwa kwa watawala na watawaliwa.Hili linawezekana kama kila mmoja atatimiza wajibu kwa Mungu na Taifa lake.

Imeandikwa na
Mch.Emanuel Malembela (Mwanataaluma katika Diplomasia,teolojia,utawala na uongozi wa kimkakati)
Simu; 0752-175649
email:[email protected]

13/08/2026,Dar-es-salaam.
 
Ni lini hasa umeona haki na amani zikipigana kiss kwenye siasa zetu bila nguvu ya umma?
 
Back
Top Bottom