Hivi karibuni umeibuka uhasama mkali kati ya Rais wa Kenya William Ruto na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambao umefikia hatua ya kurushiana maneno makali ikiwa ni mwaka mmoja kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo 2027.
Miongoni mwa aliyoyasema Gachagua alibainisha kuwa,
"How much is enough, William Ruto? Just how much is enough? Unataka pesa ngapi? Lakini uzuri hata akiwa na hiyo pesa yote halali... tutahakikisha William Ruto, you are not going to sleep for the next 15 months. Utalala ukifika Sugoi. Tutakuanika na hivi vijana wangu hapa."
Akijibu mapigo na kuwabeza viongozi wa upinzani (akiwemo Gachagua) kuhusu muonekano wao na tabia zao, Rais Ruto alisema,
"Use the mirror... muone vile mmekaa. Kichwa kimefimba, tumbo ndio hiyo karibu inararua mashati. Tafuteni gym kwanza mwende mfanye exercise kidogo, na mupunguze kukula chakula mingi ndio muache kulala huko kwa mikutano... hata mnaharibu hewa huko mkutano mkiwa mmelala bure kabisa."
Kutokana na kauli ya Rais Ruto akisema 'Tafuteni gym kwanza mwende mfanye exercise kidogo' kumekuwapo na video inayosambazwa mtandaoni ikimuonesha Rigathi Gachagua akiwa sehemu ya mazoezi 'na kwamba ameingia 'GYM' ndiyo wamenyane vizuri na Ruto.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia nyenzo za kidigitali umejiridhisha kuwa video hiyo inapotoshwa muktadha wake.
Kwa kutumia Google Reverse Image Search imebainika video hiyo ilichapishwa Aprili 07, 2020 na
Inooro TV.
Katika video hiyo Rigathi Gachagua wakati huo akiwa Mbunge wa Mathira inaonesha jumba la kifahari lenye mapambo na samani za hali ya juu, likiwa na bwawa la kuogelea, bustan pamoja na gym ya kisasa ambapo ilielezwa Gachagua hutumia muda mwingi wa asubuhi kufanya mazoezi kama njia ya kupunguza msongo wa mawazo.
Katika mahojiano na Inooro TV, alisema alipunguza uzito kutoka kilo 92 hadi 86 kwa kufanya mazoezi, huku pia akionesha nyumba yake na kuelezea shughuli zake za kila siku.