Mwananchi mmoja kutoka kata ya Buhala halmashauri ya Mji wa Geita, aliyejitokeza kupiga kura kwenye kituo cha Mwatulole alilalamika awali kwamba jina lake halikuwepo kwenye orodha ya wapiga kura.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa haraka uliofanywa na maafisa wa uchaguzi, jina lake lilionekana kwenye orodha rasmi.
Tukio hilo limesababisha sintofahamu ya muda mfupi, ambapo mwananchi huyo ameomba radhi kwa msimamizi wa uchaguzi wa halmashauri ya Mji wa Geita kwa lawama alizotoa kabla ya kufahamu ukweli wa jambo hilo.
Msimamizi wa uchaguzi ameeleza kuwa changamoto kama hizi hutokea mara chache kutokana na baadhi ya wapiga kura kushindwa kufuatilia taarifa zao za usajili kwa wakati, huku akibainisha kuwa Tume ya uchaguzi imejipanga kuhakikisha kila mpiga kura aliyejiandikisha anapata haki yake bila vikwazo.
Mwananchi huyo amemaliza kwa kuwataka wananchi wengine kuhakikisha wanakagua majina yao mapema kwenye orodha za wapiga kura ili kuepuka sintofahamu kama hiyo siku ya uchaguzi.