Kwanza ni lazima nikiri wazi kuna hakuna timu ambayo isiyofungwa duniani. Lakini povu ninaliona kwa wanasimba wengi ni kwa kuwa Simba imefungwa halafu imecheza hovyo sana huku wachezaji wao wakionekana kabisa hawana morali (hawakuwa aggresive kabisa) na mbaya zaidi ni kuona lile pira biriani linapigwa na wapinzani wao Simba wakibaki na butua butua. Kwa kweli kile ni kipigo kibaya sana kwa Simba dhidi ya Yanga na hakitosaulika siku za karibuni kwani Yanga wangetulia kidogo tu nilikuwa naziona goli tatu. Kilichotokea jana kwa Simba kwao ni "surprise" lakini lazima wajiandae kwani mwaka huu timu zote za ligi zimesajili vizuri sana na zitakuwa na pesa za kutosha kutokana na udhamini wa Azam. Nawapa saluti sana Yanga kwa pira lile waliopiga jana kwani sio la nchi hii. Simba walipoteana kabisa walipaniki sana kwani ni mara chache sana kuwaona Kapombe na Zimbwe wakifokeana na waamuzi kwa kiasi kile.
Pamoja na Simba kuzidiwa lakini mimi nitalilaumu benchi la ufundi na uongozi wa Simba kwa makosa mengi yanayojirudia kila wakati.
1. Kwenye usajili niliwataahdarisha sana hapa viongozi wa Simba kama wanahitaji "kudominate" mpira wa bongo na hata kuendela kufanya vizuri kwenye CL wasajili vizuri na nilienda mbali kuwataka wasajili mshambuliaji mmoja mahiri aliyekamilika kila kitu na hasa mwenye matumizi mazuri ya kichwa kwani Simba ina utajiri wa mawinga na mabeki wa pembeni ambao kwa pamoja wanapiga sana krosi muda wote wa mchezo. Na ilitakiwa waachane na mshambuliaji mmoja kati ya Kagere na Mugalu. Cha kushangaza wakati wanataka kuachana na Kagere na Kagere mwenyewe akiwa ameshaanza kuaga ghafula Simba wakajambishwa na Yanga kuwa wanamsajili na kwa kuogopa yaliyotokea kwa Tambwe ndipo Simba wakapiga "u turn". Hili lilikuwa kosa moja kubwa sana kwa uongozi wa Simba.
2. Pia kitendo cha uongozi kushindwa kumsajili Manyama lilikuwa ni kosa lingine baya sana. Kwa mechi ya jana kuna wakati Zimbwe alikuwa na hasira sana kiasi alitoka mchezoni akaanza kugombana na waamuzi nikajiuliza sasa Simba wakimtoa je wakimuingiza Gadiel si itakuwa majanga makubwa.
3. Watu wengi wanamlaumu sana Mugalu. Ni kweli Mugalu alikosa sana magoli ya wazi . Na hili ni tatizo kubwa sana kwake huwa anakosa utulivu hasa kwenye "big matches". Huyu mwamba Simba wamtafutie mtaalamu wa saikolojia kwani ameshadhihirisha uwanjani ana kila kitu kuanzia nguvu, mashuti, jicho la goli, positioning, ball control ya hali ya juu na umaliziaji mzuri lakini maajabu inapokuja mechi kubwa atafanya vyote kwa usahihi wa hali ya juu lakini atashindwa kutumbukiza mpira kimiani tu.
4. Baada ya kuondoka Chama benchi la ufundi limejaribu sana kuijenga timu kucheza kwa kumtumia Bwalya lakini inaonekana mzigo huo ni mzito sana kwa Bwalya. Namna Bwalya anavyocheza kwa kweli huwa anaondoka sana eneo lake na hii iliwatesa sana Simba japo hata benchi la ufundi halikugundua mateso yanatoka wapi. Haiwezekani namba 10 ambaye anategemewa kutoa pasi za mwisho au kufungwa halafu muda mwingi wa mchezo yupo chini kabisa anapiga "square pass". Ilimpasa Bwalya mara nyingi awe si zaidi ya mita tano kati yake na Mugalu pale Simba wanaposhambulia na wakati wanashambuliwa arudi si zaidi sana ya katikati ya uwanja ili kuchukua mpira na kusamabaza kwa Mugalu au mawinga wake. Lakini maajabu Mugalu anaruka na mabeki wawili wa Yanga "second ball" inaanguka mwamba ambaye jana kaupiga mwingi sana Bangala anajiokotea taratibu bila upizani wowote anaupeleka mpira popote anapotaka. Na kingine Bwalya ni mzuri sana kwenye mechi ambazo hazina matumizi sana ya nguvu kwani hawezi kabisa kugongana na viungo wa timu pinzani. Simba hawakuwa tishio kwa mabeki ya Yanga muda wote wa mchezo kwa sababu Bangala alikuwa huru muda wote wa mchezo. Kwa hili la Bwalya najua wengi watanipinga sana kwa sababu wabongo wanapenda kuona chenga hata kama hazina faida yoyote lakini ndio ukweli wenyewe japo mchungu sana.
5. Nilitegemea jana kwa kuwa mechi ilikuwa ya kugongana na matumizi ya nguvu sana basi benchi la ufundi lingeanza na Kibu kwenye winga moja na nafasi ya namba 10 acheze Sakho. Kwanini Sakho? Wepesi wake, spidi yake na pasi zake za upendo za mwisho na pia ameshaonesha ana uwezo wa kufunga.
6. Benchi la ufundi lilikuwa pia na uchaguzi wa kuanza Lwanga na Abdulswamad (kiungo aliyetoka Kagera) kama wakabaji halafu Kanoute akasogea juu. Kwa nini Abdulswamad ni kwa kuwa anakaba kwa nguvu sana, ni mtulivu na ni mzuri kwa mipira ya juu.
7. Benchi la ufundi la Simba likatae likubali kuwa Kibu ni muhimu sana kutokana na "work rate" yake. Na ndio atakuwa mchezaji muhimi sana kwao kwa sasa mpaka waje wampate mtu mwenye uwezo kama Konde Boy huko mbele ya safari. Jinsi alivyocheza mechi ya TP Mazembe ni kama vilemchezaji mzoefu wa mechi za kimataifa. Kwa nini jana hakutumika hiyo tuwaachie benchi la ufundi la Simba.
8. Pia benchi la ufundi la Simba likatae likubali Sakho ndio atawasaidia kuwatengenezea magoli kwa sasa mpaka hapo baadaye watakapokuja kumpata Chama mwingine huko miaka ijayo.
Mwisho lazima nilipongeze sana benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na Nabi kwani kwa mbinu walizotumia jana walilichanganya kabisa benchi la ufundi la Simba lisijue nini cha kufanya kiasi likianza kufanya "sub" za ovyo kabisa. Sijui wale waliotaka kumfukuza Nabi wataficha wapi sura zao. Na iwapo Yanga wasingeenda kuzurura Moroco basi kwenye CL wangetoboa na wangefika mbali sana mwaka huu. Kila nilipokuwa nikitazama mpira jana ilikuwa vigumu sana kuamini kuwa Simba ndio waliopata "pre season" nzuri kuliko Yanga.