NIACHENI na ufisadi wangu jamani, kwani sina zaidi ya kueleza katika suala hili.
Hayo ni maneno ya utangulizi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, aliyoyatoa mwishoni mwa wiki alipotakiwa na gazeti hili kuzungumzia uamuzi wake wa kufungua kesi baada ya kutajwa katika orodha ya aibu iliyohusisha watu 11 katika tuhuma za ufisadi.
Nasema kauli ya Mgonja kwamba aachwe na ufisaidi wake, haiwezi kuingia akilini hata kidogo, kwa kuwa tuhuma hizi ni nzito kwa mtendaji huyo muhimu kwenye wizara nyeti.
Nasema mtendaji muhimu kutokana na ukweli kuwa yeye ndiye anashughulikia masuala ya wizara nyeti, hivyo anaelewa vizuri mianya ya kuingiza na kutoa kila kitu.
Kabla sijaanza kumzungumzia, naomba niwakumbushe kwamba huyu Mgonja kwa mara ya kwanza alitajwa kwenye kikosi cha watu 11 waliohusishwa na ufisadi (first eleven) na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam.
Baada ya kutajwa kwenye kikosi hicho, kinachoonekana kutokuwa na wachezaji wa akiba (reserve), Mgonja aliamua kuzungumza na waandishi wa habari kwa nia ya kueleza azima yake ya kufungua kesi dhidi ya tuhuma hizo.
Lakini, kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, tulishuhudia vigogo kadhaa wakiumbuka, ghafla Mgonja na timu yake ya ushauri walikaa kimya hadi sasa anapotaka aachwe na ufisadi wake.
Kwanza, kitendo cha kushindwa kufungua kesi kama alivyotangaza awali, kinaashiria wazi kwamba, Mgonja analo neno zito moyoni kama si ufisadi, basi atakuwa analijua mwenyewe, lakini ni bora akawa wazi hivi sasa.
Sasa, mwaka mmoja umepita tangu alipotoa uamuzi wa kufungua kesi dhidi ya Dk. Slaa, lakini ameendelea kuwa bubu katika hili.
Katika mkutano huo, Mgonja alisema tuhuma zote zilikuwa na nia ya kumpaka matope, uzushi na upotoshaji mkubwa mbele ya jamii, sasa hapa nikubaliane na Mgonja au Dk. Slaa? Nadhani Dk. Slaa alikuwa katika nafasi ya juu.
Naamini Mgonja ameshikwa kihoro kutokana na ukweli kwamba wahusika wengi wa first eleven wamepata pigo, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.
Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, tumeshuhudia viongozi kadhaa akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, wakijiuzulu nyadhifa zao.
Licha ya Lowassa kujiuzulu kutokana na kashifa ya Kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, wengine waliosalia wametoka kwenye kikosi hicho ambacho sasa tunaamini kinazidi kupwaya siku hadi siku.
Kama vigogo hawa walifikia uamuzi wa kuondoka madarakani, nini kilichomzuia Mgonja asingoke licha ya kuandamwa kiasi hiki jamani!
Mgonja amekuwa mfanyakazi wa serikali kwa miaka 33, anatumia maneno haya kutaka abaki na ufisaidi wake. Tafadhali niache nibaki na ufisadi wangu, maana sitaki kabisa kuzungumzia suala hili, wewe nenda lakini uadilifu wangu ndio ulionifanya niwe kazini kwa muda wote huu.
Kama Mgonja unaelewa wazi uadilifu wako ndio umekuweka madarakani kipindi chote hicho, umeshindwa nini kutumia uadilifu huo huo kujiuzulu ili uwe mfano kwa viongozi wengine?
Binafsi nasema umefika wakati sasa Watanzania tuseme tumechoshwa kuongozwa na wanaotuhumiwa.
Ninaufahamu urafiki wako na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, bila kumsahau swahiba Basil Mramba.
Naelewa majina hayo niliyoyataja hapo juu yalivyolalamikiwa na Watanzania wakati wakiwa madarakani.
Wananchi walishuhudia ununuzi wa rada na ununuzi wa ndege ya rais haya yote ni mzigo mzito ambao tunaendelea kubebeshwa na kuulipa kupitia kodi zetu.
Napenda kumwambia Mgonja kwamba tuhuma zinatokana na machungu ya maisha yanayowakabili wananchi, kama unavyosema mwenyewe kuwa ni mwadilifu, umefika wakati sasa kukaa kando na kuwapa imani watu wengine kuhusu uadilifu wako.
Kwa nini viongozi wetu wanataka kuondolewa madarakani kwa viboko hawana utamaduni wa kuondoka wenyewe bila kushinikizwa na kupigiwa kelele kila kukicha?
Mfano mzuri tumeuona kwa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, aliyeshinikizwa kujiuzulu, naye bila kipingamizi amekubali kwa kauli moja. Huo ndio utawala bora unaozingatia masilahi ya taifa.
Mgonja akumbuke kilio hiki kinatokana na matumizi mabaya ya fedha za wananchi maskini wanaovuja jasho kila siku iendayo kwa Mungu huku wakipigwa jua barabarani.
Lakini Mgonja na wenzake wamekuwa watumiaji wa magari aina ya VX Land Cruiser, maarufu kama mashangingi, hawajui kabisa kama wapo wazalendo wanataabika mitaani.
Tunaamini kwamba kama serikali ikisema leo ifanye uchunguzi wa kina kwa kila kiongozi hapo wizarani kwako, kuanzia wewe na wengine, hakuna atakayebaki, kutokana na ukweli kwamba wengi wamejichotea mamilioni ya fedha zetu.
Wakati sasa umefika kwa Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko katika Wizara ya Fedha na Uchumi, kwa kumwondoa Mgonja, wakurugenzi na wasaidizi walio chini yake, kwa kuwa naamini kabisa kwamba wanao mtandao, hivyo usipovunjwa tutabaki kulalama tu.
Mgonja, sitakuacha hata kidogo. Nitaendelea kupambana na wewe hadi utakapoondoka kwenye wadhifa huo.