Askari waasi wamemuua kwa risasi Rais Joao Bernardo Vieira, maofisa wa serikali wamesema. Habari hizo zilikuja jana saa chache baada ya mauaji ya mkuu wa majeshi ambaye alikuwa katika mtafaruku na Rais.
Milio ya risasi ilisikika jijini hapa na mpaka leo hakukuwa na taarifa za nani anaiongoza serikali. Nchi hii ni moja ya nchi masikini sana duniani, na ina historia ya mapinduzi ya serikali na imekuwa njia kuu ya dawa za kulevya, hususan kokeni kwenda Ulaya.
Taarifa ziliwakariri maofisa wa kijeshi na serikali waliosema Rais ameuawa. "Rais Vieira aliuawa na Jeshi alipokuwa akijaribu kukimbia makazi yake ambayo yalishambuliwa na kikundi cha wanajeshi watiifu kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Tagme Na Waie, mapema asubuhi hii," msemaji wa Jeshi, Zamora Induta aliiambia AFP.
Alimtuhumu Rais Vieira kwa kuhusika na mauaji ya mkuu wa majeshi. Jenerali Tagme aliuawa baada ya mlipuko kusikika juzi na kuharibu sehemu ya makao makuu ya jeshi. Msaidizi wake, Luteni Kanali Bwam Nhamtchio, alisema Tagme alikuwa ofisini mlipuko huo ulipotokea. "Alijeruhiwa sana asingeweza kupona.
Hili ni pigo kwetu sote," alisema Nhamtchio. Takriban watu watano waliripotiwa kuuawa na mlipuko huo. Kutokana na mashambulizi hayo dhidi ya makao makuu ya Jeshi, maofisa waliviamuru vituo viwili vya redio kusitisha matangazo.
"Kwa usalama wenu waandishi wa habari, fungeni kituo na kuacha kutangaza. Ni kwa usalama wenu," msemaji wa Jeshi Samuel Fernandes aliwaambia waandishi wa habari katika moja ya vituo hivyo. "Tunakwenda kupambana na wavamizi na kujilinda," aliongeza.
Rais na Mkuu wa Majeshi inasemekana wamekuwa hawaelewani kwa miezi kadhaa sasa. Askari hao waasi Novemba mwaka jana walishambulia makazi ya Rais katika jaribio la mapinduzi ambalo halikufanikiwa. Haijajulikana nani kiongozi wa mashambulizi dhidi ya Jenerali Tagme, lakini inaonyesha jinsi amani ya nchi hii ilivyo tete bado, mwandishi wa BBC alisema.
Baada ya mashambulizi ya Novemba mwaka jana, Rais alipewa kikosi maalumu chenye askari 400 kumlinda. Januari mwaka huu, askari hao walituhumiwa kujaribu kumuua mkuu wa majeshi na kikosi hicho kikavunjwa. Nchi hii imegubikwa na mfululizo wa mapinduzi na machafuko ya kisiasa tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ureno mwaka 1974.
Rais Vieira, kama walivyokuwa viongozi waliomtangulia, alikuwa akitegemea sana Jeshi ili kubaki madarakani. Guinea-Bissau ambayo imekuwa njia kuu ya kupitisha mihadarati kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya, imeathirika kwa kiasi kikubwa pia na biashara hiyo. Baadhi ya maofisa jeshini nao wanajulikana kwa kushiriki katika biashara hiyo, chanzo cha habarti kilisema.
Marehemu Vieira ni mwanajeshi aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi, lakini akaondolewa pia na wapinzani wake wa kijeshi na akashinda uchaguzi mara mbili. Alipozaliwa mwaka 1939 nchi hii ilikuwa bado ikitawaliwa na Wareno na alijiunga na chama cha African Party for the Independence of Guinea-Bissau and Cape Verde (PAIGC) mwaka 1960 na kupigania uhuru.
Uhuru ulipatikana mwaka 1974 lakini nchi hii imekuwa katika mgogoro kwa kipindi chote hicho chini ya utawala wa kidikteta. Aliingia madarakani mwaka 1980 kupitia mapinduzi ya kijeshi wakati akiwa mkuu wa majeshi, na miaka 11 baadaye aliondoa marufuku dhidi ya vyama vya siasa kabla ya uchaguzi wa mwaka 1994, ambao alichaguliwa kuwa rais.
Lakini miaka mitano baadaye alipinduliwa baada ya kumfukuza kazi mkuu wa majeshi kwa tuhuma kuwa alikuwa akiwaunga mkono waasi waliokuwa Senegal. Alitimuliwa PAIGC kwa tuhuma za uhaini, kuunga mkono mapigano na vitendo vilivyokuwa vikikiuka kanuni za chama hicho.
Katika mapinduzi ya mwaka 2003, alirejea nchini kutoka uhamishoni Ureno na kugombea urais na kushinda kama mgombea binafsi mwaka 2005. Katika kampeni zake, Vieira alikuwa akijitambulisha kama zawadi kutoka kwa Mungu kwa watu wa Guinea-Bissau-ili arudi kuwaongoza kupata maendeleo na maisha bora. Alishinda kwa asilimia 52 katika mzunguko wa pili wa upigaji kura katika uchaguzi ambao uliitwa mtulivu na huru na waangalizi wa Ulaya.