Gunter Guillaume: Jasusi aliyosababisha Kansela wa ujerumani kujiuzulu

Gunter Guillaume: Jasusi aliyosababisha Kansela wa ujerumani kujiuzulu

mcTobby

JF-Expert Member
Joined
Feb 16, 2018
Posts
7,894
Reaction score
22,679
Hebu Fikiria kwa sekunde moja.

Unatawala moja ya mataifa yenye nguvu zaidi barani Ulaya. Kila siku unajadili siri za vita, diplomasia, NATO, na mustakabali wa taifa lako. Pembeni yako amesimama mtu unayemwamini kabisa. Anakupangia ratiba, anakusindikiza kwenye safari za kikazi, anakuletea nyaraka za siri, na wakati mwingine anajua mipango yako kabla hata mawaziri wako hawajaijua.
Willy_Brandt_Guillaume.jpg

Lakini kuna jambo moja usilolijua.

Kila siri unayomkabidhi, kila mazungumzo ya faragha, kila mpango wa serikali... usiku huohuo unasafirishwa kwa adui.

Hiyo ndiyo ilikuwa hadithi ya Günter Guillaume.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika vipande viwili. Upande wa Magharibi uliungwa mkono na Marekani na washirika wake, huku upande wa Mashariki ukiwa chini ya ushawishi wa Umoja wa Kisovieti. Katikati ya mgawanyiko huo kulizaliwa vita vya siri—vita visivyopiganwa kwa mizinga, bali kwa majasusi.

Taasis ya ujasusi ya Ujerumani Mashariki, Stasi, ilihitaji mtu ambaye angeweza kuingia ndani kabisa ya serikali ya adui bila hata chembe ya shaka.

Mtu huyo hakuwa mwingine bali alikuwa Günter Guillaume.
8ad6bed0-0001-0005-0000-000000196339_w331_r0.7880952380952381_fpx49.85_fpy60.24.jpg

Mwaka 1956, yeye na mke wake walivuka mpaka na kujifanya wakimbizi waliokimbia utawala wa kikomunisti. Walionekana kama wanandoa wa kawaida waliokuwa wakitafuta maisha mapya. Hakuna aliyeshuku kuwa walikuwa wamepewa kazi maalumu iliyoweza kuchukua maisha yao yote.

Na hapo ndipo operesheni ya uvumilivu ilipoanza.
Zaidi ya muongo mmoja.
Guillaume hakuwahi kukurupuka. Alijenga uaminifu polepole. Aliingia kwenye siasa, akafanya kazi kwa bidii ndani ya chama cha SPD, akawa mtu aliyependwa na kuheshimiwa. Wenzake walimwona kama mfanyakazi mwaminifu asiyechoka.

Hakuna aliyejua kwamba kila hatua aliyopiga ilikuwa sehemu ya mpango wa Stasi.

Mwishowe, juhudi zake zilizaa matunda.

Aliteuliwa kufanya kazi moja kwa moja katika ofisi ya Kansela Willy Brandt.
Kwa Stasi, huo ulikuwa ushindi mkubwa kuliko walivyowahi kuota.
Sasa hawakuhitaji tena kubahatisha.

Walikuwa na macho na masikio ndani ya ofisi ya kansela mwenyewe.
Guillaume alisafiri na Brandt ndani na nje ya nchi. Alihudhuria mikutano ya siri. Alishika nyaraka ambazo maelfu ya Wajerumani wasingeweza hata kuziona. Kila alichokiona kilikuwa hazina kwa Stasi.

Kwa miaka mingi operesheni hiyo iliendelea bila kosa.

Lakini hakuna siri inayodumu milele.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, maafisa wa usalama wa Ujerumani Magharibi walianza kuona dalili zisizoeleweka. Mawasiliano fulani ya siri yalionyesha kuwa kulikuwa na jasusi wa kiwango cha juu ndani ya serikali.

Uchunguzi ulifanywa kimya kimya.

Kwa miezi kadhaa walimfuatilia Guillaume bila yeye kujua.

Hatimaye, Aprili 1974, mlango ulifunguliwa.
Maafisa waliingia na kumkamata yeye pamoja na mke wake.

Operesheni iliyokuwa imefichwa kwa karibu miaka ishirini ilikuwa imefika mwisho.

Kilichowashangaza zaidi wachunguzi ni utulivu wake.

Hakubabaika.

Hakulia.

Hakujitetea.

Alikubali kuwa alikuwa ametumwa na Stasi na alikuwa ametekeleza wajibu wake kwa nchi yake.

Habari ziliposambaa, Ujerumani Magharibi ilitikisika.

Raia walijiuliza: Ikiwa jasusi aliweza kufika hadi pembeni ya kansela, ni siri ngapi tayari zilikuwa zimevuja?

Kwa Kansela Willy Brandt, pigo hilo lilikuwa kubwa. Ingawa sababu za kujiuzulu kwake zilikuwa nyingi na za kisiasa pia, kufichuliwa kwa Guillaume kuliharibu sana imani kwa serikali yake. Mnamo Mei 1974, Brandt alitangaza kujiuzulu.

Kwa upande wa Ujerumani Mashariki, Guillaume hakuwa msaliti.

Alikuwa shujaa.

Baada ya miaka kadhaa gerezani, aliachiliwa kupitia mpango wa kubadilishana majasusi kati ya Mashariki na Magharibi yaani Spy swap. Aliporudi nyumbani alipokelewa kwa heshima kubwa kama mtu aliyekuwa ameitekelezea nchi yake moja ya operesheni za ujasusi zilizofanikiwa zaidi katika historia.
guillaume-affaere-2.jpg

Mpaka leo, jina la Günter Guillaume linabaki kuwa ukumbusho kwamba wakati mwingine jasusi hatembei gizani akiwa na bastola mkononi.

Wakati mwingine huvaa suti, hubeba mkoba wa nyaraka, hutabasamu kila siku... na hukaa kiti kimoja tu karibu na kiongozi wa taifa anapoketi.
 
Back
Top Bottom