Hadithi Fupi: Vita vya Maji Mengi

Hadithi Fupi: Vita vya Maji Mengi

Abtali mwerevu

JF-Expert Member
Joined
May 5, 2013
Posts
665
Reaction score
515
Na: Mwalimu Makoba

"NI hadithi kama hadithi za sungura na fisi. Haihusiani na tukio lolote halisi."

Sehemu ya Kwanza

Hapo zamani za kale watu kutoka mbali waliwavamia Wenyeji. Watu hawa waliwachukua na kuwauza kama anavyouzwa mbuzi mnadani. Ili kujihakikishia Wananchi hawafurukuti au kuanzisha matata, walifungwa minyororo, uhuru kwisha! Jambo hili liliitwa utumwa.

Inasemekana wale walionunuliwa na wavamizi kutoka mashariki ya mbali walihasiwa pengine ndiyo sababu mbegu ya Wenyeji haionekani vyema huko!

Wenyeji walifanya kila juhudi kujinasua na msiba huu ulioitwa utumwa, lakini hawakufua dafu. Ilitokea bahati, wanyang’anyi wa upande mwingine kuona sasa waachane na unyang’anyi huu wafanye unyang’anyi ule. Basi Wenyeji wakanusurika baada ya kuwa wameteseka kwa mamia ya miaka.

Furaha haikudumu kwa muda mrefu, Wenyeji wakavamiwa na watu kutoka Magharibi na kufanywa watumwa katika nchi yao.

Mungu hamtupi mja wake, Wenyeji wakapata bahati, akazaliwa Kanyere.

Inasimuliwa mkasa wa kuzaliwa kwake unastaajabisha. Alizaliwa akiwa na meno yote tena kichwa chake kikiwa na nywele nyeupe peee! Alivyoendelea kukua nywele zikabadilika rangi na kuwa nyeusi.

Inaelezwa siku aliyozaliwa, mkunga na watu wengine waliokuwepo walipomtolea macho alifoka, “Mnashangaa nini? Nisafisheni hamuoni nimetoka tumboni mwa Mama yangu?”

Mama alipoletewa Makande, kichanga hiki kiliyarukia kikisema, “Niache nile mimi mpya, wewe umekula siku nyingi!” Na kweli kikayala makande chungu kizima.

Inaaminika kwamba siku ileile kaliomba kaletewe Wazee wote. Walipofika kakasema, “Nimekuja kwa kazi moja tu, kuwarudishia uhuru, hakikisheni mnanilinda nisije nikauawa kabla sijatimiza jambo hili. Atakayenijaribu, mchapeni.”

Inaelezwa wazee walielewana mno na kichanga hiki cha ajabu. Wakati wengine wakishangaa wazee walisema, “Imetimia, mkombozi kazaliwa.”

Tangu kilipokuwa kitoto kiliitwa Kanyere, hakuna ajuaye tafsiri ya jina hili kwani kilijipa chenyewe, kilipozaliwa tu kilisema, “Jina langu Kanyere!” kilipoulizwa nini maana ya jina hili kilijibu, “Acha umbea!”

Soma: Mfumo wa Maombi wa Ajira za Serikali Unavyoweza Kukupa Kazi
 
Sehemu ya Pili
Kijitu hiki cha ajabu kilipokua, kikaanza hekaheka. Hekaheka zilizidi mpaka wakoloni wakaikimbia nchi. Watu wanasimulia wakoloni walipolewa kaliwapasulia mayai mabovu katika makalio yao. Wakaikimbia nchi kwa aibu.

Baada ya Uhuru Kanyere hakuonekana sana, alikaa muda mfupi akapotea, hakuna aliyejua wapi alikwenda.

Hata hivyo, Shujaa Bwana Mako, mwindaji anayewinda kwa kuwakimbiza wanyama mpaka kuwakamata, alisema alimuona Kanyere akiwa msituni ndani ya pango liwakalo moto huku na huku. Walipojaribu kumtafuta hawakumpata. Wapita njia wakasema walimuona akihama na vitu vyake kwenda Kaskazini, alitembea mwendo wa haraka kiasi kwamba ni mwanga pekee ungeweza kumpata.

Wenyeji waliishi vyema chini ya wafalme wao. Mfalme anayesemwa sana ni Mfalme Komesha. Mfalme huyu alifia madarakani. Miaka yote wafalme walipozeeka, walirithisha ufalme kwa mtoto wa kwanza wa kiume. Kifo kikawakuta wakiwa wameachia madaraka. Komesha hakuzeeka, alikufa mapema kabla hajang’atuka madarakani. Haijulikani hasa ugonjwa uliomuua, jambo pekee linalojulikana ni kwamba, ALIKUFA.

Alipokufa Komesha paliibuka minong’ono mikali, “Nani atarithi ufalme, komesha hana mwana wa kiume.” Ni kweli, Hayati Mfalme Komesha aliacha watoto tisa, wote wa kike!

Nchi ilikaa siku tisini bila mfalme ikijiendea huku na huku kama kuku mgeni aliyekata kamba. Katika wakati huu wa kukosa kiongozi, uhuni mwingi ulifanyika Wenyeji wakaona umuhimu wa kuwa na mfalme.

Wakati Wenyeji wanatamani kuwa na mfalme, ndiyo siku ambayo kiu yao ilipozwa. Saa nne asubuhi katikati ya nchi alisimama mtu asiyefahamika. Katikati ya nchi ni mahali ambapo yeyote ambaye angesimama angeweza kuonwa na wananchi wote. Hivyo basi, walevi nyie mnawaita wanasiasa, walipenda kusimama katikati ya nchi ili wazungumze na Wenyeji.

Mwanaume huyu aliyevalia nguo ya moja kwa moja yenye rangi ya kahawia alikuwa na ndevu nyingi, alianza kwa kujitambulisha kwamba yeye ni Mwanafalsafa. Akawaomba Wenyeji wamsikilize.

Wenyeji wanasimulia kwamba mtu huyo hakuwa Mwenyeji, alikuwa mgeni kwani hakuna aliyewahi kumuona hapo kabla. Lakini kwa sababu walichoka kuishi bila mfalme na mambo yalianza kwenda segemnege walichagua kumsikiliza.

Soma: Uhakiki wa Wimbo wa Nipeni Maua Yangu
 
Sehemu ya Tatu

Akiisha kujitambulisha kuwa yeye ni mwafalsafa, akayamwaga maneno. “Ndugu zangu nchi haiwezi kwenda bila mfalme. Ni lazima tuchague mfalme. Mfalme lazima atoke katika familia ya kifalme lasivyo vita havitakwisha. Mimi ni mwanafalsafa na katika falsafa zangu ninayo falsafa ya haki za binadamu. Binadamu wote ni sawa wanawake kwa wanaume. Wanawake wanao uwezo wa kuongoza vizuri kama walivyo wanaume. Mfalme aliacha watoto tisa wa kike, mtoto wa kwanza yupo, anatosha kuongoza mpaka atakapomaliza muda wake.”

Akiisha kusema maneno yake, akakuna ndevu zake ndefu nyeupe, kisha akawatazama Wenyeji ambao walikuwa katika zogo. Wengine wakikubali na wengine wakikataa.

Mwanafalsafa akamualika Mkuu wa mizimu wa serikali, haraka akamuapisha mtoto wa kwanza wa mfalme kisha baada ya uapisho mwanafalsafa akatangaza, “Tayari tumemuapisha. Ili kupunguza utata kwa jambo hili jipya, asiitwe Malikia, aitwe Mfalme. Mfalme Mikaili.”

Hivyo ndivyo Mfalme Mikaili alivyoingia madarakani. Wabishi wachache wakaendelea kubishana na waelewa wengi. Mikaili katika uongozi wake alianza kwa kasi akitengeneza nchi katika mienendo mizuri hata ikafikia hatua kiongozi wa Wabishi akatamka hadharani kuwa Mikaili ni kiongozi bora asiye na mfano. Baadhi wakamdhihaki kiongozi wa wabishi kuwa aliramba tongwa. Vyovyote vile, Mikaili aliongoza vyema hata ile minong’ono ya ubaguzi wa kijinsia ikaisha, hakuna tena aliyekumbuka. Hata habari hizi zilipatikana kwa shida kwani Wenyeji hawakukumbuka vyema!

Aliongoza vyema kwa miaka mingi. Wabishi walipoona sasa hawana la kusema, wakamzulia jambo. Wakasema Mfalme Mikaili hakuwa mtoto halali wa Mfalme Komesha. Wakasema mama yake aliolewa akiwa tayari na mtoto aliyezaa na mtu mgeni. Wengine wakaenda mbali zaidi kwa kusema wakimuona mgeni huyo wanaweza kumtambua. Walipoulizwa alifafananaje, wakajibu sura wameisahau, wanazikumbuka ndevu zake tu. Habari hii kwa kukosa ushahidi na kuonekana iliyojaa chuki binafsi, ilipotea ikarudi ilikotokea kupitia njia kumi na nne.

Mfalme Mikaili alipendwa na watu wake, akajizolea umaarufu mkubwa hata nchi jirani zikaanza kumpa tuzo kwa uongozi uliotukuka. Naye hakubweteka, aliendelea kuongoza vyema hata akafikia hatua ya kuwasamehe wafungwa wa kisiasa waliofungwa wakati wa utawala wa Mfalme Komesha. Watu wakasema, Mikaili ni mwanademokrasia.

Soma: Jinsi ya Kuomba Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu
 
Sehemu ya Nne

Siku moja Bwana Mako akiwa mawindoni, akimnyatia sungura mzee, aliona mtu akija kwa kasi ya upepo. Alipofika karibu na Bwana Mako akadondoka, vumbi jingi likatimka hata wakashindwa kuonana kwa dakika mbili.

Vumbi lilipoisha mtu yule mwenye kipara na viatu vyenye kamba nene akasema, “Kimbia kawaaambie wazee, mfalme anamkataba aliosaini na mwanafalsafa. Mkataba ule hakuna aliyeusoma kwani amefanya siri na haiwezekani kuupata kwani mchana anatembea nao na usiku anapolala anauweka mchagoni.”

Akiisha kusema hayo, mtu yule alinyanyuka na kurudi kwa namna ileile aliyokuja nayo.

Bwana Mako hakupoteza muda. Alikwenda haraka kuwapasha wazee habari ile mpya. Aliwakuta wamekaa kwa kutulia wakikuna ndevu zao nyeupe. Baada ya kuwapa taarifa ile. Kengele ya dharura ikagongwa, wazee wakakusanyika wakiwa na vifaa vyao vya kazi na mazungumzo yakaanza.

“Bwana Mako itabidi uulete mkataba huo. Fanya maarifa yote tuupate hapa, tuusome.”

“Atawezaje?” Mzee mmoja alidakia. “Kama alivyoleta habari, huo mkataba mchana anatembea nao na usiku analala nao, tena anauweka mchagoni!”

“Bwana Mako hakosi maarifa.” Mzee mfupi alisisitiza.

“Hili jambo ni nyeti kuliko nyeti tulizonazo,” alisema Mzee mzee kuliko wote. “Lazima kwa kujua hivyo mfalme amejipanga vyema kuulinda mkataba wake usiwafikie wazee na Wenyeji kwa ujumla. Pia ni jambo la hatari sana na pengine itamkwaza mfalme endapo mkataba huo utakuwa mzuri na hauna tatizo lolote. Atahisi hayuko huru na anahujumiwa. Hata hivyo, wazee lazima wajue mambo yote kwani ndiyo waliobeba busara ya Wenyeji. Bwana Mako anapokwenda huko, tuhakikishe anapata baraka za Kanyere. Kiongozi wa mizimu ni wakati wako sasa kufanya hivyo.”

“Tchaa! Tchaa! Tchaaa!” Kiongozi wa mizimu alianza kwa chafya mkononi ameshika ugoro. Kisha akabadilika sura yake na kuanza kumeremeta kama anayemulikwa na taa. “Kanyere! Kanyere! Kanyere! Nimekuita mara tatu. Wewe ulipozaliwa ulituita mara moja, wazee tukaja kukusikiliza. Nasi tunakuita leo. Njoo Kanyere.”

Kilipita kimya cha dakika tano. Katika ukimya huo, sisimiza mdogo angeweza kusikika akipita. Mara ghafla katika hali ya upepo usiopuliza, akaibuka Kanyere, mkononi kabeba fimbo nyeusi.
 
Sehemu ya Tano

“Nimekuja wazee,” alisema Kanyere akizungukazunguka. “Mnataka msaada wa kufungua nywila, wazee msipitwe na jambo, mjue yote na hiyo ndiyo salama ya Wenyeji.”

“Ndiyoo,” wazee waliitika. Kanyere akatembea mpaka alipokaa Bwana Mako, akanyanyua fimbo yake kama anayetaka kumpiga nayo, Bwana Mako akashtuka anayefumba macho yake.

“Bado hujawa.” Kanyere alimwambia Bwana Mako. Kisha akazungukazunguka halafu akamrudia tena na kumtisha kama anayetaka kumpiga na fimbo yake, safari hii Bwana Mako hakushtuka, alibaki amemkazia macho kwa ujasiri. Kanyere akatabasamu, “Sasa umekuwa!” Wazee wakashangilia.

Mwanamume aliyevalia mavazi meusi tena yaliyofunika sura yake alionekana akitembea kwa kunyata pembezoni mwa ukuta mrefu wa Ikulu ya Mfalme. Alipofika karibu na lango la kuingia, akawaona walinzi wawili. Akatoa kitu kama filimbi halafu akakipuliza, kitu mfano wa mshale mdogo kikatoka na kumchoma mlinzi wa kwanza ambaye alidondoka hapohapo. Yule mwenzake akamsogelea akimshangaa, naye akadondoka chini.

Mtu huyu aliyevaa kama ninja, akautambaa ukuta mithili ya mjusi alipofika juu akajiachia na kujikuta akiwa katikati ya walinzi wawili. Kwa kasi ya radi, akapuliza kile kifaa chake huku na huku, walinzi wakadondoka.

Alitembea kwa mwendo wa kilomita mbili akijificha kunako miti mirefu ili asionekane na walinzi wengine. Mwisho alilifikia dirisha la chumba cha mfalme. Akatoa kichupa kidogo na kuanza kupulizia ndani ya chumba. baada ya dakika mbili akazunguka kuliko mlango wa kuingia chumba kile mahali palipofungwa, alitumia funguo bandia kupafungua. Hatimaye alikuwa ndani, haraka akashika mchagoni akitafutatafuta kitu. Kisha akaona bahasha ya kaki, alipofungua ndani akautoa mkataba. Bila kupoteza muda, alitoa kitu mfano wa mashine ndogo aliyokuwa ameificha nyuma ya mgongo wake. Mashine hiyo iliandikwa maandishi madogo yaliyosomeka, ‘Teknolojia ya Mizimu’ akachukua karatasi zile za mkataba na kuwa kama anayezipiga picha. Kisha akabonyesha mahali fulani, mashine ile ikatoa karatasi sawa na zile za mkataba. Alipomaliza akarejesha karatasi za mkataba wa awali sehemu yake akahakikisha kila kitu kipo sawa na kutoka akifunga alipofungua. Alitoka kwa shida kuliko alivyoingia, hata hivyo aliweza kufika salama kwa wazee na aliwakabidhi walichomtuma.

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi
 
Sehemu ya Sita

Usiku wa manane wazee walikaa kikao. Wote walikusanyika, hakuna aliyekosekana hata mmoja. Sura zao hazikuonyesha masihara hata kidogo, walikuwa makini kuliko wakati wote wa maisha yao.

Kabla kikao hakijaanza, Kiongozi wa mizimu alimchukua mbuzi mmoja kwa ajili ya sadaka ya kulikinga eneo hilo. Isivyo bahati akiwa pembezoni mahali pa kutolea sadaka, akagundua alisahau kisu, kwa unyeti wa siku hiyo, muda usingetosha ili kuokoa muda hakuwa na namna nyingine isipokuwa aliiamuru radi imchinje mbuzi yule. Kitendo cha kufumba na kufumbua kwa amri ya Kiongozi wa mizimu, radi ilimkata shingo mwana mbuzi akagawanyika vipande viwili.

Mahali hapo hapakuwa na mtu mwingine isipokuwa wazee, hata Bwana Mako alipomaliza kuwapatia mkataba ule hakuruhusiwa kuwa sehemu ile kwani ili kukaa hapo zilihitajika nguvu za ajabu zilizohifadhiwa katika uzee.

Wazee wakiwa wamekaa kwa utulivu. Walimsikiliza Mzee mzee kuliko wote aliyekuwa ameshikilia karatasi tayari kuanza kusoma.

“MKATABA WA KUUZA MAJI MENGI,” alianza kusoma. “Sisi Wenyeji, tumeuza maji mengi kwa Wageni kwa vipande thelathini vya fedha…” kabla hajaendelea kusoma, Kiongozi wa mizimu akasikika, “Usaliti mkubwa.” kisha akaokota jiwe kubwa na kuanza kuelekea kaskazini. Ilitumika busara ya hali ya juu kumtuliza. Alipokubali kutulia, msomaji akarudia tena.

“MKATABA WA KUUZA MAJI MENGI. Sisi Wenyeji tumeuza maji mengi kwa Wageni kwa vipande thelathini vya fedha. Maji haya siyo yetu tena milele na mkataba huu hauvunjiki kwa kiapo cha kimataifa.”

Wazee wote walishika vichwa.

“Usaliti!”

“Tumeuzwa!”

“Hatutakubali!”

“Tuamshie Kanyere!”

“Wachape radi wasaliti!”

Kila Mzee alisema lake hata pakawa sehemu ya gumzo mahali pale. Mzee mzee kuliko wote alipoonyesha dalili za kusema, wazee wakanyamaza.

Alianza kwa kupiga chafya, kisha machozi matatu yakambubujika. “Historia ya kweli inaandikwa na watu wenye mavazi, watu wasio na nguo hawana mchango wowote! Hizi ni juhudi za kuwavua nguo wazee na kujaribu kwa makusudi kuwafuta Wenyeji katika historia. Tunaweza kuuza maji yetu wenyewe. Tutakunywa nini? Maji tuliyokukwa tunayapata bure, tumeyauza na sasa tujiandae kuuziwa. Uhuru uko wapi? Itambulike kuwa harakaharaka haina baraka. Pesa tutapata taratibu na si busara kuuza Maji Mengi kwa wageni kwa tamaa ya kupata pesa za haraka. Kila kitu kinakwenda hatua kwa hatua, huwezi kuwapa mimba wanawake tisa kwa siku moja kisha utegemee kupata mtoto ndani ya mwezi mmoja. Kuna mambo yanahitaji muda kama yalivyo maendeleo…”

Kabla hajamaliza hotuba yake, Kiongozi wa Jeshi la Wazee akaibuka akigawa panga mpya kwa kila mzee. Akiisha kumaliza kuzigawa, wazee wakanyanyua panga zao juu nazo zikameremeta na kutengeneza mwanga mmoja. Wakasikika wakisema kwa sauti isiyokuwa na masihara, “Mapanga haya yatatoa damu itakayotupatia uhuru!”

MWISHO

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Back
Top Bottom